Tunataka kujuwa moja tu, Meremeta ni ya nani?

Kauli ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuwa MEREMETA ni ya jeshi na haiwezi kutolewa maelezo Bungeni kwani ni kutoa siri za Jeshi, hivyo kuhatarisha usalama wa nchi, ni majibu ya kushangaza. Wanahisa wa MEREMETA ni wageni na hivyo siri za jeshi ni salama kwa wageni kuliko wabunge au Bunge lako? Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe majibu sahihi na sio kutoa majibu ya kisiasa tu. Kambi ya Upinzani imekwisha kusema iwapo kuna jambo kweli la siri basi liwasilishwe kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge au Kamati ya Uongozi. Lakini kauli kuwa Serikali haiwezi kusema lolote haiwezi kamwe kukubalika na Bunge hili. Bunge linapaswa kusimamia hata jeshi kwa mambo yasiyohusu mikakati ya kijeshi. Dhahabu ni biashara na hakuna siri ya kibiashara kwa Bunge. Ni imani yetu kuwa serikali itatuelewa na, hivyo, kutoa majibu ya kuridhisha.

Mohamed Habib Mnyaa

Mohamed Habib Mnyaa

Hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani – Wizara ya Nishati na Madini – kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2008/2009

UTANGULIZI

1.1 Mheshimiwa Spika,

Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uzima na kuniwezesha kusimama hapa leo hii kwa niaba ya Kambi ya Upinzani ili kutoa maoni na ushauri kwa mujibu wa  Kanuni za Bunge kifungu  Na 99(7) Toleo la 2007 kuhusu mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa Fedha 2008/2009.

1.2 Mheshimiwa Spika,

Kwa vile nimewasilisha mezani ninaomba inukuliwe kama ilivyo katika Hansard hata Kama sitomaliza kuisoma yote.

1.3. Mheshimiwa Spika,

Kwa ruhusa yako napenda kutumia fursa hii  kuwapongeza wananchi wa Jimbo langu la Mkanyageni na Chama changu cha CUF walioniwezesha kufika hapa Bungeni.

Nawaahidi kuwatumikia kwa  kadri Mwenyezi Mungu atakvyonijaalia maana wao ndio walio sababisha kuwepo hapa Bungeni leo na kutoa mawazo yao kwa taifa letu la Tanzania.

1.4 Mheshimiwa Spika,

Napenda kuwapongeza viongozi wangu wa Kambi Mhe. Hamad Rashid na naibu wake Dr.Willibrod Slaa, pamoja na wale wote waliotoa michango yao kwa kunipa moyo muda wote wa maandalizi ya hotuba hii. Na wa mwisho lakini si kwa umuhimu ni Msaidizi wangu wa Wizara hii Mheshimiwa Severina Mwijage

2.0 MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MIPANGO KATIKA   BAJETI YA MWAKA 2007/2008

2.1 Mheshimiwa Spika,

Mambo muhimu yaliyopangwa kutekelezwa katika bajeti ya mwaka 2007/08 ni pamoja na yafuatayo:–

2.1.1:   Ukuwaji wa sekta ya Nishati

2.1.2: Ukuwaji wa sekta ya  Madini

UCHAMBUZI WA MIRADI ILIYOPANGWA KUTEKELEZWA KATIKA MWAKA 2007/2008

3.1 Mheshimiwa Spika,

Katika bajeti ya mwaka uliopita Bunge lako tukufu lilipitisha matumizi ya Wizara hii jumla ya shilingi 353.959.143.900/- ambapo shilingi 41.549.559.000/- kwa matumizi ya kawaida ambayo ni asilimia 11.7 ya bajeti yote na shilingi 312.409.584.900/- kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambyo ni asilimia 88.3 ya bajeti yote.

3.2 Mheshimiwa Spika,

Hapa napenda kuweka angalizo kwamba bajeti ya mwaka 2006/07 matumizi ya kawaida yalikuwa ni asilimia 7 na ya maendeleo ilikuwa ni asilimia 93. Kwa maana nyingine bajeti ya 2007/08 tuliongeza matumizi ya kawaida na tukapunguza matumizi ya maendeleo.

3.3 Mheshimiwa Spika,

Kwa upande mwingine katika bajeti hiyo ya mwaka jana makadirio ya makusanyo ya mapato yalikuwa shilingi 57.958.480.800/-, na hadi kufikia mwezi wa Machi 31, 2008 makusanyo yalikuwa shilingi 42.177.017.005/02 sawa na asilimia 72.77 zilikuwa zimekusanywa.

3.4 Mheshimiwa Spika,

Fedha za maendeleo zilizopatikana katika bajeti hiyo ya mwaka jana hadi kumalizika kwa robo ya tatu ni shilingi 4.950.321.000/- kati ya Shilingi  312.409.584.900/- zilizotengwa sawa na asilimia 1.58, lakini katika muhtasari kwa ajili ya Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilicho fanyika hapa Dodoma siku ya Jumatatu na Jumanne (tarehe 16 na17 juni 2008), sura ya nne ukr.11. aya ya 4.3. Mheshimiwa Waziri alitueleza kiasi hicho ni asilimia 86.95 ya kiasi kilicho kasimiwa kwa kipindi hicho ambacho ni 5.693.000.000/-.

3.5 Mheshimiwa Spika,

Hapa Kambi ya Upinzani na Wabunge wengine waliomakini tumepata wasiwasi na kujiuliza ikiwa kiasi kilicho kasimiwa kwa robo tatu ya mwaka ni bilioni 5.693 je hiyo robo ya mwisho zilizopatikana zilikuwa ni Shilingi 306.716.584.900/-?  au hazikupatikana tena?  Vipi hali hii?

Kumbukumbu za Bunge ni kuwa tumepitisha bajeti ya maendeleo ya Shilingi bilioni 312.409.Kwa lugha sahihi asilimia 86.5 aliyosema bajeti ya maendeleo imetekelezwa siyo sahihi, na ni ya kulidanganya bunge lako tukufu.

3.6 Mheshimiwa Spika,

Suala hili ukilitizama kwa upande mwingine ni kwamba, katika fedha ya maendeleo iliyoombwa katika bajeti ya 2007/08 Shilingi 115.716.584.900/-zilikuwa fedha za nje sawa na asilimia 37 (bajeti tegemezi) na Shilingi 196.693.000.000/- ni fedha za ndani (ambazo ni asilimia 63) ambazo zimeweza kupatikana na kuingizwa katika miradi ya maendeleo ni bilioni 4,950,321,000/-sawa na asilimia 2.5 tu ya fedha za ndani.

3.7 Mheshimiwa Spika,

Hii ni hatari na ni dhahiri basi, kwamba pesa inayokadiriwa na kupitishwa na Bunge lako na ile inayo patikana ni kitendawili. Tunalidhihaki Bunge na bajeti kwa jumla na hali  hii isipokemewa na kusimamiwa vyema maendeleo tabu sana kupatikana   tunalidanganya Bunge – tunawadanganya Watanzania.

MITAMBO YA KUZALISHA UMEME SOMANGA FUNGA

4.1.1 Mheshimiwa Spika,

Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini ya mwaka jana 2007/08 (u.k wa 7) katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo  chini ya mradi mkubwa wa gesi asilia ya songo songo, Mheshimiwa Waziri alilieleza Bunge lako tukufu kuwa ujenzi wa kituo cha MW 6 kinachojengwa katika eneo la Somanga Funga umekamilika kwa asilimia 90, na umeme utakaozalishwa na kituo hiki utasambazwa katika miji ya Kilwa Masoko, Kilwa Kivinje, Singino, Nangurukuru, Utete, Ikwiriri, Kibiti na vijiji ambavyo bomba la gesi asilia linapita.

4.1.2   Mheshimiwa Spika,

Hadi hivi leo tunapozungumza hapa Bungeni na baada ya mwaka mmoja kupita hizo asilimia 10 zilizokuwa zikamilishwe kwa kipindi cha mwaka mzima bado hazija kamilika.

Ufungaji wa mashine haujakamilika, hiyo miji iliyosemekana kupata umeme hata nguzo hazija simamishwa na zilizosimamishwa hakuna nyaya n.k.

Ndio maana hata katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya mwaka huu u.k wa 34 bado inazungumzia kukamilisha ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Somanga Funga.

Kuna habari eti mkandarasi kacheleweshewa fedha ya msamaha wake wa kodi ya mafuta na kuna taarifa kuwa mkandarasi ana-urafki na wakubwa na hagusiki na ndio sababu za ucheleweshaji wa miradi hio.

Hapa kambi ya upinzani inamuomba Waziri atuelezee ni sababu zipi zilizopelekea kwa muda wa mwaka mzima hizo asilimia 10 zilizobaki ambazo hazijakamilika, ukizingatia kazi ya ujenzi wa kituo hicho ulitarajiwa kukamilika mwezi Mei 2007.

4.1.3 Mheshimiwa Spika,

Itakuwa ni vyema Mheshimiwa Waziri kuchunguza tuhuma hizo za kuchelewa vibaya kwa miradi hii na kulitaarifu Bunge lako ipasavyo na kubainisha kuhusu taarifa ya urafiki huo wakuchelewesha kazi za maendeleo vyenginevyo dhana ya rushwa haziwezi kuepukika.

4.2.0   TEGETA

4.2.1 Mheshimiwa Spika,

Kuna mradi huu wa Tegeta wa kuzalisha umeme wa MW 45 ambao katika maelezo ya Waziri wa Nishati na Madini aliyoyatoa katika kamati tarehe 28/3/07, kwamba mradi huu unagharamiwa na serikali ya Uholanzi chini ya mpango wa ORET ambapo serikali ya Uholanzi itatoa msaada (grant) kugharamia nusu ya gharama na nusu nyengine kama mkopo wa masharti nafuu kwa serikali ya Tanzania. Mradi huu ulitarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2007,  Mheshimiwa Waziri alituhakikishia kwamba matayarisho ya uundaji wa mashine na vifaa kutoka kampuni ya WARTSILA (Finland) yalikuwa yanaendelea ikiwa ni pamoja na kazi ya usanifu na utayarishaji wa michoro. Baadae yakatolewa maelezo kwamba mradi huu sasa ungekamilika Agosti 2008 (yaani mwezi ujao) ikiwa ni ucheleweshaji wa mwaka mmoja.

4.2.2 Mheshimiwa Spika,

Gharama za mradi huu zilielezwa kuwa ni Euro 31.000.000,-(Tsh. Bilion 55.8). Hadi hivi sasa mradi huu haujakamilika na tayari ni wastani wa ucheleweshaji wa miaka miwili. Kambi ya upinzani inamtaka Mhesimiwa Waziri atueleze kulikuwa na sababu gani za msingi zilizosababisha kucheleweshwa kwa mradi huo hadi kufikia muda wa miaka miwili. Hii sio bure Waziri ni vyema alieleze bunge lako tukufu kama kuna uzembe au vyenginevyo.

Katika bajeti ya mwaka 2006/2007 zilitengwa Tsh billion 50.6 (kasma 3001-3136). Katika bajeti ya mwaka 2007/2008 zilitengwa Tsh 25.643.161.500,-(kasma 3001-3136). Kwa maana hiyo katika kipindi cha miaka 2 mradi huu tayari umeshatumia jumla ya Tsh 76.243.161.500,-kama tulivyopitisha katika bajeti au Mheshimiwa Waziri athibitishe kama nazo hazikupatikana vinginevyo kuna ziada ya Tsh. 20.443.161.500- ya gharama halisi za mradi huu ambazo ni Tsh. billion 55.8.

4.2.3 Mheshimiwa Spika,

Tunamuomba Waziri wa Wizara hii alieleze Bunge lako tukufu lililoidhinisha matumizi hayo ambayo pamoja na kuzidi gharama halisi lakini bado hayajaleta matunda ya mradi huu wa Tegeta na tunaarifiwa hadi leo haujakamilika.

4.2.4 Mheshimiwa Spika,

Pamoja na yote tuliyoyabainisha hapo juu bado mradi huu umetengewa Tsh Billioni 30.6 katika bajeti ya mwaka huu. Sijui Mheshimiwa Waziri mara hii atatueleza nini na kutoa ahadi gani kwa Bunge lako tukufu ili kukamilisha mradi huu unaosubiriwa kwa hamu kuongeza uwezo wa uzalishaji umeme wa Tanesco.

4.2.5 Mheshimiwa Spika,

Kambi ya upinzani inamtaka pia Waziri alifafanulie Bunge lako tukufu ni kwa nini katika Muhtasari kwa ajili ya kikao cha Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa muda wa miaka 3 sasa (2006/07, 2007/08 na 2008/09) katika kasma 3001-3136 maelezo ya utekelezaji wa mradi huu ni kwamba uko katika hatua ya uzabuni na utekelezaji wake utaanza mara baada ya kumpata mkandarasi atakaejenga mradi kinyume na maelezo ya Waziri pamoja na  Tanesco. Sasa tunajiuliza nani anasema ukweli ni Waziri au waandaaji wa Bajeti ya Wizara? Hapa lipo tatizo na linafaa lipatiwe ufumbuzi.

4.3.0 ALSTOM POWER RENTALS

4.3.1 Mheshimiwa Spika,

Katika hotuba yangu ya mwaka jana nilihoji juu ya uhalali wa kampuni ya uzalishaji umeme ya Alstom Power Rental inayotumia mafuta ya mazito(heavy oil HA4) tuliyoarifiwa kuwa ilianza kuzalisha umeme wa MW40  tarehe 19 Machi 2007 kwa mkataba wa mwaka mmoja, mradi uliogharimu USD 116 milioni, ingawa kwenye ripoti ya Kamati ya kuchunguza zabuni ya Richmond ilibainisha kuwa gharama halisi ya mradi huo ni USD 130.181 milioni.(Tsh Bilioni 162.726)

4.3.2 Mheshimiwa Spika,

Pia  nilihoji miradi ya  kukodi ya kutumia mafuta wakati tayari tunauzoefu wa IPTL inayokausha uwezo wa kifedha wa Serikali pamoja na Tanesco na kwa bahati nzuri ripoti hiyo ya Richmond ilonyesha njia mbadala ya kuzalisha umeme  kama huo kwa kutumia gesi asilia na kwa bei nafuu.

4.3.3 Mheshimiwa Spika,

Leo hii imebainika kwamba Tanesco wameshindwa kuingiza hata MW1 katika Grid ya taifa mpaka mkataba wa mradi huo umemalizika kinyume na majibu ya Waziri wa wakati huo aliyolieleza Bunge lako tukufu kama ilivyo katika HANSARD ya tarehe 16 Julai 2007 uk.143.

4.3.4 Mheshimiwa Spika,

Kwa kuwa serikali imegharamika kwa kiasi kikubwa kuileta kampuni hiyo hapa nchini na kwa kuwa hatukuweza kufaidika na umeme wa kampuni hiyo na kwa kuwa kuna taarifa kuwa mitambo hiyo ilikuwa ni mibovu iko haja ya Bunge lako tukufu kupata maelezo ya kina kutoka kwa Waziri muhusika na ikiwezekana kamati yako ya kudumu ya Bunge inayohusiana na sekta hii kutafuta ukweli wa suala hili ulioisababishia serikali hasara kubwa ya kiasi hicho na kuishauri Serikali kuepuka miradi mingine ya zima moto kama hio, kuepuka kuwabebesha wananchi gharama za juu za umeme zinazo sababishwa kama fidia ya makampuni kama hayo.

4.4.0 IPTL

4.4.1 Mheshimiwa spika,

Ili kupunguza gharama za uendeshaji wa umeme na kupata maendeleo endelevu nchini serikali  iliona kuna umuhimu wa kubadilisha mitambo ya IPTL ya MW 100 ili itumie gesi asilia badala ya mafuta, na kwa mujibu wa MKUKUTA, mradi ulikadiriwa kuanza julai 2005 na kukamilika 2007 na makadirio ya gharama yalikuwa ni Tsh. B 23.76 kwa wakati huo. Katika bajeti ya 2006/07 mradi ulitengewa Tsh.18.458.000.000,- (kasma 3001-3198), katika bajeti ya mwaka 2007/08 mradi huu ulitengewa Tsh. 15.545.923.800,- (kasma 3001-3198).

4.4.2 Mheshimiwa Spika,

Hii inaonyesha kwa muda wa miaka 2 jumla ya fedha zilizotumika ni Tsh. 34.003.923.800- ambayo hii ni ziada ya Tsh. 10.243.923.800,- ukilinganisha na gharama halisi ya mradi huu kwa mujibu Mkukuta wa Tsh. 23.760.000.000,-

4.4.3 Mheshimiwa Spika,

Hapa kambi ya upinzani inamtaka Mheshimiwa Waziri atoe ufafanuzi wa kina ndani ya Bunge hili tukufu juu ya fedha tuliyopitisha katika Bunge na ile iliyotumika kwa miaka yote hiyo na thamani ya kazi iliyokwisha fanyika kuhusiana na mpango/mradi huu, ni kwa nini kukawa kuna ziada hii ya fedha zilizotumika na hata bila ya mradi wenyewe kuanza.

4.4.4 Mheshimiwa Spika,

Jambo la kushangaza zaidi ni kuwa mradi umetengewa tena mwaka huu jumla ya fedha Tsh. 24.000.000.000,-  Hivyo tunamtaka Waziri atueleze lengo halisi la kutenga tena kiasi hiki cha fedha kwa mradi huu ambao utekelezaji wake hauonekani na wamiliki wa kampuni hiyo hawaonekani kama wako tayari kukubaliana na wazo hilo la kubadilisha mitambo hii kuwa ya gesi.

4.4.5 Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inataka ufafanuzi wa mradi kama huu usiotekelezeka na  haja ya kuingizwa kwenye bajeti kwa miaka mitatu mfululizo bila ya mafanikio na kuharibu program ya Mkukuta.

4.5.0 KINYEREZI

4.5.1 Mheshimiwa Spika,

Katika kitabu cha mpango wa maendeleo na bajeti ya matumizi ya kawaida mwaka 2006/07, mradi wa Kinyerezi ulitengewa jumla ya Tsh. 200.000.000,- (kasma 3001-3138) kwa lengo la kuengeza MW 200 ili kuzalisha umeme wa bei nafuu kwa kutumia gesi asilia ya Songo Songo, mradi huu ulitarajiwa kuchukua miaka mitatu hadi kukamilika kwake.

4.5.2 Mheshimiwa Spika,

Hakuna maelezo yeyote yaliotolewa juu ya mradi huu si katika bajeti ya mwaka 2007/08 wala 2008/09. Hivyo Kambi ya upinzani inamtaka Waziri atueleze maendeleo ya mradi huu ambao tayari ulikwisha kutengewa Tsh. 200.000.000,- ukizingatia hadi sasa hakuna maelezo yeyote angalau juu ya upembuzi yakinifu wa mradi huu, au tulipitisha mradi hewa?

5.0 MIRADI YA USAMBAZAJI UMEME VIJIJINI

5.1 Mheshimiwa Spika,

Katika bajeti ya mwaka 2006/07 miradi 21 ya kupeleka umeme vijijini hasa Makao makuu za Wilaya ilipangwa katika bajeti tuliyopitisha mwaka huo kifungu cha 3001-3112 jumla ya Tsh. 16.226.000.000/-, zilipitishwa na Bunge lako tukufu. Na katika bajeti ya mwaka 2007/08 miradi 20 ilikuwa ni uendelezaji wa miradi hiyo hiyo ya 2006/07 ukiacha ule wakupeleka umeme Makambako na Bunge lako lilipitisha jumla ya Tsh. 9.799.729.200,- ambapo milioni 870 zilikuwa ni fedha za ndani.

5.2 Mheshimiwa Spika,

Kwa maana hiyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita Bunge lako tukufu tayari lilishapitisha bajeti ya Tsh. 26.025.000.000,- kwa miradi hiyo ya usambazaji umeme vijijini. Katika miradi hiyo ya usambazaji umeme vijijini, jumla ya miradi 13 bado haijakamilika na imo katika bajeti ya mwaka huu 2008/09, na imepangiwa jumla ya Tsh. 1.378.533.000- katika kasma hiyo ya 3001-3112.

5.3 Mheshimiwa Spika,

Katika taarifa iliyotolewa na Tanesco kwenye Kamati ya Nishati na Madini Mei 2008 tulielezwa kwamba gharama halisi ya kukamilisha miradi hii ni Tsh. Bilioni 22.087. Kutokana na sababu hizo zilizotolewa na Tanesco na kwa kuwa nilimuomba Mheshimiwa Waziri kunipatia idadi ya fedha iliyopatikana na kutumika katika kila mradi wa usambazaji umeme vijijini kwa mwaka 2005/06, 2006/07 na 2007/08 lakini kwa bahati mbaya suala hilo hajalifanikisha na kwa kuwa miradi hii inaendelea na ni miradi inayowagusa na kupigiwa kelele na Waheshimiwa Wabunge wengi kwa niaba ya Wananchi wao. Hivyo basi naomba kutumia nafasi hii kwa niaba yangu, kambi ya Upinzani na kwa niaba ya Wabunge wengine wa Chama tawala, Waziri wa Wizara hii atuletee kabla ya majumuisho ya bajeti yake jedwali kamili litakalo onesha kwa usahihi jina la mradi, makisio ya mradi huo, fedha iliyoombwa na iliyotumika kwa kila mwaka katika kipindi hicho cha miaka mitatu, ili Wabunge tuweze kujiridhisha na kuona kwamba hatupitishi bajeti hewa na idadi wanayohitaji Tanesco kukamilisha miradi hii ni sahihi.

6.0 SHIRIKA LA UMEME TANZANIA (TANESCO)

6.1.0 Maendeleo endelevu ya rasilimali Nishati na namna ya kupunguza gharama za uzalishaji

6.1.1 Mheshimiwa Spika,

Ni muhimu sana kwa Serikali kuwajibika ipasavyo katika kuhakikisha sekta ya nishati inapewa umuhimu wa pekee unaostahili  kwa kuitengea bajeti ya kutosha na kuwa na rasilimali watu waliobobea na utendaji makini.

Zaidi ya hayo, mikataba yote inayohusiana na  umeme tutakayo katibiana na makampuni ya Kitanzania au ya Kigeni ni lazima ifanywe kwa uangalifu  na uwazi mkubwa ili yapatikane mafanikio kwa pande zote(win-win situation) na ni muhimu sana kuepukana na mikataba ya gharama inayoifilisi Tanesco au Serikali kama ile ya IPTL, ALSTOM, RICHMOND na kadhalika.

Pia iko haja sasa ya kubadili tabia, kuwa na mwamko na ubunifu wa njia zitakazotupunguzia gharama za uzalishaji na upotevu wa umeme usio walazima.

6.1.2    Mheshimiwa Spika,

Inakisiwa kwamba msongo(grid) wetu unaupotevu wa umeme takriban asilimia 25. Ni rahisi kurekebisha miundombinu inayosababisha upotevu huu kuliko gharama za kuzalisha kima kama hicho kinachopotea. Hivyo ni rahisi kupunguza upotevu wa umeme (energy losses) unaosababishwa na watumiaji wasiowaangalifu, kwa mfano upotevu wa umeme katika maofisi ya serikali unaosababishwa na kuacha wazi (on) taa pamoja na viyoyozi vinafanya kazi hata kama ofisini hamna mtu na mara nyengine sio siku za kazi, baadhi ya taa za barabarani kuwaka hata nyakati za mchana na baadhi ya watumiaji umeme majumbani hawana mwamko wa kutumia balbu maalum zinazotumia umeme kidogo na kutoa mwangaza mkubwa ( energy saving bulbs).

6.1.3 Mheshimiwa Spika,

Kuna nchi nyingi ambazo wamepanga mipango madhubuti ya kutumia energy saving bulbs kwa ajili ya kupunguza gharama za uzalishaji mfano mzuri ni Nchi ya Uganda ambao wanampango wa kusambaza balbu 800.000 ili kuweza kuokoa kiasi cha zaidi ya US $ 1.000.000 kwa punguzo la MW 30. Na Serikali ya nchi hiyo tayari wameondoa VAT ya asilimia 18 na import duty ya asilimia 25 katika bajeti ya mwaka jana kwa kampuni ya Osram ya Ujerumani  kwa uingizaji wa taa hizo ili kupunguza gharama za manunuzi na kutoa bure kwa wale wasiokuwa na uwezo wa kununua balbu.

6.1.4 Mheshimiwa Spika,

Kutokana na tafiti zilizofanywa nchini Kenya zinaonesha kuwa nchi hio inapoteza kiasi cha sh. Bilioni 10 kwa mwaka kwa kutumia taa ambazo zinatumia umeme mkubwa ambazo fedha hizo zingeweza kuwasomesha Wanafunzi wa Shule zote za Msingi Nchini humo. Na laiti kama kila nyumba itatumia “energy saving bulbs” basi wangeliweza kuokoa kiasi cha MW 131 ambazo ni sawa na punguzo la asilimia 80. Hii inaonyesha kwa kupitia mpango huu “line” yenye uwezo wa kuwahudumia wateja wapatao 1.000 basi ingeliweza kutoa huduma kwa watu 5.000.

6.1.5 Mheshimiwa Spika,

Kutokana na mpango huu pia Nchi ya Ghana wameweza kuokoa kiasi cha fedha US$ 12 milioni kwa kuweza kupunguza GW 2. Nchi ya Australia tayari wameshapitisha sheria ya upigaji marufuku wa uuzaji wa taa za zamani ambazo hutumia umeme mkubwa na badala yake kuhamasisha utumiaji wa “energy saving bulbs” nchi nzima.

6.1.6 Mheshimiwa Spika,

Wakati tukiona nchi mbali mbali duniani zinafanya juhudi hizo ni dhahiri kuna nafuu kwa mfano, mtu mwenye kipato cha wastani na anae ishi kwenye nyumba ya kawaida yenye familia ya kiafrika huwa anatumia wastani wa unit 380 za umeme kwa mwezi kwa wale wanaotumia balbu ya watt 60 lakini familia hio hio inapotumia balbu ya watt 20 (energy saving bulb) angetumia wastani wa unit 125, ikiwa ni punguzo la matumizi la asilimia 67.

6.1.7 Mheshimiwa Spika,

Kwa tafiti zilizofanywa imebainika kwamba kampeni ya kutumia energy saving bulbs imeweza kupunguza gharama za uzalishaji wa nishati hii ya umeme, zaidi ya yote utumiaji wa taa za zamani unaongeza utumiaji mkubwa wa umeme ambao hupelekea utumiaji mwingi wa gharama za uzalishaji umeme (mafuta/gesi/ maji) ambayo husababisha ongezeko  la joto duniani.

6.2.0    Hali ya usalama ya miundo mbinu ya umeme

6.2.1 Mheshimiwa Spika,

Katika jiji la Dar es salaam na miji mingi ya Tanzania kuna miundo mbinu ya umeme ambayo haiko katika hali ya kawaida inavyohitajika kwa mfano baadhi ya transfoma zilizowekwa chini ambazo hazina uzio na waya za umeme mkubwa zilizounganishwa na transfoma hizo hazina ngao (shield) pia baadhi ya nguzo zimelala(inclined) sana kiasi cha kuhatarisha maisha ya wapita njia kwani wakati wowote zinaweza kuanguka, vivyo hivyo baadhi ya waya za taa za barabarani ziko wazi.

6.2.2 Mheshimiwa Spika,

Hii sio sura nzuri ya miji yetu katika Tanzania ya leo na kitengo cha usalama cha Tanesco (Safety Department) inafaa kitengewe fedha kurekebisha hali hiyo.

6.3.0 Power system master plan

6.3.1 Mheshimiwa Spika,

Naipongeza Wizara ya Nishati na Madini angalau kwa kuwasilisha DRAFT ya Power System Master Plan mnamo tarehe 28 na 29 April 2008 katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempisk kwa kupata maoni ya wadau na nimategemeo yetu kwamba Wizara itasikiliza maoni ya Kamati ya Nishati na Madini  ya kuiwasilisha hapa Bungeni kupata maoni ya Wabunge ambao ndio wadau wakubwa wanao wakilisha Wananchi.

6.3.2    Mheshimiwa Spika,

Kwa wale tuliobahatika kuiona tulishangazwa kuona ongezeko la 3.595MW kwa kipindi cha miaka 25 ijayo lakini plani hiyo imeanzia 2006 hadi 2031 pamoja na kuwasilishwa mwezi Aprili 2008. Ni nini kilicho wafanya Wataalam hao wasifanye “simulation”kuanzia mwaka wa kuwasilisha plani hiyo. Na je, walifikiria ongezeko la idadi ya watu katika kipindi cha miaka 25 ijayo? Tunategemea Mheshimiwa Waziri atalifafanulia Bunge lako tukufu swala hili.

6.3.3 Mheshimiwa Spika,

Katika plani hiyo pia inajumuisha  ile dhamira ya “interconnector” baina ya Tanzania , Kenya na Zambia ambalo ni jambo zuri kwa maendeleo ya nchi zetu.Hata hivyo ningependa kutahadharisha kwamba, ili Tanzania tuweze kufanikiwa na kupata kuuza umeme kwa majirani zetu hatuna budi kujitosheleza kwa soko letu la ndani kwanza na kuzalisha zaidi ya kiwango kilicho pangwa kwenye “DRAFT Power System Master Plan” hiyo.

6.3.4    Mheshimiwa Spika,

Sababu kuu ya maoni hayo ya Kambi ya Upinzani ni kwamba Afrika ya Kusini wamenukuliwa wakisema katika toleo maalum la “ENGINEERING NEWS” (April 25  – May 1, 2008 volume 28 no 15) kwamba kutokana nakuongezeka kwa matumizi ya nishati ya umeme wanampango wa kuongeza 40GW ifikapo mwaka 2025. Na mipango ya kupata umeme wa mkaa wa mawe kutoka Botswana na Msumbiji , umeme wa gesi asilia kutoka Namibia na Msumbiji na umeme wa maji kutoka Jamhuri ya watu wa Kongo  imeshaanza.

6.3.5 Mheshimiwa Spika,

Kampuni ya umeme ya S.A (ESKOM) inasema kutokana na nyimbo ya Carlos Santana inasema: “life is a game of give and take” (nipe nikupe), lakini kutokana na tatizo la nishati hii Afrika ya Kusini wanaangalia zaidi kuingiza umeme kutoka nje na sio kutoa.

7.0 MADINI

7.1 Mheshimiwa Spika,

Sekta ya Madini ni sekta nyeti na ambayo inakua kwa kasi kubwa kulinganisha na Sekta nyingine katika uchumi. Aidha ni sekta ambayo kama ikishikwa na kupaliliwa vizuri inaweza kuibadilisha nchi yetu, kutoka kuwa omba omba na kuwa toshelezi.

Kambi ya Upinzani inaelewa na inaamini kuwa kazi kubwa imefanywa na Kamati ya Madini ya Mhe.Jaji Bomani. Hivyo basi inaitaka Serikali kuyafanyia kazi mapendekezo yote ambayo yametolewa na Kamati hiyo kuhusiana na Sekta ya Madini.

7.2 Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali iwe mwanachama wa Extractive Industries Transparency Initiative (EITI) ambayo ni asasi ya kimataifa yenye makao makuu yake Oslo nchini Norway ambayo inasisitiza uwazi wa mapato yatokanayo na maliasili ambazo nchi imejaaliwa na Mwenyezi Mungu, asasi hiyo inasisitiza nchi mwanachama zenye dhamana ya kulinda rasilimali za wananchi kuwa wazi katika mapato yote yatokanayo na rasilimali zao.

7.3 Mheshimiwa Spika,

Ili kuwa na uwazi huo asasi hiyo inasisitiza kuwa Serikali zinachapisha kwa wazi mapato yote inayopokea toka kwenye makampuni ya migodi na jinsi mapato hayo yanavyotumika, aidha Kampuni za madini zichapishe malipo yote wanayotoa kwa Serikali.

Kambi ya Upinzani inasisitiza na kuitaka Serikali kuwa mwanachama wa asasi hii. Hii itasaidia kwanza wananchi kuwa na imani na Serikali yao kuhusu matumizi ya raslimali zao ambazo Serikali ni mlezi wake. Hii itapunguza maswali ambayo wananchi wanajiuliza bila ya Serikali kuwa na majibu stahiki.

7.4 Mheshimiwa Spika,

Sambamba na hilo ni dhahiri udanganyifu unaofanywa na makampuni ya madini unaweza kupungua kwa kiasi kikubwa kwani watakuwa wamejifunga minyororo wenyewe.

MEREMETA

KAULI YA WAZIRI WA NISHATI NA MADINI ALIOITOA BUNGENI KATIKA MPANGILIO WA KIUTAWALA (CHART)

8.1 Mheshimiwa Spika,

Tumeshuhudia wakati wa uchangiaji bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali imetoa majibu ambayo hadi sasa bado yanawachanganya Watanzania kutokana na utata wake kuhusiana na suala zima la MEREMETA.

8.2    Mheshimiwa Spika,

Katika kipindi cha bajeti ya 2006/07 tuliuliza maswali mengi kuhusiana na Kampuni ya MEREMETA iliyokuwa imeundwa kwa minajili ya kuiongezea nguvu kimapato Kikosi cha  Nyumbu cha JWTZ Kati ya majibu yaliyojibiwa na Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini wa wakati huo kwa mujibu wa HANSARD ni  kuwa nanukuu  “Sasa kwa ufupi, nataka niseme yafuatayo: Kwanza Meremeta amesema imeanzishwa off-show, hata mwanzo ndiyo ilivyokuwa na sasa iko katika process ya winding up. Kwa hiyo, kinachoendelea sasa ni katika mtiririko huo.” Mwisho wa kunukuu.

8.3 Mheshimiwa Spika,

Mhe. Waziri wa Fedha katika kuhitimisha bajeti yake tarehe 23 Juni, 2006 alisema yafuatayo kuhusiana na MEREMETA nanukuu: “Mheshimiwa Spika, suala lingine ni juu ya nani ni wamiliki wa MEREMETA na Mwananchi?  Kwa maelezo niliyokuwanayo ni kwamba MEREMETA ni Kampuni ya Serikali iliyoanzishwa kwa lengo la kununua dhahabu kutoka wachimbaji wadogo wadogo. Baadaye Kampuni ilianza mradi wa kuchimba dhahabu katika eneo la Buhemba Mkoani Mara .”   Mwisho wa kunukuu.

8.4 Mheshimiwa Spika,

Lakini wakati Mhe. Waziri wa Nishati akitoa maelezo ya Serikali kuhusiana na ombi la Mhe. Dk.Slaa la kutaka maelezo toka Serikalini kuhusu tuhuma za ubadhirifu katika BOT, alijibu yafuatayo, nanukuu:

8.5 Mheshimiwa Spika,

Serikali inapenda kukanusha kauli hizi kwamba Kampuni ya MEREMETA imeuzwa kwa RandGold. Kampuni ya MEREMETA haijauzwa kwa mtu yeyote au kwa Kampuni yeyote, iwe kwa bei ya kutupwa au kwa bei ya kuruka. Kama nilivyoeleza hivi punde, MEREMETA imesitisha shughuli zake kwa mujibu wa sheria. Kutokana na hatua hiyo, mali na madeni ya MEREMETA yamehamishiwa kwenye Kampuni mpya ya TANGOLD ambayo inamilikiwa na Serikali kwa asilimia mia moja. Mali hizo zinajumuisha pia mgodi wa dhahabu wa Buhemba.” Mwisho wa kunukuu

8.6 Mheshimiwa Spika,

Kauli hizi za Serikali zinapingana na zina utata, kwanza tumeelezwa iko katika katika hatua za mwisho za “winding up” na Waziri mwingine anasema Serikali imeinunua. Haya kama Serikali imeinunua ilikuwa ni ya nani hapo mwanzoni na ni kwa nini ilikuwa chini ya JWTZ? Haya, ndio masuali ambayo hadi leo hii hayajapata majibu tangu mwanzo na ndio msingi wa manung’uniko na malalamiko ya Watanzania, yaani kutokupata majibu ya moja kwa moja kutoka Serikalini.

WANAHISA WA MEREMETA KWA UTAFITI WA KAMBI YA UPINZANI

8.6 Mheshimiwa Spika,

KAMBI YA UPINZANI INATAKA KUJUA   hii Meremeta hasa ni ya nani, na hawa London Law Services na London Secretarial Services ni akina nani hasa. Kampuni ya Meremeta ina hisa ASILIMIA NGAPI? Haya ni mambo yanatufanya tuwe na mashaka makubwa sana. Hivi serikali inaogopa nini kuweka mambo haya wazi hadharani, angalau kwa kamati husika ya Bunge basi ili kama kuna sababu ya msingi wawakilishi wa wananchi waweze kufahamu.

8.7 Mheshimiwa Spika,

Kauli ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuwa MEREMETA ni ya jeshi na haiwezi kutolewa maelezo Bungeni kwani ni kutoa siri za Jeshi, hivyo kuhatarisha usalama wa nchi, ni majibu ya kushangaza. Wanahisa wa MEREMETA ni wageni na hivyo siri za jeshi ni salama kwa wageni kuliko wabunge au Bunge lako?

8.9 MHESHIMIWA Spika,

Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe majibu sahihi na sio kutoa majibu ya kisiasa tu. Kambi ya Upinzani imekwisha kusema iwapo kuna jambo kweli la siri basi liwasilishwe kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge au Kamati ya Uongozi. Lakini kauli kuwa serikali haiwezi kusema lolote haiwezi kamwe kukubalika na Bunge hili. Bunge linapaswa kusimamia hata jeshi kwa mambo yasiyohusu mikakati ya kijeshi. Dhahabu ni biashara na hakuna siri ya kibiashara kwa Bunge. Ni imani yetu kuwa serikali itatuelewa hivyo na kutoa majibu ya kuridhisha.

Mheshimiwa Spika,

Baada ya kuyatoa hayo kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

…………………………………………………………

Mohamed H. J. Mnyaa (Mb)

MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI- WIZARA YA NISHATI NA MADINI

08.07.2008


Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s