Ile Real Madrid inakuja lini?

“…Miongoni mwa mafanikio ambayo yalisemwa kuwa ni kutokana na ziara za Mheshimiwa Rais nje ya nchi, ni pamoja na ujio wa timu ya mpira wa miguu ya Real Madrid ya Hispania. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa tamko la kuthibitisha kuwa timu ya Real Madrid ingelifika Tanzania rasmi kwa michezo ya kirafiki Julai mwaka 2007 ikiwa na msafara wa watu wapatao 80. Hili ni tamko rasmi la Serikali ndani ya Bunge. Kambi ya Upinzani inauliza ujio wa timu hii ni lini? Je, Rais alipotoshwa? Kuna jambo gani hapo? Kama imeshindikana, ni kwanini Serikali inakosa ujasiri wa kulieleza Taifa kilichojiri kama ilivyotamka rasmi na kwa mbwembwe wakati wa kutangaza uwepo wa utaratibu huo?”

real-madridHotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani – Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2008/2009 iliyosomwa Bungeni na Mhe. Mwanawetu Said Zarafi (Mb) tarehe 28 Julai, 2008

I. UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kutumia fursa hii kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, kanuni ya 99(7), toleo la Mwaka 2007 Kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kwa mwaka wa fedha 2008/2009.

2. Mheshimiwa Spika, kwanza na kwa nafasi ya kipekee kabisa, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema na Amani, kwa kutuwezesha sote kufika hapa tukiwa wazima wa afya, tukiwa tayari kuwajibika kama tulivyo agizwa na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

3. Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kambi ya Upinzani Bungeni, chini ya Uongozi thabiti wa Mhe. Hamad Rashid Mohamed, pamoja na Mhe. Dr. Willibrod Slaa kwa kuniamini na kunichagua tena kuwa msemaji mkuu wa kambi katika Wizara hii. Nami naendelea kuwaahidi kuwa nitaendelea kuitumikia kambi pia nawahakikisha wananchi wote kuwa nitaendela kutetea haki ya watanzania kila itakapo stahiki.

4. Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitakishukuru chama changu, Chama Cha Wananchi CUF, chama kinachojikita katika kusimamia na kutetea haki na usawa kwa Watanzania bila kujali itikadi, dini wala rangi. Pamoja na hao napenda pia kuwashukuru viongozi na wanachama wote wa CUF wilaya ya Kilwa. Kwa pamoja napenda kutambua ushirikiano wanaonipa ndani na nje ya Bunge.

5. Mheshimiwa Spika, aidha napenda nichukue fursa hii pia kuipongeza timu ya vijana chini ya miaka 17 ya mkoa wa Ruvuma kwa kuibuka kidedea katika michuano ya Copa Cocacola. Ushindi wao huo umetudhihirishia kuwa vipaji haviko tuu katika jiji la Dar-es-Salaam bali hata katika mikoa iliyopo pembezoni mwa nchi hii. Naipongeza pia timu ya mpira wa pete ya Dar es Slaam katika mashindano hayo ya taifa. Wakati huo huo kwa niaba ya Kambi ya Upinzani naipongeza timu ya mpira wa miguu Ilala kwa kufanikiwa kutwaa kombe la Taifa Cup. Pia sijaisahau timu yetu ya Copa Cocacola ambayo imetuletea fahari baada ya kutupatia ushindi katika mashindano ya kimataifa.

6. Mheshimiwa Spika, aidha natoa pole kwa Mheshimiwa Savelina Mwijage pamoja na familia yake kwa msiba mwingine wa mjukuu wake aliyepata ajali na kwa kipindi chote alikuwa hospitalini. Mwenyezi Mungu ampe roho ya ustahimilivu. Amin

7. Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa utangulizi huo, sasa naomba nianze moja kwa moja kutoa hoja ya Kambi ya Upinzani katika wizara hii.

II. AHADI ZA WIZARA KATIKA MWAKA WA FEDHA 2007/2008

8. Mheshimiwa Spika, Ni jukumu la msingi la Kambi ya Upinzani kuikosoa na kuikumbusha Serikali juu ya wajibu wake kuwatumikia wananchi. Napenda kuikumbusha Serikali juu ya ahadi ambazo Wizara hii iliahidi kukamilisha ndani ya mwaka wa fedha uliopita 2007/2008.

1. UPANUZI WA SHIRIKA LA UTANGAZAJI TANZANIA (TBC)

9. Mheshimiwa Spika, moja kati ya haki za msingi za mwananchi wa Tanzania kama inavyotambuliwa kikatiba katika ibara ya 18, kifungu kidogo cha (b) ni kuwa “kila mtu anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi”. Hii inadhihirisha kuwa kupata habari ni moja ya haki za msingi za raia. Serikali ina jukumu la kusimamia haki na kutetea haki za wananchi wake. Hivyo kusambaza habari ni jukumu la Serikali, ingawaje hata vyombo binafsi vinayo majukumu hayo.

10. Mheshimiwa Spika, natanguliza hili kwanza kwa nia ya kuweka bayana jukumu la Serikali kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).  Ahadi hizo zilitolewa na wizara wakati wa Hotuba ya Bajeti ya Mwaka 2007/2008. Hata hivyo, ili Shirika liweze kufanya kazi yake na kutekeleza matakwa ya Katiba, linatakiwa kusambaa nchi nzima na kuwa na ubora wa usikivu na hivyo kuwafikia wananchi wote.

11. Mheshimiwa Spika, wakati nasoma maoni ya Kambi ya Upinzani kwa mwaka wa fedha wa 2007/2008 nilitilia msisitizo kuhusu suala la majengo kwa lililokuwa Shirika la Utangazaji ya Taifa na Mheshimiwa Waziri alitanabaisha kuwa wizara tayari ilikuwa kwenye mazungumzo yanaendelea na wafadhili na wadau mbalimbali na kuwa walikuwa wamefika hatua nzuri. NSSF walielezwa kuwa tayari kuyakarabati majengo yaliyoko Pugu Road na Mikocheni.

12. Mheshimiwa Spika, leo hii kwenye taarifa za Kamati yetu zinaonyesha kuwa marekebisho ya majengo haya bado yanabakia kuwa ni malengo ambayo wizara hii inapanga kuyatimiza ndani ya mwaka huu.  Kambi ya Upinzani inataka kujua ni lini hatua zitachukuliwa ili majengo ya shirika hili yatakarabatiwa na kuboreshwa kwa lengo la kuwapa watumishi wa shirika hili nafasi na mazingira bora ya kufanyia kazi?

2. VAZI LA TAIFA

13. Mheshimiwa Spika, suala la vazi la Taifa sasa limekuwa donda ndugu au gonjwa lisilo na dawa. Kila mwaka watu kutokea kada tofauti wanaihoji serikali juu ya vazi la Taifa. Mungu ameibariki sana Tanzania kwa kuipamba kwa makabila mengi na tamaduni nyingi, wanyama wa kila aina na rasilimali zinazofautiana. Vyote tunavyo lakini vazi la taifa hatuna. Inashangaza tumeshindwaje kuchukua hatua ya kupata vazi la Taifa ambalo ni kielelezo muhimu la uzalendo na utaifa wetu?

14. Mheshimiwa Spika, mchakato wa kutafuta vazi la Taifa ulijitokeza toka wakati wa Serikali ya awamu ya tatu. Serikali ya awamu ya nne sasa imebakiza miaka miwili hivi kumaliza muda wake. Mwaka wa fedha 2007/2008 Wizara  iliahidi kuwa mchakato unaendelea vizuri, na wizara ilikiri kuwa imeshabainisha mavazi matatu ambayo wanafikiri ni rasmi, pia walikwisha andaa waraka wa Baraza la Mawaziri kuwawezesha  mawaziri waweze kufanya uamuzi wa pamoja kama Serikali kwa kusema sasa hili ndilo vazi la Taifa.

15. Mheshimiwa Spika, hivi uamuzi kutoka katika Baraza la Mawazrii huchukua muda gani? Kama kweli Waraka huo ulikuwa umekwisha tayarishwa takriban mwaka mmoja uliopita! Hivi nini hasa nia ya Wizara kutoa ahadi ambayo wala haitajwi tena mwaka huu? Hapa ni dhahiri kunja fumbo. Fumbo hili namwachia mtanzania alifumbue.

16. Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu umuhimu wa vazi la taifa. Nchi nyingi Afrika ikiwemo Nigeria na Ghana zimeweka bayana vazi lao ambalo husaidia kujitambulisha duniani. Kambi ya Upinzani inataka ufafanuzi wa kina juu ya sababu ya msingi inyosababisha kucheleweshwa kuwepo kwa vazi la Taifa? Hivi ni kweli mpaka  wananchi wapige kura za maoni kupata Vazi la Taifa?

17. Mheshimiwa Spika, Vazi la Taifa ni  pamoja na mavazi ya makabila mbalimbali hivyo basi ni vyema Wizara ikaja na mkakati wa kuhamasisha na kuhakikisha kuwa mavazi ya makabila mbalimbali yanaenziwa kwani hii nayo ni sehemu ya utamaduni wa Taifa. Serikali lazima iweke sera na mikakati ya kuhamasisha mavazi ya makabila mbalimbali ama sivyo yatapotea. Sasa hivi watanzania wengi wanafahamu tu vazi la Wamasai wakati ambapo makabila karibu yote nchini yana mavazi yao ya asili.

3. BARAZA LA KISWAHILI TAIFA (BAKITA)

18. Mheshimiwa Spika, Baraza la Kiswahili la taifa liliundwa kwa sheria Na.27 ya mwaka 1967 na kufanyiwa marekebisho mwaka 1983. Sasa ni takribani miaka 25 yaani robo karne tangu kuundwa kwa Baraza hilo. Madhumuni ya kuanzishwa kwa baraza ni wazi yana manufaa sana kwa maendeleo ya jamii yetu yote kwa ujumla.

19. Mheshimiwa Spika, lakini moja kati ya kero kubwa katika baraza hili ni ukosefu wa majengo kwa ajili ya baraza hili. Pamoja na ukweli kuwa baraza la Kiswahili ni moja kati ya mabaraza ambayo yameundwa kwa muda mrefu sana uliopita lakini ujenzi wa ofisi zake unaendelea kusuasua.

20. Mheshimiwa Spika, Serikali iliyoko madarakani imechukua takribani miaka 41 kuweza kugundua tatizo hili. Lakini hiyo si hoja sana, suala tunalolihoji ni ukweli kuwa katika bajeti ya mwaka 2006/2007 Serikali kupitia Bunge lako Tukufu liliidhinisha jumla ya shilingi milioni 400. Na katika bajeti ya mwaka jana tulipitisha jumla ya shilingi milioni 100. Hiyo ni jumla ya shilingi milioni 500, jasho la walipa kodi wanaotaabika wakichangia nchi yao.

21. Mheshimiwa Spika, Hiyo ni miaka mitatu sasa, lakini la kustaajabisha wizara hata kiwanja bado haijapata. Mchakato bado unaendelea! Mpaka lini? Wizara inajinadi kuwa ipo kwenye hatua ya kuaanda michoro ya kiusanifu ya majengo na kukadiria gharama za jengo ilhali kiwanja bado. Kambi ya Upinzani inauliza Kama kupatikana kwa kiwanja kunachukua muda mrefu kiasi hiki je kujenga itachukua muda gani?

4. BODI YA UKAGUZI WA FILAMU NA MICHEZO YA KUIGIZA

22. Mheshimiwa Spika, bodi ya filamu iliundwa kwa Sheria Na. 4 ya Mwaka 1976. Hii ni takribani miaka 32 iliyopita. Mazingira ya dunia yamebadilika miaka ya sabini haifanani na wakati tulionao sasa. Serikali ambayo inajisifu kwa kusoma alama za nyakati iliahidi ndani ya mwaka kufanya marekebisho kutokana na ukweli kuwa sheria hiyo ilikuwa imepitwa na wakati. Wizara ilitanabaisha kuwa mchakato wa kuiangalia upya sheria ile ulianza kwa sababu kweli walitambua kuwa haifanani na mazingira ya sasa.

23. Mheshmiwa Spika, huu ni mwaka tayari, muswada wa marekebisho ya sheria hiyo uko wapi? Kwa nini wizara inakuwa nzito kuwasilisha ahadi zake? Tatizo ni nini? Kambi ya upinzani inahitaji majibu ya kina kuhusiana na hili na si vinginevyo.

5. UJIO WA TIMU YA REAL MADRID

24. Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mafanikio ambayo yalisemwa kuwa ni kutokana na ziara za Mheshimiwa Rais nje ya nchi, ni pamoja na ujio wa timu ya mpira wa miguu ya Real Madrid ya Hispania. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa tamko la kuthibitisha kuwa timu ya Real Madrid ingelifika Tanzania rasmi kwa michezo ya kirafiki Julai mwaka 2007 ikiwa na msafara wa watu wapatao 80. Hili ni tamko rasmi la Serikali ndani ya Bunge. Kambi ya Upinzani inauliza ujio wa timu hii ni lini? Je, Rais alipotoshwa? Kuna jambo gani hapo? Kama imeshindikana, ni kwanini Serikali inakosa ujasiri wa kulieleza Taifa kilichojiri kama ilivyotamka rasmi na kwa mbwembwe wakati wa kutangaza uwepo wa utaratibu huo?

25. Mheshimiwa Spika, Na kwa kuzingatia hilo kambi ya Upinzani inahitaji kupata uhakika kama kweli timu hii itakuja, na kama itakuja ni lini? Pia inaitaka Wizara husika kutoa takwimu sahihi ya je Kama timu hii itakuja serikali itatumia Shilingi ngapi kwa safari nzima? Sambamba na hilo inataka kufahamu mpaka sasa Serikali imetumia kiasi gani cha pesa kwenye maandalizi ya ujio wa timu hiyo, hasa ukizingatia kuwa kamati ilikwisha undwa na shughuli za uaandaaji na kazi zilikwisha anza kama ilivyotangazwa ndani ya Bunge hili Tukufu!

III. MAONI YA KAMBI YA UPINZANI BAJETI YA MWAKA WA FEDHA 2008/2009

A. SEKTA YA UTAMADUNI

  • Maafisa Utamaduni wa Wilaya

26. Mheshimiwa Spika, nchi yetu imekuwa ikiweka malengo katika kukuza vipaji ili kujenga wanamichezo bora. Na katika kuwekeza huko viongozi ambao wanajukumu la kuaanda vijana wetu wako katika ngazi ya wilaya. Pamoja na mapungufu mengi, viongozi hawa ambao huitwa maafisa Michezo katika wilaya zetu ni wachache sana. Na katika wilaya nyingi maafisa Utamaduni hufanya kazi za maafisa michezo na maafisa vijana.

27. Mheshimiwa Spika, hii inawazidishia mzigo wa kazi, na hawana marupurupu yoyote, wao wanabakia kufanya kazi tatu kwa pamoja. Kweli huku ndio kuwekeza ili kuibua vipaji? Pamoja na hilo, kutokana na ukubwa wa wilaya zetu bado tumekuwa tukiona matatizo makubwa wanayoyapata katika kutimiza majukumu yao. Sote tunajua ukubwa wa wilaya zetu, matatizo ya miundombinu yetu tunayafahamu, lakini tunamsaidia vipi mtumishi huyu?

Kambi ya upinzani inaitaka wizara husika kutoa takwimu zinazoonyesha jee nchi yetu ina maafisa Michezo wangapi  katika wilaya zetu? Maafisa Utamaduni na maafisa Vijana jee?

28. Mheshimiwa Spika, Sanjari na hilo, maafisa hawa bado wanapatwa na matatizo makubwa katika utekelezaji wa kazi zao. Katika uandaaji wa mpango kazi, maafisa hawa huandaa bajeti inayoonyesha ni kiasi gani wanahitaji katika kutimiza majukumu yao ya mwaka mzima. Lakini maafisa hawa hutegemea pesa kutoka katika halmshauri zao.

29. Mheshimiwa Spika, Utaratibu huu si mbaya iwapo utawezeshwa na ukafanya kazi. Lakini matatizo wanayoyapata ni kwamba, pamoja na mpango kazi mzuri wanaopanga, halmashauri haiwapatii pesa kama mahitaji yanavyosema kwa vile Halmashauri hazina vianzio vya kutosha, na hivyo michezo au utamaduni kuwa si kipaumbele kwao.

30. Mheshimiwa Spika, pale wanapopatiwa fedha na nyenzo, na kukatokea tatizo kwenye masuala mengine wao ndio hupunguziwa na kuambiwa kuwa hayo ni masula nyeti na yanahitajika zaidi kuliko wao. Kwa utaratibu huu utamaduni utajengeka vipi na au michezo itakuzwa vipi. Daima Tanzania kwa mtindo huu itabaki kuwa wasindikizaji katika michezo ya Kimataifa.

Kambi ya upinzani inapenda kutoa rai wizara husika iwapangie mafungu kutoka wizarani ili kupunguza kero zinazowapata maafisa wetu katika halmshauri.

31. Mheshimiwa Spika, lakini hilo halitoshi, maafisa hawa wamekuwa wanarushwa rushwa kama mpira wa kona. Kwa mfano halmashauri ya wilaya ya Hanang, afisa michezo ameondolewa na kwenda kufanya kazi za elimu wakati tupo katika harakati za kukuza vipaji? Hii inaaonyesha dharau ya wazi kwa maafisa hawa. Kambi ya upinzani inaitaka wizara husika kuchukua jukumu la kuangalia na kusimamia maafisa hawa moja kwa moja na kuwa na mipango madhubuti ya kuwaendeleza na kuwamotisha.

  • Ngoma za Asili

32. Mheshimiwa Spika, moja kati ya kazi za msingi za maafisa hawa ni pamoja na kuendeleza vikundi mbali mbali vya sanaa. Katika miaka ya 1990, hata katika wilaya mijini kama Temeke tulikuwa tukiona vikundi vya ngoma vikitumbuiza katika viwanja vya wazi kwa muda wa wiki moja. Hizi ngoma zilikuwa zikijulikana kama ngoma za kibisa. Kutunza tamaduni zetu ni jambo la msingi sana. Na katika kuzitunza pia tuna jukumu la kuzirithisha kwa watoto wetu.

33. Mheshimiwa Spika, inasikitisha kuona katika Tanzania ya leo, kama mkazi wa jiji la Dar es salaam anataka kuona ngoma za asili anatakiwa asubiri Mgeni atoke nje, na yeye awahi kiwanja cha ndege. Kwa sababu ni pale ndio zinaonekana, au asubiri siku za sherehe za kitaifa na awahi uwanja wa Taifa. Hii ni fedheha, kwani lile lengo letu la kuutunza na kuuenzi Utamaduni wetu limeishia wapi? Kambi ya upinzani inatoa rai kuwa wizara iandae mkakati ambao wiki ya Utamaduni iadhimishwe katika ngazi za mikoa na wilaya zote, na sio kwenye ngazi ya Taifa kama ilivyo sasa. Hii itasaidia kuenzi na kudumisha mila zetu kwetu wenyewe kabla ya kuzionyesha kwa wageni.

B. SEKTA YA MICHEZO

  • Ubadhirifu katika vyama vya Michezo

34. Mheshimiwa Spika, Majukumu ya wizara ni pamoja na kuimarisha utawala bora katika Michezo nchini, kuratibu shughuli za asasi zilizo chini ya wizara ya habari, Utamaduni na Michezo. Na hapo ndipo vyama vya michezo vinapopata uangalizi. Hapa nchini kwetu vyama vya michezo ni vingi sana. Na mojawapo ya kero kubwa katika vyama hivi ni ubadhirifu wa fedha.

35. Mheshimiwa Spika, wizara hii ndio yenye jukumu la kufuatilia uwajibikaji na maadili katika vyama hivi kupitia kwa msajili wa vyama vya michezo. Pamoja na ukweli wa kuwepo kwa mikingano mingi ya kikatiba inayolinda kuingiliwa kwa vyama hivi na taasisi au wizara yoyote kutoka nje. Lakini wizara kupitia ofisi ya msajili wa vyama vya Michezo inaweza kumwita mkaguzi wa kutoka nje ya chama na hivyo kutambua kama kuna ubadhirifu wowote, pia msajili ana uwezo wa kuhakikisha kuwa vyama hivi vyote vinakuwa na vikao vya mwaka na kutaarifiana juu ya mapato na matumizi kwa wanachama.

36. Mheshimiwa Spika,njia pekee ambazo wizara inaweza kuzuia matatizo mengi ambayo yana malalamiko mengi katika vyama hivi ni kwa kupeana taarifa. Kambi ya upinzani inapenda kutoa rai katika wizara husika kumwezesha msajili wa vyama ili aweze kufanya kazi zake kwa umakini na hivyo kusaidia kupunguza kero nyingi ambazo zinawapata wanachama wa vyama hivi

.

  • Vituo vya Michezo

37. Mheshimiwa Spika, katika nchi yetu tumebahatika kuwa na vituo vya Michezo viwili, cha Arusha pamoja na Ruvuma. Hivi ni vituo ambavyo vinalengo la kukuza vipaji vya wanamichezo wetu. Wizara husika hupanga mafungu kwa ajili ya maendeleo ya vituo hivi. Pamoja na ukweli kuwa kila mwaka katika vituo hivi hupanga mpango kazi wake wa mwaka na hivyo huwasilisha kiasi cha fedha ambazo wanahitaji kwa mwaka mzima. Na kupitia bunge lako tukufu bunge huidhinisha fedha hizo.

38. Mheshimiwa Spika, lakini kinachowanyong’onyesha watumishi wa vituo hivi ni ukweli kuwa wizara inakuwa ngumu sana kutoa pesa hizo, ambazo ni halali kwa matumizi ya vituo hivyo.Kwa nini wizara inakuwa ngumu katika kutoa fedha ambazo imeviombea vituo hivi?

39. Mheshimiwa Spika, Pamoja na hilo, vituo hivi huanda mafunzo ya muda mfupi kwa maafisa Michezo ya wilaya, na katika mafunzo hayo maafisa huja kutoka halmshauri mbali mbali. Hii ni mipango madhubuti na endelevu katika kuimarisha Michezo katika wilaya zetu na Tanzania nzima kwa ujumla. Lakini kero kubwa inakuja kutokana na ukweli kuwa vituo hivi haviwezeshwi na wizara kwa njia yoyote katika kuandaa mafunzo hayo. Hili si zuri hata kidogo kwa Serikali kama kweli imedhamiria kuwa na lengo la kuibua vipaji katika michezo mbalimbali.

40. Mheshimiwa Spika, hii hupelekea vituo hivi kuwatoza fedha maafisa hawa ili kuandaa mafunzo hayo. Hivi kweli unatoa mafunzo kwa ajili ya kuboresha kazi za maafisa Michezo halafu hao hao pia unawatoza fedha? Jambo hili haiingii akilini hata kidogo!

Kambi ya Upinzani inaitaka wizara kutoa majibu ya kina ni kwa nini  vituo hivi havipati kasma yoyote katika kuandaa mafunzo hayo ya maafisa wa Michezo wa wilaya.

41. Mheshimiwa Spika, pamoja na kutambua kuwa suala la michezo mashuleni lipo chini ya wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi, ila wizara hii haina budi kuhakikisha kuwa wanaweka mkakati maalum kwa ajili ya kukuza michezo mashuleni na vyuoni. Kambi ya Upinzani inapendekeza kuwa pawepo na shule maalum kwa ajili ya michezo angalau shule moja kila wilaya na Serikali itoe fungu maalum kwa ajili ya kuzisaidia shule hizi kupata vifaa vya michezo pamoja na wataalamu ili kuinua sekta ya michezo hapa nchini.

42. Mheshimiwa Spika, Nchi za wenzetu ambao wanathamini michezo huwa wanakuwa na mkakati maalum wa kuvisaidia   vilabu kuanzisha timu za watoto ambao hupelekwa kwenye Academies za vilabu, na huko watoto hao wanasoma elimu ya kiada pamoja na elimu ya michezo. Kambi ya Upinzani inaishauri serikali kuiga mfano huu na kuanza kuvisadia vilabu ambavyo vitaanzisha Academy hizo kwa kuvipatia ruzuku, na hilo lianze sasa kwani bila kuwa na mkakati wa muda mrefu wa kulea vipaji haitasaidia kukuza michezo kwa kuleta makocha wa kigeni pekee. Sambamba na hilo Serikali iangalie uwezekano wa kutoa ruzuku kwa shule na vyuo binafsi ambavyo vimejihusisha na kukuza vipaji vya michezo.

  • Michezo ya Jadi

43. Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu kuwa hata kabla ya ukoloni, Tanzania tulikuwa na Michezo mingi ya kijadi, hii ni pamoja na mieleka,  bao na mingineyo. Na moja kati ya mambo yalioanishwa wazi kwenye sera yetu ya Michezo ni kukuza Michezo ya jadi. Kambi ya Upinzani inataka kufahamu, je wizara ina mikakati gani ya kukuza Michezo hii? Na katika suala hili zingatio liwe katika Michezo Yote ya kijadi. Michezo hii ikiimarishwa itakuwa ni sehemu muhimu ya kuvutia watalii na hivyo kuliingizia Taifa Fedha za kigeni.

  • Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza

44. Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, moja kati ya majukumu muhimu ya bodi hii ni kuhakikisha kuwa filamu na kanda za video zinazotengenezwa ndani na nje ya nchi hii zinakaguliwa na kupewa madaraja husika kabla ya kuonyeshwa kwa watumiaji au kuonyeshwa mbele ya hadhara ya watu wengi.  Huu ni mpango mzuri kwani taasisi inakuwa na jukumu la kulinda maadili ya nchi yetu.

45. Mheshmiwa Spika, kambi ya upinzani inahitaji kufahamu kama ni taasisi hii ndio yenye mamlaka ya kukagua filamu zinazoingizwa nchini. Na kama hivyo ndivyo ni kwa nini filamu ambazo maudhui yake hayaendani na utamaduni wa Kitanzania zinaingizwa nchini bila ya angalizo lolote? Je maadili ya mtanzania kupitia filamu yanalidwa na nani? Na kama bodi hii inafanya kazi yake kwa makini, mpaka sasa ni filamu ngapi za nje zimekwisha kaguliwa na kukataliwa kuingia nchini kutokana na utafauti wa maadili tulionao na nchi za wenzetu.

46. Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hilo, bodi hii ambayo ilianzishwa miaka ya 70, mpaka leo haina wakurugenzi wa bodi na wala haina mtendaji mkuu. Na imekuwa hivi kwa muda mrefu sana sasa, toka hata nchi yetu haijaingia katika mpango wa vyama vingi. Hii ni ajabu sana.

47. Mheshimiwa Spika, kambi ya upinzani inataka kufahamu hili tatizo litaisha lini? Au hakuna wananchi wenye uwezo wa kuweza kushika nafasi hizi? Tunaitaka wizara kuwa wazi kwa hili na kama hawana uwezo wa kufanya hili tupeni kambi ya upinzani jukumu hilo tuwatafutie watu wenye sifa za kushika nafasi hizo ambazo zimekaa wazi kwa takribani zaidi ya miaka ishirini sasa.

  • Jinsia na Michezo

48.  Mheshimiwa Spika, Kuendeleza usawa Kwa jinsia ni jambo la muhimu kwa maendeleo ya maisha ya wananchi wote kwa pamoja. Kwa kuzingatia hilo, napenda kuipongeza Serikali kwa kutambua kuwa michezo si tu mahitaji ya wanaume pekee bali na wanawake pia na hivyo kutoa fursa sawa kwa watu wote. Hili liko dhahiri katika sera ya Michezo ya taifa ya mwaka 1995.

49.  Mheshimiwa Spika, lakini mizizi ambayo inaendeleza utofauti wa kijinsia, haupo tuu katika ushiriki wa watu wa Jinsia tofauti katika Michezo bali upo pia katika aina za Michezo. Kwa hili, naomba nieleweke vizuri. Napenda kutoa pongezi kwa chama cha Mpira wa miguu Tanzania, kwani kwa nafasi ya kipekee imeweza kupiga hatua katika masuala ya Jinsia. Hili ni kwa sababu sasa, imefanikiwa kuwa na marefa wanawake, pia sasa hivi Tanzania tunayo timu ya mpira ya wanawake katika ngazi ya kitaifa (Twiga Stars).

50.  Mheshimiwa Spika, sanjari na hilo, nguvu zinazoelekezwa katika kuboresha Usawa wa kijinsia kinadharia zinatakiwa zitoke katika pande zote mbili. Na kwa kuzingatia hili naomba kwa nafasi ya kipekee kabisa nigusie mchezo wa mpira wa pete nchini maarufu kama netiboli. Kabla sijaendelea zaidi, naomba kuwapongeza timu ya wanaume ya mpira wa Pete ya POLISI, kutoka Zanzibar kwa kuendelea kutetea ubingwa wao katika mchezo huu, Afrika Mashariki na Kati. Wenzetu wa visiwani, kwa hili wametuzidi na wanastahili pongezi kwani wanadhihirisha wazi kuwa wao elimu ya Jinsia wameielewa vizuri.

51. Mheshimiwa Spika, baada ya kuweka hayo bayana nirudi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sote tunatambua kuwa, bunge ndio kioo cha jamii, ndio taswira ya jamii, pamoja na hilo bunge linatakiwa kuwa chachu ya mabadiliko ya jumuiya yote. Bunge limeweka wazi kuwa usawa wa kijinsia ni moja ya vitu muhimu kwa maendeleo ya wabunge wote. Na ushiriki wa wabunge kwenye Michezo haujatofautiana kwa minajiri ya kijinsia.

52. Mheshimiwa Spika, wabunge wanawake wanashiriki katika Michezo ya mpira wa miguu vizuri kabisa. Lakini mpira wa pete ni tofauti. Timu ya mpira wa pete ya bunge ni ya wanawake tu. Hapa kuna tatizo. Kwa nini wabunge wanaume hawashiriki katika mchezo huu? Hili linaweza kuonekana kuwa si tatizo lakini kwa wanaojali na wanaotaka mabadiliko ya kweli wanaliona hili kama tatizo?

C: SEKTA YA HABARI

  • Tovuti ya Wananchi

53.  Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2007/2008, wizara hii ilikamilisha uanzishwaji wa Tovuti ya wananchi na mkandarasi alikabithi mradi serikalini mwezi wa Aprili 2008, baada ya muda wa majaribio wa mwaka mzima. Wizara husika kwa unyoofu wake inakiri kuwa Tovuti inafanya kazi vizuri kwa ushirikiano kati ya Idara ya Habari (MAELEZO), wizara zote za Serikali pamoja na mikoa katika kujibu hoja za wananchi

.

54. Mheshimiwa Spika, hii inatia fedheha, kwani Tovuti hii ya wananchi imegharimu fedha nyingi sana ambazo ni kodi za wananchi ambao ni masikini na wanazitoa kwa uchungu mkubwa kwa kuzingatia ugumu wa hali ya maisha uliopo nchini.

55. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia hilo, Kambi ya Upinzani inaomba kuchukua nafasi hii kufikisha mezani malalamiko ya wananchi juu ya Tovuti hii. Wananchi wanalalamika kuwa ufanisi wa Tovuti hiyo ni sawa na hakuna. Hii inatokana na ukweli kuwa pamoja na kuwa wananchi wanatumia mwanya huo kutaka majibu kutoka kwa wizara au taasisi zote za Serikali lakini majibu hawapati. Hivi ni ya nini kama haifanyi kazi yake? Kuna umuhimu gani wa kuwa nayo ilhali haisaidi chochote. Hii ni Tovuti tuu bado hatujaangalia simu wala barua.

Kambi ya Upinzani inahitaji majibu ya kina kuhusiana na sakata hili, ni kwanini Tovuti hii haitoi majibu ya hoja za wananchi? Je kazi yake ni nini? Je ni watu gani ambao wako chini ya wizara ambao wamepewa mamlaka ya kufuatilia maswali ya wananchi na kufuatilia majibu?

56. Mheshimiwa Spika, tatizo la tovuti hii linafanana sana na ile ya Ikulu ambayo kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa haifanyi kazi pamoja na ukweli kuwa hivi sasa kuna Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Ikulu ambaye analipwa fedha za walipa kodi kwa ajili ya kuwapatia wananchi habari mbalimbali .

57. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani pamoja na kutambua kuwa Tovuti hii ipo chini ya Ofisi ya Rais inatambua pia kuwa jukumu la kuhabarisha umma lipo chini ya wizara ya habari. Hatuoni umuhimu wa Kuwepo na Mkurugenzi wa Habari kama utendaji kazi wake ndio huu , tunashauri kuwa badala ya kuanzisha vyeo ambavyo havina ufanisi katika utendaji basi sasa ni wakati wa kurudisha utamaduni wa hapo awali wa kuwa na mwandishi wa habari wa Rais na huku majukumu mengine yakiwekwa chini ya wizara hii.

  • Uhuru wa Vyombo vya Habari

58. Mheshimiwa Spika, suala la habari ni suala linalowagusa watanzania wote kwa ujumla na hata wakazi wasio raia wa Tanzania. Haki ya kupata habari kwa wananchi ni haki ya msingi tena inayotambulika kikatiba. Katika nchi yetu ya Tanzania pamoja na ukweli kuwa radio ndio Chanzo kikubwa cha kusambasa habari mikoani, asilimia 56%, runinga na magazeti pia ni vyanzo vikubwa vya habari katika miji, ambao ni asilimia 44% na zaidi ya asilimia 20% (Chanzo: Taarifa ya hali ya umasikini na maendeleo ya watu-2007).

59.  Mheshimiwa Spika, Uhuru wa vyombo vya habari ni jambo la msingi hasa kwa kuzingatia kuwa ndio njia pekee inayoweza kuwapasha wananchi habari zile za uhakika kwa maendeleo ya jamii yote. Na nchi yenye kuheshimu Uhuru wa vyombo vya habari ni nchi ambayo inatambua nini maana ya maendeleo.

60.  Mheshimiwa Spika, Vyombo vya habari ndio vyenye uwezo wa kuweka wazi maovu yanayofanywa na watu na au viongozi wanaotumia nafasi zao vibaya. Hivyo Uhuru wa kufanya kazi yao bila kuingiliwa na nguvu za dola unatuhakikishia uwajibikaji na pia kuchochea utawala bora.

61. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapongeza kazi na majukumu ambayo yamekuwa yakifanywa na waandishi wa habari hapa nchini na jinsi ambavyo wameweza kufanya kazi zao kwa ufanisi pamoja na mazingira ya kazi zao kuwa ni magumu.Tunapenda kupongeza kazi ambayo imefanywa na mwandishi wa habari wa BBC, Vicky Ntetema, kuhusiana na mauaji ya Maalibino hapa nchini mwetu pamoja na wale wote waliofanya vizuri kama Richard Mgamba kwa kushinda Tuzo mbalimbali za kimataifa katika uwanja wa Uandishi wa Habari. Mauaji ya Albino kama alivyofanya Vicky Ntetema ni Habari iliyokuwa ngumu kuifuatilia na kuchunguza na hata ya kuhatarisha maisha yake kwani aliweza kwenda na kuwahoji waganga wa jadi ambao wamekuwa wakijihusisha na mauaji ya Alibino hapa nchini. Taarifa ile inapaswa kuchukuliwa na Serikali na kufanyiwa kazi kwa kina kwani sasa Serikali imeweza kupata taarifa kuhusiana na ni nani haswa hao wanaojihusiha na mauaji hayo. Pia tunataka kujua ni hatua gani zimechukuliwa na serikali ili kumlinda mwandishi huyu kwani kutokana na taarifa yake pamekuwepo na taarifa kuwa waganga wale pamoja na watu wengine wasiojulikana wanamtishia maisha yake.

62.  Mheshimiwa Spika, katika siku za karibuni tumeona viongozi wengi wakishutumu gazeti la MwanaHALISI, ambalo linaongozwa na Mkurugenzi wake Ndugu Saed Kubenea. Mara ya kwanza Alivamiwa ofisini kwake na kumwagiwa kimiminika kinachosemekana kuwa ni Tindikali, lakini hilo halikutosha hivi majuzi  Serikali kupitia vyombo vyake vya dola na hapa tunamaanisha polisi walienda  katika ofisi za gazeti hilo na nyumbani kwa mhariri huyo na kukagua bila ya kuweka wazi nia yao ni nini? Wanakagua bila kusema sababu, na ni dhahiri Polisi haikufuata utaratibu uliowekwa na Sheria katika ukaguzi huo.

63. Mheshimiwa Spika, Je Polisi wako juu ya Sheria hata kama walikuwa na Hati ya Mahakama? Isitoshe, ni vipi polisi badala ya kufuatilia ukweli au la wa Taarifa inapoteza muda na fedha za walipa kodi katika kufuatilia chanzo cha habari? Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri atoe ufafanuzi wa kina katika hali hii ambayo kwa dhahiri inalenga kuua kazi na uhuru wa Vyombo vya Habari.

64. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inadhani waandishi wa habari wenye kutoa taarifa za ubadhirifu kama hizo wanatakiwa kupewa tuzo badala ya kunyanyaswa na kutishwa kwani kwa siku za hivi karibuni ni dhahiri vyombo vya habari vimekuwa mhimili muhimu wa demokrasia na wa mali na rasilimali za nchi yetu.

65. Mheshimiwa Spika, hii si haki hata kidogo. Kambi ya upinzani inahitaji Serikali kutoa tamko juu ya sababu ya msingi ya polisi kuvamia ofisi za magazeti haya na kupekua na kuchukua vitendea kazi kama kompyuta bila ya kutoa sababu. Je, huku sio kuingilia haki ya Uhuru wa vyombo vya habari? Lakini pamoja na hilo, Kambi ya Upinzani inaitaka wizara husika kuleta haraka muswada wa sheria ya habari ndani ya Bunge hili ili mambo kama haya yaweze kudhibitiwa na kisheria ni si kufuata matakwa ya mtu au kundi la watu.

66. Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani, inalaani na kukemea kitendo hiki kwa nguvu zote na  tunapenda kuchukua nafasi hii kuwahakikishia waandishi wa habari wote kuwa tu pamoja nao kwa hali zote. Na katu hatutakaa kimya kuona haki zao zinanyang’anywa kwa njia yoyote. Tutadumisha ushirikiano wetu na kama wana lolote wasisite kututaarifu nasi tutalifanyia kazi.

HITIMISHO

67. Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia Kambi ya Upinzani inataka waziri atoe majibu ya ni kwanini hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Mhe.Dr.Slaa haikuonyeshwa moja kwa moja na shirika la utangazaji la Taifa siku akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi Ofisi ya Waziri Mkuu, Bajeti ya mwaka 2008-2009 na badala yake kituo hicho kikawa kinarudia kurusha hotuba ya Waziri Mkuu kinyume na ilivyozoeleka kuwa hotuba za wabunge wote zinakuwa zikionyeshwa moja kwa moja yaani live. Tatizo hili limejirudia pia siku ya Alhamisi iliyopita, wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu ambapo maswali takriban yote ya Wabunge wa Upinzani kuanzia na Kiongozi wa Upinzani Bungeni hayakuonyeshwa, na mara baada ya hapo Televisioni ya TBC ikaendelea na kipindi cha maswali kama kawaida.  Suala hili linapaswa kutolewa majibu kwani pamekuwapo na malalamiko na manung’uniko kutoka kwa wananchi juu ya tukio hilo. Hili ni Shirika la Utangazaji la Taifa na siku za karibuni imejizolea sifa kwa kuwa na vipindi vizuri. Ni kitu gani kinaanza kujitokeza tena? Dalili hii ya ubaguzi isipokomeshwa na kuchukuliwa hatua basi tunaanza kuporomoka na kuelekea kubaya tena.

68. Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia ningependa kujua juu ya kijiji cha Michezo, jee kimeishia wapi?

69. Baada ya kusema hayo, naomba nitoe angalizo kuwa Kambi ya Upinzani inahitaji majibu ya kina kuhusiana na masuala yote yaliyoulizwa na ni matarajio yetu kuwa majibu yatakayotolewa na wizara yataendana na maswali yaliyoulizwa na si vinginevyo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hivyo naomba kuwasilisha.

………………………………

Mwanawetu Said Zarafi (Mb)

MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI –WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI NA MICHEZO

28.7.2008

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s