Kuna uhusiano mkubwa kati ya demokrasia na maendeleo ya kiuchumi

Na Prof. Ibrahim Haruna Lipumba

Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Tanzania katika mitaa ya Mji wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa 2005. Kwa kisingizio cha kulinda amani na utulivu, serikali za CCM zimekuwa zikitumia vyombo kama hivi vya dola kuviza demokrasia na hivyo kudumaza maendeleo ya kiuchumi visiwani Zanzibar
Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Tanzania katika mitaa ya Mji wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa 2005. Kwa kisingizio cha kulinda amani na utulivu, serikali za CCM zimekuwa zikitumia vyombo kama hivi vya dola kuviza demokrasia na hivyo kudumaza maendeleo ya kiuchumi visiwani Zanzibar

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

“Mfumo wa demokrasia ikiwa ni pamoja na kufanyika uchaguzi ulio huru na wa haki unaishinikiza serikali ifuatilie matatizo ya wananchi. Serikali za kiimla zinatafsiri kero za wananchi zenyewe bila kujali maoni ya wananchi. Minara na majengo ya kifahari, sherehe za kumbukumbu za utawala zaweza kutengewa kiasi kikubwa cha fedha wakati wananchi hawapati huduma bora za afya. Ujenzi wa uchumi wa soko unahitaji uhimili wa serikali. Haitoshi kuwepo kwa sekta binafsi kuweza kuimarisha uchumi wa soko utakaoleta maendeleo kwa watu wote.”

 

Mada iliyotolewa katika Semina ya Baraza la Vijana la CUF- Chama Cha Wananchi, Chake Chake, Pemba katika Ukumbi wa Hoteli ya GT, 26 Januari 2002

 

 

Utangulizi

 

Katika dunia ya leo, nchi zilizopiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ni nchi za magharibi ambazo zina mfumo wa demokrasia unaowapa uhuru wa kisiasa na kiuchumi wananchi wao. Uhuru wa kisiasa ni pamoja na haki ya kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi zilizo huru na za haki kushika nafasi za uongozi wa kisiasa kuendesha shughuli za serikali kuanzia serikali za mitaa mpaka serikali kuu. Pamoja na kushiriki katika chaguzi, mfumo wa demokrasia lazima uwe na utawala unaofuata sheria, Mahakama ni huru, kuna uhuru wa vyombo vya habari, kuna uhuru wa kusema na kujumuika na wananchi wengine. Nchi hizi zina uhuru wa kiuchumi wa kumiliki mali na kufanya biashara kwa utaratibu unaoeleweka na kutabirika.

 

Wataalam wa historia ya uchumi wa ulimwengu wamejenga hoja kuwa ukuaji wa uchumi endelevu kwa muda mrefu unategemea sana mfumo mzima wa kiutawala na kiuchumi. Kama nchi ina mfumo ambao maamuzi ya watawala yanafuata taratibu zinazoeleweka na kutabirika, mfumo wa utawala una uhalali machoni mwa wananchi, utawala unafuata sheria na haki za kumiliki mali zinalindwa na kutoa motisha kwa wananchi kuchapa kazi kwa bidii, kuwa wabunifu kwani wana uhakika kuwa matunda ya jasho lao na ubunifu wao hayataporwa na dola au watu wenye nguvu au silaha basi uchumi unaweza kukua kwa muda mrefu.

 

Wanahistoria wa mlengo wa kushoto wametoa hoja kuwa, kuendelea kwa nchi za Ulaya magharibi na Marekani ni matokeo ya unyonyaji wa biashara ya utumwa na kupora mali ya Makoloni. Ni kweli watumwa walitoa mchango mkubwa katika ujenzi wa rasilimali na makoloni ya Afrika, Asia na Marekani ya kilatino yalinyonywa na Wakoloni wa Ulaya. Lakini unyonyaji huu hauelezi maendeleo ya nchi zote za magharibi. Hispania na Ureno ambao walishiriki katika uporaji wa mali ya Marekani ya Kilatino, Afrika na Asia wamekuwa nyuma kimaendeleo ukilinganisha na nchi za Scandinavia na Ulaya ya Kaskazini ambazo hazikushiriki katika uporaji wa makoloni ya dunia ya tatu.

 

Nchi kama Finland, sio tu haikushiriki katika kupora makoloni, lakini wao pia walitawaliwa na Waswidi na Warusi na walipata uhuru baada ya mapinduzi ya Urusi ya mwaka 1917. Pamoja na kuwa nchi ndogo yenye watu milioni 5, uchumi wa Finland unaoimarika hasa katika miaka ya tisini. Kampuni ya Nokia inayotengeneza simu za mkononi ni maarufu duniani kote. Finland inaongoza katika utumiaji wa simu za mkononi na mtandao wa Internet. Ina mfumo mzuri wa hifadhi ya jamii (Social Security) na huduma za msingi za jamii ni haki ya kila mwananchi.

 

Miongoni mwa nchi zinazoendelea kumekuwa na mjadala mkali kuhusu demokrasi na maendeleo ya kiuchumi. Nchi za Asia ya mashariki na hasa Hongkong, Singapore Korea na Kusini na Taiwan wamepata maendeleo makubwa ya kiuchumi kwa muda mfupi. Waziri Mkuu wa zamani wa Singapore, Lee Kuan Yew, ametoa hoja kwamba nchi za Asia ya Mashariki zimepata maendeleo ya haraka kwa sababu ya utamaduni wa kiasia unaothamini kuheshimu wakubwa, mshikamano ndani ya familia na nidhamu. Lee anadai kuwa mfumo wa demokrasia unaotoa uhuru kwa wananchi kuhoji maamuzi ya viongozi haujengi nidhamu ya kuendeleza uchumi. Nchi zinazokabiliwa na matatizo ya maendeleo zinahitaji serikali madhubuti zitakazosimamia kwa makini uhamasishaji wa ukusanyaji wa akiba na uwekezaji na kuhakikisha kuwa wafanyakazi wana nidhamu na hakuna migogoro ya migomo. Lee anaiona demokrasi ni kikwazo kwa maendeleo kwani inapunguza nidhamu na uwezo wa serikali kuhamasisha na kusimamia maendeleo. Ni kweli kwamba Singapore imeendelea haraka chini ya utawala ambao uliminya demokrasia na uhuru wa kisiasa.

 

Hata hivyo, nchi za Asia ya Mashariki ziliwapa wananchi uhuru wa kiuchumi. Vile vile kuna nchi kama Botswana ambayo imepata maendeleo ya haraka ya kiuchumi chini ya misingi ya demokrasia. Singapore iliibana demokrasia, lakini iliwapa wananchi wake uhuru wa kiuchumi na haki za kumiliki mali na kuweza kupata maendeleo makubwa ya kiuchumi. Nchi ambazo hazijajenga misingi imara ya demokrasia na utawala bora hukabiliwa na tishio la kusambaratika kiuchumi hata baada ya maendeleo ya miungo miwili au mitatu. Indonesia ambayo ilifanikiwa kupata maendeleo ya kiuchumi kwa muda wa miaka thelathini lakini ikasambaratika baada ya kukabiliwa na dharuba ya mgogoro wa fedha mwaka 1997 kwa sababu ya kukosa misingi ya demokrasia na utawala bora. Inawezekana kabisa kuunganisha sera nzuri za uchumi na demokrasia ya kweli. Maendeleo ya kiuchumi yanapatikana katika nchi yenye sera nzuri za uchumi zinazovutia uwekezaji na uchapaji kazi wenye tija ya juu na sio kwa vitisho vinavyowanyima uhuru na haki raia wa kawaida.

 

Mchango wa demokrasia katika maendeleo ya uchumi

 

Mfumo wa demokrasia unatoa msukumo wa maendeleo ya uchumi ya muda mrefu kwa kuhakikisha kuwa kuna utulivu wa kisiasa. Uongozi wa serikali unaopatikana kikatiba kupitia uchaguzi ulio huru na wa haki unajenga uhalali wa mfumo mzima wa utawala na serikali iliyoko madarakani. Mfumo wa demokrasia unaoambatana na utawala wa sheria na kuheshimu haki miliki unawapa imani wawekezaji, wafanyabiashara wabunifu, wafanyakazi na wakulima kuwa kipato cha halali hakitaporwa na dola au watu wengine.

 

Katika mfumo wa demokrasia serikali inakuwa na uwazi na inawajibika kwa wananchi kupitia Bunge. Vyombo vya habari vilivyo huru vinafuatilia vitendo vya serikali na kashfa zinafichuliwa hadharani. Matumizi mabaya ya fedha za umma hayafichiki. Ahadi za serikali katika utoaji wa huduma za jamii, ujenzi wa miundo mbinu kama vile barabara, bandari na mawasiliano unafuatiliwa. Serikali ambayo inashindwa kutimiza ahadi zake inaadhibiwa wakati wa uchaguzi. Kimsingi, mfumo wa demokrasia ni mzuri asilia kwani unalinda haki za binaadamu na kuwapa uhuru wananchi.

 

Pamoja na kulinda haki za binadamu mfumo wa demokrasia ni nyenzo ya kujenga uchumi na kukidhi mahitaji ya wananchi. Hakuna nchi iliyo huru na yenye mfumo wa demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari ambayo imepata kukumbwa na balaa la njaa lililosababisha raia kufariki kwa njaa. Serikali inalazimika kushughulikia tatizo la upungufu wa chakula hata katika nchi maskini kama vile India na kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata chakula kwani kama watu watakufa kwa njaa serikali itasakamwa na vyombo vya habari, taasisi zisizokuwa za kiserikali, vyama vya upinzani na wananchi kwa ujumla. Ikiwa serikali sio ya kidemokrasia tatizo la njaa linaweza kufichwa kwa sababu ni aibu kwa serikali. Katika miaka ya 1958 – 60 wakati wa sera za Great Leap Forward katika China ya Mwenyekiti Mao, kulitokea njaa kubwa sana katika nchi hiyo. China ilikuwa haina vyombo vya habari vilivyo huru au vyama vya upinzani. Serikali iliamua kuficha balaa hili la njaa na matokeo yake inasadikiwa watu milioni 30 walikufa kwa njaa. ukweli huu ulifahamika miaka ya ‘70 baada ya Deng kuingia madarakani.

 

Mfumo wa demokrasia ikiwa ni pamoja na kufanyika uchaguzi ulio huru na wa haki unaishinikiza serikali ifuatilie matatizo ya wananchi. Serikali za kiimla zinatafsiri kero za wananchi zenyewe bila kujali maoni ya wananchi. Minara na majengo ya kifahari, sherehe za kumbukumbu za utawala zaweza kutengewa kiasi kikubwa cha fedha wakati wananchi hawapati huduma bora za afya.

 

Ujenzi wa uchumi wa soko unahitaji uhimili wa serikali. Haitoshi kuwepo kwa sekta binafsi kuweza kuimarisha uchumi wa soko utakaoleta maendeleo kwa watu wote. Zaire ya Mobutu ilikuwa na uchumi wenye sekta binafsi lakini haukuwa uchumi endelevu. Uchumi wa soko unaoweza kuleta maendeleo kwa wengi unahitaji kuwepo kwa ushindani wa kibiashara na wote wanaoshiriki katika uchumi wanafuata taratibu na sheria zinazofanana. Huwezi kuwa na ushindani wa soko ikiwa kampuni ya ndugu wa Rais haifuati taratibu na sheria ambazo makampuni mengine wanapaswa kufuata.

 

Kazi ya serikali ni pamoja na kuweka sheria na taratibu ambazo zitaheshimiwa na wote na watakakiuka wataadhibiwa ipasavyo. Polisi na mahakama wafanye kazi kwa kufuata sheria na kutoa haki. Kama mahakama zimejawa rushwa au zinafanya kazi kwa upendeleo wa kisiasa itakuwa vigumu kujenga uchumi wa soko ulio imara na utakaoleta maendeleo kwa walio wengi. Kuheshimu haki miliki ni jambo la msingi katika kujenga uchumi endelevu. Nikilima mikarafuu, nisinyanganywe na serikali au majambazi. Kama nitanyang’anywa nitakosa motisha wa kuiangalia mikarafuu yangu.

 

Sekta binafsi haiwezi kutoa huduma zote zinazohitajiwa katika kukuza uchumi. Serikali inawajibika kujenga miundombinu kama vile barabara na bandari, kuweka taratibu nzuri za kusimamia utoaji wa huduma ya maji na umeme na kujenga mfumo mzuri wa kutoa elimu na huduma za afya za msingi kwa wote.

 

Ukosefu wa demokrasia na kuzorota kwa maendeleo Tanzania

 

Ukosefu wa demokrasi na uhuru wa kujadili na wa vyombo vya habari umechangia katika kuzorotesha maendeleo ya uchumi. Sera za kutaifisha makampuni na biashara zilitekelezwa bila kuwa na majadiliano ya kina kuhusu athari zake katika maendeleo ya nchi yetu. Utaifishaji ulizorotesha motisha wa kujiwekea akiba na kuwekeza vitega uchumi.

 

Sera ya ujamaa vijijini na operesheni Vijiji ziliwahamisha kwa nguvu raia walioko mashambani na wengi walivunjiwa nyumba na kupelekwa mbali ya mashamba yao, zilirudisha nyuma maendeleo ya kilimo vijijini. Kama nchi yetu ingekuwa na demokrasia ya kweli na uchaguzi ulio huru na wa haki serikali isingethubutu kuwahamisha raia kwa nguvu na kuwavunjia nyumba zao. Wanavijiji wangeishitaki serikali mahakamani na pia wangetumia kura zao kuiondoa serikali madarakani.

 

Serikali ilianzisha ukiritimba wa ununuzi wa mazao ya wakulima na kwa hiyo kuondoa ushindani katika soko la mazao ya wakulima. Wakulima walipata bei ndogo ya mazao yao. Serikali pia iliamua kuvunja vyama vya ushirika vya wakulima wenyewe na baadaye wakaanzisha vyama vya ushirika kama taasisi za chama tawala. Mali ya wakulima iliporwa na huduma kwa wakulima ikaporomoka.

 

Kama Tanzania ingekuwa na demokrasia, serikali isingetekeleza operesheni maduka iliyoendeshwa Tanzania bara katika miaka ya sabini. Maduka ya watu binafsi hasa vijijini yalifungwa na kuanzishwa maduka ya ushirika ya kijiji yaliyokuwa na ukiritimba wa hali ya juu. Sera hii ilipunguza biashara na kuchangia katika kuadimika kwa bidhaa muhimu na kuongezeka kwa biashara ya magendo. Kama tungekuwa na demokrasi sera hii ingepingwa na wananchi na isingetekelezwa. Sera ya serikali ya kubana biashara na kuanzisha mashirika yenye ukiritimba wa biashara za bidhaa muhimu kama vile shirika la Ugawaji ilisababisha kuongezeka kwa biashara za magendo. Badala ya kurahisisha masharti ya biashara, serikali iliamua kupambana na wafanya biashara. Wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati walikamatwa na kuwekwa ndani. Kuna baadhi wanakamatwa na carton moja ya sabuni au kilo tano za sukari na wakafungwa eti kwa sababu ya kuhujumu uchumi. Kwa kukosa demokrasia, sera za Serikali za biashara sio tu zimedidimiza uchumi bali pia zimevunja haki za binadamu za msingi za wafanya biashara wengi.

 

Kwa upande wa huduma za jamii, ukosefu wa demokrasia umechangia kuporomosha maendeleo ya elimu na afya. Miaka ya sitini serikali iliamua kutopanua elimu ya sekondari. Shule za mashirika ya dini zilitaifishwa. Ilikuwa vigumu kwa wazazi au taasisi zisizokuwa za kiserikali kupata kibali cha kuanzisha shule ya sekondari. Matokeo ya sera hii ni Tanzania kuwa ya mwisho duniani katika maendeleo ya elimu ya sekondari na vyuo vikuu.

 

Ubora wa elimu yetu umeshuka kwa sababu ya kusisitiza siasa badala ya utaalamu. Mipango ya kuimarisha elimu na huduma za jamii kwa utaratibu wa zima moto kama vile mpango wa upe, wa miaka ya sabini umechangia katika kuporomosha viwango vya Elimu.

 

Demokrasia sio uchaguzi huru na wa haki na kuheshimu matokeo ya uchaguzi. Nchi yenye demokasia inaheshimu haki za binadamu za raia wote na inalinda uhuru wa kusema na kujadili na kupeana taarifa. Wananchi wanaojielimisha kuhusu matatizo ya jamii yao wanakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kufanya maamuzi bora katika kuchagua viongozi na vyama vya siasa. Uhuru wa kujadili na kujenga hoja unaipa jamii uwezo wa kuchagua sera zilizo bora katika kjenga uchumi na kuboresha huduma za jamii.

 

Masuala ya Uchumi Katika Siasa

 

Masuala ya uchumi katika nchi zenye mfumo wa demokrasia ya kweli yanatawala mijadala na hoja zinazotumiwa na wananchi katika kuchagua Rais, Wabunge na vyama vitakavyoendesha nchi. Masuala muhimu ya uchumi ni pamoja na;-

 

(a)Ajira

 

Kwa kawaida serikali iliyoko madarakani huwa na wakati mgumu wa kuchaguliwa ikiwa katika kipindi chake cha uongozi ukosefu wa ajira utaongezeka. Rais George W. H. Bush (Baba yake Rais Bush wa sasa) alishindwa uchaguzi wa mwaka 1992 kwa sababu ya ongezeko la ukosefu wa ajira. Wengi walitegemea Rais Bush atashinda uchaguzi kirahisi baada ya Marekani kushinda vita vya Gulf na kuyaondoa majeshi ya Iraq toka Kuwait. Lakini ushindi wa vita dhidi ya Saadam Hussein haukutosha kumpa kura za kutosha kuchaguliwa tena kama Rais. Bill Clinton aliyesisitiza kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya kiuchumi ndie aliyeshinda uchaguzi 1992 na 1996. Rais Bush wa sasa pia atapata wakati mgumu katika uchaguzi wa mwaka 2004 ikiwa kutakuwa na ongezeko kubwa la ukosefu wa ajira.

(b)Kukua kwa mapato ya wananchi

 

Ongezeko la ajira kwa kawaida huambatana na ongezeko la mapato ya wananchi. Ikiwa ajira inakuwa na mishahara inaongezeka, serikali iliyoko madarakani huwa na nafasi nzuri ya kushinda uchaguzi.

 

(c)Sera za na Viwango vya kodi

 

Watu matajiri Marekani, hupendelea kodi za mapato ziwe za viwango vidogo. Matajiri wana uwezo mkubwa kwa sababu ya michango yao katika kampeni za wagombea. Pia Marekani watu wengi wenye umri wa kupiga kura hawafanyi hivyo. Wengi wasioshiriki kupiga kura ni raia wenye vipato vya chini. Marekani ina viwango vya chini vya kodi ukilinganisha na nchi za Ulaya Magharibi. Katika nchi ambako watu wengi wanashiriki katika kupiga kura viwango vya kodi ni endelevu. Matajiri wanalipa viwango vikubwa kuliko watu wenye vipato vidogo.

Huduma za jamii na hifadhi ya jamii

 

Katika nchi nyingi Serikali ina wajibu wa kutoa huduma za jamii ikiwa ni pamoja na elimu na tiba na huduma nyingine za afya. Ubora wa huduma za jamii ni suala muhimu katika chaguzi za nchi zenye mfumo wa demokrasia. Vile vile serikali imechukua jukumu la kutoa malipo ya uzeeni na malipo kwa watu wasiokuwa na ajira. Suala la hifadhi (social security) ya jamii ni nyeti katika medani ya siasa kwenye nchi zenye misingi mizuri ya demokrasia.

 

Lengo la kuwa na kodi zenye viwango vya chini na lengo la kutoa huduma za jamii na kujenga miundo mbinu iliyo imara inagongana. Utoaji wa huduma za jamii na za kiuchumi zilizo bora zinahitaji fedha. Bila kukusanya kodi ya kutosha sio rahisi kutoa huduma bora. Nchi ambazo wananchi wengi wanashiriki katika uchaguzi kama vile nchi za Scandinavia, mara kwa mara wamekua na huduma za jamii na kodi za juu. Marekani ambako utumiaji wa fedha katika chaguzi ni wa hali ya juu na wanaoshiriki katika uchaguzi ni nusu tu ya wapiga kura wote, viwango vya kodi vimepunguzwa na huduma za jamii ni hafifu.

Mfumko wa bei

 

Mfumko wa bei unaweza kuwa tatizo la kisiasa hasa katika nchi za Latin Amerika ambako kumekuwa na tatizo sugu la mfumko wa bei. Nchi kama Argentina mfumko wa bei ulifikia zaidi ya asilimia 3070 mwaka 1989. Kama kilo ya nyama iligharimu peso 1000 mwanzoni mwa 1989, kilo hiyo hiyo iligharimu zaidi ya peso 30,000/= mwishoni mwa 1989.

 

Mfumko wa bei ulikuwa tatizo la kisiasa. Rais Menem wa Argentina alichaguliwa kwa kuahidi kuwa atamaliza tatizo la mfumko wa bei kwa kuunganisha thamani ya fedha ya Argentina na thamani ya fedha ya Marekani. Reali I ya Argentina ikawa sawa na dolla moja ya Marekani. Baada ya kufanya hivyo mwanzoni mwa miaka ya tisini mfumko wa bei uliteremka toka zaidi ya asilimia 2300 mwaka 1990 mpaka kufikia asilima 4 mwaka 1994. Kati ya mwaka 1996 – 2001 Argentina haikuwa na ongezeko la bei. Hata hivyo mfumo huu uliiwezesha Argentina kukopa nje. Madeni ya serikali yakaongezeka kwa kasi na kuwa makubwa kiasi cha serikali kushindwa kulipa riba. Pia bidhaa za Argentina zimekuwa ghali katika masoko ya dunia ukilinganisha na nchi nyingine kama vile Brazil ambako sarafu yake haikuunganishwa na dola ya Marekani na imeshuka thamani. Serikali ya Argentina imeanguka kwa kushindwa kusimamia vizuri sera ya sarafu na fedha.

 

Maendeleo ya Demokrasia na Uchumi Tanzania

 

Kwa Tanzania maendeleo ya kiuchumi na kijamii yatategemea maendeleo ya demokrasia. Baada ya kuwa madarakani kwa muda wa miaka 40 Tanzania Bara, na Miaka 38 Zanzibar, CCM haina uwezo wa kujenga mazingira ya kuboresha uchumi, kuendeleza huduma za jamii hasa elimu na Afya na kulinda haki za binadamu. Kazi hiyo itakuwa ni jukumu ya Chama mbadala na kwa hivi sasa chama kinachowapa matumaini Watanzania ya kujenga nchi yenye haki sawa kwa wote na kuimarisha uchumi utakaokuwa na manufaa kwa wananchi wote sio kingine bali ni CUF Chama Cha Wananchi.

 

Chama chetu kitakuwa na kazi kubwa kwani tutarithi uozo wa CCM lakini pia wananchi watakuwa na kiu kubwa ya maendeleo. Itabidi chama kiwe makini na kujenga mazingira yatakayowezesha uchumi na ajira kuongezeka kwa kasi kubwa. Ili uchumi ukuwe kwa kasi kubwa ni muhimu uwekezaji wa raslimali na utumiaji wa maarifa katika utendaji wa kazi ushamiri. Itatulazimu tujenge mazingira yatakayowapa imani wawekezaji wa ndani na wa nje kuwa rasilimali yao haitaporwa na dola au majambazi. Sera zetu za kushamirisha uchumi wa Soko unaotabirika hazitabadilika kiholela. Tutakuwa na utawala unaofuata sheria na kuheshimu haki miliki. Rushwa itapigwa vita. Kazi kubwa ya serikali itakuwa kuweka miundo mbinu mizuri hasa barabara, bandari, nishati na kuimarisha huduma za afya na elimu.

 

Rushwa ni adui wa haki na maendeleo ya demokrasia. Rushwa pia ni adui wa maendeleo ya uchumi. Inaongeza gharama za kufanya biashara na inawakatisha tamaa wawekezaji waadilifu na kuwakumbatia matapeli. Chama chetu kina azima ya kujenga Demokrasia ya kweli Tanzania yote. Tujijengee uwezo ndani ya chama wa kupambana na rushwa, kwanza kwa kuhakikisha kuwa vitendo vya rushwa havijipenyezi ndani ya chama chetu. Pili kujenga uwezo wa kuyaelewa kwa kina mazingira yanayoashiria rushwa ndani ya dola. Ukiritimba na ukosefu wa uwazi katika maamuzi unashamirisha rushwa.

 

Utekelezaji wa Muafaka wa Zanzibar kama tulivyokubaliana tarehe 10 Oktoba 2001 ni muhimu katika ujenzi wa demokrasia. Ikiwa Muafaka utatekelezwa tutakuwa na nafasi nzuri ya kujenga mazingira ya kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuboresha huduma za jamii. Chama cha CUF kinawajibika kufafanua vizuri sera zake za uchumi na ustawi wa jamii na kuzijadili na wananchi kwa kujiandaa kwa chaguzi zijazo.

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s