Kuna mgogoro wa Kikatiba

Kwa bahati nzuri siku ya Alkhamis ya tarehe 3 Julai, 2008, Waziri Mkuu alitamka ndani ya Bunge hili kwamba Zanzibar sio nchi. Tarehe 9 Julai, 2008, Mhe. Iddi Pandu Hassan, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alisema katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kwamba Zanzibar ni nchi. Je, huu sio mgogoro wa kutosha wa kuonyesha haja ya kuwepo Mahakama ya Katiba? Na hili sio jambo la kusema litatatuliwa na tafsiri ambayo itatolewa kwa mashirikiano ya wanasheria wakuu wawili, yaani yule wa Zanzibar na wa Jamhuri ya Muungano, kwa sababu ni mgogoro wa kikatiba ambapo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza litatuliwe na Mahakama ya Katiba ya Tanzania. Vile vile jambo hili sio swali la kujadiliwa na CCM kama alivyotamka Mheshimiwa Waziri Mkuu katika Bunge lako tukufu, ikizingatiwa kuwa Tanzania siyo mali ya CCM wala ya wana CCM pekee.

Fatma Mussa Maghimbi, Mbunge wa Chake (CUF)

Fatma Mussa Maghimbi, Mbunge wa Chake (CUF)

Hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani-Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba , Mhe. Fatma Maghimbi (pichani) kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2008/2009

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika,

Kwa niaba ya Kambi ya Upinzani napenda kutoa maoni kuhusu bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2008/2009 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, kanuni ya 99 (7) toleo la mwaka 2007.

Kwanza, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa rehema kunipa afya njema na kuweza kusimama mbele yenu ili niweze kutoa maoni kwa niaba ya Kambi ya Upinzani kuhusu Wizara hii ya Katiba, Sheria na Utawala. Napenda pia kuendeleza shukrani zangu kwa wananchi wa Jimbo la Chake Chake kwa imani yao kwangu na mimi nawaahidi nitaendelea kuwatumikia kwa uadilifu mkubwa. Kwa umuhimu mkubwa sana napenda kumshukuru mume wangu Bwana Mussa Maghimbi kwa uvumilivu mkubwa alionao, wakati ninapokua katika shughuli za siasa.

Mheshimiwa Spika, pili napenda kuishukuru kambi ya upinzani kwa utendaji wake bora na ushirikiano unaoifanya kila leo ionekane kuwa imara na muhimu katika kupelekea utendaji bora wa serikali. Pia nahisi nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitatoa shukrani zangu za dhati kwa chama changu cha CUF kwa uongozi wake makini chini ya mwenyekiti wake Prof. IBRAHIM LIPUMBA na Katibu Mkuu wake Maalim SEIF SHARIF HAMAD na nia zao za kuwatetea Watanzania, ustawi na maendeleo ya taifa letu, naahidi kukilinda chama changu, kutetea na kupigania utekelezaji wa sera zake makini ili kuhakikisha haki sawa inapatikana kwa Watanzania wote popote walipo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa nitoe maoni ya kambi ya upinzani katika bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2008/2009 kama ifuatavyo:

1. HOJA YA KATIBA MPYA YA TANZANIA

Mheshimiwa Spika, moja ya kazi ya Kambi ya Upinzani ni kutoa maoni hasa ya kupendekeza marekebisho ya mambo ya msingi katika Serikali yetu na taifa kwa jumla.  Inapofikia mapendekezo ya kurekebisha jambo kubwa kama Katiba, Wizara ya Katiba na Sheria isipuuze kile tunachopendekeza. Katika hotuba yetu ya bajeti ya mwaka 2007/2008 nilipendekeza kupitia vipengele 12 haja ya kupata Katiba mpya, lakini hadi leo hii hakuna dalili ya mabadiliko yoyote. Naomba nikumbushe kwamba hoja ya kuwa na Katiba mpya si ya kambi ya Upinzani tu bali ni kilio cha Watanzania wote. Hii ni kwa sababu marekebisho 14 yaliyofanywa katika Katiba, hayatoshelezi kuleta maendeleo na wala mustakabali wa kitaifa.  Katiba imempa Rais Madaraka makubwa kupita kiasi. Kuna sehemu imebana utendaji kama ilivyojitokeza wakati tunapitisha sheria ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za za Serikali.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inashauri kuwa suala la  kuwa na Katiba mpya  ya Tanzania ni la msingi, haliepukiki kwa sasa na lisifumbiwe macho, hivyo basi Katiba mpya itungwe kwa kuwashirikisha wananchi wote kwa utaratibu utakaoandaliwa na pia kupitia vikundi mbali mbali vya kijamii, vyama vya siasa na viongozi wa kidini.

2. HOJA YA MGOMBEA BINAFSI WA URAISI

Mheshimiwa Spika, nchi yoyote inayopenda utulivu ni lazima iheshimu sheria, demokrasia ya kweli na Haki za Binadamu ikijumuisha kutoa haki za msingi za Raia. Tanzania inaonekana inayumba katika kuheshimu mambo hayo matatu. Suala la kuwa na mgombea binafsi ni la msingi, kilio cha muda mrefu na hatuwezi kulipuuza kwa sababu linaungwa mkono na Watanzania walio wengi. Mgombea binafsi inapaswa aruhusiwe katika ngazi zote za uchaguzi – yaani katika nafasi ya Urais, nafasi ya Ubunge na chaguzi za Serikali za Mitaa.

Hii ni kutokana na sababu zifuatazo:-

Haki ya kupiga kura au kupigiwa kura ni haki ya msingi kikatiba kwa kila Mtanzania. Hivyo kuwalazimisha watu kujiunga na vyama vya siasa ili wawe na haki ya kuchaguliwa itakuwa sawa na kuwanyima haki yao hiyo ya msingi.

Ni Watanzania wachache ambao ni wanachama wa vyama vya siasa.  Hivyo basi, kuwalazimisha watanzania kujiunga na vyama vya siasa inainyima Tanzania kupata viongozi wazuri ambao hawapendi kuwa katika vyama vya siasa.

Nchi nyingi duniani na hata za kiafrika kwa sasa zinaruhusu mgombea binafsi  kwa mfano Ghana, Namibia na Rwanda.  Kwa msingi huu haitakuwa suala jipya iwapo Tanzania nayo itaruhusu mgombea binafsi katika nafasi mbali mbali za uchaguzi.

Nikirejea ripoti iitwayo “Report of Short term Consultancy on Electoral Law and Procedure of Tanzania” ya mwaka 1995, iliyotolewa na Tume Maalum, iliyoongozwa na Prof. G. Mgongo Fimbo, (Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) uliyoiteua mwenyewe Mheshimiwa Spika, ukiwa Waziri wa Katiba na Sheria wakati huo, ililiangalia suala hili na kutoa mapendekezo yanayofaa na ya msingi kabisa kama yatafanyiwa kazi.

Katika ukurasa wa 12 wa ripoti hiyo ilipendekeza yafuatayo:-

Mabadiliko yanayofaa ya Katiba yafanywe ili kuruhusu Mgombea binafsi katika nafasi ya Urais, Ubunge na uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Mgombea binafsi asiwe mwanachama wa chama chochote kilichosajiliwa au kisichosajiliwa kwa mwaka mmoja kabla ya uchaguzi.

Mgombea binafsi katika nafasi ya Ubunge lazima aungwe mkono kwa kupata sahihi (signatures) za angalau asilimia tano (5%) ya wapiga kura katika jimbo – nusu wakiwa wanawake na nusu wakiwa wanaume.

Mgombea binafsi katika nafasi ya urais lazima aungwe mkono wa angalu asilimia 5 (tano) ya wapiga kura kutoka angalau mikoa kumi ya Tanzania bara na Mikoa miwili ya Zanzibar.

Je, Mheshimiwa Spika, mapendekezo haya yalifanyiwa kazi kwa kiasi gani?

Ili kuhakikisha haki ya msingi ya kuchagua na kuchaguliwa, hatuna budi kuruhusu mgombea binafsi.

Katiba ya Ghana, 1992, ibara ya 28(4) na Sheria ya Uchaguzi, 1993 kifungu cha 178 na 184 inaruhusu kuwepo mgombea binafsi.

Vile vile Katiba ya Namibia, ibara ya 28(4) na Sheria ya Uchaguzi 1992, kifungu cha 34 zinaruhusu suala la kuwa na mgombea binafsi.

Mahakama zetu pia zimeonyesha ukomavu wa hali ya juu kwa  kutengua vipengele, 39(1)(c) vya  Katiba ya Jamuhuri ya Muungano vinavyomlazimisha mtu kushiriki katika chaguzi mbali mbali kwa kupitia dhamana ya chama . Inasikitisha kuona kwamba  serikali badala ya kutekeleza hatua hii muhimu ya upanuzi wa demokrasia katika nchi yetu imeamua kukata rufaa.

Kambi ya Upinzani inaamini  kwamba rufaa hii ni mkakati wa dhahiri wa kuchelewesha mabadiliko haya muhimu ya kikatiba.

3. MPANGO WA MABORESHO/MAREKEBISHO YA SEKTA YA SHERIA [LEGAL SECTOR REFORM PROGRAMME]

Mheshimiwa Spika, zipo sekta mbali mbali za umma nchini ambazo kwa makusudi serikali imekuwa ikizifanyia maboresho ili ziweze kutoa huduma bora kwa jamii. Miongoni mwao ni sekta ya afya, kilimo, maji na hata sekta ya sheria. Masikitiko yangu yapo katika Maboresho ya sekta ya sheria. Maboresho haya yamekuwa yakifanywa kwa kasi ndogo na hayaendelei. Mpango wa maboresho ya sekta ya sheria ni muhimu sana katika kuhakikisha utawala bora, utoaji na upatikanaji wa haki kwa wakati, hifadhi ya haki za binadamu na mfumo bora wa uchumi kwani sekta ya sheria kimsingi ni sekta kiongozi katika taifa lolote lile kwa kuwa ni sekta mtambuka na utendaji kazi wa sekta zote unategemea sheria nzuri na mfumo mzima wa utoaji haki.

Mheshimiwa Spika, katika utafiti wangu nimegundua kuwa maboresho ya sekta hii yanakabiliwa na matatizo mengi ikiwemo sera yake kutozingatiwa ipasavyo, kutokuwepo utaratibu maalum wa kufadhili maboresho, lakini hasa tatizo ni matumizi ya World Bank Procurement Regulations and Procedures. ‘Procedures’ hizi hupelekea kuwepo  mlolongo mrefu na ukosefu wa  uwazi.

Mheshimiwa Spika, kuna mkanganyiko juu ya taratibu sahihi za kufuatwa baina  ya  zile za  Benki ya Dunia (kama ilivyoelezwa hapo juu) na zile za Public Procurement Act, 2004. Hili pia linapelekea utekelezaji wa mpango huu kutokuwa na ufanisi kwani ni wazi kuwa “faster procurement leads to faster programme implementation”. Hali hii inaonesha kuwepo utegemezi uliokithiri wa taratibu za Benki ya Dunia jambo ambalo sio muhimu kwani hata hizo World Bank Procurement Guide lines zinaonesha ni manunuzi gani yanatakiwa yafuate taratibu hizo na yepi yasifuate taratibu hizi. Mfano kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004, chini ya kifungu cha 4(1)(a) and (b) Serikali inatakiwa kuzingatia matakwa ya mkataba au makubaliano kati yake na taasisi za fedha, nchi wahisani au washirika wa maendeleo iwapo Sheria ya Manunuzi ya Umma ya  Tanzania inakinzana na mkataba husika.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo kifungu hiki pamoja na 4(1) (b) vinaeleza kuwa kwa hali yoyote manunuzi yatafanywa au yataendeshwa kwa kuzingatia sheria hii ya Tanzania ingawa hakikuonyesha kuhusiana na mikopo na credit agreements ya aina hii ambayo Tanzania imeingia na World Bank katika kuendeleza sekta hii.

Mheshmiwa Spika, tatizo jingine la msingi ni kutokuwepo uwazi juu ya nafasi ya vyombo vya manunuzi vya serikali. Hili linapelekea mkanganyiko, ucheleweshaji wa manunuzi na kuhusisha mamlaka mbali mbali ikiwemo bodi za zabuni za Wizara. Mfano inatokea baadhi ya wakati nyaraka za manunuzi ambazo zinatangaza zabuni zinakubalika na bodi ya zabuni ya Serikali lakini zinakataliwa na Benki ya Dunia, jee hii ina maana kwamba bodi hizi za zabuni ni kwa ajili ya rubber stamping maamuzi ya manunuzi tu? Na hii inaonesha kuwa Ministerial Tender Boards hazina nafasi yoyote katika hili.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali ichukue hatua za makusudi na haraka kuhakikisha kwamba mpango huu unakuwa na ufanisi na lengo la kuasisiwa kwake linafikiwa. Kama tatizo linatokana na Sheria yetu ya Manunuzi ya Umma ni muhimu irekebishwe ili mipango na miradi yetu isishindwe kuendelea kwasababu ya kuingiliwa kati na taratibu za taasisi za fedha, nchi wahisani au washirika wa kimaendeleo kutokana na kutupatia kwao mikopo na ruzuku. Ni kweli sisi maskini lakini umaskini wetu usiwe sababu ya kupangiwa kila kitu na kushindwa kutekeleza sera na mipango yetu ipasavyo.

4. MAHAKAMA YA KADHI

Mheshimiwa Spika, Suala la uanzishaji wa Mahakama ya Kadhi ni jambo la msingi na lisiloepukika kwa sasa. Ilani ya Chama Cha Mapinduzi iliona umuhimu wa Mahakama hiyo. Hii ni kwa sababu kutokuwepo kwa Mahakama hiyo ni kikwazo katika utatuzi wa masuala ya msingi yanayowahusu waislam. Utetezi wa Mahakama hii ni kutokana na msingi kwamba kuna uthibitisho wa wazi kwamba yapo mambo maalum yanahitaji kuwepo na kushughulikiwa na Mahakama Maalum.

Mfano:  Kwa sasa kuna Mahakama za biashara, mahakama za ardhi, mahakama za kazi, hivyo Mahakama ya Kadhi itakuwa ni sawa na kuwa na Mahakama maalum kama hizo nilizozitaja.

Mheshimiwa Spika, Msingi mwingine pia ni kuwa Mahakama ya Kadhi kwa Tanzania sio suala la kuianzisha bali itakuwa ni kuirudisha tu baada ya kuondolewa kwa muda kwani ilikuwepo hata kipindi cha ukoloni.

Kuna hoja mbalimbali zinazotolewa kupinga kuwepo kwa Mahakama ya Kadhi miongoni mwa Watanzania. Baadhi ya hoja hizo ni:-

Kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi kwa kutumia sheria ya Bunge itakuwa ni kuvunja au kwenda kinyume na Katiba ya nchi. Hii hutetewa kwa maelezo kuwa Serikali ya Tanzania haina dini, hivyo kuwepo mahakama hiyo itakuwa inakwenda kinyume na vifungu 107A, 3, 9, (a) (f) na (h), 13 na 19 vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambavyo vinapinga na vinazuia kuanzishwa kwa chombo chochote cha Sheria chenye misingi ya kibaguzi. Tafsiri ya vifungu hivi inayotolewa kutetea hoja hii si sahihi kwasababu, ni kweli Serikali haina dini lakini raia au wananchi wana dini zao na wanaruhusiwa kuabudu na kufanya mambo yao kwa mujibu wa misingi ya dini zao.

Hoja hii ni dhaifu, kwa msingi kwamba nchi nyingine jirani na za kiafrika zina Mahakama ya Kadhi kwa muda mrefu sasa na mahakama hizo hazijaleta udini. Mfano:  Kenya, Rwanda na Uganda.  Na hata Tanzania ilipokuwepo Mahakama hiyo, hapakuwa na Ubaguzi wowote.

Kwa mfano:  Sheria ya Ndoa ya Tanzania ya mwaka 1971, inaeleza wazi kwamba ndoa zifungwe kwa kutumia au kufuata misingi na taratibu za sheria za Kiislam, Kikristo, Kimila au Kiserikali;

Vile vile talaka zinatolewa au zinathibitishwa na Mahakama nchini lakini baada ya kupitia BAKWATA au Mabaraza ya Makanisa.

Kimsingi, Mahakama ya Kadhi haitakuwa inavunja katiba kwa sababu mahakama hiyo itaanzishwa kwa kufuata sheria, itatumia Sheria za nchi zikiwemo Sheria za Kiislamu ambazo zinaruhusiwa kutumika kama inavyosemaJALA/Judicature and Application of Laws Act, Cap. 358 2002, Section 2 na chini ya Sheria ya Mwenendo wa Madai ya

Mahakama za Mwanzo

Mfano halisi ni mfumo wa mahakama hizo uliopo Zanzibar chini ya Kadhi’s Court Act, 1985 katika kifungu cha sita kinatoa wazi mamlaka ya Mahakama hizo ambayo ni mambo yanayohusu ndoa, talaka, mirathi na matunzo ya watoto katika kesi ambazo wahusika wote ni waislam, na walioowana kwa mila na desturi za Kiislam.

Mheshimiwa Spika, Wakati wa kuwa na mahakama hiyo umefika na hoja zote za kuipinga hazina msingi, hivyo hatua za haraka zichukuliwe ili kuhakikisha Mahakama hiyo inaanzishwa haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba CCM ilizunguka nchi nzima katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 ikiomba kura, kwa ahadi kwamba itairudisha Mahakama ya Kazi. Kura wakazipata, ni jukumu lao sasa kutekeleza kile walichokiahidi.

5. CHAGUZI ZA SERIKALI ZA MITAA

Mheshimiwa Spika, Chaguzi za Serikali za Mitaa kuendeshwa na kusimamiwa na TAMISEMI badala ya Tume ya Taifa ya uchaguzi ni kukejeli demokrasia na mifano hai tumekwisha kuitoa mara kadhaa, mathalan barua ya Mkuruenzi wa Manispaa ya Singida Bernadett Kinabo kwa Watendaji na WEO wote, ya 2005 akiwaonya “Watendaji wasishirikiane kwa namna yoyote ile na Kambi ya Upinzani vinginevyo watachukuliwa hatua za kinidhamu”.

Katiba yetu inatuongoza katika misingi ya demokrasia na Utawala wa Sheria. Lakini chaguzi hizo kwa hivi sasa haziko huru na haki haitendeki. Tukiangalia Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa (The Local Government Election Act, cap 292) ambayo inaweka mazingira ya uchaguzi kuendeshwa na kusimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ni sawa kabisa kuiruhusu Serikali kuwa Mchezaji na Muamuzi (rifarii) kwa wakati mmoja katika uwanja wa Mapambano.

Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa majibu kwa nini Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa isifutwe na chaguzi hizo zisiendeshwe na Tume  ya Taifa ya Uchaguzi katika mazingira hayo? Wakurugenzi wanajipa mamlaka ya kufuta matokeo ya uchaguzi pasipo kuwa na  mamlaka. TAMISEMI inajulishwa haichukui hatua! Ni chaguzi gani hizi zinazofuata matakwa ya mtu mmoja mmoja? Je kwa mtindo huu Tanzania itajiita kweli ni nchi inayofuata “utawala wa sheria”? Japo swala hili liko chini ya TAMISEMI, lakini kinachovunjwa ni Sheria ya Nchi.

6. SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

Mheshimiwa Spika, Msingi mkuu wa demokrasia  na utawala bora duniani ni kuwa na serikali inayowajibika kwa wananchi na viongozi  wanaowatumikia wananchi kwa uadilifu katika kuwapatia maendeleo na maisha bora. Hii ni kwa sababu uongozi ni dhamana na madaraka yanapaswa kutumiwa kwa manufaa ya wananchi wote na sio maslahi ya watu binafsi au kikundi fulani cha watu.

Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu litakubaliana na mimi kwamba hiki ni chombo muhimu sana katika kuhakikisha utawala bora. Hii ni kwasababu chombo hiki kina mamlaka ya kisheria chini ya ibara ya 132 ya Katiba.  Kazi yake ni kuchunguza tabia na mwenendo wa kiongozi yeyote wa umma ili kuhakikisha maadili ya viongozi wa umma hayakiukwi ikiwemo kuepusha kiongozi kuweka maslahi binafsi mbele.  Pia chini ya kifungu cha 18 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, yaani (The Public Leadership Code of Ethics Act, cap 398) sekretarieti hii imepewa mamlaka ya kuanzisha na kuendesha uchunguzi juu ya ukiukwaji wa maadili ya viongozi, lakini kama kawaida Tanzania huwa inaanzisha kitu kizuri lakini hakiwezeshwi wala hakipewi nafasi kufanya kazi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, Kutokana na malalamiko na matukio ya ufisadi dhidi ya viongozi wakubwa hapa nchini, Kambi ya upinzani inaitaka serikali itueleze kama sekretarieti hii iko hai au imekufa. Na je Kiongozi anapokiuka Maadili, inatosha kwa kiongozi huyo kujiuzulu kutoka nafasi moja na kubaki katika nafasi nyingine?

Na je sekretarieti hii inasimamiaje utekelezaji wa sheria hii?  Kambi ya Upinzani inaomba ijue idadi ya viongozi waliokwishatiwa hatiani na Sheria hii.  Au tokea Sekretarieti hii iundwe hakuna kiongozi aliyekosa Maadili? Jee, sote tuko safi?

Mheshimiwa Spika, Moja ya masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni viongozi hao kutoa au kuwasilisha tamko rasmi la maandishi linaloorodhesha mali na rasilimali zake; jee ni kwa kiasi gani viongozi wanatekeleza hili? Kwa mujibu wa gazeti la THIS DAY, toleo la tarehe 3 Julai 2008, inaelezwa kuwa hata hapa Bungeni baadhi ya Wabunge na Mawaziri hawajazi fomu au wanajaza kwa kuchelewa muda maalum uliowekwa. Kambi ya Upinzani inaomba kujua kuna ukweli gani kuhusu taarifa hiyo, na kama ni kweli Waheshimiwa hao wapo juu ya sheria (above law)?

Mheshimiwa Spika, Pamoja na hayo yote Sekretarieti hii inafanya kazi katika mazingira magumu sana.  Serikali imeipuuza na kuifanya isiweze kufanya kazi ipasavyo.  Hivi sasa ina upungufu mkubwa wa wafanyakazi ambapo kwa mwaka 2005/2006 ilikuwa na wafanyakazi 55 na  mwaka 2007/2008 wanao wafanyakazi 115  ambao ni wastani wa wafanyakazi 10 kila Kanda, (Kanda maana yake ni mikoa 3) idadi hii haiwezi kupelekea chombo hiki kufanya kazi ya kuridhisha.

Mheshimiwa Spika, Tunashuhudia idadi ya viongozi inavyoongezeka nchi nzima.  Hivyo ofisi hii bila kuwezeshwa ili iweze kuwafuata viongozi nchi nzima, ufanisi utakuwa mdogo sana.  Hivi sasa Sekretarieti imeanza kufanya Random Check kwa baadhi ya viongozi nchi nzima hata mimi nilipata barua kuwa watakuja lakini sijawaona.

Mheshimiwa Spika, Ukaguzi wa aina hii utasaidia sana kwa viongozi kuogopa kukiuka maadili na forms zitajazwa kwa ukweli. Rais Kikwete katika hotuba yake ya kuzindua Bunge Desemba, 2005 aliiomba Sekretarieti ieleze jamii kuhusu matamko ya viongozi na yahakikishwe kwamba matamko hayo ni ya kweli lakini hadi hii leo hilo halijafanyika.

Kambi ya Upinzani inaomba kujua kwanini hilo halijafanyika.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inashauri kuwa sekretarieti hii ifanye majukumu yake ipasavyo na isisite kuchukua hatua zinazofaa kwa wale wote wanaokiuka Maadili ya Viongozi wa Umma kama Rais Kikwete alivyoagiza.

7. RITA (Registration, Insolvency and Trusteeship Agency)

Mheshimiwa Spika, Wakala huu kwa sasa umeshakuwa na mtandao mzuri katika kusajili na kutoa vyeti vya vizazi na vifo nchini, kwa mantiki hii inaonekana kuwa ni chombo pekee kinachoweza kutoa takwimu bora na sahihi zaidi za watanzania. Kwa msingi huo basi wakala huu unaweza kupewa uwezo ili ihusike moja kwa moja katika utoaji wa vitambulisho vya uraia (National Identities), hati za kusafiria (Passport) na kurekebisha daftari la wapiga kura (Register of Voters).

Inasikitisha kuona hati za kusafiria zinatolewa na Idara ya UHAMIAJI, daftari la wapiga kura linatolewa na Idara OFISI YA WAZIRI MKUU, Vitambulisho vya Uraia vinatolewa na wakala mpya. Na ni vyeti vya kuzaliwa na vifo tuu ndio vinatolewa na RITA, wakati Habari zote za kupata Passport, kurekebisha daftari la Wapiga kura zinapatikana Ofisi ya RITA. Ni kwanini Tanzania tusiwe na utaratibu mzuri wa kuhuisha mambo, hata pale uhuishaji huo unapokuwa na manufaa makubwa kwa Taifa?

Mheshimiwa Spika, Hali hii inaashiria matumizi mabaya ya rasilimali za taifa na inapelekea mlolongo mrefu na usumbufu usio wa lazima. Kambi ya upinzani inaitaka Serikali kuangalia upya maamuzi yake yasiyo na tija kwa Taifa na kuifanya RITA kuwa ndio wakala pekee kupewa majukumu yaliyoainishwa hapo juu jambo litakalo leta tija katika nyanja zote za matumizi ya rasillimali za walipa kodi.

8. SHERIA YA ADOPTION (The Adoption of Children Act, cap 335 R.E 2002)

Mheshimiwa Spika, Hii ni sheria muhimu sana katika kuhakikisha maendeleo na ustawi wa mtoto lakini utaratibu uliowekwa na Sheria hii ni kikwazo katika kuhakikisha  mtoto anapata  wazazi kwa haraka. Hii ni kwa sababu inaweka mlolongo mrefu wa kupatikana amri ya ‘adoption’ kwani ni Mahakama Kuu pekee ndio imepewa mamlaka ya kusikiliza mashauri ya adoption na kutoa maamuzi. Urasimu ulioko unatisha.Tunasikia sababu ni kwamba Serikali inaogopa “Human Traffiking” lakini mtu mpaka akienda Mahakamani basi ni dhahiri huyo kwa kiwango kikubwa ana nia njema na mtoto huyo.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapendekeza kuwa Mahakama za chini kama vile za Wilaya na za Hakimu Mkazi zipewe mamlaka ya kusikiliza na kutoa maamuzi ya adoption ili kurahisisha mtoto kupata wazazi haraka. Mfumo huu pia ndio unaotumika katika nchi nyingi kwa sasa hata majirani zetu Kenya na Uganda wameteremsha Adoption kusikilizwa na Mahakama za Chini ili kurahisisha mtoto apate wazazi. Inasikitisha kwa Tanzania kuona shauri la adoption linachukua miaka 2 hadi 3 kabla halijamalizika na kutolewa maamuzi. Tuwaonee huruma hasa.

9. UMUHIMU WA KUWA NA MAHAKAMA MAALUM YA KATIBA {CONSTITUTIONAL COURT}

Mheshimiwa Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka Mahakama Maalum ya Katiba katika mfumo wa mahakama nchini.  Kambi ya Upinzani inataka kufahamu Mahakama hii  imekwisha kufanya Vikao mara ngapi na kuamua mambo mangapi  tangu ilipoanzishwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano na ni mambo gani yameshughulikiwa hadi leo? Au ndiyo kusema hapajawahi kutokea jambo lililohitaji Tafsiri ya Mahakama hii tangu Mwuungano ulipoanza?

Mheshimiwa Spika, Vile vile inashangaza kuona Katiba yetu inatoa mamlaka finyu sana kwa mahakama hii kwa kule kuipa uwezo wa kushughulikia migogoro ya kikatiba kwa jambo ambalo litabishaniwa baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tu.  Nchi nyingi duniani zina Mahakama za Katiba ambazo mara nyingi huwa ndizo za juu kabisa hasa katika mambo yote ya kikatiba.

Mfano, Afrika ya Kusini chini ya kifungu cha 166 na 167(3) vya Katiba ya nchi hiyo inaweka Mahakama ya Katiba kuwa ndiyo ya juu katika matatizo yote ya Katiba.  Ni mahakama ya kudumu na ina majaji wa kudumu.  Vile vile mahakama hii ipo nchini Ghana, Zambia, Kenya na sio katika mfumo kama huu wa Tanzania. Je jinsi kila kukicha kunapotokea mambo yanayohitaji ufafanuzi na au tofauti za tafsiri hadi watu wanataka kuandamana, si jambo jema iwapo Mahakama hii ikawa sasa ya kudumu na ikashughulikia migogoro hii kabla haijawa kubwa.

Mheshimiwa Spika, Kwa bahati nzuri siku ya Alhamisi ya tarehe 3 Julai 2008, Waziri Mkuu alitamka ndani ya Bunge hili kwamba Zanzibar sio nchi. Tarehe 9 Julai 2008, Mhe. IDDI PANDU HASSAN, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alisema katika BARAZA LA WAWAKILISHI LA ZANZIBAR kwamba Zanzibar ni nchi. Jee huu sio mgogoro wa kutosha wa kuonyesha haja ya kuwepo Mahakama ya Katiba. Na hili sio jambo la kusema litatatuliwa na tafsiri ambayo itatolewa kwa mashirikiano ya Wanasheria Wakuu wawili yaani yule wa Zanzibar na wa Jamhuri ya Muungano kwasababu ni mgogoro wa kikatiba ambapo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza litatuliwe na Mahakama ya Katiba ya Tanzania. Vile vile jambo hili sio swali la kujadiliwa na CCM kama alivyotamka Mheshimiwa Waziri Mkuu katika Bunge lako Tukufu, ikizingatiwa kuwa Tanzania siyo mali ya CCM wala ya wana CCM pekee.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona kwamba kuna haja ya kuboresha Mahakama hii ili iwe ya juu katika mfumo wetu wa mahakama nchini ili ishughulikie na kutafsiri mambo ya msingi ya kikatiba yanayohusu taifa la Tanzania. Hivi sasa kuna mambo ya msingi yanayohitaji Mahakama ya Katiba. Mfano:

(a)        Tafsiri ya Mambo ya Muungano/Zanzibar ni Nchi

(b)        Suala la Mahakama ya Kadhi.

(c)        Suala la Zanzibar kujiunga na OIC ambalo lilipata kusikilizwa na kuamuliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania katika kesi ya MWALIMU JOHN PAUL MUHOZYA .V. MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI.

10. MATUMIZI MABAYA YA SHERIA

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaomba kujua hatua aliyochukuliwa yule Mgambo wa jimbo la Solwa, Shinyanga vijijini, aliyemuweka Mama Mjamzito katika Selo pamoja na wanaume na akajifungua ndani ya Selo hiyo eti kwa sababu mumewe hajalipa kodi. Kashfa hiyo ilitajwa hapa Bungeni na Mheshimiwa Ania Chaurembo tarehe 24/6/2008.

Mheshimiwa Spika, nawaomba wanawake wenzangu ambao ni wanaharakati wa kutetea haki za mwanamke walifuatilie swala hilo kwa kushirikiana na Tume ya Haki za Binadamu.

Pia Mheshimiwa Spika, naamini kwamba Waziri Mkuu, Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Katiba na Sheria pamoja na wewe Mheshimiwa Spika tukishirikiana na Wanasheria wenzetu waliomo humu Bungeni, na waliko nje ya Bunge hili hatutalipuuza jambo hili.

11. LAW SCHOOL OF TANZANIA

Mheshimiwa Spika, Mwaka jana Waziri wa Katiba na Sheria alikiri upungufu wa Wanasheria nchini.  Tukategemea kuanzishwa kwa law school  kutaongeza wanasheria lakini lakini sheria inayoanzisha LAW SCHOOL OF TANZANIA ya mwaka 2007 inazidi kuchochea kuendelea kwa upungufu huo ingawa ilisemwa kuwa lengo la kuanzishwa kwake ni kuboresha sekta ya sheria kwa kuwapatia wanasheria wa hapa nchini mafunzo bora ya vitendo yanayoendana na mazingira ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, Hii ni kwasababu sheria hii inapiga marufuku kwa wahitimu wa shahada ya kwanza ya sheria kutoka Vyuo Vikuu mbali mbali nchini kutoajiriwa katika taasisi za umma kabla hawajapata mafunzo ya mwaka mmoja kutoka Law School.  Lengo la kupata Wanasheria wengi halitafikiwa endapo sharti la kupata ajira ni lazima kupita Law school kwa sababu:-

Hivi sasa hakuna Law School inayoweza kuchukua wahitimu wa shahada ya sheria kutoka vitivo 10 vya sheria vilivyopo Tanzania na kupata mafunzo hayo kwa wakati mmoja.

Bodi ya Mikopo inaondoa uwezekano wa wanafunzi hao kupewa mikopo kutokana na nature ya mafunzo hayo.

Law School yenyewe mpaka sasa haina majengo yake inatumia majengo ya UDSM ambapo haiwezi kuchukua idadi kubwa ya wanafunzi wanaozidi mia tano (500).

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona hili ni tatizo katika taasisi hii muhimu nchini na inapendekeza yafuatayo yafanyike:

(a)        Mfumo wa Law School uliopo sasa ubadilishwe na kila Chuo Kikuu kinachotoa shahada ya sheria kiendeshe mafunzo haya na baadae kuwe na mtihani wa pamoja wa Law School kwa wanafunzi wote

b. Mafunzo ya law school yawe ni sehemu ya mafunzo ya shahada ya kwanza na gharama zake zitolewe kama sehemu ya gharama za shahada ya kwanza na ziwe chini ya bajeti ya Wizara ya Sheria na Katiba.

(c)  Serikali iboreshe miundombinu ya Chuo cha Mahakimu cha Lushoto na kitumike kama sehemu ya kuendeshea mafunzo hayo.

(d)    Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ifanyiwe marekebisho ili kuruhusu wanafunzi wa Taasisi hiyo wapate mikopo.

12. HUKUMU YA KIFO

Mheshimiwa Spika, Suala la kuwepo na utekelezaji wa hukumu ya kifo lina upinzani mkubwa duniani na nchi nyingi zimefuta adhabu hiyo, bado Tanzania inabaki katika mfumo wa adhabu ya kifo kwa kunyongwa.

Mheshimiwa Spika; Kuendelea kubaki na adhabu ya kifo karibu tutabaki kama Kisiwa, na nchi zipatazo 133 zimeshafuta hukumu ya kifo.  Hivi sasa bado nchi 64 tu ambazo hazijafuta adhabu hiyo, Tanzania ikiwa mojawapo ya nchi hizo.

Kambi ya Upinzani, inapendekeza sheria hii ifutwe kwa sababu:

  • adhabu ya kifo si adhabu ya kibinadamu.
  • hakuna uthibitisho kuwa adhabu ya kifo inasaidia kupunguza makosa ya jinai katika jamii kwani inaonekana pamoja na kuwepo kwa adhabu hiyo idadi ya kesi za mauaji haziwapungui.

Mheshimiwa Spika, wataalamu wanasema, naomba kunukuu:-

“Adhabu ya Kifo sio nzuri kwa sababu mtu atakaetoa hukumu ya kifo na yule atakaelekeza hukumu hiyo wote nao watakuwa wamefanya kosa la mauaji.  Na mkosaji hatakuwa amejifunza chochote kwani atakuwa ameshakufa”

Mheshimiwa Spika, Tanzania kwa miaka 13 iliyopita hakujatekelezwa hukumu ya kifo na zaidi ya watu 400 walikaa wakisubiri adhabu hiyo.  Katika Utawala wa Mheshimiwa Rais Mkapa hakusaini utekelezaji wa hukumu yoyote ya kifo. Na mwaka 2002 alibadilisha hukumu za watu 100 ambao walihukumiwa kifo akawapunguzia adhabu hiyo ili wapate vifungo vya maisha na kufanya idadi ya hukumu za kifo 500 zilizobadilishwa kuwa vifungo vya maisha katika kipindi cha utawala wake. Inaelezwa hata katika utawala wa Rais ALI HASSAN MWINYI alisaini utekelezwaji wa hukumu ya kifo kwa watu/wafungwa 21 tu ambao walinyongwa mwaka 1994. (Source: Sunday News 15 July 2008, Ukurasa wa 8).

Mheshimiwa Spika, Hata Marais wamegundua kuwa hukumu ya kifo imepitwa na wakati. Sasa hebu tumpunguzie Rais kazi ambayo kimsingi sio ya kwake, yaani kutengua hukumu na kuweka kifungo cha maisha, Waziri alitueleza kwamba yapo majadiliano ya kina yanayoendelea ya kufuta hukumu ya kifo, lakini huenda yakachukua hata miaka 20.

Mheshimiwa Spika, Naomba nilikumbushe Bunge lako Tukufu kwamba adhabu ya Kifo ambayo imo katika “Kanuni ya Adhabu” na pia imo chini ya “Sheria ya Usalama wa Taifa” ni kati ya zile sheria 40 ambazo Tume ya Nyalali (Mungu amlaze pema) ilipendekeza zifutwe, ni adhabu ambayo hamfaidii aliyeua, aliyeuliwa wala haisaidii Serikali kuondoa kosa kama hilo kutokea.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2006 ulifanywa utafiti kuhusu adhabu ya kifo, asilimia 68 ya waliohojiwa waliipinga hukumu hiyo. Pia Mahakama za Tanzania katika kesi mbali mbali ilishaamua kuwa hukumu ya kifo ni mbaya. Jee, tunasubiri Mitume iteremke ije kufuta hukumu hii?

13. MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA MAHAKAMA

Mheshimiwa Spika, katika nchi nyingi duniani teknojia ya ICT hutumika hata katika kuendesha mashauri ikiwemo kutafuta na kupokea ushahidi, lakini kwa Tanzania hili linaonekana ni gumu. Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa AGUSTINO RAMADHAN alinukuliwa katika makala moja inayoitwa ’TECHNOLOGICAL ADVANCEMENT TO STREAMLINE THE JUDICIARY’ akisema matumizi ya ICT katika utoaji haki (administration of justce) bado yapo katika hatua za chini na inapaswa kuangaliwa kwa makini.

Mheshimiwa Spika, naomba ninukuu maneno ya ADISH AGGRAWAL (the President of International Council of Jurists and Chairman of all India Bar Associations) alisema: ‘judicial system need to be well equipped with new technological know how to deliver better services to the public. These new technologies offer opportunities for judicial system to render justice more accessible, transparent and effective’

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani ina kiu ya kuona Mahakama zetu zinafanya mabadiliko ya haraka.

14. MLIPUKO WA MAUAJI YA MAALBINO NA VIKONGWE

Mheshimiwa Spika, ni muda mrefu sasa vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti juu ya taarifa za kuuwawa kwa makundi fulani ya wanajamii kama vile maalbino na vikongwe. Siku ya tarehe 3/7/2008 Mheshimiwa Mbunge wa Tandahimba alieleza wakati akiuliza swali kwa Waziri Mkuu kuwa kumezuka aina nyingine ya mauaji ya wanawake kwa kukatwa makoromeo. Hii inaonesha jinsi watu wasivyoheshimu sheria za nchi na kutothamini maisha ya watu wengine. Sina hakika kuwa Wizara ya Katiba na Sheria kupitia taasisi zake imeifuatilia kadhia hii.  Kambi ya Upinzani inaomba kupata Takwimu kamili ya watu waliopoteza maisha yao.

Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze Waziri Mkuu pale aliposema atalichukulia swali hili uzito unaostahili.

Pia Kambi ya Upinzani inaiomba Wizara ya Katiba na Sheria iwachukulie hatua za hasira (Drastic Measures) wale wanaohusika na mauaji hayo.

MWISHO

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa narudia shukrani zangu za dhati kwa kupata fursa hii. Pia nawashukuru waheshimiwa wabunge na watu wengine wote kwa kunisikiliza.

Na kwa heshima na taadhima naomba kuwasilisha.

Ahsanteni sana.

Fatma Maghimbi (Mb)

MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI

WIZARA YA SHERIA NA MAMBO YA KATIBA

13 Agosti, 2008

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s