‘Punguza makongamano ya Ukimwi, hudumia waathirika’

Dr Alli Tarab

Dkt Ali Tarab

“….ni jambo la kusikitisha sana kusikia ya kuwa 19% ya maambukizi ya VVU hapa nchini ni kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT+). Kiasi hicho cha watoto wachanga wasio na hatia, wanakuja duniani wakiwa tayari wameshaambukizwa VVU. Maambukizi haya yanatokea ikiwa virusi vitaingia katika mfumo wa damu wa mtoto kutoka katika damu ya mama wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua au wakati wa kunyonyesha.”

Hotuba ya Dkt. Ali Tarab Ali (Mb), Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2008/2009

I. Utangulizi

Mheshimiwa Spika, Mwanzoni kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kunipa uhai na kuniwezesha hivi leo kusimama hapa mbele yenu. Pili, nakushukuru wewe Mheshimiwa Spika kwa kuniruhusu kutoa maoni ya kambi ya upinzani kuhusiana na bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kwa mujibu wa kanuni za Bunge kanuni ya 99(7) toleo la mwaka 2007.

1. Aidha, namshukuru Naibu Waziri kivuli wa Afya, Mhe Omar Ali Mzee kwa msaada mkubwa katika kutayarisha hotuba hii. Pia nawashukuru wapiga kura wa jimbo la Konde kwa kuwa na imani isiyoyumba kwa mkombozi wao, Chama cha Wananchi CUF.

2. Mheshimiwa Spika, nitakuwa mnyimi wa shukrani kama sitowashukuru viongozi wetu wa Kambi ya Upinzani hapa bungeni, Mhe Hamad Rashid Mohammed na Mhe Dr Slaa, kwa umahiri na uongozi wao mzuri na ushauri wao katika matayarisho ya hotuba hii. Hatimaye, na si kwa umuhimu, nawashukuru nyinyi wabunge wenzangu pamoja na wananchi wote wa Tanzania popote walipo, kwa kuniazima masikio yenu na kunisikiliza kwa makini hivi sasa.

3. Mheshimiwa Spika, mara baada ya uhuru, katika miaka ya sitini, tulipiga mbiu na kusema ya kuwa tunao maadui watatu – umasikini, ujinga na maradhi. Ni kweli, tumepiga hatua kubwa tangu siku hizo kufuta ujinga na katika nyanja ya elimu kwa ujumla. Ingawaje, leo bado wa-Tanzania wengi ni masikini wa kutupwa na bado sekta ya afya inabidi kuendelezwa ili kuondokana na maradhi yanayotusumbua.

4. Mheshimiwa Spika, moja katika matatizo ya msingi yanayoikumba sekta ya afya ni upungufu mkubwa wa wafanyakazi. Ripoti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya 2006 inathibitisha ya kuwa katika sekta hii wapo wafanyakazi 32% tu wakati wengi wao ni wenye umri wa miaka 40 na zaidi, hivyo wanaelekea kustaafu.

5. Mheshimiwa Spika, tumesema haya mara nyingi kwa madhumuni ya kuizidua serikali, ya kuwa nchi yetu inayo uiyano mbaya sana wa madaktari kulingana na idadi ya watu nchini. Kwa mujibu wa takwimu za karibu kabisa za Shirika la Afya Duniani (WHO) (2004), ukiwacha visiwa vingi vidogo vidogo (island states) vya Polynesia na vilivyopo katika bahari ya Atlantic, ambavyo takwimu zao hazikupatikana, Tanzania ni karibu nchi ya mwisho duniani tukilinganisha idadi ya madaktari kwa idadi ya watu. Tanzania ni nchi ya 183 tukiwa mbele ya Malawi na Rwanda tu. Kwa takwimu hizo Tanzania inayo madaktari 2.3 kwa kila watu 100,000 wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza nchi zetu ziitwazo Ulimwengu wa Tatu kuwa na angalau madaktari 10 kwa kila watu 100,000. Huu ni msiba mkubwa Mheshimiwa Spika.

6. Mheshimiwa Spika, hebu tuangalie basi uyiyano huu kwa nchi zinazotuzunguka. Lesotho inayo madaktari 5.4 kwa watu 100,000, Zimbabwe inayo madaktari 5.7 kwa watu 100,000, Zambia inayo madaktari 6.9 kwa watu 100,000, Madagascar inayo madaktari 8.7 kwa watu 100,000, Kenya inayo madaktari 13.2 kwa watu 100,000, Swaziland inayo madaktari 17.6 kwa watu 100,000, Congo Brazaville inayo madaktari 25.1 kwa watu 100,000, Namibia inayo madaktari 29.5 kwa watu 100,000 na Botswana inayo madaktari 28.8 kwa watu 100,000.

7. Mheshimiwa Spika, hata nchi jirani zilizokuwa na migogoro na vita miaka mingi, bado zinazo uwiano bora zaidi kushinda wetu. Mfano, Mozambique inayo madaktari 2.4 kwa watu 100,000, Ethiopia inayo madaktari 2.9 kwa watu 100,000, Eritrea inayo madaktari 3 kwa watu 100,000, Somalia inayo madaktari 4 kwa watu 100,000, Uganda inayo madaktari 4.7, Burundi inayo madaktari 5.2 kwa watu 100,000, D. R Congo inayo madaktari 6.9 kwa watu 100,000 na Comoro inayo madaktari 7.4 kwa watu 100,000 na Angola inayo madaktari 7.7 kwa watu 100,000.

8. Mheshimiwa Spika, hali hii inayotisha na kuvunja moyo inaweza kuboreka tu ikiwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, iliyo na jukumu la kusomesha madaktari kukaa pamoja na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Chuo Kikuu cha Sayansi za Afya Muhimbili (MUCHS), ambacho ndio chuo pekee cha umma kinachosomesha madaktari hivi sasa kwa kusudi la kutengeneza mpango mkakati, kama ule wa MMEM na MMES wenye madhumuni ya kuongeza kwa kiasi kikubwa kusomesha madaktari nchini.

9. Mheshimiwa Spika, vyenginevyo hata lile lengo letu la kuifanya Tanzania iwe nchi yenye kipato cha kati ifikapo 2025 (vision 2025) inaonekana kuwa ni ndoto tu. Mfano wa nchi yenye kipato cha kati ni Afrika ya Kusini. Lakini nchi hiyo inao madaktari 69.2 kwa watu 100,000 kwa takwimu za 2004.

10. Mheshimiwa Spika, mwaka 2025 utafika baada ya miaka 17 kutoka sasa. Sijui itokee miujiza gani hata tufikie uwiano wa madaktari kwa idadi ya watu kama ulivyo kwa Afrika ya Kusini kwa kipindi hichi kilichobaki!

11. Mheshimiwa Spika, kusomesha wafanyakazi wa kada ya afya peke yake haitoshi. Jambo jengine muhimu ni kuwafanya wabaki katika hospitali zetu (retantion). Hii itafanyika tu ikiwa maslahi yao yataboreshwa.

12. Mheshimiwa Spika, wafanyakazi wa sekta ya afya, juu ya uchache wao, lakini kwa ujumla wanafanya kazi katika mazingira magumu, kwa bidii, kwa kujituma na kwa upendo. Hivyo hapana budi kuwapongeza.

13. Mheshimiwa Spika, madaktari nchini kila siku wanalazimika kutibu watu zaidi ya 50, idadi ambayo huathiri utendaji wao wa kazi. Ingawaje, mishahara yao haikidhi hata mahitaji muhimu. On call allowance haitoshelezi hata kununua petrol ya kumfikisha hospitali.

Mheshimiwa Spika, wauguzi wenye shahada (B.Sc Nursing) hawathaminiwi. Shahada zao hazitambuliwi na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na mishahara yao iko chini, wakilinganishwa na Ofisa Wauguzi Daraja la 3 wakiwa na mshahara wa TGS D.4. Hili linawavunja mno mori na ari ya kazi wauguzi hawa. Tukumbuke, ni wauguzi hawa wenye shahada ndio wanaokwenda kufundisha kwenye vyuo vya afya.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka Waziri alieleze Bunge lako Tukufu ni kwa nini shahada za wauguzi hawa, ambazo zinatunukiwa na MUHAS, hazitambuliwi na kwa nini hawalipwi kulingana na kiwango cha taaluma zao.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2004/2005 MUHAS, wakati huo chuo hicho kikiwa bado kinajulikana kama ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi za Afya Muhimbili (MUCHS), kilidahili wanafunzi 84 ili kusoma Shahada ya Uuguzi. Mwaka 2005/2006 chuo hicho kilidahili wanafunzi 82, mwaka 2006/2007 kilidahili wanafunzi 71, lakini mwaka 2007/2008 ni wanafunzi 4 tu ndio waliodahiliwa. Mwaka huu wa 2008/2009 ni wanafunzi 2 tu ndio walioomba kudahiliwa kusoma shahada ya Uuguzi. Hii imeletea udahili kwenye fani hii kusitishwa kabisa. Hichi ni kigezo kinachoonesha kiasi cha kuvunjwa moyo kwa wahitimu wa fani hii na kiasi vijana wenzao wanavyokimbia sasa kusomea Shahada ya Uuguzi.

Kambi ya Upinzani, inataka maelezo kwa takwimu hizi kweli tuko makini kukidhi malengo ya Mkukuta katika afya au tunacheza na kodi za watoka jasho?

Mheshimiwa Spika, wauguzi wa diploma pia ni wachache. Kwenye wodi ya wazazi Muhimbili, muuguzi mmoja anawahudumia watoto wachanga 50 wanaozaliwa. Kwenye wodi za watu wazima ambapo wakati mwengine panakuwa na wagonjwa kiasi cha 50 au 60 wengine wakilala chini anakuwepo muuguzi mmoja au wawili.

Mheshimiwa Spika, mishahara yao ni duni, vitendea kazi vina ubora hafifu. Ni aibu ya kuwa hata on call allowance ya wauguzi ni sh 150 tu, na overtime allowance hawapati kabisa!

Mheshimiwa Spika, mafundi maabara (laboratory technitians) wanahitaji motisha kwani wamekata tamaa. Mishahara yao ni duni. Wanafanya kazi bila ya risk allowance hasa ukitilia maanani ni wafanyakazi hawa ndio wanaofanya vipimo vya damu, kinyesi na uchafu mwengine wa mgonjwa. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuangalia upya maslahi ya watendaji hawa.

Mheshimiwa Spika, Kuna watumishi ndani ya wizara ambao hawakubahatika kusoma Sekondari na wana ari ya kufanyakazi na pia wanatafuta vyuo lakini vyeti vya kidato cha nne hawana, je wizara inawasaidiaje ili wapate nafasi ya kusoma elimu ya Sekondari ili baadae wajiunge na vyuo?

III. VVU/UKIMWI

Mheshimiwa Spika, mwaka uliopita wa 2007/2008 tulipata msaada wa sh. billioni 595.7 na serikali ikachangia sh. Billioni 27.5 katika vita dhidi ya kusambaa VVU/UKIMWI nchini. Mchango huu wa serikali ni 5% tu ya fedha zote zilizotengwa katika vita dhidi ya gonjwa hili hatari. Tunaomba Mheshimiwa Waziri atueleze, kwa nini Serikali ilitoa mchango mdogo kiasi hichi na itakuwaje pindipo wadau wa maendeleo wakipunguza au kusitisha msaada wao.

Mheshimiwa Spika, kati ya fedha hizi 48% zilipelekwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, 31% zilipelekwa katika wizara, Idara & wakala mbali mbali, 16% zimepelekwa TACAIDS na 5% tu ndio zilizogawiwa halmashauri.

Mheshimiwa Spika, 5% zilizogawiwa Serikali ya Mitaa ni kidogo mno. Na hata hivyo, si zote katika pesa hizo zinazofika huko ambako ndiko waliko walengwa.

Mheshimiwa Spika, niruhusu nitoe mfano:

  • Halmashauri ya Wilaya ya Ngara ilipangiwa bajeti ya sh millioni 130. Lakini kilichofika ni sh millioni 18, (14% tu).
  • Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo ilipangiwa bajeti ya sh millioni 99. Lakini kilichofika ni sh millioni 62, (63% tu)
  • Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ilipangiwa bajeti ya sh millioni 124. Lakini kilichofika ni sh millioni 48.7, (39% tu)
  • Halmashauri ya Wilaya ya Kyela ilipangiwa bajeti ya sh. millioni 86. Lakini kilichofika ni sh millioni 33, (38% tu).

Hii inathibitisha ya kuwa fedha kidogo tu ndio zinazowafika walengwa vijijini.

Kambi ya Upinzani inataka kuelezwa fedha zinakwenda wapi? Kwa kuangalia mifano hiyo hapo juu.

Mheshimiwa Spika, taarifa za matumizi ya fedha za VVU/UKIMWI kwa kiasi kikubwa haziainishwi hasa kwenye halmashauri (not classified). Hivyo, ingawa kambi ya upinzani inapendekeza ya kuwa fedha nyingi zaidi zipelekwe kwenye halmashauri ili ziwafike walengwa, lakini kuwe na uwazi katika matumizi yake na mahesabu yarejeshe kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, Tunaitaka Serikali kupunguza matumizi kwa makongamano, warsha na mikutano ambayo yanatumia fedha nyingi. Ili fedha hizo ziongezewe kwenye dawa za kupunguza makali ya VVU/UKIMWI lakini pia tuwekeze vyema katika kukinga maambukizi mapya.

Mheshimiwa Spika, ni jambo la kusikitisha sana kusikia ya kuwa 19% ya maambukizi ya VVU hapa nchini ni kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT+). Kiasi hicho cha watoto wachanga wasio na hatia, wanakuja duniani wakiwa tayari wameshaambukizwa VVU. Maambukizi haya yanatokea ikiwa virusi vitaingia katika mfumo wa damu wa mtoto kutoka katika damu ya mama wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua au wakati wa kunyonyesha.

Mheshimiwa Spika, programu ya kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ilianzishwa mwaka 2002 hapa nchini. Mpango huu unahusisha kuwapatia dawa wajawazito wenye VVU za kupunguza uwezekano wa mama kumuambukiza mtoto na pia kutoa dawa hizo kwa watoto saa72 baada ya kuzaliwa.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwaka 2006 ni 11% ya vituo nchini ndivyo vilivyokuwa vikitoa huduma hii. Pia, ni wajawazito wachache wanaofahamu uwezekano huu wa kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Kwa vile zipo fedha nyingi zilizoelekezwa kwenye vita dhidi ya VVU/UKIMWI, kuzuia maambukizi haya yatiliwe uzito zaidi ili kuwakinga malaika hawa wa Mwenye Enzi Mungu kutokana na ugonjwa huu hatari.

Mheshimiwa Spika, na ni kwa lengo hilo, Kambi ya Upinzani inataka Waziri aeleze ni hatua gani madhubuti zinazochukuliwa kupunguza kwa kiasi kikubwa kama sio kukomesha kabisa maambukizi haya.

IV. Madhara ya Mionzi ya X-Ray

Mheshimiwa Spika, mgonjwa anapokwenda kufanyiwa x- ray hospitali ni lazima apate kinga na kiwango (dose) sahihi cha mionzi. Mashine ni lazima itoe kiwango cha mionzi inayokubalika kimataifa. Mgonjwa anaweza kupata kiwango zaidi cha mionzi ikiwa mashine haifanyi kazi ipasavyo au chumba kinachofanyiwa uchunguzi wa x-ray hakitimizi vipimo maalumu vilivyowekwa (special specification) kimataifa.

Mheshimiwa Spika, mionzi ya x-ray inapenya kwenye kuta na kusambaa kwenye vyumba na sebule za jirani. Hivyo iwapo mashine inayo matatizo ya aina yeyote, ni lazima inyimwe leseni ya kufanya kazi mara moja. Tukumbuke ya kuwa nchi yetu imetia sahihi mikataba ya kimataifa kuhusu mionzi, hivyo tunawajibika kuitekeleza.

Mheshimiwa Spika, tunasema hivi kwa sababu baadhi ya taasisi zitumiazo vyanzo vya mionzi (hasa mashine za x-ray) zikiwemo hospitali hapa nchini, zimeshindwa kutii sheria ya Tume ya Taifa ya Nguvu za Atomu (Tanzania Atomic Energy Commission). Nyingi kati ya taasisi hizo ni zile za serikali ambazo zinadai zina tatizo la ukosefu wa fedha zinazohitajika kufanya marekebisho yaliyoshauriwa na Tume.

Mheshimiwa Spika, kuendelea kutumia mashine hizo za x-ray zenye kasoro ni kuhatarisha maisha ya wa-Tanzania wengi waendao hospitali kila siku. Hii inaweza kusababisha saratani, bone marrow kushindwa kutengeneza chembe chembe za maisha (red and white blood cells) hali ijulikanayo kama ni aplasia kwa kitaalamu, ugumba na kuharibika kwa vinasaba (genetic deformation) inayoweza kusababisha kuzaliwa watoto wasio wa kawaida.

Mheshimiwa Spika, hivyo ni vyema Waziri akatueleza ni hatua gani zinatumika kunusuru afya za wananchi wasioelewa hatari zinazoweza kuwapata wanapokwenda kila siku kutafuta matibabu hospitali.

Mheshimiwa Spika, ni vyema hapa tukaongea pia kuhusu udhibiti wa biashara ya vyuma chakavu. Vyanzo vya mionzi (sources of radiation) vinaweza kuchanganyika na vyuma na hasa kwenye viwanda au maeneo ya machimbo ya madini. Baada ya kumalizika uzalishaji kiwandani au kiwanda kuuzwa kwa mmiliki mwengine au pia machimbo ya madini kuachwa baada ya uchimbaji kumalizika, vyuma vilivyobakia ambavyo inawezekana ya kuwa vimechanganyika na vyanzo vya mionzi vinaweza kuuzwa na kuyeyushwa hivyo vikileta madhara makubwa kwa wengi ambao hata hawaelewi juu ya hatari inayowazunguka.

Mheshimiwa Spika, hivyo, biashara ya vyuma chakavu inaleta hasara za uharibifu sio tu za miundombinu, bali pia inaweza kuleta hasara kubwa za afya ya wananchi wetu.

V. Huduma ya Mama Wajawazito na Watoto Wachanga

Mheshimiwa Spika, zaidi ya wanawake 8,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na matatizo ya ujauzito, uzazi na hata baada ya kujifungua. Uzazi 578 kati ya uzazi 100,000 hai husababisha vifo vya mama. Hii inamaanisha ya kuwa wanawake 24 kila siku wanapoteza maisha. Kwa kila mwanamke mmoja anayepoteza maisha, 30 hupatwa na magonjwa yanayosababisha maisha duni.

Mheshimiwa Spika, Malengo ya Maendeleo ya Millenia (Millenium Development Goals), MKUKUTA pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005-2010 yanataka kupunguzwa kwa vifo vya wajawazito nchini kutoka 529 mpaka 265 kwa uzazi 100,000 ifikapo 2010.

Mheshimiwa Spika, tumebakiwa na miaka miwili tu kufikia 2010 na kwa dalili zote, malengo hayo yatabaki kuwa maandiko mazuri kwenye vitabu tu. Tunasikitika kusema, lakini ni vigumu kuyatimiza malengo haya kwa kipindi hichi kilichobakia.

Mheshimiwa Spika, tunalazimika kukumbusha pia ya kuwa katika bajeti ya mwaka jana ya 2007/2008 bunge liliidhinisha matumizi ya sh. billioni 1.7 kwa ajili ya kununulia pikipiki 222 za tairi tatu kwa ajili ya kurahisisha usafiri katika maeneo yenye miundombinu mibovu ya barabara ili zije kuwahudumia wajawazito nchini katika jitihada ya kupunguza vifo.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri pikipiki hizo hazikununuliwa. Hivyo tunataka kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, ni kwa nini manunuzi hayo hayakufanyika na jee, pesa zilizoidhinishwa na bunge zimepelekwa wapi?

Mheshimiwa Spika, kiasi cha wanawake wanaopoteza maisha kutokana na matatizo ya ujauzito kimebaki kile kile kwa takriban miaka 20 sasa. Mikakati ya kimataifa imeonyesha kuwa vifo hivi vinaweza kupungua kama tukiwa na wahudumu wenye ujuzi. Wahudumu hao ni lazima wawe na mafunzo yakiwemo ya ukunga, mazingira mazuri ya kufanyia kazi, vifaa, madawa, miundombinu, rufaa, usafiri pamoja na huduma ya dharura ya uzazi.

Mheshimiwa Spika, tunaambiwa ya kuwa mama mjamzito hapaswi kwenda na vifaa vya kujifungulia (delivery kits) aendapo kujifungua hospitali. Lakini ni kweli pia ya kuwa mpaka hivi leo wajawazito wanadaiwa vifaa hivyo wanapokwenda kujifungua. Kambi ya Upinzani inaona ni vyema basi agizo hilo litolewe kwenye hospitali na vituo vyote vya afya nchini ili wahudumu wajuwe hilo na hivyo kuondowa utata huu mara moja.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka Mheshimiwa Waziri atueleze pia, ni katika kifungu gani kwenye bajeti ya wizara ambapo zimetengwa fedha za vifaa vya kujifungua kwa wajawazito?

VIII. Dawa za Malaria zenye Ubora Hafifu

Mheshimiwa Spika, gazeti la Los Angeles Times (USA) la tarehe 30 Juni 2008 linatoa taarifa ya kuwa timu ya watafiti wa kimataifa ambao walijifanya kuwa ni wateja wa kawaida na kununua dawa za malaria kwenye maduka ya dawa ya miji mikuu saba ya nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania wamegundua ya kuwa 48% ya dawa zinazotengenezwa Afrika na kuuzwa katika maduka yetu, ambayo ni tumaini kubwa ya watu wa kipato cha chini, yanakosa ubora wa viwango. Kitu ambacho watafiti hawa hawakuweza kuthibitisha ni kwamba jee, dawa hizi ni feki (counterfeit), ni dawa za zamani ambazo zimetiwa kwenye paketi zinazoonesha tarehe nyengine za mwisho wa matumizi yake au ni dawa zilizokosa utunzaji bora (improper storage) kwenye maduka yetu.

Mheshimiwa Spika, jambo la kutisha hapa ni kwamba dawa hizi zina uwezekano mkubwa wa kuongeza usugu wa malaria kwa dawa, hali ambayo itatuweka kwenye ugumu zaidi kwa nchi zetu kuweza kutokomeza ugonjwa huu. Hili ni jambo hatari kwa afya ya watu wetu. Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri atoe maelezo kwa suala hili. Aidha tujiulize, jee si dawa hizi zisizo na kiwango, ndio sababu sahihi ya vifo vya maelfu ya wa-Tanzania wanaougua malaria kila mwaka?

Mheshimiwa Spika, wakati tunaipongeza Mamlaka ya Chakula na Dawa (Tanzania Food and Drugs Authority) kwa kutimiza miaka mitano tarehe 01 July, 2008 na pia kwa kazi nzuri inayofanya, basi tukumbushe tu ya kuwa kazi iliyoko mbele yake ya kulinda afya za wananchi bado ni kubwa mno. Kwa kwa mujibu wa Jarida hilo la Marekani ni dhahiri Mamlaka hii bado haijafanya “homework” yake vya kutosha.

IX. Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Muhimbili National Hospital – MNH)

Mheshimiwa Spika, Ujenzi unaofanyika kwenye hospitali hii kubwa ya Rufaa nchini ni wa hali duni. Jengo la Maabara Kuu ya hospitali (Central Pathologic Laboratory) ambalo imekabidhiwa rasmi kwa Muhimbili miaka 2 iliyopita tayari linavuja. Milango na vyoo vilivyoweka ni vya ubora hafifu hata ya ile iliyokuwepo kabla ya ukarabati.

Mheshimiwa Spika, vifaa na madawa (reagents) ya vipimo Maabara Kuu hivi sasa vinafadhiliwa na shirika la ABBOTT. Upo wasiwasi wa upatikanaji endelevu wa vifaa na dawa pale ABBOTT wataposita ufadhili wao. Wasiwasi huu ni mkubwa hasa ukitilia maanani ya kuwa pesa zote zinazokusanywa kwa huduma za maabara (cost sharing) zinachukuliwa na hospitali (kwenye pool).

Mheshimiwa Spika, hali ni hiyohiyo kwenye jengo la mpango wa uzazi (reproductive health) lililokwisha na kukabidhiwa miaka michache nyuma. Lift ya jengo hilo tayari haifanyi kazi tena na hivi sasa imegeuzwa store.

Mheshimiwa Spika, ukarabati wa majengo mengine unaotarajiwa kufanyika hivi sasa haujakamilika na tayari umesimama kabisa. Taarifa tulizozipata zinaeleza ya kuwa mkandarasi bado hajapata malipo yake. Uongozi wa Muhimbili unashindwa kufuatilia ujenzi kwa sababu kampuni inayojenga inadai ya kuwa mikataba ya ujenzi imewekwa baina yao na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na siyo Muhimbili yenyewe.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, majengo yanajengwa chini ya kiwango. Kwa mfano, wodi ya watoto wachanga ilimaliza kutengenezwa bila mfumo wa hewa ya oxygen (oxygen system). Muhimbili ililazimika kuingia gharama nyengine binafsi kuweka mfumo huo wa oxygen.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa theatre umesimama. Hii inasabisha list ya wagonjwa wa upasuaji kuwa kubwa hata ya kuleta hisia kwa wagonjwa ya kuwa pengine inabidi kutoa rushwa ndio ufanyike upasuaji wenyewe.

Mheshimiwa Spika, tunataka maelezo ya kina kuhusu ukarabati huu kutoka kwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, katika kanuni za wafanyakazi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kanuni ya 11.2 (d) kinachohusu kiinua mgongo cha ukomo wa ajira kinazuia mtumishi anayestaafu kulipwa kiinua mgongo hicho,lakini sheria ya kazi ya mwaka 2004 kifungu cha 42(4) kinataka malipo hayo yasiingiliane na mafao yake mengine.

Kambi ya Upinzani inamtaka Mhe Waziri atoe ufafanuzi kuhusu utata huu, ni kipi kina nguvu kati ya sheria ya Bunge na Kanuni za Wafanyakazi za Hospitali ya Muhimbili?

X. Muhtasari wa Bajeti za Nyuma za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii

Mheshimiwa Spika, sasa tuangalie bajeti za miaka mitano ya nyuma za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuanzia 2002/2003 mpaka 2006/2007.

A

B

C

D

E

Mwaka

Bajeti

Kiasi Kisichotumika

Tofauti

B – C

CAG *

2002/2003

192.77 bill

18 bill

174.77 bill

7.2 bill

2003/2004

201.02 bill

0

0

17.1 bill

2004/2005

308.28 bill

20 bill

288.28 bill

31 bill

2005/2006

425.77 bill

42 bill

383.77 bill

8.93 bill

2006/2007

521.07 bill

94 bill

427.07 bill

9.76 bill

Jumla

1,648.91 bill

174 bill

1,474.91 bill

73.99 bill

CAG* – Pesa hazikutumika vizuri/hati zenye mashaka

Mheshimiwa Spika, kwa kuangalia takwimu hizi ni dhahiri kuwa bajeti ya Afya imekuwa ikiongezeka kila mwaka. Swali la kujiuliza ni je, ongezeko hilo linaenda sambamba na ubora wa huduma kwa wananchi? Kambi ya Upinzani inadhani swali hili watanzania ndio wanaoweza kulijibu kwa usahihi zaidi kuliko Serikali.

Mheshimiwa Spika, tunaomba tupate maelezo kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, ni kwa nini karibu kila mwaka kipo kiasi kikubwa cha fedha ambazo hazitumiki? Jee, tunaweza kupata maelezo ya fedha hizo ambazo hazikutumika? Ni kwa kiasi gani kazi zilizotengewa fedha hizo ziliathirika? Jee, Wizara inatekelezaje maelekezo ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ya miaka yote?

Mheshimiwa Spika, zaidi ya yote haya, kiasi cha pesa ambazo hazikutumika na Wizara kwa miaka hii mitano tu zifikazo 174 bill zingetosha kujenga zahanati 2,900 nchini.

Xi. Ujenzi va Vyoo (Sanitation)

Mheshimiwa Spika, hivi leo wa-Tanzania millioni 5 hawana vyoo kabisa, wakati wa-Tanzania milioni 20 hawana vyoo safi na salama, hivyo wakiwa hatarini kuambukizwa maradhi yanayoweza kusababisha vifo.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa takwimu za karibuni zaidi za WHO/UNICEF ni 33% tu ya wa-Tanzania ndio wenye vyoo safi na salama. Kwa mujibu wa ripoti ya UNDP, kwa miaka 14 yaani kutoka 1990 mpaka 2004 hapana ubora katika matumizi ya vyoo Tanzania. Ni 37% tu ya shule nchini ndizo zenye vyoo vya kutosha. Kwa kasi hii itatuchukua miaka 67 kufikia Malengo ya Maendeleo ya Millenia (MDGs) kuwa na vyoo safi na salama.

Mheshimiwa Spika, vyoo ni muhimu kwa afya, ukuwaji wa uchumi, elimu na heshima ya kila mmoja wetu. Iwapo vinyesi vya watoto vitaondolewa (disposed) kwa salama, hii itapunguza maradhi ya kuharisha (diarrhoea) kwa watoto kwa 40%. Kuna taarifa ya kuwa watoto wengi hivi leo wanakufa kutokana na maradhi ya kuharisha kuliko wanaokufa kwa malaria na VVU/UKIMWI pamoja.

Mheshimiwa Spika, ukosefu wa vyoo unasababisha vifo vya maelfu ya wa-Tanzania kila mwaka. Kuna ripoti zinazoelezea ya kuwa hapa nchini katika mwaka 2004 – 2005 kumekuwa na wagonjwa 12,923 wa kipindupindu (cholera) ikisababisha vifo 350, wagonjwa 154,551 wa kuharisha damu (dysentry) ikisababisha vifo 170 na wagonjwa 863,488 wa typhoid ikisababisha vifo 1,167. Juu ya yote haya ugonjwa wa kuharisha (diarhoea) unasababisha vifo vya maelfu ya wa-Tanzania, 90% ya hao ikiwa ni watoto.

Mheshimiwa Spika, lengo la MKUKUTA ni kuwa 100% ya shule ziwe na vyoo salama ifikapo 2010. Kwa mambo yalivyo hivi sasa, hii ni ndoto. Lengo hili linaazimia kupunguza miripuko ya kipindupindu (cholera) nchini kwa 50% ifikapo 2010. Hii itawezekana tu ikiwa tutaelimisha jamii umuhimu wa kuosha mikono kwa sabuni hasa watokapo chooni na ujenzi wa vyoo salama.

Mheshimiwa Spika, mafanikio ya muda mfupi kwa ujenzi wa vyoo salama ni kuongeza uzalishaji, kuongeza uwezo wa matumizi, kuongeza uchumi. Mafanikio ya muda mrefu ni elimu bora, kuongeza kipato, kupunguza utegemezi.

Mheshimiwa Spika, wataalamu wanatueleza ya kuwa kwa kila shillingi tunayoiwekeza kwenye ujenzi wa vyoo tunaokoa shillingi tisa kwenye afya na uchumi.

Mheshimiwa Spika, tunataka kujua kutoka kwa Waziri, ni kiasi gani kinachotumika katika ujenzi wa vyoo salama nchini na juhudi gani zinafanyika kufikia Malengo ya Maendeleo ya Millenia katika suala hili.

XII. Mfuko wa Bima ya Afya

Mheshimiwa Spika ,mfuko huu ni muhimu sana kwa ajili ya ustawi wa Taifa letu na wafanyakazi wa Taifa hili, ila mfuko huu unatakiwa kufanya kazi ya ziada ili kushindana na mifuko mingine kwa ajili ya kuweza kupata wanachama wengi.

Kwa mwaka 2007 Serikali iliendelea na mkakati wa kuzijengea uwezo Halimashauri za Wilaya katika kuwashirikisha wananchi ili kupanga mikakati ya kufanikisha utekelezaji wa mfuko wa afya ya jamii. Mikakati hiyo ni mbinu za kufanya makisio sahihi ya bajeti na namna ya kusimamia kanuni za za usimamizi wa fedha za wananchi. Kambi ya Upinzani inahoji inakuwaje kwa kipindi cha mwaka mzima Wizara ilijikita kwenye kupanga mikakati ya jinsi ya kuweza kufanya makisio ya kibajeti?

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inauliza kama mwaka mzima ni kwa ajili ya mikakati utekelezaji utaanza lini kwenye Halmashauri zote?

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2007 serikali ilifanikiwa kuhamasisha na kuziwezesha mamlaka za miji 9 kutunga na kuridhia sheria ndogo za mfuko wa Tiba kwa Kadi (TIKA), Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri kulieleza Bunge na wananchi kwa ujumla wake ya kuwa ni Wilaya ngapi mpaka sasa ambazo bado hazijatunga na au kuridhia sheria za mfuko wa Tiba kwa Kadi na ni lini wilaya husika zitaanza kutumia mfumo huo.

Ni kitu gani kilichopelekea wizara kuweza kuzifanya mamlaka za miji tisa (9) tuu kujiunga na huduma hiyo, na je? Kuna vikwazo gani mbona zoezi linaenda kwa kusuasua sana?.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba kuwasilisha.

………………………

Dkt. Ali Tarab Ali (Mb),

Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani

Wizara Ya Afya na Ustawi wa Jamii.

16.07.2008

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s