Kwa nini serikali imemilikisha ardhi kwa mgeni?

“Sheria ya ardhi ya mwaka 1999 inakataza ardhi kumilikishwa kwa wageni. Wawekezaji wageni wanakodishiwa ardhi kwa muda fulani wa makubaliano. Kitendo cha Serikali kummilikisha mwekezaji ‘reserve’ ya Grumeti na akajenga VIP Hotel ndani ya ‘reserve’ hiyo yenye eneo la kilomita za mraba 149 ni kinyume na utaratibu na kanuni za nchi. Kambi ya Upinzani inataka majibu kutoka kwa Serikali ni taratibu gani zilifuatwa kumilikisha ardhi ya wananchi wa mkoa wa Mara kwa mwekezaji huyo raia wa Marekani, Johnes Tudor? Kuna usiri mkubwa wa shughuli zinazofanywa kwenye eneo hili na mtu yeyote haruhusiwi kuuliza. Tuna wasiwasi hata mapato yanayokusanywa na serikali kutoka eneo hili siyo sahihi. Mwekezaji huyu amekuwa anawanyanyasa sana wananchi wanaozunguka eneo hilo. Amekuwa anatumia askari wake kuwapa kipigo kikali mwananchi yeyote anayekutwa hata jirani na eneo lake. Kumekuwepo na malalamiko kuwa askari hawa wanawalazimisha wananchi kula nyama mbichi pale wanapokamatwa na mnyama. Hii ni haki kwa nchi inayoendeshwa kisheria?”

Mhe Magdalena Sakaya

Mhe Magdalena Sakaya

Hotuba ya Mheshimiwa Magdalena Sakaya, Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Wizara ya Maliasili na Utalii kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2008/09

Mheshimiwa Spika,

Kwanza kabisa napenda kuchukua nafasi ya kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kuniwezesha leo hii kuwakilisha, kwa mujibu wa kanuni za Bunge, kanuni ya 99(7) toleo la 2007, maoni ya Kambi ya Upinzani kwa Wizara ya Mali Asili na Utalii  kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2008/09.

Aidha Mheshimiwa Spika, natoa shukrani zangu kwako binafsi kwa kunipa fursa hii adimu.

Mheshimiwa  Spika, natoa salaam za pole kwa ndugu, jamaa na watumishi wote wa Idara ya Wanyamapori kwa kupoteza watumishi wenzao watatu katika ajali mbaya ya ndege iliyotokea tarehe 3.07.2008 huko Arusha. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.

Mheshimiwa Spika,

Pia napenda kuchukua fursa hii kutoa shukurani zangu za dhati kwa viongozi na wanachama wa chama changu kwa kuniwezesha kuwepo hapa kutetea haki na maslahi ya wananchi wa nchi yetu. Nawaahidi nitaendelea kuwa mwaminifu na nitasimama kidete katika kuwatetea na kusimamia haki na rasilimali zetu mpaka dakika ya mwisho.

Mheshimiwa Spika

Napenda kuwapa shukurani zangu za pekee viongozi wangu wa Kambi ya Upinzani Mhe Hamad Rashid (Mb) na Naibu wake Dr.Willibrod Slaa (Mb) kwa kunipa ushirikiano katika muda wote wa maandalizi ya hotuba yangu hii. Pia namshukuru Naibu wangu Mhe. Ali Khamis Seif katika maandalizi ya hotuba hii.

Mheshimiwa Spika,

Napenda kutambua jitihada za Mheshimiwa Waziri, dada yangu Shamsa Mwangunga kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha Sekta hii inatoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi, bila kumsahau Naibu wake Mhe. Ezekiel Maige pamoja na timu nzima ya watendaji ikiongozwa na Katibu Mkuu wake Mama Blandina  Nyoni.

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MIPANGO KATIKA BAJETI YA MWAKA 2007/2008

Mheshimiwa Spika,

Katika kuyatekeleza malengo ya Wizara kwa mwaka wa Fedha 2007/2008, Bunge lako tukufu lilipitisha matumizi ya Wizara kiasi cha shilingi 55,493,625,000/- ambapo kati ya fedha hizo shilingi 30,817,624,000/- ni kwa ajili ya mishahara na matumizi mengineyo ambayo ilikuwa ni sawa na asilimia 55.5% na shilingi 24,676,001,000/- kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo ambayo ilikuwa ni sawa na asilimia 44.5%.

WANYAMAPORI

Mheshimiwa Spika,

Tanzania ni nchi moja wapo iliyobahatika kuwa  na wanyama pori wa kila aina ambao ni rasilimali kubwa kwa nchi yetu na ni muhimu sana katika kuchangia pato la taifa. Hadi kufikia March 2008 sekta hii iliingizia taifa jumla ya shilingi 10,554,562,182.77. Ingawa ninapata wasi wasi juu ya kiasi hiki cha makusanyo kwani kuna utofauti mkubwa uliojitokeza kati ya kitabu cha hali ya uchumi 2007/08 ambacho kinaonyesha makusanyo yanayotokana na wanyamapori yalikuwa 7,567,819,341/= na kile kilichowasilishwa kwenye kamati ya Bunge ya ardhi, mali asili na mazingira ambacho kinaonesha hadi kufikia march 2008 makusanyo yote ya sekta hii ni 10,554,562,183/=, ambayo ni sawa na tofauti ya 2,986,742,842/=.

Mheshimiwa Spika,

Utofauti huu mkubwa wa vitabu hivi viwili umetupa wasiwasi mkubwa juu ya makusanyo sahihi ya sekta hii. Hivyo kambi ya upinzani inamtaka Mh. Waziri atueleze ni makusanyo ya kitabu kipi ambacho ni sahihi? Pia atupe ufafanuzi wakina juu ya utofauti huu. Ni vema Serikali ikawa makini na Takwimu zake kwani hizi takwimu ndizo zinazoletea hisia tofauti kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika,

Kuna njia nyingi kama Wizara ingelikuwa na mipango madhubuti ingeliweza kuongeza pato la taifa. Kwa mujibu wa takwimu za Maliasili, kuna vitalu 163. Kwa wakati huu Serikali inakodisha kwa wastani wa USD7500 (kwa miaka 3) mara nyingi wamiliki nao hukodisha kwa wenye fedha kwa wastani wa USD100,000 kwa mwaka. Mwaka 2007/2008 Kambi ya Upinzani ilipendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe ili kuongeza mapato kama ifuatavyo :-

 • Kuwajasirimisha Watanzania vitalu vyote vya uwindaji
 • Ili kupata thamani halisi washauriwe kuingiza Vitalu hivyo katika soko la mitaji kwa kutumia ‘eletronic commerce’
 • Kupandisha viwango vya kodi ya Uwindaji
 • Kutoza 30% ya mapato yatokanayo  na Mtanzania atakayekodisha kwa mtu mwingine.

Mwaka huu wa Fedha, 2008/2009 Kambi ya Upinzani inataka kupata taarifa ya kina ni hatua zipi zimechukuliwa kati ya hizo na zimeipatia fedha kiasi gani, na kama hakuna ni sababu zipi hasa imeifanya Serikali kutokuchukua ushauri huo?

Mheshimiwa Spika,

Kuna wizi uliokithiri unaofanywa kwenye sekta ya Utalii, ambapo hotel za Sopa Lodge ambazo zinatoza ghali sana kwa wageni na zinapokea wageni wengi sana kwa siku, kwa mgeni mmoja zinatoza dolla 60-100 kwa mtu kwa siku. Lakini wanalipa dolla 1-3 kwa hifadhi husika na hawachangii chochote kuendeleza hifadhi hizo. Hali hii inapelekea kukosekana kwa fedha za kutosha kwa ajili ya uhifadhi na vile vile manufaa kwa raslimali kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,

Lingine ni ukwepaji wa ulipaji wa kodi kwa baadhi ya ‘Camp Operators.’ Kuna Camps ambazo hazikulipa ‘concession fees’ na ‘park fees’ kwa miaka zaidi ya 10 na zimeendelea kufanyakazi.  Mfano wa camps ambazo hazikulipa kodi hizi ni kama zifuatazo:

 1. Tembo Camp ambayo mwanzoni ikijulikana kama Stieglers George
  1. Concession fee 1995-2005 (miaka 11) @ USD 12,000 = USD132,000
  2. Minimum park fees @ USD 30,000 = USD330,000

2. ‘3 sites at Kinyanguru’

 1. ‘Conservation fee’ kwa kila ‘camp’ kwa mwaka  USD 12,000 na Minimum ‘park fee’ kwa kila ‘camp’ kwa mwaka ni USD 30,000
 2. Kinyaguru camp/ Hippo tours: ‘conservation fees’ kwa miaka 4 = USD12,000x 4 = USD 48,000

Minimum park fee 3 = USD 30,000×3 = USD 90,000

  1. Ladwa Camp

a. Conservation fee kwa miaka 4 = USD12, 000x 4 = USD 48,000

Minimum park fee kwa miaka 3 = USD 30,000×3 = USD 90,000

4. Pilot camp

Conservation fee kwa miaka 4 = USD12, 000x 4 = USD 48,000

Minimum park fee kwa miaka 3 = USD 30,000×3 = USD 90,000

5. 2 Other Ladwa sites

Conservation fee kwa miaka 4 = USD12, 000x2x 4 = USD 48,000

Minimum park fee kwa miaka 3 = USD 30,000x2x3 = 90,000

6. Beho Beho Camp

Concession fee imelipwa:

Minimum Park fee 1995-2005 (miaka 11) = USD 30,000×11 = USD 330,000

7. ‘Sites 5’ mpya ambazo wamepewa operators wapya   na Mkurugenzi wa wakati huo.

Conservation fee   = USD 12,000×5 = USD 60,000

Jumla ya fedha zote ambazo hazikulipwa ni USD 1,542,000 ambayo ni sawa ni Tshs 1,850,400,000/=

Mheshimiwa Spika,

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inamtaka Mhe. Waziri aeleze kama kweli zabuni ya wazi ilifanyika, je ni kiasi gani cha fedha kililipwa kwa Serikali? Pili fedha hizi zote zimekwenda wapi kama kweli zililipwa? Kama hazikulipwa ni kwa vipi au nani aliwapa ruhusu ya kuendelea na biashara kinyume na sheria na mpango mkuu wa usimamizi wa Selou game reserve? Watanzania wanahitaji ufafanuzi wa kina katika hili.

Mheshimiwa Spika,

Kwa Takwimu hizi tunaweza kuona ni kiasi gani nchi yetu inavyoporwa. Watumishi tuliowapa dhamana ya kusimamia na kutunza rasilimali zetu badala yake wakiangaliana au kushirikiana na wawekezaji wasio waadilifu, au kwa kushindwa kuweka miongozo sahihi yenye maslahi kwa Taifa.

Mheshimiwa Spika,

Ili kuwezesha sekta hii muhimu kuongeza pato la Taifa zaidi inavyochangia sasa, Waziri aliyepita Mhe. Maghembe alitembelea nchi nyingi na kuangalia jinsi wanavyoendesha swala zima la uwindaji wa Kitalii. Aligundua utofauti mkubwa sana wa bei za vitalu pamoja na wanyamapori kati ya wenzetu na sisi. Serikali ilileta mapendekezo ya bei mpya za wanayamapori hapa Bungeni na Bunge lako Tukufu liliridhia kwa furaha kubwa ili Taifa na wananchi wake liweze kufaidika na uwindaji wa kitalii tofauti na ambavyo miaka yote makampuni ya kitalii ndio yamekuwa yananufaika.

Mheshimiwa Spika,

Jambo la kushangaza Wizara ilibadili bei hizo kinyemela na kurudia bei za awali bila hata Bunge kufahamishwa. Kwa taarifa tulizo nazo hii ilitokana na shinikizo la wafanyabiashara wenye makampuni ya uwindaji ambao lengo lao ni kuendelea kufaidika zaidi. Hawana uchungu na raslimali hii wala wananchi wetu wanaoendelea kuteseka na hali ya umaskini. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge na Watanzania kwa ujumla ni vigezo gani vya msingi vilivyopelekea kubadilishwa kwa viwango vilivyoridhiwa hapa Bungeni?

Mheshimiwa Spika,

Ni dhahiri kuwa kabla ya pendekezo la bei mpya kuletwa Bungeni, utafiti ulifanyika wa kutosha. Pia ni ukweli uliowazi kuwa pamoja na nchi yetu na wanyama wengi, wa aina mbali mbali, wanene na wanaoishi kwenye mazingira halisia, sifa hizi zinaifanya Tanzania kuwa nchi ya pekee na hivyo kuwavutia wawindaji kutoka sehemu mbali mbali za Ulimwengu kuja kuwekeza kwenye sekta hii ya uwindaji. Lakini bei za wanyama wetu zimekuwa chini sana ukilinganisha na nchi nyingine za bara la Afrika. Na hivyo kusababisha taifa kutonufaika na maliasili hiyo.

Mheshimiwa Spika,

Katika kupata maendeleo ya kweli katika sekta hii ni muhimu sana kuwepo kwa mipango madhubuti na watendaji wabunifu na wanaoaminika. kuna mifano mingi inayoonyesha majirani zetu wameendelea sana kwa rasilimali hii na ukizingatia kwamba sisi tuna rasilimali zaidi ya wao,  hii imetokana na mipango madhubuti walionayo wenzetu na watendaji wabunifu na kuweza kuingizia pato kubwa la nchi. Mfano mzuri ni Afrika Kusini ada yao ya kuulia mnyama aina ya ‘cape buffallo’ ni us $ 16,200, wakati Tanzania ni US$ 2200.  Ada ya kuulia ‘Nyasaland wildebeest’ Afrika Kusini na Namibia ni US$ 1100, wakati kwetu Tanzania ni US$750

Mheshimiwa Spika,

Moja kati ya mambo muhimu ya kuendeleza wanyamapori ni wanajamii kuwa na elimu ya kutosha na ufahamu juu ya umuhimu wa wanyamapori, pia kushirikishwa kikamilifu katika suala zima la uendelezaji wa sekta hii kuanzia upangaji wa sera na ushirikishwaji kwenye mgao wa mapato kwani wao ndio waangalizi wakubwa wa wanyama hao pia wanaweza kuwa waharibifu wakubwa ikiwa watadharauliwa na kukosa elimu ya kutosha. Sekta nyingi nchini zinashindwa kufikia malengo yaliyowekwa kwa sababu ya kuwatenga wanajamii, au kuwashirikisha lakini kwa njia ya maneno na si kwa vitendo.

Mheshimiwa Spika,

Sheria ya wanyapori inaeleza kuwa asilimia 25 ya pato litokanalo na wanyamapori lirudi kwenye Halmashauri zinazozunguka maeneo hayo ili ziweze kuendeleza uhifadhi pamoja na wananchi kunufaika na raslimali hiyo. Kambi ya Upinzani inataka kupata maelezo kwa nini halmashauri 13 kati ya 44 zinazozunguka maeneo ya hifadhi hazikupata mgawo wa asilimia 25 mwaka 2007/08, wakati fedha zilikusanywa?

Mheshimiwa Spika,

Katika historia za nchi zetu za Afrika hakuna jambo lolote lenye lengo la kuleta maendeleo kwa wananchi kufanikiwa bila ya ushirikishwaji wa wanajamii kikamilifu. mfano mzuri ni nchi ya Ghana kabla ya mwaka 1920 walikuwa wanaendeshwa na sera ya wildlife community base, na mafanikio makubwa yalipatikana. Mwishoni mwa miaka ya 1980s Ghana walianzisha sera mpya za umiliki binafsi na matokeo yake kiasi cha zaidi ya 70% ya misitu iliharibiwa na wanyama pori wengi walitoweka na hii ilipelekea hadi leo hali ya wanyama pori kuwa ni ya wasiwasi.

Mheshimiwa Spika,

Kutokana na athari hizo mbaya, nchi kama Namibia wako mbioni  kubadilisha mfumo mzima wa Katiba kwa ajili ya kuwashirikisha kikamilifu wanajamii baada ya maendeleo mabaya yaliyotokana na mfumo wa awali.

Mheshimiwa Spika,

Kutokana na umuhimu wa wanavijiji katika suala zima la uhifadhi kambi ya upinzani inaiomba serikali kuziwezesha jumuia za vijijini kuweza kumiliki na pia kusimamia wanyamapori, kutoa msaada unaohitajika katika kuzipatia jumuia za vijijini miliki na kuweka mipango ya matumizi ya wanyamapori, kuwalazimisha wafanyabiashara wenye leseni kuajiri vibarua kutoka maeneo ambayo shughuli za matumizi ya wanyama pori zinafanyika kwa lengo la kuwapatia ajira na kunyanyua mapato yao.

Mheshimiwa Spika,

Tanzania ni nchi inayoongoza duniani kwa kuwa na sera nzuri na  za kuvutia. Kwa bahati mbaya utekelezaji wake unaishia kwenye makaratasi na majukwaani kwa wanasiasa. Kwa upande mwingine ni miongoni mwa nchi chache kwa kutokutekeleza sera zake. Mfano halisi ni kuwa kwenye kitabu cha sera za wanyama pori, zimeorodheshwa sera nyingi nzuri ambazo kama ingelikuwa kuna utekelezaji basi leo hii tusengilikuwa hapa tulipo. Moja ya malengo ya sera za wanyamapori ni kama zifuatavyo nanukuu  “ kushirikiana na kutumia vyema ushirikiano na jamii za vijijini,  kukabidhi madaraka ya wanyamapori kwa jumuiya za vijijini, kuruhusu jumuiya za vijijini kufaidika na miradi ya uhifadhi na kushirikishwa kwa jamii za vijijini  na wadau wengine katika usimamizi wa rasilimali za wanyama pori” mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika,

Kama sera hizi zingelikuwa zinafuatwa na kutekelezwa kikamilifu basi leo hii wananchi wanaoishi kuzunguka maeneo yenye rasilimali ya wanyama pori wangekuwa na hali nzuri ya maisha tofauti na walivyo sasa.

Mheshimiwa Spika,

Tatizo jingine ni lugha inayotumika katika kuandaa sera zetu. Lengo kuu la sera za Serikali ni kuwafikia wananchi ambao ndio walengwa wakuu. Jambo la kushangaza sera hizo zimeandikwa kwa lugha ya kingereza ambayo wananchi wengi hawaifahamu vizuri. Hivyo basi watawezaje kuyafahamu na kuyatekeleza yaliyomo ndani ya sera? Zaidi ya hayao sera hizi zinaishia maofisini kwenye makabati tu haziendi vijijini.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya upinzani inaitaka serikali kuzitafsiri sera hizi kwa lugha inayofahamika na wananchi na kuzisambaza kwa wananchi hasa zile sehemu zilizozunguka hifadhi za wanyamapori.

Mheshimiwa Spika,

Katika suala zima la uhifadhi wanyamapori, njia/mapito ya wanyama ni suala muhimu sana kwani hutumiwa na wanyama kuhama kutoka eneo moja kwenda lingine kwa shughuli mbali mbali, ikiwemo kufuata malisho pamoja na kwenda kuzaliana.

Mheshimiwa Spika,

Zaidi ya miaka 40 wabarbaig wamekuwa wakiishi vizuri katika njia kuu  ya wanyama inayounganisha Tarangire na Ziwa Manyara bila matatizo na njia hiyo wanyama wameendelea kuitumia hadi leo hii.

Mheshimiwa Spika,

Kijiji hicho ambacho kina zaidi ya familia 70 kimehamishwa kwa nguvu na eneo hilo limeuzwa kwa mwekezaji wa Kifaransa anayejulikana kama EN-Lodge Afrique. Amepewa eneo la hekta 4,084 za kijiji cha Vilima-vitatu kwa lengo la kujenga hotel katika njia ambayo hupitisha wanyamapori toka na kurudi Tarangire na ziwa Manyara, tena bila wanakijiji kushirikishwa katika uamuzi huo.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo ya kina ni kwa nini hoteli hiyo ijengwe katikati ya njia hiyo ya wanyamapori na kwa nini Wanakijiji hao wameondolewa kwa nguvu bila kufuata utaratibu unaoeleweka?

UTALII

Mheshimiwa Spika,

Utalii ni miongoni mwa sekta ambayo ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Tanzania imebahatika kuwa na eneo la ufukwe lipatalo kilimita 804, maporomoko ya maji, mito mikubwa, chemchem za maji moto (hot spring water), hifadhi za wanyama zilizokusanya wanyama mbali mbali, sura ya nchi na hali ya hewa nzuri, ambayo ni muhimu kwa kuvutia watalii.

Mheshimiwa Spika,

Licha ya umuhimu wa sekta hii lakini bado mchango wake ni mdogo katika kuchangia pato la taifa licha ya vivutio vingi tulivyonavyo ukilinganisha na nchi nyingine, hadi sasa sekta hii inachangia si zaidi ya 17% katika pato la taifa (GDP), ambalo ni dogo sana hasa ukizingatia rasilimali tulizonazo ni za kipekee duniani.

Mheshimiwa Spika,

kuna mifano hai ya nchi ambazo hata si maarufu kwa Utalii na hazina vivutio ukilinganisha na Tanzania lakini kutokana na mipango mizuri walionayo sekta hii imeweza kuchangia na kunyanyua pato lao kwa kiasi kikubwa, mfano mzuri ni Namibia , India, hata Zambia ambayo wala si maarufu  kabisa kwa sekta hii ya Utalii.

Mheshimiwa Spika,

Licha ya Wizara kujisifia juu ya sekta hii, lakini  hali ya kushangaza na ya kusikitisha, ni kuwa katika nchi 15 za Sub-Sahara (nchi za ukanda wa jangwa la Sahara) ambazo ni maarufu kwa kujishughulisha na sekta hii ya Utalii basi nchi yetu ni ya tatu kutoka mwisho imeshindwa hata na majirani zetu wa Kenya. Ama Katika nchi 20 ambazo ni maarufu kwa Utalii katika nchi zinazoendelea basi Tanzania haipo kabisa na inashindwa na hata nchi ya Zimbabwe. Katika nchi 50 zinazoendelea Tanzania ni ya 19 ambayo tumepitwa na Kenya, Msumbiji, Madagaska, Mali, Ethiopia na Nigeria. (We maintain peace and stability yet development remains patchy).

Mheshimiwa Spika,

Kwa upande wa ajira ilitarajiwa sekta hii iwe ni mfano kwa sekta nyingine kwa kufungua nafasi nyingi zaidi za ajira kwa wazawa na kuweza kupunguza na kama si kuondosha kabisa tatizo la ajira nchini, lakini hali ni tofauti, hii inatokana na kutokuwepo kwa  manufaa ya pande zote kwenye mzunguko wa uzalishaji na sekta hii, ukilinganisha na nchi nyengine zinazoendelea kwa mfano nchi ya India inachangia 4.1% na jumla ya watu walioajiriwa ni zaidi ya milioni 25 mbali ya ajira hizo, ajira nyingine ambazo zimechangiwa kutokana na sekta hii ni milioni 38.6.

Mheshimiwa Spika,

Ikiwa Serikali itahakikisha mahusiano ya moja kwa moja ya sekta ya Utalii na sekta nyingine kama vile Kilimo na ufugaji basi tutaweza kusaidia sana wakulima na wafugaji kunufaika sana na sekta hii kwa kupata soko zuri la mifugo yao, nafaka zao, matunda na mboga mboga na hivyo kuinua hali za maisha za Watanzania walio wengi.

Mheshimiwa Spika,

Ni jambo la ajabu katika hoteli zetu nyingi za Utalii wanaagizia nje karibu vyakula vyote vikiwemo vitoweo, nafaka, matunda na hata mboga mboga. Hii ni kwa nini? Mfano mwaka 2007 tumepata wageni 719,031, na kama tutakadiria kwa mgeni mmoja kwa mlo wa asubuhi atakula mayai mawili kwa wastani wa kila yai ni Tsh. 200 basi tungewaingizia wafugaji hawa kiasi cha Tsh. 287,612,400. Na kwa mlo wa usiku ikiwa kila mgeni mmoja atakula nusu kuku, na kwa kila kuku mmoja anagharimu Tsh 5,000, basi tungeweza kuwaingizia wafugaji hawa kiasi cha Tsh. 1,797,577,500.  Kwa mantiki hiyo tunaweza kuinua hali ya uchumi kwa wafugaji wa kuku wa mkoa wa Singida kwa kuuza kuku na mayai ya kienyeji tu. Vivyo hivyo kwa vitu vyingine kama vile matunda, mboga, nafaka na mazao mengine.

Mheshimiwa Spika,

Kwa kukosekana kwa miundombinu mizuri, watalii wengi wamekuwa wanashukia Kenya, wanamalizia siku zao huko na kupita Tanzania wakiwa wanarudi makwao. Mfano mzuri watalii wengi wanafika hifadhi ya Masai Mara kama kituo kikuu cha utalii na kuifanya hifadhi ya Serengeti kama kipitio tu (transit).

Mheshimiwa Spika,

Hii inaleta athari kubwa katika ukusanyaji wa mapato na unyanyuaji wa uchumi wa nchi, katika mwaka 2006/07 Masai mara ilikusanya US D. 750 milioni, wakati mbuga yetu ya Serengeti imekusanya US D 30 milioni ambao ni sawa na tofauti ya US$ 720milioni ambazo ni sawa na Tsh B.864.

Mheshimiwa Spika,

Ningependa ifahamike kuwa maendeleo mazuri ya Utalii kwa nchi wenzetu kama ya India hayakuja kirahisi bali yanatokana na mipango mizuri walionayo wenzetu. kwa mfano nchi ilianzisha “India railway catering and tourism development corporation limited” tokea 1999, ambayo huwa inatumika kutoa huduma za usafiri wa treni kwa watalii kuwafikisha Sehemu zinazotakiwa, kuboresha na kuanzisha ushindani wa mawasiliano, ukarabati wa viwanja vya ndege, kuanzishwa kwa ‘Pradhan mantra Gram sadak yojaina’ kwa ajili ya kuboresha na kurahisisha maingiliano na maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Spika,

Kwa juhudi zinazochukuliwa na Wizara kuitangaza Tanzania na vivutio vyake ni matumaini yetu kuwa watalii wataanza kuongezeka.  Kambi ya upinzani inaitaka Serikali iangalie kwa makini suala la kuongeza hoteli nyingi na zenye hadhi ya juu ili kuongeza ushindani. Aidha tunatoa angalizo ujenzi wa hoteli uzingatie uhalisia  wa hifadhi zetu na athari zake kwa mazingira  yanayozunguka hifadhi. Pia taratibu zote lazima zifuatwe na kutilia maanani maslahi ya Taifa na wananchi wake. Sambamba na hayo kuboresha mambo muhimu ambayo yatapelekea kuleta maendeleo ya sekta hii ikiwa ni kuwa na usafiri wa uhakika, mawasiliano, mahoteli na wahudumu waliopewa elimu ya kutosha na ambao watatoa ushindani wa kutosha kwenye sekta hii inayokuwa kwa haraka.

Mheshimiwa Spika,

Na hii inadhihirika pale ambapo majirani wetu wa Kenya kwa mwaka 2007 kabla ya uchaguzi waliingiza watalii wa kimataifa wapatao milioni mbili huku nchi yetu tunatarajia tutafikia kiwango cha milioni 1.2 ifikapo 2012 kutoka 700,000. 2007/08, hii inaonyesha kiwango cha watalii wanaongia Kenya tutakifikia mnamo 2020 hivyo hii inathibitisha kuwa tuko nyuma kimaendeleo katika sekta ya Utalii kwa muda wa miaka 12 ukilinganisha na Kenya. Tunahitaji mpango madhubuti wa kubadirisha sekta hii.

Mheshimiwa Spika,

Sheria ya ardhi ya mwaka 1999 inakataza Ardhi kumilikishwa kwa wageni. Wawekezaji wageni wanakodishiwa ardhi kwa muda fulani wa makubaliano. Kitendo cha Serikali kummilikisha mwekezaji Reserve ya Grumeti na akajenga VIP HOTEL ndani ya reserve hiyo yenye eneo la kilomita za mraba 149 ni kinyume na utaratibu na kanuni za nchi.

Kambi ya Upinzani inataka majibu kutoka kwa Serikali ni taratibu gani zilifuatwa kumilikisha ardhi ya wananchi wa mkoa wa Mara kwa mwekezaji huyo raia wa Marekani Ndg. Johnes Tudor.?

Mheshimiwa Spika, kuna usiri mkubwa wa shughuli zinazofanywa kwenye eneo hili na mtu yeyote haruhusiwi kuuliza. Tuna wasiwasi hata mapato yanayokusanywa na serikali kutoka eneo hili siyo sahihi.

Mheshimiwa Spika,

Mwekezaji huyu amekuwa anawanyanyasa sana wananchi wanaozunguka eneo hilo. Amekuwa anatumia askari wake kuwapa kipigo kikali mwananchi yeyote anayekutwa hata jirani na eneo lake.kumukuwepo na malalamiko kuwa askari hawa wanawalazimisha wananchi kula nyama mbichi pale wanapokamatwa na mnyama.  Hii ni haki kwa nchi inayoendeshwa kisheria?

Jamaa huyu ana jeuri ya ajabu hatuelewi anapata wapi kiburi hicho?  Amefikia hatua ya kukataza kamati ya Bunge kufanya kazi zake ndani ya hotel kwa kisingizio kuwa watasumbua wageni wake!

Mheshimiwa Spika,

Mwaka jana kamati tulitembelea wananchi waozunguka eneo hilo,tulipata malalamiko mengi sana kutokana na manyanyaso wanayopata kutoka kwa mwekezaji huyu.Wakati wa kikao kati ya wabunge na Uongozi wa hotel ,Mkuu wa Wilaya alionyesha wazi kumtetea mwekezaji na kuwaacha wananchi wake.Kwa taarifa tulizo nazo ni kwamba mwekezaji mahusiano yake ni yeye na viongozi wa juu tu hana habari na wananchi.Tunaitaka serikali ifuatilie swala hili na kutupatia majibu hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuangalia upya uwekezaji wa mahoteli makubwa yanayojengwa ndani ya hifadhi kwani yana haribu uhalisia wa mbuga zetu.

Mheshimiwa Spika,

Mwaka 2007 katika Hotuba yake Waziri  wa mali asili na Utalii  katika kipengele cha changamoto zinazotukabili katika sekta ya Utalii alilieleza Bunge lako Tukufu kwamba Wizara kwa kushirikiana na serikali ya Ufaransa itaanza rasmi ujenzi wa chuo kipya cha Utalii mwezi Agosti 2007 ambao utachukua mwaka mmoja kukamilika uk.110. Lakini katika Kamati ya Bunge ya ardhi mali asili na mazingira mh. Waziri mwaka 2008 alieleza kuwa ujenzi wa chuo hicho cha Utalii ndio kwanza unaanza.

Mheshimiwa Spika,

Hapa kambi ya upinzani inataka maelezo ya kutosha juu ya ucheleweshaji wa ujenzi wa chuo hicho ambacho mwaka huu kilikuwa kinatarajiwa kiwe tayari kimeshakamilika. Kambi ya upinzani pia inawasiwasi juu ya kutengwa tena kwa bajeti ya chuo hiki kwa mara ya pili baada ya bajeti 2007 na chuo hakikumaliza.

Mheshimiwa Spika,

Mojawapo ya rasilimali tuliyojaliwa ni uwepo wa Ziwa Natron lililotengwa chini ya mkataba wa kamataifa wa kuhifadhi ardhioevu. Eneo hili linakadiriwa kuwa na ndege aina ya Heroe wadogo (lesser flamingoes) wapatao 2.5million. Kiasi cha asilimia 70 ya ndege hawa Duniani huzaliana hapa. Ni ndege wa pekee wanaopenda utulivu.

Mheshimiwa Spika,

Ni jambo la ajabu kuona Serikali inataka kuteketeza mazalia haya Na kuwafukuza ndege hawa ambao hawapatikani mahali pengine popote na wamekuwa ni kivutio kikubwa kwa watalii.

Uridhiwaji wa ujenzi wa kiwanda cha magadi na Serikali ndicho chanzo cha kuwafukuza ndege hawa, hata kiwanda kikijengwa mbali lakini malighafi yatatoka katika ziwa hili na hivyo kusababisha usumbufu kwa ndege hawa.

Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutambua kwamba zipo njia nyingi za kuongeza pato la Taifa bila kusababisha uharibifu wa mazingira wala kupoteza maliasili zetu tulizopewa na Mwenyezi Mungu. Tunasisitiza Kiwanda kisijengwe kama hakuna eneo lingine lakupata malighafi zaidi ya ziwa Natron.

MISITU NA NYUKI

 • MISITU

Mheshimiwa Spika,

Nchi yetu imebahatika sana kuwa na rasilimali kubwa ya misitu ambayo ni hazina kubwa kwa maendeleo endelevu ya nchi yetu, afya na mazingira kwa ujumla ingawa serikali hawaitumii hasa sekta hii inavyotakiwa. Nchi yetu ina takriban hekta milioni 33.3 za misitu. Kati ya hekta hizo Serikali imetenga na kuhifadhi kisheria hekta 13millioni katika sehemu mbali mbali, na eneo la hekta millioni 20.3 hazihifadiwi kisheria.

Mheshimiwa Spika,

Maendeleo ya sekta hii kwa kiasi kikubwa yanategemea sana ushirikishwaji wa jamii na uwepo wa mwamko juu ya umuhimu wa misitu kwa maendeleo ya nchi. Serikali inatakiwa kuishirikisha jamii kikamilifu katika ngazi zote kuanzia utunzaji, utaratibu wa uvunaji na hata kwenye mapato na sio katika uhimizaji wa upandaji wa miti tu. Kwani wanavijiji hao wanauwezo mkubwa wa kusaidia katika kuzitumia mila na tamaduni zao katika utunzaji wa rasilimali hizi bila hata ya kutumia gharama yoyote.

Mheshimiwa Spika,

Kutokana na kutokushirikishwa kikamilifu kwa wanajamii katika sekta hii, athari zake ni kubwa kwani uchambuzi unaonyesha kuwa ukataji holela wa misitu umeongezeka kutoka hekta 300,000 nakufikia hekta 400,000. Na leo hii ndio maana Tanzania imekuwa nchi ya nne duniani kwa uharibifu wa misitu ikiongozwa na Indonesia, hali hii ni hatari kwa usalama wa maisha yetu na kizazi kinachofuatia.

Mheshimiwa Spika,

Sekta ya misitu pia inakabiliwa na matatizo kama vile uhaba wa watendaji, elimu ndogo ya watendaji, rushwa iliyo kithiri, kutokuwajibika na kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya wafanyakazi na ushirikishwaji mdogo wa wadau katika mambo muhimu ya maendeleo ya sekta.

Hivyo Kambi ya Upinzani inaitaka wizara kuyatekeleza mambo yafuatayo ili iwe ni chachu ya maendeleo kwa sekta hii:-

 • Kuwapatia elimu ya kutosha wafanyakazi wa idara ya misitu, ikiwa ni pamoja na kupewa maadili ya kazi.
 • Kuweka uwazi juu ya ukusanyaji wa mapato yaya mazao ya misitu.
 • Kuwahusisha wadau muhimu katika usimamizi wa misitu wakiwemo wanavijiji.
 • Kuwepo kwa mipango mizuri ya uvunaji maliasili yetu, unaofuata sheria.
 • Kubuni vianzo mbadala vya fedha kama ulipaji kwa matumizi ya huduma za mazingira.

Sheria ichukue mkondo wake kwa wale wote wataohusika na biashara haramu ya kusafirisha magogo na mbao na wale wanaobainika kufanya hujuma hiyo watangazwe wazi kwenye vyombo vya habari.

Mheshimiwa Spika,

Kuna vyanzo na njia nyingi za kuweza kuongeza mapato katika sekta hii ya misitu. Chanzo kikubwa  ambacho mapato yake hayakusanywi kikamilifu ni bidhaa za magogo na mbao. Katika taarifa za kiutafiti kutoka kwa kundi la wahisani na pia Asasi kadhaa zisizo za kiserikali, (Kama TRAFFIC) (2005/2006) wametoa mapendekezo mbali mbali pia katika hotuba yetu ya Mwaka jana tulitoa ushauri jinsi ya kukusanya mapato zaidi kwenye sekta ya misitu na Serikali imeshindwa kabisa kutumia fursa ambayo Kambi ilizionyesha.

Mheshimiwa Spika,

Kuwepo kwa njama na kulindana kati ya asasi mbali mbali za Serikali na Sekta binafsi sio tu kumeendelea kuwahusisha watu muhimu katika wizara ya Maliasili na Utalii bali hata wafanyabiashara wa mbao kwenye chama chao cha wasafirishaji wa mbao nje ya nchi. Hii ni moja ya mambo yaliyobainishwa kwenye taarifa ya TRAFFIC. Mambo ambayo bado hadi sasa yanaendelea.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inataka kuelewa taarifa ya TRAFFIC iliyowasilishwa kwenye semina ya wabunge mwaka 2007, yenye mapendekezo kuhusiana na njia za kunufaika na mapato yatokanayo na sekta ya misitu. Je ni kwa kiasi gani Serikali imeyatekeleza?

Mheshimiwa Spika,

Pamoja na Sheria kukataza usafirishwaji wa miti aina ya mipingo (African Black wood) mwaka 2007 jumla ya ‘containers’ 52 za mipingo zilisafirshwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam. Kambi ya Upinzani inataka Serikali itoe majibu ni hatua zipi zimechukuliwakwa wahusika au kurejesha magogo hayo au tunasubiri tukanunue vinyago na mapambo ya mipingo kutoka Asia wakati miti hiyo Mungu ametupa Watanzania?

Mheshimiwa Spika,

Kama ambavyo tumeuza viwanda vyetu vya mbao na sasa tunanunua samani zisizo na ubora kwa gharama kubwa kutoka nje, wakati magogo na mbao vinapelekwa nje kwa bei karibu na bure.

Kambi ya Upinzani inataka kujua hatma ya viwanda vya mbao vilivyokuwa chini ya TWICO baada ya kubinafsishwa, vinaendelea kufanyakazi ya misitu au ilikuwa ni njama ya kuviua na kuwakoseaha ajira watanzania?

Mheshimiwa Spika,

Serikali ilipopiga marufuku usafirishaji wa magogo nje ya nchi, magogo yaliyokuwa tayari yamekatwa na yalikuwa porini, hatua gani zilichukuliwa na Taifa limepata kiasi gani cha fedha?

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inataka kujua tangu Januari 2006 hadi Juni 2008 kwa utaratibu mpya uliowekwa wa uvunaji wa mazao ya misitu, magogo na mbao kiasi gani kimesafirishwa nje nje ya nchi na nchi imepata kiasi gani?

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inataka majibu ya timu iliyoundwa na Serikali na kutumwa China kwenda kuchunguza ni kiasi gani cha magogo kinauzwa uchina na kwa bei gani kwa cubic mita moja, kwani Serikali iliahidi hapa Bungeni kuwa  ndani ya wiki mbili ingetoa taarifa  lakini  hadi leo hatuna majibu ya timu hiyo.

Mheshimiwa Spika

Kambi ya upinzani inashauri bidhaa za mazao ya misitu yaongezewe dhamani hapa nchini ili watanzania wengi wapate ajira na kuviwezesha viwanda vyetu kufanya kazi ya kutengeneza samani na kuziuza nje.Tuachane na utaratibu usio na tija tunaoutumia sasa wa kuwasafirisha magogo na mbao kuwapelekea wachina,wao wanatengeneze samani na kukuzilete hapa na tunazinunua ghali sana.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inataka hatua zifuatazo zichukuliwe:-

i. Halmashauri za Wilaya zilizo katika maeneo ambayo bidhaa hizi zinapatikana ziwe mawakala wa kukusanya mapato kutokana na bidhaa za maliasili. Uamuzi huu utapunguza kwa kiasi kikubwa ufisadi uliopo sasa katika Wizara ya Maliasili. Kila Halmashauri inayokusanya kodi ipatiwe gawio kutoka sehemu ya makusanyo;

ii. Mapato yote yakusanywe na TRA kwa kutumia stakabadhi za TRA kupitia Halmashauri za Wilaya kama ilivyo elezwa hapo juu;

iii. Mtu yeyote atakayekamatwa kwa kutorosha maliasili afilisiwe kwa mujibu wa sheria kama haipo itungwe;

iv. TRA mbali na kukusanya mapato ishirikiane na Bodi ya Mauzo ya Nje kuhakiki bei za bidhaa zetu zinazouzwa nje ili kupata mapato halali ya Rasilimali zetu.

UFUGAJI WA NYUKI

Mheshimiwa Spika,

Sekta ya ufugaji wa nyuki ni muhimu katika kuchangia juhudi za kunyanyua pato na uchumi wa Tanzania ingawa sekta hii haipewi msukumo unaostahili. Lakini umuhimu wake ni mkubwa kwa jamii na kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla. Sekata hii imekuwa inakabiliwa na changamoto mbali mbali zikiwepo uvunaji usioendelevu wa misitu, kufyeka na kuchoma misitu, upungufu wa wataalam, upatikanaji wa taarifa zahihi na ukosefu wa masoko ya uhakika imekuwa ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya ufugaji nyuki wenye tija.

Mheshimiwa Spika,

Wafugaji wa nyuki wamekuwa wakipata matatizo makubwa ya ardhi kwa sababu ya kutokuwa na maeneo ya ufugaji yanayotambulika kisheria.

Mheshimiwa Spika,

Katika jumla ya idadi yote ya mavuno karibu asilimia 75 ya mavuno hayo yanauzwa katika masoko ya nyumbani na 25% tu ndio yanayosafirishwa nje ya nchi, kwa mfano katika mwaka 2007/08 tani 413 tu za nta kwa mwaka ndizo zinazosafirishwa nje. Hii inaonesha jinsi gani sekata hii inavyohitaji msukumo mkubwa toka Serikalini hasa suala la kuwatafutia wafugaji masoko ya nje na kuweza kuitangaza biashara hii kwa ajili ya kuwawezesha wafugaji.

Mheshimiwa Spika,

Nchi yetu inakadiriwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi makundi ya nyuki karibu milioni 10 katika maeneo mbali mbali ya misitu na mashamba, maeneo haya yangeweza kuzalisha tani zipatazo 9,200 za nta na tani 138,000 za asali kama serikali ingelielekeza nguvu zake katika sekta hii. Katika mwaka 2007/08 wizara iliarifu uuzaji wa tani 413 tu za nta ambazo ni kidogo sana ukilinganisha na idadi ya makundi ya nyuki yaliomo katika mashamba na misitu mbali mbali nchini ambayo ilikuwa ni sawa na 4.5% kwa maana nyengine 95.5% hazijazalishwa.

Mheshimiwa Spika,

Hata bei wanayopewa wafugaji hawa wa nyuki hairidhishi ukilinganisha na ubora wa hali ya juu na uhalisia wa  bidhaa hii na ya kipekee inayozalishwa nchini, na kazi kubwa wanayoipata wafugaji hawa hadi kupatikana kwa mavuno hayo.

Hivyo basi, kambi ya upinzani inaitaka Serikali iangalie tena upya uhalisia wa bidhaa hii na kazi kubwa na ngumu wanayoipata wafugaji na hivyo kuwatafutia soko zuri na la uhakika pamoja na vifaa vya kisasa vya ufugaji wa nyuki ili ufugaji wao uwe na tija na hivyo kuinua hali zao za maisha.

MAMBO YA KALE

Mheshimiwa Spika,

Katika kutekeleza kuhifadhi na kuendeleza maeneo ya mambo ya kale kiutalii mwaka 2007/08. Wizara ya maliasili na Utalii iliahidi kuweka umeme na maji katika kituo cha Amboni na Olduvai kwa ajili ya kuboresha zaidi.uk.119.

Kambi ya upinzani inaona wazo hili ni zuri na ingelisaidia sana katika kuvifanya vituo hivi viwe vya kisasa na kuweza kuwavutia watalii wengi wa ndani na wa nje ya nchi. Kambi ya upinzani inauliza mbona hakuna mabadiliko yoyote ya kimaendeleo katika Sehemu hizi ambazo ni rasilimali kubwa kwa taifa hili? Lakini zaidi ya yote serikali imeshindwa kuboresha kabisa Sehemu hizi zaidi ya kujikaza kwa ukusanyaji wa mapato. Ingawa wanasema mwanzo wa safari ni hatua lakini mbona matayarisho na dalili za safari hazionekani?. Na pia wanadai kuwa ukiweza kujenga mlango wa nyasi basi wa chuma unafuatia, mbona miaka inapita na nyasi wenyewe zinaanza kuliwa na mchwa? na dalili ya mvua mawingu mbona kukoshwari?

Mheshimiwa Spika,

Nchi yetu imebahatika kuwa na vivutio vingi sana vya mambo ya kale lakini bado havijatangazwa wala kuendelezwa, na mifano mizuri ni ya Magofu ya Kilwa Kivinje yameanguka na mengine yamemilikiwa na watu binafsi, na Serikali inayafahamu haya lakini inaendelea kukaa kimya.

Mheshimiwa Spika,

Kutokana na umuhimu wa sekta hii kwa maendeleo la taifa hili. Kambi ya upinzani inafikiria kuna umuhimu mkubwa wa kuitangaza sekta hii katika nchi za nje kwa ajili ya kukuza soko na pato la taifa kwa ujumla, kwani kuna mambo mengi yanayohusiana na mambo ya kale bado hayajulikani kitaifa wala kimataifa. Hivyo katika kukuza sekta hii kambi ya upinzani inashauri yafuatayo:-

 • Kusambaza picha na mikanda ya video mbali mbali zinazohusu mambo ya kale ndani na nje ya nchi.
 • Kuweka majarida mbali mbali na vitabu ambavyo yanazungumzia mambo ya kale.
 • Kuajiri watumishi wa kutosha na kuwapatia mafunzo kuhusiana na mambo kale ili kuleta ufanisi
 • Kuboresha na kuyatunza maeneo ya kale kwa ajili ya kuvutia watalii.
 • Kuwashirikisha wanajamii kikamilifu kuanzia utunzaji hadi ugawaji wa mapato.

UTAFITI

Mheshimiwa Spika, Hakuna uhifadhi endelevu bila kuwepo utafiti. Ni utafiti ndio utakaotufanya tuelewe mwelekeo wa hifadhi zetu na viumbe vinavyoishi katika hifadhi hizo pamoja na bahari na maziwa. Baadhi ya taasisi zinazofanya utafiti katika sekta hii ni Tanzania Wildlife Research Institute (TAWIRI) na Tanzania Forestry Research Institute (TAFORI). Pamoja na umuhimu mkubwa wa taasisi hizi katika swala zima la uhifadhi bado zimekuwa zinatengewa fedha kidogo sana na hata hizo kidogo zinatoka kwa wahisani.

Mheshimiwa Spika, kutegemea fedha za wahisani katika utafiti ni hatari mno kwani dhahiri kabisa pale ambapo wahisani hao wanasitiza misaada yao na miradi mingi ya utafiti haifanyiki.  Ni muhimu Serikali ikahakikisha inatenga fedha za kutosha kwa ajili ya tasisi za utafiti.

Mheshimiwa Spika,

Hata wakati mwingine fedha zinazotolewa kwenye taasisi hizi zinakuwa hazina mipangilio mizuri na kutolewa kwa wakati zinapohitajika. Mfano mzuri ni pale Wizara ilipotenga kiasi kikubwa cha fedha na kupelekwa TAWIRI kwa ajili ya kuidadi mamba nchi nzima (Mapitio ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo na bajeti ya mwaka 2007/08 u.k 6), huku katika hotuba ya Waziri wa mali asili na Utalii 2007/08 u.k 71 ikionesha idadi ya mamba tayari imeshajulikana ambao ilikadiriwa kuwa 72,000.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya upinzani inaona utafiti huo ulikuwa ni ufujaji na uharibifu wa fedha za wananchi. Tunamuomba Mhe. Waziri atueleze kulikuwa na umuhimu gani wa utafiti huo na idadi kamili ya mamba hao ilikuwa inajulikana? Je, hakuna tafiti nyingine muhimu ambazo zingeweza kufanyika?

HOJA ZINAZOHITAJI MAJIBU

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inahitaji majibu ya hoja zifuatazo kutoka Serikalini:

 • Wizara itueleze tofauti ya mapato ya wanyamapori iliyopo kwani hadi March 2008, mapato yalikuwa ni billion 10.554 kwa mujibu wa Wizara, wakati kitabu cha Hali ya Uchumi 2007/2008 ni billion 7.567. Kambi ya Upinzani inamtaka Mhe. Waziri aeleze kama kweli zabuni ya wazi ilifanyika kwa ‘camps’ za Selous, Je ni kiasi gani cha fedha kililipwa kwa Serikali?
 • Pili fedha hizi zote zimekwenda wapi kama kweli zililipwa? Kama hazikulipwa ni kwa vipi au nani aliwapa ruhusu ya kuendelea na biashara kinyume na sheria.
 • Kwanini Serikali ikaruhusu kujengwa EN LODGE AFRIQUE kwenye njia ya kupitia wanyama kati ya Tarangire na Ziwa Manyara?
 • Kwanini Serikali ikammilikisha ardhi Johnes Turdor wa Marekani eneo la kilometa za mraba 149 kinyume na sheria ya ardhi ya mwaka 1999?
 • Serikali iliahidi kujenga Chuo cha utalii kuanzia Augosti 2007. Tunataka maelezo kwanini ujenzi huo ulichekewa kuanza?
 • Kambi ya Upinzani inataka Serikali itoe majibu ni hatua zipi zimechukuliwa kwa wahusika au kurejesha magogo yaliyokamatwa yakisafirishwa kinyume na sheria?
 • Kambi ya Upinzani inataka kujua hatma ya viwanda vya mbao vilivyokuwa chini ya TWICO baada ya kubinafsishwa.
 • Serikali inasemaje juu ya uvunaji wa magadi (soda ash) kutoka ziwa Natron.

Mheshimiwa Spika,

Baada ya kuyasema hayo nawashukuruni wote kwa kunisikiliza,kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

……………………………………………………..

Magdalena H. Sakaya (Mb)

MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI,

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

10.07.2008

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s