Tume basi, sasa kura ya maoni!

“…Kwa mujibu wa taarifa tulizonazo, SMZ pekee na baadhi ya wakati kushirikiana na SMT imewahi kuunda takriban kamati 12 kutoa maoni juu ya kutatua kero za muungano, jee mapendekezo haya yalishughulikiwa kwa kiasi gani? Kana kwamba haitoshi, SMZ na SMT kwa pamoja, zimeunda takriban kamati 8 na kufanya vikao vya pamoja takriban 80 kuzungumzia kero za Muungano, lakini hadi leo hakuna mafanikio yoyote katika kero za msingi. Je, Wizara ya Muungano inaweza kulieleza Bunge hili na Watanzania kwa ujumla tatizo la kutofaninikwa hasa ni nini?…Kambi ya Upinzani inaona kwamba njia ya kutumia vikao baina ya serikali ya SMZ na SMT vinavyoongozwa na Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi wa Zanzibar kama sehemu au mkakati wa kutatua kero au matatizo ya Muungano si muafaka na hazina ufanisi. Hivyo basi, Kambi ya Upinzani inashauri kuwa kura ya maoni na mjadala wa wazi wa kitaifa juu ya muundo na mfumo wa muungano utakaozingatia na kuhakikisha maslahi ya pande zote mbili za Muungano na unaohitajika uitishwe nchi nzima.

Hayati Mwalim Julius K. Nyerere, akichanganya udongo wa Tanganyika na wa Zanzibar kama ni ishara ya Munngano wa nchi mbili hizi mamo mwaka 1964

Hayati Mwalim Julius K. Nyerere, akichanganya udongo wa Tanganyika na wa Zanzibar kama ni ishara ya Munngano wa nchi mbili hizi mamo mwaka 1964

Hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mhe. Riziki Omar Juma (Mb), kuhusu Makadirio na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais Mambo ya Muungano kwa Mwaka wa Fedha 2008/2009

1. Utangulizi

Mheshimiwa Spika, Napenda kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano kwa mwaka wa fedha 2008/2009, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, kanuni ya 99 (7). Toleo la Mwaka 2007.

Mheshimiwa Spika, Napenda kwanza kutoa shukrani zangu za dhati kwako wewe binafsi, Naibu Spika pamoja na wenyeviti wote, kwa kunipa fursa hii ya kutoa maoni ya Kambi ya Kambi ya Upinzani ili kufaniksha lengo letu la kukomaza demokrasia ya kweli katika nchi hii. Naushukuru pia Uongozi mzima wa chama changu, Chama cha Wananchi (CUF- The Civic United Front), na viongozi wa Chama changu Taifa. Pia viongozi wangu wa Kambi ya Upinzani, Mhe. Hamad Rashid Mohammed na Mhe. Dk. Wilbrod Slaa, kwa imani, miongozo na ushirikiano wao mkubwa kwangu.

Mheshimiwa Spika, mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa natoa shukrani zangu za dhati kwa Mume wangu mpenzi Bwana Hamad Abdallah Faki, Mama yangu mpendwa, watoto wetu na familia kwa ujumla kwa kunivumilia kwa kuwa mbali nao kwa muda mrefu nikitekeleza majukumu yangu.

2. Muundo wa Muungano

Mheshimiwa Spika, muundo na mfumo wa Muungano tulionao ambao unaelezwa kuwa ni wa kipekee duniani ndio sababu ya kero zote za Muungano. Hii ni kwasababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano na sheria nyingine zimeshindwa kuzingatia na kutambua maana, dhamira na matakwa halisi ya Muungao huu kupitia hati asili za Muungano kwa kule kuthubutu kubadilisha hata mmbo ya msingi ambayo yaliwekwa na waasisi wa muungano ndani hati ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, tunaweza kusema kuwa kwa msingi huu hati asili na matakwa yake zilikiukwa ili kukidhi matakwa ya watu fulani ambayo kwa wakati huo hayakuwekwa wazi. Naomba nitoe mfano halisi wa hili pale ambapo ulipitishwa muswada wa kubadilisha nafasi ya Makamo wa Rais kutoka kwa Rais wa Zanzibar na kuweka mfumo uliopo sasa, kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za bunge, ibara ya 98(1)(b) haikuzingatiwa hali ambayo ilileta mabadiliko yaliyoondoa dhana mzima ya kuwa na Muungano unaotokana na pande mbili. Mabadiliko haya mbali ya kuwa yalishindwa kuzingatia matakwa ya Katiba ambayo tunaitita kuwa ni sheria mama ya nchi lakini pia yalifuta kipengele muhimu katika Makubaliano halisi ya Muungano. Hili kwa wakati huo lilionekana kuwa ni dogo lakini kwasasa madhara yake ni makubwa.

Mheshimiwa Spika, Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni vizazi vya makubaliano ya Muungano. Hivyo haziwezi na hazitakiwi kuwa na nguvu kuliko Mkataba wenyewe wa Muungano ambao kwa kitaalam ndio Grand norm ndani ya Muungano. Lakini hali ilivyo sasa ni tofauti na ukweli huu, kuna mambo mengi yaliyofanywa chini ya Katiba hizi mbili nje ya Mkataba wa Muungano. Mfano nyongeza ya kwanza ya mambo 11 yanayosemwa nayo ni ya Muungano kwa sasa. Hata ukiuliza nyongeza hii iliwekwa kupitia Sheria ipi ni ngumu kupewa jibu la uhakika na la kuaminika.

Mheshimiwa Spika, yote haya yanatokana na kukiukwa na kudharauliwa hati asili za muungano wetu na yale yaliyoasisiwa ndani yake. Ukweli wa kauli hii unathibitishwa hata na mtaalam maaurufu wa sheria marehemu Jaji Nyalali, alinukuliwa akisema:

“Kwa kuwa Makubaliano ya Muungano ndiyo chimbuko la Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ipo haja ya kuisoma Katiba na na makubaliano hayo ili kuilewa vizuri. Kwa mantiki hiyo, katiba haiwezi kubadili Articles of Union. Kwa kuwa Articles of Union zilitungwa na serikali mbili, na kwa kuwa moja ya serikali mbili hizo haipo tena, wenye mamlaka ya kuamua kimsingi ni wananchi wan chi mbili hizi, ambao ndiyo chimbuko la mamlaka yote ya dola. Hii ina maana kwamba kama lipo sasa katika Katiba ya 1977 au katika marekekebisho yake ambalo linakiuka Articles of Union jambo hilo haliwezi kuwa na nguvu za kikatiba isipokuwa kama lina ridha ya wenye mamlaka ya mwisho yaani watu. Hivvyo basi katika mazingira ya Tanzania ingawa ni kweli kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ni sheria kuu ya nchi, ni kweli pia kuwa Articles of Union zina nguvu zaidi ya Katiba, aidha ni kweli kuwa mbali na Articles of Union hakuna sheria nyengine iliyo na nguvu zaidi ya katiba.”

Mheshimiwa Spika, tukiangalia miungano ya nchi zingine, hali ni shwari kwani nchi wanachama au washirika wa miungano hiyo wanaheshimu na kutambua misingi halisi na makubaliano ya msingi waliojiwekea. Mfano, makubaliano yaliyofikiwa baina ya U.K na Jersey. Katika muungano huu U.K imekubali utaratibu mzuri kwa maendeleo ya Jersey kuwa na uhusiano wa kimataifa.

Tarehe 1/10/2007, makubaliano yalifikiwa baina ya Waziri Kiongozi wa Jersey na Waziri wa Nchi, Mambo ya Katiba wa Uingereza kuweka vizuri mahusiano yao kwa kuweka misingi ifuatayo:

  • U.K haitofanya chochote kimataifa kinachohusiana na Jersey bila kwanza Jersey kutoa ridha/kukubali.
  • U.K inajua kwamba baadhi ya matakwa yanatofautiana na ya Jersey kimataifa na hivyo U.K haitaamua tu moja kwa moja kwa mambo yanayohusu Jersey kama mambo ya EU.
  • Jersey ina utambulisho wa kimataifa ambao ni tofauti na wa U.K.
  • U.K inafahamu kwamba Jersey ni nchi ndogo na hivyo kuna mambo lazima Jersey ijifanyie yenyewe kwa maendeleo yake.

Mheshimiwa Spika, mifano iliyotajwa hapo juu ni misingi bora kwa maendeleo ya muungano huo na ustawi wa nchi hizi, lakini kwa Tanzania misingi hii hakuna. Sisi kila leo matatizo ya Muungano tunayafichaficha na hata tunathubutu kutoa kauli kuwa anaYezungumzia matatizo au kero za Muungano anataka kuvunja Muungano. Tunakwenda wapi?

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona kwamba muundo wa Muungano uliopo unazo kasoro na Serikali ya Muungano kwa sasa haijawa na nia njema ya kutatua matatizo yaliyopo. Hivyo basi tunaitaka Serikali iweke mpango mkakati wa muda maalum kuhakikisha kwamba kero na matatizo yote ya Muungano yanatatuliwa kwa ufanisi na haraka iwezekanavyo.

3. Shughuli za Muungano

Mheshimiwa Spika, uwepo wa wizara maalum ulitegemewa kuwa chachu ya kuimarisha Muungano kwa kutumia nafasi yake kutatua matatizo yote yanayohusu Muungano wetu. Lakini hali halisi iliyopo ni kinyume na matarajio hayo. Ni imani yetu kuwa fedha nyingi zimeshatumika na wataalam mbali mbali wameshaitwa na mapendekezo mengi yametolewa, lakini kwa nini mafanikio hayaonekani bali kero zinazidi kuongezeka? Je, Serikali inaweza kulieleza Bunge hili kiini hasa cha tatizo ni nini na kwa nini hakielezwi kwa uwazi? Je, kama ni vigumu kuyatatua, basi hata kuyaeleza?

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa tulizonazo, SMZ pekee na baadhi ya wakati kushirikiana na SMT imewahi kuunda takriban kamati 12 kutoa maoni juu ya kutatua kero za muungano, jee mapendekezo haya yalishughulikiwa kwa kiasi gani? Kana kwamba haitoshi, SMZ na SMT kwa pamoja, zimeunda takriban kamati 8 na kufanya vikao vya pamoja takriban 80 kuzungumzia kero za Muungano, lakini hadi leo hakuna mafanikio yoyote katika kero za msingi. Je, Wizara ya Muungano inaweza kulieleza Bunge hili na Watanzania kwa ujumla tatizo la kutofaninikwa hasa ni nini?

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona kwamba njia ya kutumia vikao baina ya serikali ya SMZ na SMT vinavyoongozwa na Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi wa Zanzibar kama sehemu au mkakati wa kutatua kero au matatizo ya Muungano si muafaka na hazina ufanisi. Hivyo basi, Kambi ya Upinzani inashauri kuwa kura ya maoni na mjadala wa wazi wa kitaifa juu ya muundo na mfumo wa muungano utakaozingatia na kuhakikisha maslahi ya pande zote mbili za Muungano na unaohitajika uitishwe nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 mambo ya nje ni ya Muungano ikijumuisha Mashirikiano katika Jumuia mbali mbali kama vile SADC, EAC, COMMONWEALTH na nyinginezo. Kwa mfumo wetu huo huo, katika serikali kuna Mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano, kama vile, kilimo, mazingira, miundombinu, uvuvi n.k. Je, Wizara inaweza kulieleza Bunge hili kwa namna gani Zanzibar inawakilishwa katika mambo yasiyo ya Muungano katika jumuia hizo na kuhakisha kwamba maslahi ya Zanzibar katika mambo yasiyo ya Muungano yanalindwa ipasavyo?

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona kwamba katika hili kuna tatizo kubwa na kwa maelezo yoyote ya waziri athari inayopata Zanzibar kutokuwa na uwakilishi unaotambulika katika jumuia za kimataifa mfano wa hizo nilizozitaja ni kubwa. Hivyo tunashauri tungetumia mfano ule nilioutoa awali wa Jersey na UK wa kutambua uwepo wa baadhi ya maslahi tofauti katika jumuia mbali mbali na kuipa Zanzibar uwakilishi wa kutambulika ndani ya jumuia hizo.

4. Mambo ya Muungano

Mheshimiwa Spika, Ukiangalia ibara ya 4(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano mambo ya Muungano ni 22, lakini bado kuna matatizo mengi katika mambo haya. Hali hii inatokana na nyongeza mbali katika Mambo ya Muungano kinyume na Makubaliano ya msingi ambayo yalikuwa ni mambo 11 tu, na hili limesababisha matatizo yafuatayo:

(a) Uendeshaji na Utekelezaji wa Mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano

Mheshimiwa Spika, Katiba inaeleza kuwa mambo yasiyo ya muungano ya Zanzibar yanashuhulikiwa na SMZ na ya Tanzania bara yanashuhulikiwa na SMT. Malalamiko makubwa yanayotokana na hali hii ni kuhusu gharama katika mambo haya hasa kwa msingi kwamba Serikali ya Muungano ndio hiyo hiyo ya Tanzania Bara. Tatizo ni kuwa hakuna utenganisho wa mapato na namna ya kutoa gharama za kuziendesha shughuli hizo, vyanzo vya mapato ni hivyo hivyo.

(b) Mambo mengi hayana tafsiri na hayajulikani mipaka yake

Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa mambo ya Muungano ni mengi mno lakini miongoni mwao hayaeleweki kwa upana wake na mipaka yake. Hata ukiangalia katiba zote mbili za Tanzania, hazifafanui kwa uwazi juu ya mambo haya. Mfano elimu ya juu haijuilikani inaanzia wapi hasa na inaishia wapi. Hali ya kuchanganya ni hivi sasa ambapo elimu ya juu na elimu ya sekondari zimechanganywa na kuwa katika wizara moja. Kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano, elimu ya msingi si ya Muungano lakini elimu ya juu ni ya Muungano. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutolea ufafanuzi suala hili.

Mheshimiwa Spika, elimu ni jambo la kuliangalia kwa makini kwani kutokuwa na uwazi kwake kunapelekea mkanganyiko mkubwa. Mfano, Baraza la Mitihani la Taifa Tanzania na kazi zake ni suala la Muungano, sasa inakuwaje elimu ya sekondari na msingi si suala la Muungano wakati Baraza ndilo lenye mamlaka ya kutunga mitihani? Hili ni suala ambalo Serikali inatakiwa kulitolea ufafanuzi.

5. Muungano, ‘Mpasuko’ na Muwafaka wa Wazanzibari

Mheshimiwa Spika, Sote tunaelewa kauli ya Mhe. Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa hapa Bungeni kuhusu mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar, ambapo Rais wa Jamhuri yetu ya Muungano alikuja kutamka maneno hayo kwa nia njema sana. Kwa hivyo sasa umefika wakati wa Bunge lako hili pia kutaka kujua kutoka kwa Rais wetu wapi amefikia katika kusimamia kauli yake hiyo.

Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza ni hatua gani ya utekelezaji wa agizo hilo la Mhe. Rais kwa faida ya nchi yetu hasa katika siku zijazo?

6. Mapungufu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano

(a) Nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mheshimiwa Spika, Tunapozungumzia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunazungumzia Jamhuri iliyotokana na nchi mbili, yaani Tanganyika na Zanzibar. Lakini, mwaka 1994, miaka miwili baada ya kurudishwa tena kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa na takriban mwaka moja kabla ya uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya mfumo huo, Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipata pigo kubwa na hivyo kuujeruhi Mkataba wa Muungano.

Pigo hilo ni Mabadiliko ya 14 ya Katiba, ambayo yalimuondolea Rais wa Zanzibar nafasi yake ya kuwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kifungu cha III (b) cha Mkataba (Makubaliano) wa Muungano kinasema hivi:

“….ofisi za Makamu wa Rais wawili, ambapo mmoja wao (akiwa ni mtu ambaye kwa kawaida anaishi Zainzibar ) atakuwa mkuu wa utawala uliotajwa kabla katika na kwa Zanzibar, na ndiye atakayekua msaidizi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika utekelezaji wa shughuli za uongozi kuhusiana na Zanzibar.” Mwisho wa kunukuu. Au mabadiliko haya yalifanywa kwa kumlenga mtu na siyo taasisi?

Mheshimiwa Spika, naomba ninukuu kauli ya Mhe. Jaji Nyalali aliyoitoa hapa DODODMA mwaka 1996 kuwa “…….Hivvyo basi katika mazingira ya Tanzania ingawa ni kweli kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ni sheria kuu ya nchi, ni kweli pia kuwa Articles of Union zina nguvu zaidi ya Katiba, aidha ni kweli kuwa mbali na Articles of Union hakuna sheria nyengine iliyo na nguvu zaidi ya katiba”

Mheshimiwa Spika, Kuwekwa kwa kifungu hiki kwenye Mkataba wa Muungano kulikusudiwa kumhakikishia Rais wa Zanzibar nafasi ya kudumu katika Serikali ya Muungano kama mmoja wa Makamu wa Rais wawili na pia kulinda heshima na hadhi ya Zanzibar ndani ya Muungano huu. Sasa hivi, ambapo Rais wa Zanzibar anachukuliwa kama waziri wa kawaida tu katika Serikali ya Muungano, ile dhana nzima ya Makubaliano ya Muungano imevunjwa na imepotoshwa kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa nukuu hiyo hapo juu ni dhahiri kuwa mabadiliko yoyote yanayofanywa kinyume na yale yaliyomo kwenye Mkataba wa Muungano (Articles of Union) ni batili na hivyo basi, tukubaliane kimsingi kuwa sasa hivi kuna Makamu wawili wa Rais, mmoja akiwa Rais wa Zanzibar na Mgombea Mwenza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

(b) Nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 59 (1) cha Katiba kinazungumzia kuwepo kwa Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, na kwa kuwa Jamhuri ya Muungano ni pamoja na Zanzibar (kama ilivyo kwenye Kifungu cha 2 (1) cha Katiba), nafasi hii ya Mwanasheria Mkuu ni kosa kisheria, kwani kila moja kati ya Tanzania Bara na Zanzibar ina mfumo wake wa sheria, na ambapo Sheria si katika Mambo ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, Katika hotuba yangu kama hii ya mwaka jana, tulilalamikia kutokuwepo kwa dhamira njema katika upande wa utawala kuhusiana na kile kinachoitwa ‘kushughulikia na kuondoa kero za Muungano.’ Kitu kama hiki, kinathibitisha kwa dhamira hiyo, maana ni maoni ya Kambi yangu kwamba hili lilifanywa kwa makusudi ili Mwanasheria Mkuu wa Tanzania Bara awe na sauti juu ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kwa mambo yote ya Muungano. Na hivyo ndivyo ilivyo leo.

(c) Matumizi ya Tanzania Bara ndani ya Muungano

Mheshimiwa Spika, Upekuzi wangu wa Katiba umeshindwa kunionesha sehemu yoyote ambayo inataja Matumizi ya Tanzania Bara kama Tanzania Bara ndani ya Muungano au angalau matumizi kwa mambo yasiyo ya Muungano kuhusiana na ‘Tanzania Bara’. Badala yake Katiba imeingiza vifungu 133 mpaka 144 ambavyo vinahusika na Mambo ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano na ambavyo vinaashiria kuwepo kwa Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano tu.

Mheshimiwa Spika, Hii ni dosari kubwa iliyomo kwenye Katiba yetu na ambayo inaonyesha sura halisi ya Muungano wetu. Kwamba Katiba inaelezea wazi kuwapo kwa Serikali ya Zanzibar na pia Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambayo ina madaraka ya kushughulikia mambo yote ndani ya kwa Jamhuri ya Muungano na yote mengine ndani ya, na, kwa Tanzania Bara, lakini haiitengi Tanzania Bara katika matumizi na, hivyo, mchango wake kwa Muungano.

Mheshimiwa Spika, Dhamana hizi mbili kwa Serikali ya Muungano zimeleta mtafaruku na suintofahamu kubwa. Hii ni pamoja na Mgawanyo wa Mapato, Mahkama ya Katiba, Mahkama ya Rufaa kwa Tanzania, orodha ya mambo ya Muungano na Mwenendo wa Mabaraza ya Sheria.

Mheshimiwa Spika, Tuchukulie mfano na ukweli huu: kuna mfuko mkuu kwa Jamhuri ya Muungano ambao unaingiza mapato yote au pesa zote kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Hapa tafsiri safi na isiyo na mashaka ni kwamba mfuko huu unapaswa kutumiwa kwa mambo ya Muungano tu, kama yalivyoorodheshwa katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba. Lakini, Tanzania Bara haina mfuko mkuu kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano yanayohusu Tanzania Bara tu, ingawa Zanzibar inao mfuko wake mkuu kwa mambo yasiyohusu Muungano, yanayohusu Zanzibar tu. Sasa kwa nini matumizi ya Tanzania Bara kwa mambo yasiyo ya Muungano yagharamiwe na mfuko mkuu wa Jamhuri ya Muungano?

7. Akaunti ya Pamoja ya Fedha

Mheshimiwa Spika, Ibara ya 133 cha Katiba kinazungumzia Akaunti ya Fedha ya Pamoja ya Jamhuri ya Muungano, ambapo zinawekwa fedha kutoka michango ya serikali mbili kwa viwango vitavyowekwa na Tume ya Pamoja ya Fedha. Kwa hiyo, kikatiba ni Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambazo zina wajibu wa kuchangia huduma na uendelezaji wa Muungano. Tanzania Bara haichangii kitu na wala haiwajibiki kuchangia kwa mujibu wa Katiba.

Mheshimiwa Spika, Ni hapa ndipo sasa unapoona kwamba kumbe kulitakiwa kuwepo na Serikali ya Tatu ya Tanzania Bara, maana ilivyopaswa hasa iwe ni hivi: suala la mapato lihusishe Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanzania Bara. Hapo pasingekuwa na hoja wala haja ya Tume ya Pamoja ya Fedha, ambayo, hata hivyo, mfumo wa kuteuliwa kwake unalalamikiwa.

8. Benki Kuu na Nafasi ya Zanzibar

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na utata mkubwa juu ya nafasi ya Zanzibar katika Benki Kuu ya Tanzania hasa katika uanzishwaji na umiliki wa hisa. Kwa muda mrefu imekuwa ikielezwa kuwa Zanzibar haikutoa mchango wowote katika kuanzishwa BoT, na katika hali hiyo haimiliki hisa.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo ni kuwa kuendelea kutoa madai haya ni kutoitendea haki Zanzibar kama mshirika halisi na halali wa Muungano. Hii ni kwa hesabu kwamba:

  • Mchango wa Zanzibar uliotoka Bodi ya Sarafu ya Afrikaya Mashariki ili kuzisaidia nchi zilizokuwa wanachama kuanzisha Benki Kuu zao ulitumika kuanzisha Benki Kuu zao ulitumika kuanzisha Benki Kuu ya Tanzania.
  • Mchango wa Serikali ya Tanganyika ulikuwa ni Pauni za Kiingereza 668,884
  • Mchango wa Serikali ya Zanzibar ulikuwa Pauni za Kiingereza 82,840.
  • Jumla ndogo (ST+SZ) ni pauni 751.724

82,840:668,884(11.02: `88.08)

  • Sehemu za mali (assets) za Zanzibar zilizokuwa kwenye bodi ya sarafu ya Afrika Mashariki zilipelekwa katika Serikali ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe ufafanuzi wa wazi juu ya utata huu, pia sheria iliyoanzisha Benki Kuu ifanyiwe marekebisho kwani hadi sasa haitaji na kuweka wazi nafasi ya Zanzibar katika BoT.

10. Mahakama ya Katiba, Jaji Mkuu na Mahakama ya Rufaa

Mheshimiwa Spika, Suala ya Mahakama ya Katiba ni tatizo jengine. Ingawa kuwepo kwa mahakama hiyo kunatajwa katika katiba zote mbili, ya Jamhuri ya Muungano na ya Zanzibar, lakini haisemwi kama hilo ni suala la Muungano. Halafu kuna suala la mahkama hii itasikiliza malalamiko baina ya nani na nani? Baina ya Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanzania Bara ambayo haipo au baina ya Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano ambayo Zanzibar ni sehemu yake?

Mheshimiwa Spika, Kuna pia hili suala la nafasi ya Jaji Mkuu wa Tanzania Bara ambaye pia ndiye pia mkuu wa Mahkama ya Rufaa isiyomshirikisha Jaji Mkuu wa Zanzibar. Ibara 99 (2) (a) cha Katiba ya Zanzibar kinaizuwia Mahkama ya Rufaa kusikiliza rufaa yoyote inayohusu tafsiri ya Katiba ya Zanzibar. Ibara hii inapingana na Ibara ya 117 (1), (3) na (4) cha Katiba ya Muungano. Katika Ibara ya 125 imeelezwa kwamba itakuwepo Mahakama maalum ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano lakini katika masuala 22 ya Muungano Mahakama hiyo haimo, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili kuhusiana na suala uhalali wa Mahakama hii kuwa ya Jamhuri ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, Kwa hivyo, mapungufu yote hayo hapo juu, yanatupa indhari kwamba suala la Serikali Tatu haliepukiki ikiwa kweli tunataka kuwa wakweli wa nafsi zetu.

11. Hoja ya Serikali Tatu

Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu lina historia iliyotukuka kwa kuwa chombo kilichowahi kutumiwa na Wabunge 55 wa Tanzania Bara kudai kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika. Ni maoni ya Kambi yangu kwamba, hoja ile ilikuwa sahihi wakati ule kama ilivyo sahihi hivi leo na itakavyokuwa sahihi kesho. Tanzania inahitaji aina ya Muungano wenye Serikali Tatu ili kuondoa mkanganyiko, manung’uniko yasikwisha kila upande, tume zizizokuwa na mwisho, vikao visivyokwisha na kupoteza raslimali za wananchi walipa kodi, ambao ndio wanaotupa mamlaka na kutuwezesha kukaka hapa kujadili masuala yao ya maendeleo na mustakbali wa nchi kwa jumla.

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Katiba ya Muungano kuna Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano, ambayo pia itashughulikia mambo ya Tanzania Bara ambayo si ya Muungano. Kwa maneno mengine, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ingeshughulikia tawala mbili (two jurisdictions), ya Muungano na ya Tanzania Bara, wakati Katiba ya Zanzibar inashughulikia utawala mmoja.

Mheshimiwa Spika, Mtu yoyote anayejua hesabu ataona kuwa, unapokuwa na tawala mbili katika katiba moja na ukaongeza utawala mwengine mmoja katika katiba nyengine, jumla yake ni kuwa tawala tatu. Kwa lugha nyepesi, machungwa mawili katika kikapu kimoja na chungwa moja katika kikapu kingine yanakuwa machungwa matatu, na sio mawili. Hivyo ndivyo Makubaliano ya Muungano yalivyoashiria, yaani kuwa na mfumo wa shirikisho. Tunajidanganya sisi wenyewe kuamini kuwa Tanzania Bara haipo kama serikali, maana kilichofanyika hasa ni kuingiza uongozi wa serikali (Executive) na sheria (Legislature) katika Jamhuri ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni mshiriki halali wa Serikali ya Jamhuri ya Zanzibar, ambayo mwaka 1964 ilitia saini Mkataba, yaani Makubaliano ya Muungano. Mshiriki mwengine wa mkataba huu ni Serikali ya Tanganyika. Kwa maelezo ya Makubaliano hayo, Jamhuri ya shirikisho yenye mamlaka kamili (Sovereign Federal Republic) ya mfumo wa Serikali tatu (triangular) ilianzishwa. Kutokana na hayo basi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikua chini ya nguvu, taasisi au chombo chochote cha dola.

Mheshimiwa Spika, Kwa maana hiyo, Zanzibar inatakiwa ibaki dola inayojitegemea (sovereign state), na pia kama sehemu nzima (integral part) ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, kwa mujibu wa maelezo na masharti yaliyowekwa katika Makubaliano ya Muungano baina ya dola ya Zanzibar, yaani, Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, na Jamhuri ya Tanganyika. Tanganyika nayo ipo kama sehemu nzima (integral part) ya Jamhuri ya Muungano, ingawa imeingizwa katika Katiba ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, Mwaka jana tulisema na leo tunarudia kwamba tunazikhofia dhamira njema kwa upande wa watawala kuhusiana na uendeshaji na hatima ya Muungano wetu. Khofu zetu hizi zinajitokeza kila tukiingalia Katiba yetu ya Muungano na mwendelezo (development) wake. Kwa mfano, hivi sasa Sehemu ya Kwanza ya Katiba hiyo inasomeka kwamba “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano,” ambapo katika asili yake, kwanza nchi hii iliitwa “Jamhuri ya Muungano ya Tanganyika na Zanzibar” na baadaye “Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.” Sisi tunaamini kwamba kama tutaendeleza jina sahihi, tutajua asili ya Muungano huu na ukweli kwamba ulitakiwa uwe wa Shirikisho.

Mheshimiwa Spika, Mfano wa pili unaozusha wasiwasi ni Ibara ya 2 (1) katika sehemu hiyo hiyo ya kwanza ambapo zinatajwa nchi mbili zilizounda Jamhuri ya Muungano kuwa “Tanzania Bara” na “Tanzania Zanzibar.” “Tanzania Bara” ni jina jipya lililobuniwa kuchukua mahala pa Tanganyika na waliotunga Katiba ya 1977, lakini hili la Tanzania Zanzibar hatujui lilipotokea. Hata hivyo, ni vyema ikafahamika kwamba yote mawili yana tafsiri ile ile kama jina la asili la 1964, “Jamhuri ya Muungano ya Tanganyika na Zanzibar.”

Mheshimiwa Spika, Ibara ya 34 (3) kinaeleza kwamba “Mamlaka yote ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya Muungano, na pia juu ya mambo mengineyo yote yahusuyo Tanzania Bara, yatakua mikononi mwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.” hofu hapa ni kwa nini pamebanwa mamlaka ya Jamhuri ya Muungano katika masuala ya Muungano na yaliyohusu Tanzania Bara tu kama nia ilikua ni kuwa na mfumo wa serikali moja? Bila ya shaka, hizi zilitakiwa ziwe serikali mbili, ya Tanzania Bara na ya Muungano.

12. HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, Kwa heshima zote kwako na kwa chombo hiki kitukufu, Kambi ya Upinzani inaendelea kumshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Jakaya Kikwete, kuelekeza ari, nguvu na kasi yake mpya katika kutatua tatizo la Zanzibar ambalo, kama tulivyoonyesha kwenye hotuba hii, ni kubwa sana na linatishia utangamano na mustakbali wa Tanzania yetu. Yeye ndiye mlinzi mkuu wa Katiba yetu ambayo inahimiza umoja wa raia na inapinga kabisa ubaguzi wa aina yoyote. Zanzibar inahitaji uongozi (leadership) “and Mr. President is the one to provide it.” Kama ufa haukuonekana na ukazibwa mapema, kuna hatari huko mbele ya safari kuja kulazimika kujenga ukuta mzima kama siyo nyumba yote baada ya kuporomoka.

Mheshimiwa Spika, Kwa mara nyengine nitoe uhakikisho wa Kambi ya Upinzani kwamba tuko tayari kushirikiana na Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa karibu na kwa muda wote ili kujenga nchi hii. Tanzania ni yetu sote na hakuna mwenye hatimiliki ya taifa hili. Muungano huu ni Muungano wetu. Tuuimarishe kwa nia njema ya kuzijenga pande hizi mbili za Muungano.

Mungu ibariki Afrika. Mungu ibariki Tanzania.

Mheshimiwa Spika, Naomba kuwasilisha.

Riziki Omar Juma (Mb)

Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani,

Ofisi ya Makamu wa Rais -Muungano

19.08.2008

Advertisements

One thought on “Tume basi, sasa kura ya maoni!

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s