Ni wakati wa kuwa na jeshi la kisasa

“Kambi ya Upinzani, inalitaka jeshi letu lifikirie kwa   kina namna ya kuongeza kasi ya kuleta mapinduzi ya maendeleo katika nchi yetu kama wanavyofanya wenzetu kwa ajili ya kunyanyua uchumi wa nchi zao jambo litakalosaidia kupatikana kwa fedha za kutosha kwa bajeti ya jeshi letu…Kambi ya Upinzani ilikwishashauri jinsi ya kupata vijana wenye vipaji maalum ambao tunaamini kama vipaji hivyo vikitumiwa vizuri jeshi letu litakuwa ndiyo hazina kubwa ya chimbuko la teknolojia mpya na rahisi kwa maendeleo ya watanzania. Jeshi waanze kuwatafuta vijana wenye vipaji tangu wakiwa mashuleni…”

Masoud A Salim

Masoud A Salim

Hotuba ya Mhe. Masoud Abdalla Salim (Mb) Msemaji Mkuu Kambi ya Upinzani Wizara ya Ulinzi wa JKT kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka wa fedha 2008/2009

Mheshimiwa Spika, Awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu ALLAH SUBHAWAHU/ WATAALA aliyenijalia uzima na afya njema kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani kwa mujibu wa kanuni za Bunge kifungu 99(7) Toleo la Mwaka 2007, kuhusiana na Bajeti ya Wizara ya Ulinzi na JKT kwa mwaka wa fedha 2008/2009.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchache wa fadhila kama sitakishukuru chama changu cha CUF kwa uongozi wake makini chini ya Mwenyekiti Prof. Ibrahim  Haruna Lipumba, Makamu wake Machano Khamis Ali na Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad kwa imani yao ya  kuelimisha na kuwatetea wananchi kujua haki zao katika dhana nzima ya kuboresha maisha ya watanzania.

Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Mtambile kwa msaada na imani waliyonayo kwangu katika kutekeleza majukumu yangu ndani ya Jimbo la Mtambile na hata nikiwa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, itakuwa sikuwatendea haki hata kidogo kama sikumshukuru Kiongozi wa Upinzani Bungeni Mhe. Hamad Rashid Mohamed na Naibu wake Dr. Slaa pamoja na Wabunge wote wa Upinzani kwa ushirikiano walionipa katika kufanya kazi zangu kwa ufanisi.

SERA NA SHERIA YA ULINZI WA TAIFA

Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu sera na sheria yetu ni ya zamani tangu 1966 huku dunia ikishuhudia mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kisiasa, kijamii, kisayansi n.k.  hivyo  pamoja na mabadiliko madogo katika Sheria na Sera hizo bado kuna haja ya kuziangalia kwa upeo Sheria za Jeshi ili ziendane na wakati huu wa maendeleo ya Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ni imani ya Kambi ya Upinzani kuwa ni vyema Sera na Sheria za Ulinzi wa Taifa kuangaliwa upya ili kuweza kuboresha mazingira ya Kijeshi zaidi. Aidha mfumo wa   Mahakama ya Kijeshi na Viwango vya adhabu zinazotolewa uangaliwe upya kwa lengo la kuboresha nidhamu.

Mheshimiwa Spika, Tanzania imeingia kwenye mikataba mbalimbali ya Kimataifa na   ili mikataba hiyo iweze kutekelezwa ni sharti ijumuishwe katika Sheria ya Ulinzi jambo ambalo halijafanyika, hivyo Kambi ya Upinzani imeona si vyema kuridhia jambo ambalo huwezi kuliingiza kwenye sheria na kulitekeleza.

MAENDELEO YA NCHI NA TEKNOLOJIA

Mheshimiwa Spika, Mbali na shughuli zinazofanywa na sekta ya ulinzi nchini za kuimarisha usalama wa taifa lakini bado sekta hii haijaleta tija inayotakiwa na kuweza kunyanyua uchumi wa nchi hii kama inavyotegemewa na wananchi walio wengi na hasa kwa kuzingatia  wanavyofanya majeshi na askari wa nchi nyengine duniani.

Mheshimiwa Spika, Kwani sekta hii inatakikana iwe mstari wa   mbele katika kuleta maendeleo na hasa katika shughuli za uvumbuzi wa kila siku, wao wawe ndio chachu ya maendeleo na sekta nyengine ziwe zinafuatia kama vile wanavyofanya taasisi za ulinzi za nchi nyengine. Mfano mzuri mnamo mwaka 1740 na 1805 majeshi ya ulinzi ya Ulaya mbali na shughuli nyingine za kiulinzi na usalama lakini walifanya utafiti na kugundua mfumo mpya wa kijeshi ambao umewapelekea mafanikio makubwa katika kuleta maendeleo kiuchumi na utulivu nchini mwao.

Mheshimiwa spika, hata nchi ya United Kingdom wanajeshi wao walichangia kwa kiasi kikubwa uvumbuzi wa kutumia ndege katika vita, na submerine ambayo ilitumika kwa kubebea, kutulia na kurukia ndege za kivita pia walichangia kwa kiasi kikubwa katika uvumbuzi wa rada ambayo inawasaidia sana katika kuleta na kulinda usalama nchini mwao.

Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa shirika la kutengeneza magari Nyumbu bado halijafikia kiwango kinachotakikana katika uzalishaji. Kambi ya Upinzani inalishauri jeshi letu, ni vyema wabuni magari ambayo yataendana na mazingira halisi ya barabara za Tanzania ambayo yatatumia gharama nafuu, badala ya kutumia fedha nyingi kutengeneza gari la kisasa ambalo linagharama kubwa. Nivyema kutumia raslimali zetu chache kwa   kuongeza tija. Isitoshe, Serikali nayo itenge fedha za kutosha au kuwawekea utaratibu bora wa magari hayo kuzalishwa kibiashara yaani “Assembly line of production”.

Mheshimiwa Spika, mbali na shughuli za kiulinzi, Askari na wanajeshi wa Marekani wanaoshughulikia kitengo cha afya, huwa mara kwa mara wanafanya tafiti za kisayansi kuhusiana na afya ya wanajeshi na jamii kwa ujumla. Lakini kama  hiyo haitoshi Military infection deseases research programme (MIDRP) iliendelea kufanya tafiti kwa ajili ya kuwalinda askari na wananchi na kutokomeza kabisa maradhi ya malaria na maradhi ya ngozi kwa wafanyakazi wake, sambamba na hilo wamefanikiwa kuanzisha Army Research Institute (ARI) ambayo wameweka maabara ambayo inashughulika na shughuli za kutoa mafunzo ya utafiti.

Mheshimiwa Spika, Katika kuonesha majeshi na askari wa wenzetu wamepiga hatua kubwa kimaendeleo majeshi ya Marekani wameanzisha tovuti-Deplay Med Research LINK kwa ajili ya kusambaza taarifa za kiserikali zinazohusiana na utafiti wa kisayansi ambao unalengo la kuboresha upatikanaji wa habari za kiutawala, idara na huduma za kiafya na huduma nyengine za kijamii. Hii ni hatua kubwa za kimaendeleo. Kambi ya Upinzani inataka kujua mbali ya kuwa na tovuti ya jeshi, je Serikali yetu imewaandaa vipi wanajeshi wetu kutumia huduma za mtandao kwa ufanisi?

Mheshimiwa Spika, Ili taasisi zetu za ulinzi zifanikiwe zinahitaji kuwa wazi, kuwa wavumbuzi na kukubali kubadilika na kuendena na maendeleo ya kisayansi na technolojia. Mtaalamu wa Physics, Rutherford, alinukuliwa akisema kwamba “we have short of money so we must think.” Wanajeshi wetu wafahamu kuwa tuna tatizo la umaskini hivyo inatulazimu kila wakati kufikiri, kwani uvumbuzi unahitaji zaidi vipaji binafsi (talented military personnel).

Mheshimiwa Spika, Nchi kama Canada sekta ya ulinzi haikufanikiwa tu katika kuchangia maendeleo ya nchi yao ila taasisi husika zilijiuliza masula mengi kwa mfano:-

a) Kitu gani tunaweza kukifanya na   kuleta maendeleo?

b) Sisi tunauwezo kiasi gani ili kuleta mageuzi ya kimaendeleo?

c) Na tutafanya nini?

Kambi ya Upinzani, inalitaka jeshi letu lifikirie kwa   kina namna ya kuongeza kasi ya kuleta mapinduzi ya maendeleo katika nchi yetu kama wanavyofanya wenzetu kwa ajili ya kunyanyua uchumi wa nchi zao jambo litakalosaidia kupatikana kwa fedha za kutosha kwa bajeti ya jeshi letu.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani ilikwishashauri jinsi ya kupata vijana wenye vipaji maalum ambao tunaamini kama vipaji hivyo vikitumiwa vizuri jeshi letu litakuwa ndiyo hazina kubwa ya chimbuko la teknolojia mpya na rahisi kwa maendeleo ya watanzania. Jeshi waanze kuwatafuta vijana wenye vipaji tangu wakiwa mashuleni (primary na secondary).

Mheshimiwa Spika, Jeshi la ulinzi Israel limeisaidia sana nchi hiyo katika kupiga hatua mbele za kimaendeleo. Serikali ya Israel ilipanga mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa sayansi inapewa kipaumbele kwa kila sekta kwa kuzisaidia kifedha na kuwaunga mkono kisera, kwa mfano sekta ya biashara ilichangia pato la taifa kwa asilimia 5 mwaka1990 hadi asilimia 14 mwaka 2000, si hivyo tu lakini leo hii Israel ina makampuni 68 ya kibiashara ambayo ni ya tatu baada ya Marekani na Canada, na huku ikiwa na makampuni ya teknolojia yaliyotoa ajira kwa watu zaidi ya wastani wa 120,000 mwaka 2005, kubwa zaidi leo hii Israel wana wanasayansi na engenneer 140 kila penye wafanyakazi 10,000 ukilinganisha na 83 Marekani na 60 Ujerumani. Kwa mantiki hiyo ni vyema vyombo vyetu vya ulinzi vikajifunza katika kuleta maendeleo na mapinduzi ya kweli ya kiuchumi.

Mheshimiwa  Spika, Kigali Institute of Science, Technology and Management (KISTM) imeonesha jinsi gani taasisi za kielimu zinavyoweza kutumika kuibadilisha jamii kimaendeleo kutoka hatua ilipo. Taasisi hii muhimu ilianzishwa na kufanyakazi chini ya jeshi la Rwanda na kuleta maendeleo makubwa kiuchumi kabla ya mauaji ya 1990, na hili ni somo kwa nchi yetu kuona umuhimu wa kubadilisha mfumo na kulifanya jeshi kuwa ndio kituo kikuu cha maendeleo kwa kutoa wasomi na wa wataalamu wa fani mbali mbali kama vile mapailot, madereva wa gari, madaktari, watafiti, wakandarasi, walimu wa vyuo vikuu na hii ingesaidia hata kuweza kukabiliana na ufisadi ambao unaathiri uchumi wa nchi yetu

.

POSHO YA NYUMBA NA CHAKULA CHA WANAJESHI

Mheshimiwa Spika, Utaratibu uliowekwa kwa askari wa jeshi la Tanzania ambaye yuko nje ya Kambi analipwa 10% ya mshahara wake kama posho ya nyumba.  Inasikitisha kuona kwamba Askari JWTZ anapewa Sh.9, 000/-   kwa mwezi kama posho ya nyumba au ya makaazi.

Mheshimiwa Spika, Lakini tujiulize hivi kuna chumba gani cha Sh.9,000/- ambacho kinastahili chenye umeme na chenye hadhi inayotakiwa, je, hivi kweli ni busara kwa mila, desturi na haki za kibinadamu Askari kuweza kuishi kwenye chumba kimoja na watoto wote hatuoni kwamba tunawadhalilisha na hatuwatendei haki, hivi Sh.9,000/- posho ya nyumba ni kwa mshahara wa mwaka gani?

Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali kuongeza posho la nyumba kwa angalau asilimia 20% ya mshahara wa Mwanajeshi kwani itawapelekea wanajeshi wetu kupata vyumba vya kutosha kwa kuishi kwa kuridhika, kwa kutenganisha vyumba vya wazazi na vile vya watoto.

Mheshimiwa Spika, Posho ya chakula cha Askari Sh.75,000/-    kwa mwezi ni kiwango kidogo sana kwani ni wastani wa Shs.2,500/- kwa siku, fedha ambayo awezi kujikimu kwa milo mitatu; na kuna malalamiko kwamba ikiwa uko kazini fedha zako zinapunguzwa kwa sababu umekula Kambini, lakini swali je, hivi askari kupata chakula chake kambini unapunguza nini, hatuoni mlo huo ni sehemu ya motisha, na sio kumpunguza posho lake?

Tunaitaka Serikali kuwapatia posho ya chakula wanajeshi angalau 10,000/-. kwa  siku.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka kujua  kigezo gani kinatumika kuwanyima posho ya chakula ya shs.75,000/- wanajeshi wetu wanaopata nafasi ya kupangiwa mikoa hiyo ya mipakani, na ndio maana wamekuwa na msamiati mpya unaojulikana kwa jina la KUJILA,  kwa mfano, unaenda Kigoma utalazimika kutumia fedha za mshahara wako bila posho ya chakula, Kambi ya Upinzani inataka kufahamu fedha hizo za posho za chakula wanazonyimwa wanajeshi ambazo tayari huwa zipo kwenye bajeti zinapelekwa wapi na ni lini KUJILA kwa wanajeshi wanaopelekwa mikoa ya mipakani kutapatiwa ufumbuzi?

SHERIA YA NDOA JESHINI

Mheshimiwa Spika, Vijana wetu wenye elimu ya juu na hata wenye elimu inayomfanya mwombaji aweze kujiunga na jeshi wana kigugumizi na kujiunga na jeshi baada ya kuona sheria kwa mwanajeshi anapoajiliwa hawezi kuoa na kuolewa hadi ifikie miaka 6; yaani kipindi cha mkataba, lakini la kusikitisha ni kwamba hata wale wanajeshi waliomaliza   mkataba wa miaka 6; bado wengi wao hawajaruhusiwa kuoa na kuolewa. Je, tatizo ni nini?

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka kufahamu hivi tunaposhauri na kuhimiza  kupambana na UKIMWI, huku tukitaka wanajeshi wetu kuwa waaminifu wasijiingize katika vitendo viovu, lakini unamtungia sheria asioe wala asiolewe kwa muda wa miaka 6, ni kweli tunawatendea haki, na ni kweli tumedhamiria kuwalinda na UKIMWI, hivi ni kweli mwanajeshi unapokuwa unamnyima haki ya msingi ya ndoa unamtarajia aishi vipi?

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaishauri Serikali sheria hii irekebishwe na iondolewe ili wanajeshi waweze kuoa na kuolewa, na kuwafanya wale vijana wenye hofu juu ya sheria hii waweze kujiunga na jeshi hili.

MAVAZI KWA ASKARI JWTZ

Mheshimiwa Spika, Wizara bado haijaiangalia huduma hii kwa undani zaidi. Imedhihirika kwamba mpaka sasa hakuna utaratibu wa kipindi maalum kwa mwajeshi anaweza akabadilisha SARE ZA JESHI, bila kufikia kiwango cha sare hizo kupauka (kuchakaa).

Kambi ya Upinzani ina mashaka na umadhubuti wa baadhi ya SARE za wanajeshi, kwani inaonekana vitambaa vinavyotengenezwa sare hizo haviko katika viwango vinavyotakiwa, hivyo Kambi ya Upinzani inaishauri Serikali kuwabana kikalifu wazabuni wote wa sare za wanajeshi wetu aidha Kambi ya Upinzani inataka kujua SARE ZA WANAJESHI WETU zinatoka ndani ya nchi au nje ya nchi, na kama zinatoka nje ya nchi, kama inavyosadikiwa hivi tunajiuliza viwanda vyetu vya ndani ya nchi havina uwezo wa kutengeneza SARE za wanajeshi wetu, hasa JKT na MAGEREZA.

Mheshimiwa Spika, hivi hatuoni kuzipatia viwanda vyetu Zabuni ya SARE za wanajeshi wetu wa JWTZ tutaongeza ajira kwa watanzania, kwani Kambi ya Upinzani inapata mashaka kuelewa uhafifu wa vitambaa vinavyotengenezwa SARE za wanajeshi tunatumia fedha zetu kiasi gani, kwa maana hiyo Kambi inataka kueleweshwa na Serikali kila pea moja ya SARE ya wanajeshi inagharimu fedha kiasi gani.

UPANDISHWAJI VYEO JESHINI

Mheshimiwa Spika, Kuna malalamiko miongoni mwa wanajeshi kuchelewa kupandishwa vyeo hali ambayo imeathiri sana maslahi ya wanajeshi na hadhi zao huku wengine umri wao ukiendelea kuwa mkubwa.

Mheshimiwa Spika, haipendezi hata kidogo Askari ambaye analitumikia jeshi mpaka anastaafu akiwa na cheo cha LANSI-COPLO, hali hii inazusha maswali mengi sana katika mfumo mzima wa maslahi ya kuinua mgongo na pensheni yake na nikweli mtu amelitumikia jeshi kwa miaka zaidi ya 20 anastaafu akiwa LANSI-COPLO au COPLO?

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka kujua ni vigezo gani vingine unavyowapelekea baadhi ya wanajeshi kupandishwa vyeo haraka haraka zaidi na wengine wakisota taratibu mno, ukaachia mbali na ELIMU YA MUDA ALIOINGIA JESHINI na ukakamavu wake sambamba na nidhamu ya mwanajeshi.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inayasema haya ili   kuweka bayana kwamba sasa umefika wakati wa kuandaa mazingira mazuri ya kupandishwa vyeo wanajeshi wetu, kwani kuchelewa kuwapandisha vyeo si tu ni tunawavunja moyo kusaikolojia lakini pia kwa namna nyingine tunawaathiri maslahi yao wakati wanapostaafu.

Hivyo basi, Kambi ya Upinzani inaiomba Serikali kuliangalia swali hili na kulipatia ufumbuzi wa kudumu ili kuondoa kabisa manung’uniko kwa wanajeshi wetu.

ULINZI MIPAKANI

Mheshimiwa Spika, Moja kati ya kazi za wanajeshi wetu ni  kuhakikisha  mipaka yetu inakuwa salama wakati wote kwa mantiki Raia wote wa Jamhuri ya Muungano nao wote wawe salama.

Mheshimiwa Spika, Vituo teule (detarches) vilivyowekwa mipakani vinafanya kazi vizuri katika kuhakikisha wananchi wako salama, lakini vitendo vinavyofanywa na     wahalifu wanaosadikiwa toka nchi jirani baina ya Mkoa wa Kagera na Tanzania, kwa Wilaya za Karagwe, Ngara,  haviwezi tena kuvumiliwa na wananchi wa Tanzania huku tukiwaelekea na kuwatupia mzigo Jeshi la Polisi peke yake.

Mheshimiwa Spika, Haiwezekani wananchi wa Kagera waishi kwa wasiwasi ndani ya nchi yao, huku mikoa mingine ikilala kwa usingizi mnono kwani Tanzania ni moja na wote wana haki sawa mbele ya Sheria, hivi Kambi ya Upinzani inataka kujua vitendo vinavyoripotiwa vya kuuawa, kutekwa, na kuporwa mali katika mapori na misitu kadhaa ya Mkoa wa Kagera kuendelee kulalamikiwa na wabunge hadi lini kutapatiwa ufumbuzi huku tukijua kwamba sasa wakati umefika kwa JWTZ kukomesha kabisa uovu huu katika Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasikitishwa sana na kitendo kinachofanywa na majambazi toka nchi jirani kwa wavuvi wetu wa Kigoma kuwanyang’anya vyombo vyao na wengine kuuwawa, hivi kweli kama ziwa hili ni letu sote ni kwanini wanaendelea kuwatesa wavuvi wetu wa Kigoma.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka kujua vituo Teule (Detarches) zilizoko katika vijiji vya KAGUNGA, MTANGA,KARAGO, IGUNGA ,HEREMBE, KALYA, MWAKISEGA, KASEGE na KATONGA ambavyo vimetanda kandokando ya ziwa Tanganyika Kigoma vinawasaidiaje wavuvi wa Kigoma wanaonyanyaswa na wahalifu ambapo wanaendelea kudhalilishwa huku wavuvi hao wakijiuliza ni lini wanaweza kuvua wakiwa na uhakika wa usalama wao, Sambamba na hilo wavuvi katika ziwa Victoria na wao bado wanaendelea kuteseka kwa kuporwa vifaa vyao vya uvuvi na kupigwa na wahalifu,huku wakiendelea na kilio kwa Serikali yao ya kukomesha kero hili ambalo limekuwa sugu.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka kujua ni matukio mangapi ya uhalifu yameripotiwa katika Ziwa Tanganyika na ziwa Viktoria na wananchi wangapi wamepoteza mali na maisha kati ya Julai 2007 hadi Julai, 2008, na ni kwa kiasi gani JWTZ limewasaidia wavuvi wa Ziwa Tanganyika na Ziwa Viktoria kutokana na wahalifu wa nchi jirani?

SIKU YA MASHUJAA

Mheshimiwa Spika, mwezi uliopita Serikali ilifanikisha vyema maadhimisho ya siku ya MASHUJAA, chini ya Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwetu, Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, kumbukumbu ya siku hii ni ya kipekee kutokana na kuwakumbuka mashujaa wetu waliolinda nchi yetu na wale waliotumwa na Serikali kuzikomboa nchi mbalimbali Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mheshimiwa Spika, kuna malalamiko makubwa kwa mashujaa wetu walioshiriki Vita vya Kagera mwaka 1978/79 na walioshiriki Vita Msumbiji ambapo wengi wao sasa ni wastaafu na wenye ulemavu na wengine wameshafariki dunia huku familia zao wakiendelea kuteseka.

Mheshimiwa Spika, MASHUJAA hawa niliowataja ambao wengi wao ni walemavu wanaishi katika maisha ya kubahatisha, wakiwa wanyonge na ikionekana Serikali imewatekeleza muda mrefu;  na wanajiuliza hivi kulitumikia taifa na kupata ulemavu ni adhabu, na kama si adhabu ni kwanini Serikali badala ya kuwaenze wanawatekeleza wao na familia zao.

Mheshimiwa Spika, MASHUJAA wetu baada ya UHURU wanajiuliza inakuwaje MASHUJAA walioshiriki Vita vya Pili vya Dunia wanapatiwa fedha kwa msaada toka Serikali ya Uingereza, lakini Mashujaa wetu walioshiriki vita vya Kagera 1978/79, Vita vya Msumbiji na Renamo, mbona wameachwa mayatima wakitangatanga mitaani, wakilia muda wote bila kunyamazishwa na Serikali yao?

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka Serikali kulieleza Bunge hili tukufu ni  mashujaa wangapi wako hai walioshiriki Vita vya Kagera na Msumbiji je, Serikali inajua wanavyoishi na je, Serikali inafuatilia hali za maisha yao.  Ninayaleta haya kwa   sababu ni huzuni kubwa, simanzi na majonzi unapowaona mashujaa hawa hawana viungo, huku wakiendelea kulalamika bila ufumbuzi wa kuboreshewa maisha yao na wanajiuliza maswali kadhaa yasiyo na majibu.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapata kigugumizi kuelewa ni kwanini tumeweza kuondosha mabaki ya mifupa ya mashujaa wa Tanzania kule Msumbiji na kuleta mifupa hiyo kuizika kwa heshima Tanzania kule Mtwara lakini je, hivi Serikali inafahamu familia za MASHUJAA ziko wapi? Na maisha ya familia hizo zikoje? Ndio kusema kuchimba  mifupa ya marehemu mashujaa waliouawa Msumbiji ni hatua ya kwanza lakini Serikali ina mkakati gani wa kuenzi na kuzitunza familia za mashujaa hao ambazo zinateseka kwa maisha magumu, huku wakijiuliza ni kwanini wazazi wao wameuawa katika ushujaa lakini familia zinatarajiwa kufa kwa mawazo na njaa?

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaishauri Serikali kutenga fungu maalum katika bajeti kwa MASHUJAA na familia za marehemu mashujaa wetu, kwa lengo la kuwaenzi kwa dhati kabisa.

HATIMILIKI MAENEO YA JWTZ NA JKT

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, inaendelea na utaratibu wa upimaji wa maeneo ya JWTZ na JKT sambamba na kuyapatia maeneo hayo hatimiliki na hatimaye kutolewa fidia kwa yale maeneo ambayo JWTZ na JKT waliyachukua kwa wananchi kwa manufaa ya kijeshi.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka kujua, maeneo yaliyopimwa je, tayari Serikali imeshatoa hatimiliki na je, fidia imetolewa kwa wananchi.

Hivyo tunaomba ufafanuzi kuhusu maeneo yafuatayo:-

(i)  Oldonyo Sambu JWTZ – Arusha

(ii) Kunduchi Rifle Range – Dar es Salaam

(iii) Bulombora JKT – Kigoma

(iv) Kiabakari (253 KJ) – Mara

(v)  Buhemba JKT – Mara

(vi) Chita JKT – Morogoro

(vii)  Umoja Camp JWTZ – Mtwara

(viii)  Kasanga TPDF det – Rukwa, na

(ix) Mgambo JKT – Tanga

Mheshimiwa Spika, Pia Kambi ya Upinzani inataka kuelewa ni maeneo gani ya wananchi yaliyochukuliwa na Jeshi la Ulinzi wa Taifa na ambayo hadi leo hayajapimwa na ni mangapi yana mgogoro na wananchi na ni hatua zipi Serikali itachukua.

WASTAAFU NA STAHILI ZAO

Mheshimiwa Spika, wastaafu wetu wa JWTZ wamegubikwa na giza nene la maisha magumu kutokana na kiwango kidogo cha pensheni wanachopata huku bidhaa zikipanda kila kukicha, ambapo wastaafu wengine wanafanya kazi zisizostahili kulingana na vyeo walivyokuwa navyo lakini hiyo ndio hali halisi ya wastaafu kuendelea kuteseka huku umri wao ukiwa mkubwa na utegemezi wa familia, hivyo kambi ya Upinzani unaiomba Serikali kuandaa maisha yao tofauti na ilivyo sasa.

Mheshimiwa Spika, kuna malalamiko kati ya wastaafu wa zamani kupata pensheni ndogo ukilinganisha na wastaafu wa hivi karibuni, hali ambayo si kwa Ma-Jenerali wastaafu lakini hata maafisa wastaafu na ASKARI wastaafu wa kawaida wa zamani kulinganisha na kiwango cha mshahara wa vyeo wa wastaafu wa sasa, Kambi ya Upinzani inaishauri Serikali kuwapatia pensheni wastaafu wa zamani kulingana na vyeo vya sasa. Kambi ya Upinzani inasikitishwa na kitendo cha Serikali cha kuwapatia shs.21600/- wastaafu wa zamani yaani wastani wa shs.720/- kwa siku.

Kambi ya Upinzani inahoji hivi wastaafu hawa waliokuwa chimbuko la Jeshi imara na  kurithisha jeshi shupavu la sasa unawapa shs.720/- kwa siku, huku si kuwadharau na kuwakejeli? Hivi Serikali inatambua shs.720/- kwa mwanajeshi aliye na familia kwa mahitaji ya siku moja akanunue nini,je  ni kweli atamudu hata chai ya asubuhi? Hivi Serikali haielewi hili? Au haitaki kuwarekebishia  kiwango hiki cha fedha kinachostahili? Au hayo  ndio malipo yanayostahili baada ya kazi ngumu ya kulinda nchi hii katika mazingira magumu.

Mheshimiwa Spika, mapema mwezi huu wastaafu wa JWTZ walichanganyikiwa pale walipokwenda chukua pensheni yao ya miezi sita na kukuta fedha za mwezi mmoja tu. Je, tatizo hasa ni nini? Mbona Serikali haitoi jibu sahihi kwa wastaafu hawa mnawaacha wakiwa na madeni madukani huku wengine wakiadhiriwa kwa kutolipa madeni ya vyakula katika sehemu wanazokopeshwa.

Kambi ya Upinzani inaiomba Serikali kulipatia ufumbuzi tatizo hili haraka iwezekanavyo pia tunawaomba wafanyabiashara wote waliowakopesha wastaafu hawa waendelee kuvuta subira kwani hawakutegemea kama watakumbwa na mkasa huo.

Mheshimiwa Spika, kuna malalamiko makubwa kwa  wanajeshi wanaofikia muda wa kustaafu na kuongezewa muda kwa utaalamu wao kwa miaka miwili miwili, lakini akimaliza muda alioongezewa anapochukua kiinua mgongo chake kinapungua tofauti kama angelichukua muda wa miaka iliyopita sababu anaambiwa amezitumia chakula na mshahara, hivyo zimekatwa. Ikumbukwe kuwa kila mwanajeshi hivi sasa ni  MSAAFU MTARAJIWA hivi je, Serikali mnalishughulikia vipi tatizo hili?

Kambi ya Upinzani inataka kujua ni wastaafu wangapi wa aina hii wamekumbwa na mkasa huu kuanzia mwaka 2006 hadi leo 2008, na mpango huu wa kuwapunja Askari mafao yao, na je, Serikali mmeiga utaratibu huu toka Serikali ya nchi gani hatuoni kwa hili ni kichekesho cha kusadikika

.

MATUMIZI MABAYA YA FEDHA ZA SERIKALI

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Makaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni, 30, 2007, unabainisha mapungufu kadhaa katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, hivyo Kambi ya Upinzani inataka ufafanuzi wa matumizi yafuatayo:-

Vifaa vilivyolipiwa vyenye thamani ya 15,174,000/- ambavyo havikupelekwa kwenye Mradi wa Malindi na Mbweni; Je, vimepelekwa wapi?

Kutotolewa kwa taarifa ya matumizi ya jumla ya Shs.24,172,373/-;   Je, kwanini taarifa ya matumizi haikutolewa?

Malipo yenye shaka ya Sh.530, 107 ,528/-   kwa Jeshi la Kujenga Taifa, ambapo taarifa ya manunuzi haikuwekwa bayana hivyo Kambi ya Upinzani inauliza tatizo ni nini?

Malipo yaliyofanywa bila ya kuwa na hati za malipo kuwa jumla ya Sh.291, 509, 765/-

Je, Wizara inajua kufanya hivyo inatia shaka?

Malipo yenye nyaraka pungufu Ulinzi – Ngome kiasi cha Sh.381, 532, 247/-  pia vile vile malipo yenye nyaraka pungufu Jeshi la Kujenga Taifa jumla ya 3(bill) (045) mill, 290,483 hivi wizara inalionaje mapungufu haya?

Fungu 39 Jeshi la Kujenga Taifa, taswira ya matumizi haitoi picha nzuri, mfano;

Malipo yaliyofanywa bila ya kuwa na nyaraka Sh.3, 336, 800, 248/-. Hili ni tatizo lingine.

Maduhuli ambayo hayajapelekwa benki Sh.45, 892, 280/-. Je fedha zilipelekwa wapi?

Hivyo Kambi ya Upinzani inataka kujua Serikali ina mkakati gani kwa Wizara husika kuhakikisha fedha zitatumika vizuri na kuachana na mapungufu yaliyojitokeza.

JESHI LA KUJENGA TAIFA (JKT)

Mheshimiwa Spika, JKT limekuwa na chachu kwa vijana kupata mafunzo ya kijeshi na kiufundi katika kujenga nidhamu, uzalendo, na uwajibikaji wa siku hadi siku kwa lengo la maslahi ya Taifa kwa ujumla.  Hivyo stadi mbalimbali wanazopata JKT mfano Ujenzi, Kilimo, ufugaji, useremala, ni kwa kiasi gani vijana hawa wanaendelezwa kwa kuwawezesha kujiendeleza kimaisha mara tu wamalizapo mafunzo yao na kutobahatika na ajira Serikalini.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili tukufu ni vijana wangapi wameshajiunga na JKT tangu 2006 hadi leo na wangapi wamepata ajira Serikalini.

Tunayasema haya kwa kuwa na wasiwasi kwamba idadi kubwa ya vijana wa JKT ambao wamepata mafunzo ya matumizi ya silaha na kuachwa mitaani wakitangatanga bila kutafutiwa namna ya kuendelezwa, kimaisha, je. Serikali haioni kuna uwezekano wa vijana hawa kujiingiza katika vitendo vya uhalifu.

Hivyo Kambi ya Upinzani inaishauri Serikali kufanya tathmini wa kuwatambua vijana, ambao wamepitia JKT na hawajaajiriwa ili watafutiwe namna ya kuendelezwa kimaisha.

SUMA JKT

Mheshimiwa Spika, SUMA JKT limekuwa mfano bora hivi sasa katika uzalishaji mali hasa ujenzi wa nyumba bora za kisasa katika maeneo mbalimbali. Kambi ya Upinzaniinataka kujua SUMA JKT wamepata faida kiasi gani kuanzia mwaka 2006 hadi 2008.

Mheshimiwa Spika, pamoja na sifa walizonazo SUMA JKT.  Kambi ya Upinzani inataka ufafanuzi kwanini halijaunda Kamati ya Ukaguzi kinyume na Kanuni Na. 30, 31 na 32(2) ya Kanuni za Fedha za Umma kama ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni, 30, 2007 ilivyobainisha, sambamba na hilo ni kwanini, shirika la SUMA JKT halijaanzisha Kitengo cha Manunuzi kinyume na kifungu cha 44 ya Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka kujua ni lini SUMA JKT itaunda Kamati ya Ukaguzi na ni lini SUMA JKT litaanzisha Kitengo cha Manunuzi kwa mujibu wa Sheria?

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka kuelewa kiwanda cha kutengeneza madawa ya Binadamu cha TANZANSINO kinachotengeneza madawa ya binadamu kinachoendesha kwa ubia kati ya SUMA JKT na China kimefanikiwa kutengeneza madawa ya aina gani na kimepata faida kiasi gani kuanzia mwaka 2006 hadi 2008.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo pia Kambi ya Upinzani inataka kujua ni kiasi gani cha fedha zimepatikana kwa mwaka 2006 hadi 2008 kutoka kiwanda cha kushona nguo cha CAMISUMA.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, napmba kuwasilisha.

………………………………………….

MASOUD A. SALIM (MB)

MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI-WIZARA YA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA

19.08.2008

Advertisements

One thought on “Ni wakati wa kuwa na jeshi la kisasa

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s