Kwa nini Polisi iliwavamia Wapemba usiku wa manane?

Mhe. Khamis Juma Shoka, mbunge wa CUF, Micheweni, aliyesoma hotuba ya Kambi ya Upinzani kuhusu Mambo ya Ndani kwa niaba ya Mhe. Muhammad Sanya

“…Sote tunaelewa kuwa taratibu mahali pengi duniani ambapo heshima na haki za binadamu zinathamniwa, askari wanakuwa na mipaka katika kutekeleza majukumu yao. Mfano, askari hatakiwi kumpekuwa raia zaidi ya saa kumi na mbili jioni.  Kwa msingi huo, napenda Mhe. Waziri alieleze Bunge hili, ni mamlaka yapi yaliyotumika kuwavamia wakazi saba wa Pemba zaidi ya saa saba za usiku waliojiita askari walifanya fujo, wakatishia hata kuvunja milango ya nyumba za hao waliowaita watuhumiwa? Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inauliza je huu si uvunjifu wa haki za raia na kwenda kinyume na matakwa ya Umoja wa Mataifa wa kuheshimu haki za binadamu….?

I. UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, awali ya yote tunapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuwepo hapa tukiwa wazima wa afya na kujadili mambo muhimu yanayogusa maslahi ya umma wa watanzania.

2. Mheshimiwa Spika, Napenda kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani Kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya  Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi kwa mwaka wa fedha 2007/2008, kwa mujibu wa  kanuni za Bunge  toleo la mwaka 2007, kanuni ya  99 kanuni ndogo ya  (7)

3. Mheshimiwa Spika, pili ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa chama changu cha wananchi (CUF) na wapiga kura wangu wa Jimbo la mji Mkongwe Zanzibar kwa mashirikiano mazuri wanayonipatia katika kuhakikisha kuwa ninatekeleza majukumu yangu kama mbunge ipasavyo na kwa umahiri mkubwa ili kutimiza malengo na sera za chama chetu na taifa kwa ujumla.

Aidha naushukuru pia uongozi wa Kambi ya Upinzani chini ya Mhe. Hamad Rashid Mohammed pamoja na Naibu wake Mhe. Dr. Wilborad Slaa kwa mchango wao mkubwa katika maandalizi ya Hotuba hii, pia nawashukuru waheshimiwa wabunge wote ambao ni wajumbe wa Kamati ya Mambo ya nje, Ulinzi na Usalama kwa ushirikiano wao mzuri wanaonipa katika kutimiza wajibu wangu kama Waziri Kivuli wa Wizara hii.

4. Mheshimiwa Spika, Natoa shukrani zangu za dhati kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Laurence Masha pamoja na Naibu wake Mhe. Hamis Sued Kagasheki kwa ushirikiano wao. Sambamba na hilo nawapongeza Viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi kwa jitihada zao katika kukabiliana na uhalifu licha ya hali ngumu kiutendaji wanayokabiliana nayo. Pia tunawashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wote wa uhamiaji pamoja na jeshi la magereza katika kutekeleza kazi zao vyema bila ya kujali muda na hali ngumu ya maisha inayowakabili.

5. Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa utangulizi huo naomba  kutoa na kuomba ufafanuzi kwa masuala mbali mbali ili kuinua utendaji kwa wizara hii.

II.    HALI YA USALAMA NCHINI

6. Mheshimiwa Spika, inaonekana Tanzania si shwari tena, kwani ni hivi karibuni tu kumejitokeza hali inayoashiria baadhi ya watu kujilimbikizia mali isivyo halali. Hali hii italipelekea Taifa letu kutoaminiwa na hata wawekezaji pamoja na raia wavuja jasho kutoiamini tena serikali yao kutokana na mali zao kuvushwa nje ya nchi.

7. Mheshimiwa Spika, tunalitaka jeshi la polisi kufanya kazi zake kisayansi kwa hali ya juu kabisa ili wale watakao bainika na dhambi hizi wafikishwe katika vyombo vya sheria nchini. Hii ndiyo njia ya kurejesha imani kwa raia na kuona kwamba Serikali yao iko makini katika kulinda haki zao pamoja na rasilmali za nchi yao.

8.   Mheshimiwa Spika, Kwanza kabisa kambi ya upinzani inasikitishwa sana na mauaji yanayofanywa kwa makundi maalum ya watu huku serikali ikionekana kushindwa kabisa kutokomeza mauaji hayo. Tunaitaka Serikali kutoa takwimu sahihi hadi sasa ni vifo vingapi vimekwisha tokea, tangu wimbi la mauaji ya  Maalbino yaanze kujitokeza katika mikoa mbali mbali hapa nchini, na ni mkakati gani mahsusi ya  kulilinda kundi hili la watanzania walio na haki ya kuishi kwa furaha na matarajio kama walivyo watanzania na binadamu wote wengine.

9.   Mheshimiwa Spika, sote tunaelewa kuwa taratibu mahali pengi duniani ambapo heshima na haki za binadamu zinathamniwa, askari wanakuwa na mipaka katika kutekeleza majukumu yao. Mfano, askari hatakiwi kumpekuwa raia zaidi ya saa kumi na mbili jioni.  Kwa msingi huo napenda Mhe. Waziri alieleze Bunge hili ni mamlaka yapi yaliyotumika kuwavamia wakazi saba wa-Pemba zaidi ya saa saba za usiku waliojiita askari walifanya fujo, wakatishia hata kuvunja milango ya nyumba za hao waliowaita watuhumiwa.

10.  Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inauliza je huu si uvunjifu wa haki za raia na kwenda kinyume na matakwa ya umoja wa Mataifa wa kuheshimu haki za binadamu na za raia?

III. CHANGAMOTO ZINAZOLIKABILI JESHI LA POLISI

  1. Mheshimiwa Spika, ni jambo la kusikitisha kwamba chombo muhimu kama jeshi la polisi linakabiliwa na matatizo makubwa yanayolizuia kufanya kazi kwa ufanisi na huku serikali ikiyafumbia macho mambo haya.

Kambi ya Upinzani inasema hayo kwa kufanya marejeo ya taarifa ya mkuu wa jeshi la polisi nchini inayosomeka kama “CHALLENGES OF ENHANCING PERFOMANCE AND RESPONSIVENESS IN THE POLICE FORCE’’ kama alivyoitoa tarehe 18 Juni, 2008. Taarifa hiyo iliainisha yafuatayo ambayo tunaitaka Serikali iyashughulikie kwa kuyapa kipaumbele na kuyatatua:

1)    ukosefu wa rasilimali watu za kutosha

2)    muundo wa kitaasisi usio wa kiufanisi katika jeshi hilo

3)    mfumo duni wa habari na mawasiliano.

4)    vyanzo vya mapato na fedha visivyotosheleza.

13.   Mheshimiwa Spika, hali hii inasikitisha iwapo kweli tunakusudia kuwa na jeshi la polisi ambalo tunalitaka litulinde katika uhalisia wake. Kambi ya upinzani inaishauri serikali kwamba ni lazima zichukuliwe juhudi za makusudi ili kuboresha hali mbaya ya jeshi hilo kwa kuangalia undani wa matatizo hayo, chimbuko lake ni moja tu, nalo ni kuwa kasma ni ndogo. Kambi ya Upinzani inasema ni kwa nini Jeshi la Polisi nalo lisitengewe kasma kama ambavyo wanawezeshwa usalama wa taifa?

14.   Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona hiki kinaweza kuwa ni chanzo kikuu cha malalamiko toka kwa wananchi kuwa utendaji wa jeshi la polisi  huko chini na usiofuata maadili yao ya kazi. Askari ni binadamu kama wengine, hivyo kutowawezesha vizuri kwa kadri ya kukidhi mahitaji ya msingi ya familia zao kunasababisha askari hao kuingia kwenye vishawishi vya kukiuka maadili ya viapo vyao.

15.   Mheshimiwa Spika, ukweli wa mambo ni kwamba askari wote wa jeshi la polisi ni wenye nidhamu ya hali ya juu kabisa katika utendaji wao, ila tu kilichokosekana ni haki zao za msingi kutopatikana kutokana na uzito wa kazi zao. Naomba ieleweke kwamba njaa ndiyo iliyokosa nidhamu kwani ikianza kutokota basi kinachofuatia ni askari hawa kuanza kufanya mahesabu ya wapi wapenye ili kutuliza tumbo lake. Na huo ndio mwanzo wa rushwa. Hivyo ni jambo la busara mishahara na posho zao zipandishwe ili ziendane na hali ya maisha ilivyo na zitolewe katika muda mwafaka.

16.   Mheshimiwa Spika, inaeleweka vyema kwamba kazi hii haihitaji muda wa mapumziko, kwani zile siku ambazo raia au hata wafanyakazi wanapopata mapumziko au kusherehekea sikukuu mbali mbali nchini askari yeye huwa ndiyo wakati wake mgumu wa kuhakikisha kwamba kila kitu kinakwenda vizuri na salama.

17.   Mheshimiwa Spika, askari kukosa sare angalau mbili kila mmoja ni kasoro kubwa katika jeshi hili, hivi askari atakapo amua kufua sare yake na bahati nzuri ikanyesha mvua na tena bahati mbaya akahitajika ghafla kituoni atakwenda akiwa kavaa nini? Serikali iliangalie sana suala hili.

18.   Mheshimiwa Spika, cha kushangaza hata hao ambao huwa wanatoa sare na vifaa vyingine kwa njia halali za zabuni wanadai mabilioni ya shilingi na bado hawajafikiriwa kulipwa, hivi ni uhakiki gani au uchunguzi gani wa madeni hayo usiokwisha? Mdaiwa anapokuwa hodari wa kulipa basi hutoa nafasi nzuri ya kukopeshwa tena. Tusiogope kukopa kwani bado ni maskini lakini vile vile tuwe mahodari wa kulipa kwani hao wakopeshaji hutumia mikopo ya benki na wanapocheleweshwa malipo yao mwishowe hujikuta badala ya faida wamepata hasara, na hii inatokana na kiwango cha riba kuzidi kupanda kutoka katika mabenki waliyokopa.

IV.   MPANGO WA ULINZI JAMII/SHIRIKISHI

19. Mheshimiwa Spika, Mpango huu si mpya hapa Tanzania. Pamoja na kuwa haukuwepo kisheria na wala haukuwekewa utaratibu mzuri, utaratibu wa SUNGU SUNGU umekuwepo katika nchi yetu kwa muda mrefu. Wananchi katika maeneo yao waliwekeana utaratibu wa kujilinda wao na mali zao.

Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwaeleza watanzania ni sababu gani za msingi zilizosababisha mpango huo wa SUNGUSUNGU kutowekewa utaratibu mzuri na wa kisheria kuliko unavyoendelea hivi sasa katika maeneo mengi lakini hauratibiwi rasmi na Sheria. Jamii ingetakiwa kupewa mafunzo ya awali, ikiwa ni pamoja na mafunzo ya matumizi ya Silaha. Uwepo wa SUNGUSUNGU ungewekwa kisheria tofauti na ilivyokuwa ikifanya kazi. Matumizi haya si mageni sana duniani kwani hata nchi zilizoendelea kama Uswisi, Marekani ambapo ulinzi jamii wanaita “citizen on patrol- cop” wanatoa mafunzo ya kiulinzi na usalama kwa kila raia.

20.   Mheshimiwa Spika, mpango wa Polisi Jamii na au Sungusungu uliigwa kutoka katika nchi mbali mbali duniani kama vile uingereza na Marekani. Hata hivyo mpango huu katika nchi hizo umeshindikana kutekelezwa kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo ya ongezeko kubwa la idadi ya watu, maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Hizi  ni sababu ambazo kwa Tanzania hazihitaji kutafutwa ziko wazi na ni wazi kuwa mpango huu unatakiwa kufanyiwa upembuzi yakinifu na kujua sababu za kufanikiwa na kufa kwa mpango huu wa SUNGUSUNGU.

V.     KANDA MAALUM YA DAR ES SALAAM

21.   Mheshimiwa Spika, Jeshi la polisi liliamua kuanzisha kanda maalum ili kuwezesha utendaji wenye ufanisi. Pamoja na lengo hili serikali haionekani kulitia maanani jambo hili kwani inashangaza kuona kwamba katika mwaka huu wa fedha kanda hii haikutengewa fedha zikiwemo za mafuta ya magari, jee kanda hii itafanyaje kazi. Hii ni sawa na kuweka sufuria katika jifya lisilo na moto, chakula kitaivaje?

22.   Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona hali hii ndio chanzo kinachopelekea baadhi ya polisi kuwadai wananchi fedha kwa ajili ya kufuatilia matukio ya uhalifu wakati wanapopewa taarifa za kutokea kwa matukio hayo. Hivyo basi, tunajiuliza kama hali ndio hiyo uhalifu kweli utakwisha katika mkoa wa Dar es Salaam?

VI.   UTARATIBU WA KUJIENDELEZA KIMASOMO KWA ASKARI POLISI

23.   Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa hii ni karne ya sayansi na teknolojia, na ili mtu apate  ufanisi katika utendaji wa kazi yoyote anayoifanya kuna haja ya kuwa na elimu inayoendana  na wakati. Pamoja na ukweli huu jeshi la polisi linaonekana haliamini mpango huu, kwasababu suala la kutoa ruhusa kwa watendaji wake hasa wa ngazi za chini kujiendeleza kimasomo linaonekana kuwa ni gumu sana. Katika hili nitafanya marejeo kwenye barua ya wazi iliyoandikwa kwa mheshimiwa waziri wa mambo ya ndani katika gazeti la Nipashe toleo la Jumamosi tarehe 5 Juali 2008, naomba ninukuu sehemu ya barua hiyo ….    “sisi kama askari polisi hatuwezi kamwe Kuendana na hali hii ya dunia kuwa kama kijiji bila ya kuwa na elimu ya kutosha ili kuweza kuwiana na majeshi mengine duniani. Hili tunalieleza wazi kwako ili ufahamu ukiritimba tunaofanyiwa sisi wanao (askari polisi) kwani kulingana na mkataba wa kufanya kazi kulingana na mujibu wa Police General Order (PGO) kuwa unapoanza kazi utafanya kazi kwa muda wa miaka mitatu ndipo uruhusiwe kwenda kujiendeleza kimasomo kwa yule anaehitaji’. Malalamiko haya yamesikika pia kila kona ya nchi kutoka kwa askari wa ngazi za chini.

24.   Mheshimiwa Spika, kama hali hii ipo kweli, basi ni jambo la kusikitisha kwani jeshi letu la polisi kwa kawaida linaajiri vijana wengi waliomaliza kidato cha nne na kama hawapewi nafasi ya kujiendeleza tutakua na jeshi la polisi lililo bora?

<!–[if !supportLists]–>25. <!–[endif]–>Mheshimiwa Spika, kama hali hii  ipo na kwa kuwa  jeshi letu  la polisi mara nyingi huajiri vijana wengi waliohitimu elimu ya kidato cha nne, jee tutaweza kuwa na askari wenye vigezo na umahiri wa kushiriki katika harakati za kijeshi kama Interpol na nyinginezo.

Mheshimiwa Spika, ili kwenda sambamba na maendeleo ya kitaaluma kwa sasa, kambi ya upinzani inashauri kuwa utaratibu mahsusi uandaliwe utakaowawezesha askari polisi kujiendeleza katika taaluma za kawaida, kwa wale wachache au hata wengi watakaotaka kujiendeleza kielimu.

UTARATIBU WA KUPANDISHA VYEO

26.   Mheshimiwa Spika, kulingana na taratibu za kazi za jeshi la polisi PGO na Police Force Service Regulations kupandishwa cheo au vyeo ni haki ya kila askari kwa mujibu wa kanuni hiyo, pia inaeleza kwamba katika kila baada ya kipindi cha miaka 3 askari polisi atapanda cheo kutoka hatua moja kwenda nyingine iwapo katika kipindi hicho hatakuwa amehusishwa na kosa lolote la kinidhamu ambalo litasababisha kutokupanda kwake.

27.   Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kanuni za jeshi hilo kwa kipindi hicho cha miaka mitatu ni lazima askari apewe au aende katika mafunzo. Tofauti na hapo ni kumnyima haki yake ya kiutumishi askari huyo.

28.   Mheshimiwa Spika, suala hili limekuwa likilalamikiwa sana na askari wengi wa jeshi la polisi hasa kwa wale wenye vyeo vya chini au wasiokuwa na vyeo kabisa. Wako wanaodai kuwa upatikanaji wa vyeo hivi unapatikana kwa upendeleo au kwa vigezo visivyokuwa wazi.

29.   Mheshimiwa Spika, kambi ya upinzani ingependa kuiuliza serikali jee taratibu zinazotokana na kanuni hii zinafuatwa ipasavyo na kama zinafuatwa kwa nini malalamiko yamekuwa mengi. Inakuwaje askari amelitumikia jeshi hilo kwa miaka 20 lakini anastaafu akiwa hana cheo au anastaafu na cheo cha CPL au SGT?

30.   Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kuna waraka uliotolewa wa WP kwa wale wote ambao walikwisha kuwa na vyeo walivyonavyo kwa muda wa zaidi ya miaka miwili, kwenda katika mafunzo kwa ajili ya kupandishwa vyeo. Jambo la kustaajabisha ni kuwa waraka huo haukuhusisha askari wa kiume ambao nao walistahili kupandishwa vyeo.

31.   Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona huu ni ubaguzi wa dhahiri kijinsia na unachangia kwa kiasi kikubwa kuligawa jeshi la polisi. Tukumbuke katika vyombo vya Ulinzi vyeo vinatokana na muda wa utumishi na juhudi binafsi katika utendaji wa kazi. Kuweka siasa, na mipaka ya kijinsia katika vyombo vya Ulinzi ni kuharibu sifa nzuri iliyokuwepo.

32. Mheshimiwa Spika, cheo katika utumishi maana yake ni maslahi, je wanaume hawahitaji maslahi hayo? Kwa hili tunaitaka Serikali kuliangalia upya suala zima la upandishwaji wa vyeo. Sambamba na hilo kutokuwahamisha askari polisi kumesababisha matatizo mengi sana kunakopelekea hata askari hao kusahau wajibu wao na kuanza kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa sheria. Hivyo tunaitaka Serikali kuliangalia kwa makini suala hili la kuwahamisha vituo askari kulingana na kanuni na taratibu zao za utumishi zinavyosema.

VI. MRADI WA POLISI WANAOTUMIA PIKIPIKI KATIKA MPANGO WA KUPAMBANA NA UJAMBAZI

33.   Mheshimiwa Spika, huu ni mpango maalum ambao unatumika hasa na jeshi la polisi katika jiji la Dar es salaam. Huu sio mpango mbaya katika harakati za kuhakikisha jeshi la polisi linatimiza majukumu yake ya kulinda usalama wa raia na mali zao nchini.

Mheshimiwa spika, pamoja na nia njema ya kuasisi mpango huu, kambi ya upinzani inapenda kuhoji mambo yafuatayo:

(1) Je serikali imetathmini kiasi gani juu ya ufanisi wa mpango huo na lengo lililokusudiwa? Jee takwimu za matukio ya ujambazi au uhalifu ambayo yameshawahi kuzuiwa au kuepushwa ni ngapi zilizotokana na juhudi za askari wa mpango huu. Hili tunaliuliza kwa sababu askari hawa hutumia gharama kubwa za mafuta ya piki piki kwa ajili ya zunguka zunguka hiyo.

(2) Je serikali inachunguza kwa kiasi gani utendaji wa kikosi cha askari hao, kwani kumekuwa na malalimiko ya kuleta usumbufu kwa baadhi ya askari kudai rushwa hasa kwa madereva na makondakta wa madala dala  na hata raia wa kawaida. Askari hao wamekua wakipewa majina tofauti kama vile tigo kutokana na tabia zao.

34. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaomba serikali ifanye uchunguzi yakinifu kuangalia ufanisi wa mpango huu, na ikiwezekana ni vyema kila mara uwe unafuatiliwa kwa karibu isiwe ni kero kwa wananchi bali uwe ni faraja kwa raia wa nchi hii.

VII. KITENGO CHA IDENTIFICATION BUREAU

35.   Mheshimiwa Spika, Kitengo hiki ni muhimu sana kwa utendaji wa kila siku wa jeshi la polisi. Kazi nyeti zinazofanywa na kitengo hiki ni pamoja na uhakiki wa alama za vidole, kuangalia silaha lakini kwa ujumla wake ni kuhakiki vielelezo mbali mbali vinavyohitaji kufanyiwa uchunguzi wa kina na kutolewa taarifa inayokidhi haja. Pamoja na kutoa zabuni kwa kampuni ambayo iliuza vifaa hivyo kwa jeshi la polisi (Technobrain) ni jambo la kusikitisha na la ajabu kwamba inasemekana kampuni hiyo iliyouza vifaa hivyo, haikuandaa mkakati wa lazima wa kuwaelimisha askari wa jeshi la polisi kuweza kuwafunza na kuwapa taaluma ya kutumia vifaa hivyo, badala yake jeshi la polisi limeajiri watu nje ya jeshi hilo kufanya kazi hizo nyeti.

Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ieleze ni kwanini askari waliokula kiapo cha utumishi wasipewe mafunzo ya kufanya kazi hiyo nyeti? Na kwa kuwa bado hatujachelewa, ni lini sasa Askari wetu watapatiwa mafunzo ama ndani au nje ya nchi ili kitengo hiki kwa asilimia mia moja kiendeshwe na jeshi la polisi peke yake.

VIII. UTOAJI WA SILAHA

36.   Mheshimiwa Spika, umiliki wa silaha kwa watu binafsi unahitaji  kufuata taratibu za kwanza kupitia kwa watendaji katika ngazi ya Kijiji na au mtaa kwa mijini.Lengo na nia ikiwa ni pamoja na kuthibitisha makazi, uadilifu na kuaminika kwa mwomba silaha.

37.   Mheshimiwa Spika, utaratibu huu una udhaifu mkubwa sana, kwani inawezekana  rushwa ikatumika kwa wale wasiofuata utaratibu vizuri na kwa uadilifu. Kukosekana kwa uadilifu kwa viongozi katika ngazi hiyo kuna hatari ya kuruhusu wahalifu kupenya na kumiliki silaha kwa kulipa “kitu kidogo”.

Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali iangalie upya utaratibu huu na kuusimamia kikamilifu ikibidi usimamiwe na au mwombaji athibitishwe na Mkutano Mkuu wa Kijiji kuliko kazi hiyo kuachiwa WEO au VEO peke yake. Ngazi ya Polisi iwe makini kuthibitisha kuwa taratibu zimefuatwa kwa kutumia utaalamu wao kabla hatua za kuidhinisha utoaji wa Silaha kuchukuliwa katika ngazi za juu. Mahali pengine hata wanatumia kinachoitwa Kamati za  “Ulinzi na Usalama” za Kata chombo ambacho hakiko kisheria. Kwa utaratibu huu Polisi  watashindwa kukataa kutoa vibali kwani tayari kamati za Ulinzi na usalama ambazo si vyombo vya kisheria  wanakuwa wametoa baraka zao.

IX. MPANGO WA KUONDOA MAMLAKA YA KUENDESHA KESI KWA POLISI NA KUENDESHWA NA IDARA YA MKURUGENZI WA MASHTAKA

38.   Mheshimiwa Spika, huu ni mpango muhimu sana katika kuhakikisha haki za raia katika taasisi ya mahakama nchini inatendeka kwa wakati na ipasavyo. Jukumu la uendeshaji mashtaka kufanywa chini ya ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka litasaidia ufanisi mkubwa tofauti na hapo awali ambapo lilikuwa chini ya jeshi la polisi waliokuwa na kazi ya kukamata wahalifu, kupeleleza makosa, kuwapeleka magerezani na kuendesha upelelezi katika mashtaka husika, hali ambayo ilileta malalamiko mengi hasa yale ya ucheleweshwaji wa kesi kwa hoja kuwa uchunguzi na ushahidi bado haujakamilika.

39.   Mheshimiwa Spika, ufanisi huu tunaouzungumza utapatikana kwa sababu jeshi la polisi sasa litabaki na jukumu moja tu la upelelezi.

<!–[if !supportLists]–>40. <!–[endif]–>Mheshimiwa spika, pamoja na nia hii njema, kambi ya upinzani bado ina wasi wasi na upatikanaji wa ufanisi huo. Hii inatokana na kwamba hata DPP (ELIAZA FALESHI) alikiri kuwa pamoja na kuasisiwa kwa mpango huu bado kutakuwa na uhusiano wa karibu utakaoendelea kati ya polisi na idara hiyo na mawakili wa serikali, kwani upelelezi na uendeshaji wa mashtaka ni vitu vinavyohusiana sana.

Wasi wasi wetu ambao tungependa serikali iweke wazi ni kuwa itatumia mikakati gani kuhakisha ucheleweshaji na usumbufu uliokuwepo katika kipindi cha nyuma hautokei tena baada ya kazi hizi mbili kutenganishwa. Kwa mfano DPP katika taarifa yake alieleza kuwa katika kutekeleza mpango huu mawakili wa serikali au wanasheria wa serikali (state attorneys) 157 wameajiriwa na kupelekwa katika mikoa 13. Idadi hii ya mawakili hawa ni ndogo sana ukilinganisha na ukubwa wa Tanzania na haja na malengo ya mpango wenyewe. Lakini pia upelelezi lazima bado unafanywa na Jeshi la Polisi. Kambi ya Upinzani inadhani bila kuwa na sheria inayoweka viwango vilivyowazi mathalan upelelezi lazima ukamilike ndani ya muda fulani, na kama haujakamilika kibali lazima ipatikane kwa ngazi fulani nayo kibali hicho kiwekewe masharti tutakumbana na urasimu mkubwa zaidi kuliko hata awali.

41.   Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo ya mpango huu, kambi ya upinzani inataka pia mambo yafuatayo:-

(a) serikali iboreshe utendaji wa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa kuajiri watendaji wa kutosha hasa state attorneys.

(b serikali iboreshe Taasisi mpya ya mafunzo ya uanasheria (LAW SCHOOL OF TANZANIA) ili kuhakikisha inatoa wahitimu wa kutosha na walio mahiri ambao watafanya kazi katika idara ya mkurugenzi wa mashtaka na kushikilia nafasi zilizokuwa chini ya polisi. Ili kuboresha Law School ni lazima itambuliwe kama Taasisi ya Elimu ya Juu na wanafunzi wake wastahili mikopo ya kutoka Bodi ya Mikopo ili kuwawezesha watarajali hao kumudu masomo hayo.

X.     INTERPOL DEPARTMENT

42.   Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba kitengo hiki kimeanzishwa ili kurahisisha utendaji wa jeshi la polisi hasa kwa mambo yanayohusisha mataifa tofauti. Kwa mfano hivi karibuni kitengo hiki kiliendesha msako wa kuyakamata magari yaliyoibiwa kutoka japan, UK, Afrika Kusini na Kenya na kuingizwa Tanzania. Jumla ya magari 42 yalikamatwa.

<!–[if !supportLists]–>43. <!–[endif]–>Mheshimiwa Spika, katika hotuba iliyopita nilikitaka kitengo hiki kifanye kazi ya kumtafuta mtoto MARIAM FARID wa Zanzibar aliyetoroshwa na mwalimu wake ambaye ni Mganda, lakini inasikitisha kwamba hadi hii leo kitengo hiki hakijafanikisha kumtafuta na kumpata mtoto huyu hali ambayo imeleta majonzi yaliyokatisha tamaa kabisa kwa familia ya mtoto huyo mdogo. Kambi ya Upinzani inataka maelezo ya Serikali je kati ya magari na binadamu ni kipi kina thamani zaidi? Kwanini Interpol hufanya juhudi kubwa pale magari yanapoibiwa lakini kwa kumtafuta binadamu haionyeshi kama kuna juhudi zozote zinachukuliwa kumtafuta binadamu huyo. Wala hakuna taarifa inayotolewa. Huu si uwajibikaji bora wa kitengo hiki na hakijengi taswira nzuri kwa jamii ya watanzania.

XI.   MAGEREZA

44.   Mheshimiwa spika, idara ya magereza ni mojawapo ya idara muhimu katika Serikali yetu. Dira ya idara hii ni kuwa mfumo wa kurekebisha raia waliopatikana na hatia ya kuvunja sheria za nchi ili watokapo gerezani wawe raia wema katika jamii yetu.

45.   Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao hiki ni chombo muhimu kinachokusudiwa kurekebisha tabia zisizokubalika za wanajamii hasa wale wanaoshikiliwa kwa matendo ya uhalifu na yasiyo ya kimaadili.

46.   Mheshimiwa Spika, falsafa ya kuwa na chombo hiki kwa Tanzania inaonekana haileweki kwani kwa muda mrefu suala la uboreshaji wa mfumo mzima wa magereza umekuwa ukipigiwa kelele na watu pamoja na taasisi mbali mbali lakini mabadiliko katika maeneo ya msingi yanayolalamikiwa hayaonekani.

47.   Mheshimiwa Spika, dhana ya magereza duniani ni kuwa vyuo vya mafunzo ili kuwabadilisha tabia wahusika kutoka katika mwenendo mbaya na wawe raia wema. Lakini kinachosikitisha ni kwamba Tanzania tumeyageuza magereza na kuwa TORTURE CAMPS, kwa wafungwa kuwekwa katika mazingira mabaya, kupewa au kufanyishwa kazi ngumu na kutozingatiwa au kunyimwa haki nyigine za msingi zikiwemo za chakula. Hii ni dhahiri kwani hata kiwango cha kilichotengwa na Serikali katika bajeti hii ni nusu tu ya mahitaji.

48.   Mheshimiwa Spika, Katika hotuba ya mwaka jana Kambi ya Upinzani iliyataja magereza ya kilimo kama vile , Gereza la Kigongoni- Bagamoyo, Gereza la Kiberege –Morogoro, Gereza la Wami Mkuu, Gereza la Kibiti- Pwani n.k. Magereza haya  bado yanazalisha ingawaje takwimu zinaonyesha si kwa kiasi kama kile kilichokuwa kikizalishwa miaka ya nyuma. Pamoja na uzalishaji huo wafungwa katika magereza hayo wanaishi katika hali ngumu sana ya kupata chakula. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe malelezo ya kina Kuhusu hali ya kuishi na vitendea kazi kwa ajili ya uzalishaji mashambani katika magereza hayo, na kiasi gani halisi kinazalishwa katika magereza hayo katika miaka 5 iliyopita na chakula hicho kimetumika vipi?

49.   Mheshimiwa Spika, aidha, kambi ya upinzani inashauri kuwa mfumo mzima wa magereza urekebishwe ili uendane na falsafa ya kuwa na magereza na sio kuwa na torture camps kama ilivyo sasa.

XIII. UBORESHAJI WA USAFIRI WA MAHABUSU NA WAFUNGWA

50.   Mheshimiwa Spika, Hivi karibuni serikali imezindua mkakati wa kuboresha usafiri wa mahabusu na wafungwa wanaotoka na kwenda mahakamani kwa kutumia mabasi ya kisasa badala ya kutumia makarandinga.

Hili ni jambo la kutia moyo na kufurahisha kwani inaonesha kuwa Serikali imetambua na kujali kwamba mahabusu na wafungwa ni binadamu na raia wenye kuhitaji huduma nzuri.

51.   Mheshimiwa Spika, maboresho haya yasiishie tu kwa magereza ya Dar es salaam kama hali ilivyo sasa na yasiishie katika kipengele cha usafiri bali pia yaendelea katika maeneo mengine muhimu kwa mahabusu na wafungwa. Maeneo hayo ni:-

(a) makazi ya wafungwa na ya askari yaboreshwe kwa kujenga nyumba ambazo zitafuata viwango vya nyumba za kuishi binaadamu kama ilivyo katika magereza ya nchi nyingine nyingi duniani.

(b) aina za kazi na adhabu wanazopewa wafungwa na mahabusu,  yasiwe ni sehemu ya kumaliza uhai/uwezo wa kimwili wa mhusika kwa mateso makali yasiyo ya lazima bali yawe ni vyuo vya mafunzo kwa ajili kurekebisha tabia

XIV. UHUSIANO KATI YA POLISI NA MAGEREZA (symbiotic relationship)

<!–[if !supportLists]–>52. <!–[endif]–>Mheshimiwa Spika, Jeshi la polisi na Jeshi la magereza ni sawa na mtu na nduguye. Magereza wanacho kitengo chao cha ujenzi na vilevile ni watengenezaji wazuri wa samani za nyumbani na ofisini. Kitengo hiki kinaweza kutumika pia kwa manufaa ya Jeshi la Polisi.

Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri kuliangalia jambo hili kwa makini, kwani kama ukiangalia kiasi cha fedha zinazotengwa kila mwaka kwa ajili ya ununuzi wa  samani,  na eneo zima la ujenzi wa  nyumba za askari badala ya kandarasi hizo kupewa kampuni binafsi kazi hiyo inaweza kufanywa vizuri sana na jeshi la Magereza. Uhusiano huu ndio utakaokuwa wa tija kwa Wizara hii.

53.   Mheshimiwa Spika, katika hili ningependa nitoe mfano kutoka serikali ya mapinduzi Zanzibar ambayo inatumia ipasavyo symbiotic relationship katika miradi yake ya maendeleo, hali halisi kwa hili ni ule mradi wa ukamilishaji wa nyumba za maendeleo MICHENZANI Zanzibar ambazo zilijengwa na vikosi vya SMZ kama vile JKU, MAGEREZA, KVZ, KZU tu na si makampuni binafsi ambayo huwa na gharama kubwa.

54.   Mheshimiwa Spika, kama hili likiendelezwa vizuri, magereza yanaweza kutumika kama taasisi za uzalishaji na mafunzo badala ya kutumika kama torture camps kama ilivyo sasa.

55.   Mheshimiwa Spika, kambi ya upinzani inapendekeza kuwa serikali itilie maanani suala la matumizi ya ‘symbiotic relationship’ katika mipango na tasisi zake ili kuongeza kipato na kupunguza gharama kubwa zisizo za lazima.

XV. IDARA YA MAMBO YA NDANI: WAKIMBIZI NA MAKAMBI YA WAKIMBIZI

56.   Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikibeba mzigo mkubwa kwa wakimbizi kutoka nchi mbali mbali za kiafrika tulizopakana nazo kama vile Burundi. Rwanda, DRC n.k., tatizo hili mara kadhaa limekua likisumbua hata bajeti ya taifa katika kutoa huduma kwa wananchi hao wageni.

57. Mheshimiwa Spika, kuna taarifa kwamba makambi mengi ya wakimbizi yamefungwa kutokana na baadhi ya wakimbizi kurudi katika nchi zao lakini bado taifa lina mzigo mkubwa wa wakimbizi wapatao 160,000 waliopo katika makambi manne ya Lugufi 1, Nduta, Mtabila, na Nyarugusu licha ya kambi ya Lukole A kufungwa hivi karibuni.

58. Mheshimiwa Spika. pamoja na kuwa serikali inafanya juhudi kubwa katika kuwahudumia wakimbizi ikishirikiana na jumuia za kimataifa, lakini kwa sasa na kwa maoni ya kambi ya upinzani ni kwamba serikali ibadilishe sera yake kwa kukemea vikali matendo ya nchi au viongozi wakuu wa nchi jirani yanayoashiria au yatakayopelekea kutokea kwa ghasia zitakazosababisha ongezeko la wakimbizi kuliko kusubiri kuwahifadhi na kuwahudumia wakimbizi, hii ni kwa sababu kinga ni bora kuliko tiba.

59. Mheshimiwa Spika, hili linawezekana, na mfano mzuri ni kama ule ulioonyeshwa kwa Zimbabwe ambapo Waziri Bernard Membe alitoa tamko kumtaka raisi huyo ahakikishe uchaguzi unakuwa huru na wa haki ili kupunguza maafa yasiyo ya lazima. Pia njia za usuluhishi baina ya pande zinazogombana ni hatua muafaka katika kupunguza idadi ya wakimbizi. Mfano usuluhishi wa Kenya, bila usuluhishi wa aina ile leo hii tungekuwa na wakimbizi wengi kutoka Kenya.

XVII. URAIA WA NCHI MBILI

60.   Mheshimiwa Spika, Suala la kuwa na uraia wa nchi mbili limekua ni kilio cha muda mrefu katika nchi yetu, hii ni kutokana na kusambaa kwa watanzania katika nchi mbali mbali duniani. Katika bajeti iliyopita suala hili lilielezwa kuwa lipo ngazi ya baraza la mawaziri kwa maamuzi.

61.   Mheshimiwa Spika, pamoja na ahadi iliyotolewa Inasikitisha kwamba suala hili bado linaonekana halijapewa uzito wa aina yake. Hii ni kwa sababu hivi karibuni Mheshimiwa Khamis Kagasheki aliliambia bunge hili wakati akijibu swali la Mheshimiwa Jecha kwamba serikali ya muungano wa Tanzania na serikali ya mapinduzi ya Zanzibar bado inaliangalia suala hili kwa makini na mchakato utakapokamilika muswada utaletwa Bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa.

62.   Mheshimwa spika, hapa tunaona kuwa kauli ya waziri katika bajeti ya mwaka jana na kauli ya naibu waziri ya juzi zinapingana. Swali jee kwa usahihi mpango huu umefikia wapi?

63.   Mheshimiwa spika, pia kauli ya Naibu Waziri wa mambo ya ndani ilinishangaza na kukatisha tamaa kwa kusema kuwa suala la uraia wa nchi mbili linahitaji muda mrefu kwa vile linahusisha Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar kwa sababu suala la uraia ni la muungano, hivyo sheria ikipitishwa na bunge inafanya kazi na Zanzibar.

64.   Mheshimiwa Spika, naibu waziri katika jibu lake alibainisha matatizo yatokanayo na kukosekana kwa uraia wa nchi mbili kama vile watanzania wengi wanapoteza uraia wao wa kuzaliwa mara wanapopata uraia wa nchi nyigine kwa sababu kwa mujibu wa Katiba yetu kuwa na uraia wa nchi mbili sio halali.

65.   Mheshimiwa Spika, kambi ya upinzani inaitaka serikali itekeleze ahadi zake kuhakikisha Katiba inarekebishwa ili kuruhusu watanzania kuwa na uraia wa nchi mbili na visitumike visingizio visivyo na msingi.

VIII. VITAMBULISHO VYA UTAIFA

66.   Mheshimiwa Spika, suala la vitambulisho vya utaifa/uraia ni kilio cha muda mrefu cha watanzania. Kwa mujibu wa taarifa ni kuwa mchakato wa kutangaza zabuni kwa ajili ya wakala wa kulishughulikia jambo  hili umeshaanza kama ilivyotolewa na Mratibu Mkuu wa mradi huu Bwana DIKCSON MAIMU. Hoja yetu katika hili ni kuwa serikali bado inataka kuchelewesha upatikanaji wa vitambulisho hivyo. Kwa mujibu wa taarifa ya bwana Maimu ni kuwa mradi huo utakamilika ndani ya miaka mitano kutoka sasa.

67. Mheshimiwa Spika, hii ni kwa sababu hakukuwa na haja ya kuitangaza zabuni kutafuta makampuni au wakala mpya kwa ajili ya mradi huu kwani RITA ni wakala tosha na mahiri kabisa ambae anafaa kupewa kazi hii kwa vile ina takwimu za kutosha za watanzania wote.

68. Mheshimiwa Spika, serikali ibainishe wazi na kuondoa utata na hofu miongoni mwa watanzania kuwa itatoa vitambulisho vya uraia (NATIONAL IDENTITIES). Hii ni kwa sababu hizi ni dhana mbili tofauti na pia kuna taarifa kuwa vyeti vya kuzaliwa havitakuwa na umuhimu kwani vitambulisho hivi vitatolewa kwa watu ambao sio watanzania lakini wanaishi Tanzania jee ni vigezo gani vitatumika?

69. Mheshimiwa Spika, kambi ya upinzani inaomba serikali iwe makini katika kuliendea jambo hili hasa hatua mzima ya kumpata mzabuni ili isiingize ufisadi ndani yake na kuliingizia taifa gharama zisizo za lazima kama zile zilizosababishwa na uzalishaji wa umeme wa dharura kwa MAKAMPUNI YA RICHMOND NA DOWANS.

70. Mheshimiwa Spika, kambi ya upinzani inaishauri serikali kuzingatia yafuatayo katika kuunda mchakato mzima wa mradi wa vitambulisho vya utaifa.

(1) vitambulisho viwe vya kudumu na visivyoweza kufojiwa kwa haraka. Hili litawezekana kwa kutafuta makampuni yanayotoka katika nchi zinazotumia vitambulisho hivyo kwa muda mrefu sasa kama vile Uingereza, Marekani na hata Rwanda.

(2) Serikali iwe makini katika wakala wa usajili wa vizazi na vifo kwani hapa ndio sehemu ambayo mtu anaweza kupenyeza taarifa za kunghushi ili baadae apate kitambulisho cha utaifa.

(3) Kampuni itakayopewa jukumu la kutengeneza vitambulisho hivyo ishirikiane bega kwa bega na wakala wa usajili wa vizazi na vifo( RITA) ili kupata takwimu halisi na sahihi za watanzania wote.

XIX. UDHIBITI WA MAWASILIANO YA SIMU NCHINI

72.   Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa nchi yetu katika kipindi hiki imekuwa na maendeleo makubwa ya matumizi ya simu za mkononi. Hata hivyo kwa kiwango kikubwa mawasiliano haya ya simu za mikononi yanachangia katika ongezeko la vitendo vya uhalifu kutokana udhibiti mbovu wa mawasiliano hayo.

73.   Mheshimiwa Spika, inasikitisha kwamba line za simu za kila mtandao zinauzwa hovyo bila udhibiti na kwa bei rahisi kiasi kwamba mtu mmoja anaweza kumiliki hata laini 1000 kwa wakati mmoja. Hii husaidia kwa watu kununua laini akaitumia kwa matumizi yasiyo mazuri na baadae kuitupa kwa sababu hakuna usajili katika mamlaka maalum nchini.

Itakumbukwa kuwa katika hotuba ya bajeti ya mwaka jana ilisemwa ndani ya bunge hili na mheshimiwa waziri kwamba jeshi la polisi kwa kushirikiana na mamlaka ya mawasiliano ya taifa itadhibiti mawasiliano ya simu za mikononi kwani imebainika kuwa zinatumika kuwezesha kutendeka makosa ya uhalifu kama utekaji nyara, ujambazi, vitisho na matusi.

74. Mheshimiwa Spika, ni jambo la kusikitisha kwamba udhibiti huo haujafanyika, jee serikali ilishindwa kutekeleza lengo hili kwa nini? Inashangaza kwa vile tunayo mamlaka ya mawasiliano (TCRA) kwanini isipewe jukumu hili?

75. Mheshimiwa Spika, kwa mfano nchini Canada, South Afrika na australia na hata India wana utaratibu wa kurejista wamiliki wa laini za simu ili kudhibiti matumizi mabaya ya simu.

76. Mheshimiwa Spika, udhibiti wa mawasiliano ya simu unahitaji kufanywa pia kwa kuangalia umri wa watu wanaomiliki simu hizo, pia kwa kulingana na mahali walipo kwa mfano iwe ni marufuku wakati wakiendesha vyombo vya usafiri kama magari na pikipiki.

77. Mheshimiwa Spika, naomba tulizingatie hili na tusitafute mchawi wa ongezeko la mimba katika umri mdogo, ongezeko la vitendo vya kimapenzi mashuleni na hata vyuo vikuu, ongezeko la maambukizi ya ukimwi, haya yote kwa kiasi Fulani huchangiwa  na udhibiti mbovu wa mawasiliano ya simu za mikononi.

78. Mheshimiwa Spika, kambi ya upinzani inataka TCRA ipewe mamlaka ya kutengeneza taratibu za ununuzi na umiliki wa laini za simu ikijumuisha kuwepo usajili wa mmiliki wa laini husika na namba ya utambulisho wa laini hizo.

XX.   IDARA YA ZIMA MOTO

79. Mheshimiwa Spika, hii ni idara inayolalamikiwa sana katika utendaji wake hasa pale yanapotokea majanga ya moto yenye kuhitaji kushuhulikiwa kwa haraka.

Mara nyingi magari ya uokozi au kuzima moto hufika eneo la tukio kwa kuchelewa sana kiasi kwamba kama ni nyumba au kitu chochote kinachoungua kinakua kimeshateketea.

80. Mheshimiwa Spika, ni mara chache sana idara hii imefanikiwa kuepusha majanga ya moto, hii inatokana na upungufu wa vitendea kazi kama magari na vinginevyo. Inawezekana kwamba katika mkoa mzima huwa hakuna magari ya kutosha ya  kuzima moto.

86. Mheshimiwa Spika, maoni ya kambi ya upinzani ni kuwa miundombinu ya idara hii iboreshwe kwa kununua magari ya kutosha, kuongeza vituo vya kuweka magari hayo ya uokozi na kuongeza watendaji ili ifikiwe ile dhana ya kuwa ni chombo cha uokozi.

XXI. WAHAMIAJI HARAMU

82. Mheshimiwa Spika, Wahamiaji Haramu ni tatizo la dunia kwa sasa. Nchi nyingi duniani zinatengeneza sera na sheria mahususi za kupambana na tatizo hili. Kwa upande wa Tanzania tatizo la wahamiaji haramu lipo kwani kila leo tunasikia taarifa za kukamatwa watu wanaoingia nchini isivyo halali, sina hakika kwamba tuna sheria na sera mahususi zinazoweka mikakati ya kupambana na wahamiaji haramu.

83. Mheshimiwa Spika, Inasikitisha kwamba mbali ya kutokuwa na sheria na sera mahususi juu ya jambo hili, lakini pia inaonekana idara zinazohusika hazifanyi kazi ipasavyo tatizo hili. Nitatoa mfano au ushahidi wa kauli yangu kupitia taarifa ya Peter Kivuyo (Deputy Director of Criminal Investigation) alisema wakati akitoa taarifa juu ya operesheni ya idara ya Interpol kuchunguza magari yaliyoibiwa kutoka katika nchi mbali mbali na kuletwa Tanzania kwamba wamekamata wahamiaji haramu 11 kutoka Kenya, Rwanda na Somalia ambao wapo nchini.

84. Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa kama si operesheni hii wahamiaji hawa haramu wasingelikamatwa. Hivi kweli tunaipenda Tanzania yetu. Maoni ya kambi ni kuwa iwekwe sera na sheria mahususi ya kudhibiti wahamiaji haramu nchini ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea.

85. Mheshimiwa Spika, mwisho tunaiomba Serikali kuweka mtandao wa kudumu wa computer katika entry point zote nchini ili kujua na kudhibiti wageni waingiao na watokao nchini. Hii itawarahisishia idara ya uhamiaji kufanya kazi zao kwa urahisi na ufanisi mkubwa.

86. Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa nawashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Micheweni kwa ushirikiano wanaonipa pia nawashukuru waheshimiwa wabunge wote kwa kunisikiliza kwa makini, naomba kuwasilisha.

TUJITAHIDI KUTEKELEZA MAJUKUMU YETU

…………………………………………………..

SHOKA KHAMIS JUMA (MB)

K.N.Y MSEMAJI MKUU KAMBI YA UPINZANI BUNGENI-

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

29.07.2008

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s