Zi wapi zile ajira milioni moja za Kikwete?

”Utafiti wa nguvukazi wa mwaka 2001 ulionyesha kuwa kila mwaka ajira mpya 400,000 zinaanzishwa wakati nguvu kazi laki saba inaingia katika soko la ajira. Serikali ya awamu ya nne iliahidi itaanzisha ajira mpya milioni moja katika kipindi cha miaka mitano wastani wa ajira laki mbili kila mwaka. Waziri ameeleza kwamba katika kipindi cha miezi 18 kuanzia mwezi Julai 2005 hadi Desemba 2007, ajira mpya 412,608 zilikuwa zimepatikana. Ajira 194,325 zimetokana na sekta rasmi na ajira 218,283 zimetokana na sekta isiyo rasmi. Hata hivyo Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2007 hakina jedwali linaloonyesha ajira hizo na sekta zake. Kitabu hicho kinaonyesha ajira viwandani imeongezeka toka watu 89,316 mwaka 2005 na kufikia watu 91,112, ongezeko la wafanyakazi 1,796 tu. Kwa kadri muundo wa uchumi unavyobadilika ndivyo sekta ya viwanda inavyotegemewa kutoa mchango mkubwa kwa ajira mpya. Aidha, Kambi ya Upinzani inamtaka Mhe. Waziri alieleze Bunge lako tukufu, hizo ajira zaidi ya laki nne ziko sekta gani? Au ajira hizo ni ajira hewa?”

Mhe. Salim Abdallah Khalfan

Hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha – 2008/2009

I.  UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, Awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa majaliwa yake ya uzima wetu sote. Naomba kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, kuwasilisha maoni juu ya Hotuba ya Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 99 (7) toleo la 2007.

2. Mheshimiwa Spika, nawashukuru wananchi wa jimbo langu la Tumbe kwa kuendelea kuniunga mkono na kunipa hoja nyingi za kuleta mbele ya Bunge hili tukufu. Aidha naomba kutoa shukrani zangu za dhati kwa kiongozi wetu wa Kambi ya Upinzani, Mhe. Hamad Rashid na Naibu wake, Dk. Wilbroad Slaa, na wabunge wote wa Kambi ya Upinzani kwa ushirikiano wao mkubwa walionipa hadi kuniwezesha kusimama mbele yenu kuwasilisha hotuba ya Kambi ya Upinzani kutokana hoja iliowasilishwa na Mheshimiwa Waziri.

Mhe. Spika, wabunge wa upinzani na wabunge wote kwa ujumla wao, wana wajibu wa kushirikiana katika kuwatumikia Watanzania kwa lengo kuu la kuwaondolea umasikini uliokithiri, maradhi na ujinga pamoja na kujenga utaifa wetu wa dhati. Mwenyezi Mungu aziweke pamoja nia zetu na kuzibariki katika kutekeleza azma hiyo.

3. Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru wewe, na Naibu wako kwa kuliongoza Bunge letu kwa umahiri na hekima kubwa inayofanya shughuli za Bunge kwenda kwa utulivu na maelewano. Aidha niwapongeze wenyeviti wetu kwa kufuata vyema nyayo zenu katika kuliongoza Bunge letu kwa ufanisi.

II. SHERIA ZA KAZI NA HAKI ZA WAFANYAKAZI

4. Mheshimiwa Spika, kuwa na mfumo wa sheria ya kazi na usuluhishi wa migogoro ya kazi ni sehemu muhimu sana ya soko la ajira, ulinzi wa haki za wafanyakazi na kuongeza tija. Baada ya kuona kuwa sheria za kazi za zamani hazikidhi mahitaji ya soko la ajira kwa sasa, Bunge lako tukufu lilipitisha sheria mpya za kazi, namba 6 na 7 za mwaka 2004. Kutungwa kwa sheria mpya kulitarajiwa kuboreshe maslahi ya wafanyakazi na kuweka uwiano mzuri baina ya wafanyakazi na waajiri. Mojawapo ya sababu zilizochelewesha utekelezaji wa sheria hizi ni kusubiri kanuni na miongozo yake. Hatua za kutengeneza miongozo (Regulations) zitakazopelekea kuanza kutumika kwa sheria hiyo imefikia pazuri na sasa tunazo Kanuni za Mahakama ya Kazi ambazo zimechapishwa tarehe 18/5/2007.

5. Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa kwa sasa ni kuwa na wataalam wa kutosha kuendesha shughuli za mahakama hii kwa ufanisi na kwa haraka. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuweka utaratibu wa kuwapa mafunzo watendaji kuhusu utatuzi wa migogoro inayohusiana na ajira kwa ujumla wake. Kwa maana kuwa pale wasuluhishi wanapomaliza kazi yao lakini upande wa mwajiri ukakataa kukubalina na maamuzi ya usuluhishi, hivyo basi tunapendekeza hatua kali za ziada zitumiwe dhidi ya wale wanaokataa kutekeleza maamuzi yaliyofikiwa.

III.  MAHUSIANO MEMA MAHALI PA KAZI

6. Mheshimiwa Spika, Mahusiano mema baina ya wadau wakuu wa ajira yaani Serikali, Waajiri na Waajiriwa (kupitia Vyama vya wafanyakazi) ni hitaji muhimu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Uzalishaji makini na wa tija hutegemea sana uhusiano huu.

7. Mheshimiwa Spika, Uhuru halisi wa Vyama vya wafanyakazi ni nguzo muhimu siyo tu ya utawala bora, ila pia ni mhimili wa demokrasia iliyo ya kweli.  Kauli na sauti ya Wafanyakazi huwa ni kauli ya wazalishaji, ambayo pia ni kauli na sauti ya walipa kodi.  Vyama vya wafanyakazi vilivyo huru na makini ni sehemu ya jamii huru ya kiraia au “Civil Society”.  Watendaji Serikalini na katika sekta binafsi ni lazima waijue kwa kina dhana nzima ya Vyama vya wafanyakazi (trade unionism), ndani ya ukweli na mazingira ya soko huria.

8.   Mheshimiwa Spika, demokrasia ya kweli katika nchi yeyote ile duniani inaanzia kwa wafanyakazi kuwa na vyama vyao vilivyokuwa huru na vinavyoweza kudai maslahi yao ya msingi. Hivyo muendelezo huo wa uhuru wa vyama vya wafanyakazi huleta demokrasia ya kweli kwa nchi.

9.   Mheshimiwa Spika, ili kufikia mwafaka wa kiasi gani mwajiri anatakiwa kumpa mwajiriwa, majadiliano baina ya chama cha wafanyakazi na mwajiri wa sehemu husika ni muhimu sana. Kambi ya Upinzani inaipongeza Serikali kwa kuliona hilo na kuanza kulifanyia kazi.

10. Mheshimiwa Spika, tofauti na hilo ni kumlazimisha mwajiri kufanya “down sizing” ambapo mtu mmoja hulazimika kufanya kazi iliyokuwa ikifanywa na watu watano kwa msaada wa mashine. Hii inachangia kuzidisha tatizo la ajira.

IV. WAKALA WA USALAMA NA AFYA MAHALA PA KAZI (OSHA)

11. Mheshimiwa Spika, Hiki ni kitengo muhimu sana, hasa linapokuja suala la mustakabali wa afya za wafanyakazi makazini.  Pamoja na kuanzishwa kwa Wakala wa Usalama na Afya mahali pa kazi (OSHA), bado haijawa na meno na nguvu ya kusimamia kwa ukamilifu sheria ya Bunge iliyoanzisha OSHA.

12. Mheshimiwa Spika, Licha ya umuhimu wa kitengo hiki kimekuwa kinafanyakazi kwa kasi isiyoridhisha. Kambi ya Upinzani kwa mara nyingine tena inaitaka Serikali kutoa taarifa kuhusiana na:-

i) Utendaji kazi wa Kitengo husika na mipango yake katika kuhakikisha kwamba usalama na afya sehemu za kazi unazingatiwa.

ii) Mikakati ya Wizara kuhakikisha kwamba fidia kwa wafanyakazi wanaopata ajali wakiwa sehemu za kazi zinaongezwa ikizingatiwa kwamba zilizokuwepo sasa ni ndogo mno na zimepitwa na wakati.

13.  Mheshimiwa Spika, tunaitaka Serikali kutoa taarifa hizo kwa msingi kuwa sehemu nyingi za kazi kama vile za ujenzi, migodini, mashambani na kwenye viwanda bado wafanyakazi wanapata ajali mbali mbali na waajiri wao wanakataa kuwalipa haki zao za msingi.

14.  Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inazidi kusisitiza kwamba wakala hawa wa Usalama na afya mahala pa kazi (OSHA) wawezeshwe zaidi, ili waweze kufanya kazi zao vizuri na kwa ufanisi mkubwa na pia waweze kuyafikia maeneo tofauti ya nchi.

V.  SHIRIKA LA TIJA LA TAIFA (NIP)

15. Mheshimiwa Spika, Shirika hili ni muhimu kwa taifa letu kutokana na shughuli zake zinazolenga kuongeza tija katika utendaji na ufanisi wa mashirika na makampuni mengi nchini japokuwa lina rasilimali-watu ndogo sana. Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa shirika hilo linaidai Serikali shilingi milioni 213. Katika fedha hizo shilingi milioni 49 walizitumia kuendeleza kiwanja chao NA. 906/H Mbezi Beach ambacho baadaye walinyang’anywa na serikali katika mazingira ya kutatanisha kwa madai kuwa shirika limeshindwa kutimiza masharti ya kukamilisha ujenzi kwa kipindi cha miaka mitatu.

16. Mheshimiwa Spika, Ukweli ni kwamba serikali ilitoa fedha za kujenga nyumba moja katika mwaka wa fedha wa 1994/1995 na serikali ilikuwa iendelee kutoa fedha nyingine lakini miradi ya maendeleo ilisimama kutokana na hali ngumu ya fedha katika mwaka huo. Hata hivyo wakati ujenzi unaendelea, hatua ya kutaka kufuta milki ya kiwanja hiki ilianzishwa na wizara ya Ardhi mwaka 1995, Wakati ambao serikali ilikuwa inatoa fedha za kukamilisha ujenzi wa nyumba moja. Kufuatia uamuzi wa wizara ya Ardhi, Serikali iliamua shirika lipewe shilingi milioni 26 tu, tofauti na madai halisi ya shirika na cha kusikitisha zaidi hadi sasa shirika limelipwa shilingi milioni 15 tu kati ya millioni 26 zilizoamuliwa na Serikali. Kambi ya Upinzani inaomba ufafanuzi katika hili.

17. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali iweke wazi nini kimetokea mpaka Wizara ya Ardhi ikakigawa kwa watu wengine kiwanja hicho ambacho tayari shirika lilishatumia kiasi cha shilingi milioni 49 katika kukiendeleza. Ni lini Serikali italirejeshea Shirika fedha zake hizo kama linavyodai, sawasawa na gharama walizotumia kukiendeleza kiwanja hicho?

18. Mheshimiwa Spika, Sababu kubwa ya serikali kuwanyang’anya NIP kiwanja hicho na kuwapa IMTU ilikuwa ni shirika kushindwa kukiendeleza, lakini hadi sasa hakuna hatua zozote za kukiendeleza ambazo zimechukuliwa na IMTU.

19. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka kujua kama kweli kushindwa kukiendeleza kiwanja hicho ndani ya miaka mitatu ndio iliyokuwa sababu ya kuinyang’anya NIP kiwanja chake au kulikuwa na ajenda nyingine ya siri? Je serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kulirudishia shirika kiwanja chake baada ya IMTU nayo kushindwa kukiendeleza kiwanja hicho?

VI. MIFUKO YA HIFADHI ZA JAMII

20. Mheshimiwa Spika, Mifuko ya hifadhi ya jamii ni muhimu sana sio tu kwa kuwahudumia wanachama wake bali hata kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla. Mifuko hiyo imekuwa msitari wa mbele katika uwekezaji kwenye sekta mbali mbali za uchumi. Kwa Tanzania japokuwa sekta hii ya hifadhi za jamii bado iko katika hatua za mwanzo ukilinganisha na mataifa yaliyoendelea lakini inatoa ishara ya matumaini endapo udhibiti wa matumizi ya fedha zao utawekewa miongozo madhubuti na matunda yake ni dhahiri.

21. Mheshimiwa Spika, sheria iliyopitishwa na Bunge lako ya kuundwa kwa mamlaka ya udhibiti wa hifadhi za jamii (Social Security Regulatory Authority Act, 2008) itaongeza ufanisi wa mifuko hiyo na kuwa mlinzi wa fedha za wanachama. Hii itakomesha matumizi yasiyo na tija kwa baadhi ya mifuko hiyo, matumizi ambayo yamekuwa hayamnufaishi mwanachama wa mfuko husika moja kwa moja.

22. Mheshimiwa Spika, sheria hii imeainisha bayana kwamba hifadhi za jamii ziwasaidie wanachama wake kwa kuwapa mikopo ya kujengea nyumba za bei nafuu kwa wale ambao tayari wana viwanja vyao binafsi.  Kwa njia hii hifadhi zitapata mtazamo mpya toka kwa wananchi ambao wanadhani zinatumiwa kuwanufaisha matajiri tu na si kwa wanachama wake.

VII. SHIRIKA LA TAIFA LA MFUKO WA HIFADHI YA JAMII (NSSF)

23. Mheshimiwa Spika, Majukumu makubwa ya NSSF ni kukusanya michango, uwekezaji wa michango na kulipa mafao kwa wanachama. Kambi ya Upinzani inapenda kuipongeza NSSF kwa juhudi hizo za kutimiza wajibu wao. Kwa mujibu wa taarifa zilizopo ni kuwa michango imekua kwa zaidi ya asilimia 30. Mapato kutokana na vitega uchumi vyake yameongezeka kwa takriban asilimia 25. Aidha kwa utaratibu uliotajwa katika sheria namba 28 ya mwaka 1997 NSSF inajitahidi kukamilisha utoaji wa mafao yote 7 kwa mujibu wa sheria.

24. Mheshimiwa Spika, Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na NSSF, bado yapo maeneo ambayo yanahitaji kushughulikiwa haraka. Moja ya maeneo hayo ni ujenzi wa daraja la Kigamboni.

25. Mheshimiwa Spika, tunampongeza tena Mhe. Waziri Mkuu kwa kuwa muwazi na muungwana kuhusiana na kilichojiri katika kadhia nzima ya ujenzi wa daraja la Kigamboni. Kambi ya Upinzani imeuona uungwana huo wa Waziri Mkuu kwa kutangazwa Tenda ya daraja hilo kama alivyoahidi hapa Bungeni wakati akifanya majumuisho kwa hotuba ya bajeti yake mwaka huu.

26. Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya waajiri wa sekta binafsi ambao hawafuati sheria za nchi hii na hasa katika kuhakikisha kuwa wanawaingiza wafanyakazi wao kwenye mifuko ya hifadhi za jamii kama NSSF na mingineyo, na hii huwaathiri sana wafanyakazi hao pindi wanapostaafu ama kupata ajali wakiwa kazini.

27. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka maelezo ya kina kuwa ni kwanini waajiri hawa wanakiuka sheria za nchi na hawachukuliwi hatua zinazostahiki. Ukiukwaji huu umekithiri sana kwenye sekta ya utalii kama vile mahoteli ya kitalii, viwanda vya samaki, viwanda vya nguo n.k Hapa utawakuta wafanyakazi wana miaka 10 kazini lakini bado ni vibarua. Hizi ni hila na ghilba za waajiri hawa kusudi wasipeleke michango ya wafanyakazi hao NSSF. Hili limekuwa ni tatizo sugu hapa nchini kwa baadhi ya waajiri. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe kauli kuhusu ujanja ujanja wa aina hii wa makampuni hayo kwa wafanyakazi wake.

28. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka NSSF iongeze kasi wa kujenga majengo kwa ajili ya vyuo vikuu kwa kushirikiana na mifuko mingine nchini na hata kutoa udhamini wa makampuni ya nje kwa ubia. Aidha  ujenzi wa  ofisi ya Ubalozi wetu kule Nairobi uharakishwe na hilo linaweza kwenda sambamba na kujenga ofisi zetu za Balozi kwenye nchi mbali mbali duniani kwa ajili ya kupunguza gharama na adha za upangaji na ulipaji kodi.

29. Mheshimiwa Spika, Wenzetu wa Kenya wanakaribia kumaliza ujenzi wa ofisi yao kwenye kiwanja chao cha Dar es Salaam wakati sisi bado hatujaanza. Hii ni aibu kwa nchi yetu. Tuyapongeze mashirika kwa ujenzi wa hostels za Chuo Kikuu Dodoma.

VII. AJIRA

30.  Mheshimiwa Spika, Ajira ni suala la msingi sana kwa maendeleo ya Taifa lolote. Duniani kote Serikali zinahangaika kuwapatia watu wake ajira ili kukuza uchumi, kuimarisha huduma na kuboresha kiwango cha maisha. Kila kukicha mikakati inaundwa ya namna ya kutengeneza fursa za ajira.

31. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa takwimu za   utafiti wa bajeti ya kaya (Household Budget Survey) ya mwaka 2000/01.  Tathmini hii ya mapato na matumizi ya kaya inaonyesha kuwa asilimia 84.2 ya nguvu kazi ya Tanzania inaajiriwa katika sekta ya kilimo.  Kwa takwimu za zamani, nguvu kazi hii ilichangia asilimia 44.7 ya pato la taifa.  Kwa takwimu mpya kilimo na uvuvi vimechangia asilimia 30.7 tu mwaka 2001.  Ikiwa mchango wa sekta ya kilimo ni mdogo kiasi hicho wakati asilimia 84.2 ya nguvu kazi ya Tanzania iliajiriwa katika kilimo mwaka 2001, hii sio dalili njema kwa ukuaji wa uchumi na sekta ya ajira hapa nchini. Kwa kasi hii kamwe hatuwezi kufikia zile ndoto za maisha bora kwa kila Mtanzania.

32.  Mheshimiwa Spika, Utafiti wa nguvukazi wa mwaka 2001 ulionyesha kuwa kila mwaka ajira mpya 400,000 zinaanzishwa wakati nguvu kazi laki saba inaingia katika soko la ajira. Serikali ya awamu ya nne iliahidi itaanzisha ajira mpya milioni moja katika kipindi cha miaka mitano wastani wa ajira laki mbili kila mwaka. Waziri ameeleza kwamba katika kipindi cha miezi 18 kuanzia mwezi Julai 2005 hadi Desemba 2007, ajira mpya 412,608 zilikuwa zimepatikana. Ajira 194,325 zimetokana na sekta rasmi na ajira 218,283 zimetokana na sekta isiyo rasmi. Hata hivyo Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2007 hakina jedwali linaloonyesha ajira hizo na sekta zake. Kitabu hicho kinaonyesha ajira viwandani imeongezeka toka watu 89,316 mwaka 2005 na kufikia watu 91,112, ongezeko la wafanyakazi 1,796 tu. Kwa kadri muundo wa uchumi unavyobadilika ndivyo sekta ya viwanda inavyotegemewa kutoa mchango mkubwa kwa ajira mpya.

Aidha, Kambi ya Upinzani inamtaka Mhe. Waziri alieleze Bunge lako tukufu, hizo ajira zaidi ya laki nne ziko sekta gani? Au ajira hizo ni ajira hewa?

33.  Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Sekta kiongozi kwa kuajiri ni kilimo na kilimo hicho Serikali haikithamini kabisa hivyo basi ni bora ikiri kuwa umaskini vijijini ni wa kutisha zaidi kuliko ilivyokadiriwa mwaka 2001.

34. Mheshimiwa Spika, kuna matatizo makubwa sana ya vijana wa Kitanzania kupata ajira kwenye Makampuni mbalimbali ya simu za mkononi hapa nchini na hata wanapopata ajira hizo huwa hawalipwi kiwango sawa na wenzao kutoka nchi jirani za Kenya na Uganda hata kama viwango vyao vya elimu viko sawa .Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kufanya utafiti wa kina na kujua ni vigezo gani haswa vinatumiwa katika kuwaajiri na hata kuwalipa vijana wa Kitanzania kwenye Makampuni husika.

35.  Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani, inaitaka Serikali kuhakikisha kuwa inafanya tathimini ya kina na kuyajua makampuni haya ya simu za mikononi na kuangalia kama waajiriwa ambao wanatoka nje ya nchi wanasifa za kupata ajira hapa nchini ama laa, na je wana vibali vya kufanya kazi hapa nchini au hawana? Kwani kuna malalamiko kutoka kwa watanzania kuwa waajiriwa wengi wao hawana hata vibali vya kufanya kazi nchini ukiachilia sifa ambazo watanzania hawana (rare professional) ila wameajiriwa kinyemela.

36.  Mheshimiwa Spika, naomba ninukuu sehemu ya hotuba ya Waziri wa Fedha aliyoitoa hapa Bungeni mwaka 2004, alisema   “maeneo ya uzalishaji (production) ndiyo yatatuondoa kwenye ujinga na umaskini kwa haraka zaidi kuliko mengineyo ambayo ni ya ulaji (consumption). Kupanga ni kuchagua pale panapoweza kulivusha taifa letu haraka haraka.  Tutaweza kulima kwa wingi, kusindika mazao hayo kwa wingi na kusafirisha mazao ya kilimo na viwanda hadi nchi jirani” mwisho wa kunukuu. Wizara ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa sekta ya uzalishaji inakua na kuongeza ajira ili tuweze kukuza uchumi wa Taifa letu hili.

37.  Mheshimiwa Spika, vijana wa Kitanzania ambao wanajishughulisha na ajira ambazo sio rasmi na hasa biashara ndogondogo ambao tumewapa jina “wamachinga” wanafanya shughuli zao kwenye mazingira magumu sana kutokana na serikali kutokuweka mkakati thabiti wa kuwasaidia vijana hawa ambao kutwa nzima wanakuwa wakitembea na bidhaa zao maeneo ya mijini .Itakumbukwa kuwa kwa kipindi cha mwaka jana serikali iliahidi kuwa itajenga kituo kikuu cha wamachinga Jijini Dar es salaam kwa ajili ya kuwasaidia vijana hawa kufanya shughuli zao eneo moja.

38.  Kambi ya Upinzani ina wasiwasi na ujenzi wa vituo vya wamachinga nchi nzima. hii ni kuhalalisha kuwa sasa tanzania linakuwa taifa la wachuuzi badala ya taifa la wazalishaji. Hili ni jambo la hatari sana kwa mustakabali wa nchi yetu. Hivyo basi, tunamtaka waziri kuliangalia upya suala hili ambalo linatekelezwa na mfuko wa hifadhi ya jamii.

39.  Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa malengo ya MKUKUTA, ukosefu wa ajira lengo ni kushuka hadi kufikia 6.9% ifikapo 2010, mwaka 2005 ilikuwa 12.9% mwaka 2007 ni 11%. Kambi ya Upinzani inauliza: je ni kweli Serikali inafuata   miongozo na dira ya MKUKUTA au ni wimbo ambao hauna maana kwake?

40. Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia serikali kwa hatua mbali mbali ilizozichukua katika kutekeleza ilani ya CCM ya uchaguzi wa 2000 na baadhi 2005 ambazo naomba baadhi yake kuzinukuu:-

(i)  Mashirika ambayo ni ya msingi na nyeti (bandari, reli, posta, simu, mabenki ya umma na nishati) kwa maendeleo ya taifa yanaendelea kumilikiwa na dola.

(ii)  Sera za kurekebisha mashirika ya umma itakwenda sambamba na hatua  za kuwalinda wafanyakazi wa mashirika yatakayohusika, CCM itaona kuwa:-

a. Ajira ya wafanyakazi inalindwa kwa kadri itakavyowezekana. Fidia za haki kwa  wafanyakazi  watakaoachishwa kazi zinatolea.

b. Wafanyakazi wanaoachishwa kazi wanasaidiwa na waingie katika sekta ya wananchi wanaojiajiri”

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasikitishwa sana kwa jinsi serikali inavyosimamia na kutekeleza ilani ya ccm kwa kutokuitekeleza kama ilivyoahidiwa na kuwaacha patupu wasijue la kufanya. hivyo Kambi ya Upinzani inauliza kuwa, je ni kweli ajira za wafanyakazi zimelindwa baada ya kuuzwa viwanda? je wafanyakazi walioachishwa wamesaidiwa kuingia katika sekta binafsi au kuwa wajasiriamali?

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kutimiza ahadi ya lengo dogo la ajira milioni moja kwa Watanzania, na kuacha kuwafanyia wafanyakazi hadaa wakati inapohitaji msaada wa wafanyakazi hao.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasisitiza kuwa ni lazima kuwe na mkakati maalum, sera na sheria itakayoharakisha kukua kwa uchumi na upatikanaji wa ajira nchini kinyume na hali halisi ilivyo sasa.

VIII. MIKOPO YA SHILINGI BILIONI MOJA KWA KILA MKOA

41. Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa lengo kuu la utoaji wa fedha hizo lilikuwa ni kuwawezesha wananchi kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira. Huu ni uamuzi ambao kwa ujumla unastahili kupongezwa.  Ni ukweli ulio wazi kuwa hadi sasa robo tatu ya fedha hizo zimekwisha tolewa katika mikoa husika, lakini hadi sasa ni ukweli kuwa nusu ya fedha hizo hazija rejeshwa.

Urejeshwaji wa fedha hizo unaweza kuwa mgumu kutokana na sababu kadhaa zilizo nje ya     uwezo wa wakopaji.

Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri atoe tathimini ya kina juu ya mpango   huu. Je mpaka sasa ni ajira ngapi zimeweza kupatikana kutokana na mkopo huu? Je waliokopeshwa ndio walengwa? Hii ni kwa sababu wananchi wa kawaida, ambao ndio walikuwa walengwa wa mkopo huu, wanalalamika kuwa hawajauona mkopo huu ila uliwanufaisha zaidi wakubwa na matajiri kuliko kuwanufaisha wao.

42. Mheshimiwa Spika, tujiulize, hivi kinachokuja kwanza ni nini Wazo la biashara ama Mkopo? Mtizamo wa Serikali hii ni kutanguliza mbele mikopo tena midogo midogo. Kwa misingi hii, hoja ni kwamba vijana wanao utamaduni na nidhamu ya biashara.

43. Kambi ya Upinzani inasema hili ni kosa kubwa kwani Watanzania hatukulelewa kwa misingi ya biashara vivyo hivyo na kwa vijana wetu. Mikopo midogo midogo isiyotanguliwa na elimu inaweza kuwa chanzo cha umaskini kutokana na kushindwa kwa biashara kutakakozalisha madeni kwa walalahoi.

44. Mheshimiwa Spika, Serikali inaweka mkazo katika kujiajiri hususani kwa kukuza sekta isiyo rasmi. Sekta hii bado inakabaliwa na changamoto mbalimbali. Tafiti zinaonyesha kuwa zaidi ya theluthi mbili (2/3) ya biashara ndogo ndogo zilizoanzishwa na watu waliotazamia kujiajiri wenyewe zinakufa kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano kutokana na upungufu wa mafunzo ya stadi za biashara miongoni mwa vijana, elimu ndogo miongoni mwa wajasiriamali vijana na isiyojitosheleza, utamaduni wa watu wengi kupenda ajira rasmi zaidi ya kujiajiri na kutovutia au kutelekezwa kwa kilimo, ambayo ni sekta kuu ya nchi yetu.

45. Mheshimiwa Spika, Kutofanikiwa wakati mwingine kwa biashara hizi pia kunatokana na mali/mitaji ya wakinamama na vijana hawa kuharibiwa au kupotea na wao wenyewe kuishia mikononi mwa polisi na au asikari wa Jiji na mgambo kama wahalifu. Wakati mwingine tunawahamisha waende maeneo ambayo hayafikiki kirahisi na hivyo kuwakosesha wateja. Kwa misingi hii hatujengi taifa bali tunabomoa taifa hili ambalo ni changa bado kiuchumi na linalokuwa kwa taabu.

46. Mheshimiwa Spika, tatizo hili ambalo linasababisha kupotea kwa mitaji ya wajasiriamali kwa kiasi kikubwa lilitokana na kutokufanyika kwa upembuzi yakinifu juu ya fursa na vikwazo vya maendeleo kwa kila mkoa.

47. Mheshimiwa Spika, katika kuliona hilo, tarehe 5 Julai, 2007, Mheshimiwa Zitto Kabwe, (Mb) alimwandikia  Waziri wa Kazi wakati huo mhe. Prof. Jumanne maghembe akimshauri njia mwafaka ya jinsi fedha hizo za bilioni moja zitakavyofikia lengo kuu la fedha hizo.

Moja ya mapendekezo hayo ni kuwa kwa kuwa kila mkoa una viashiria tofauti vya kukuza uchumi, hivyo basi upembuzi yakinifu ufanyike kuhusiana na hilo kabla ya kutoa hizo fedha. na alishauri msimamizi mkuu wa washauri (supervisory consultant) awe ni yule anayefanya kazi na MKUKUTA.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasikitika kuwa viongozi wetu kwa sababu zao binafsi wanashindwa kuwa na maono, alichoshauri Mhe. Zitto Kabwe sasa hivi kingekuwa kimeinufaisha mikoa kwa kuongeza ajira. Kambi ya Upinzani inaamini kabisa kuwa kama ushauri huo ungetolewa na wahisani basi usingeachwa na ungefanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, mbaya zaidi hadi sasa tunapowasilisha hotuba hii majibu ya barua yake kwa waziri hajayapata.

48. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inadhani sasa ni wakati muafaka kwa serikali kuangalia upya taratibu na mipango yake ili fedha hizi zitumike vizuri na ziwasaidie walengwa. Ipo haja ya kuwapa vijana wajasiriamali mafunzo ya jinsi ya kuendesha biashara zao vizuri. Hilo likishafanyika ndipo dhana ya kujiajiri itakuwa na maana kwa vijana wa nchi hii.

Kambi ya Upinzani inasema hii inaweza kufikiwa kwa kufanyika kwa tafiti za upembuzi yakinifu kwa kila Mkoa kuangalia viashiria vya ukuaji uchumi kwa Mikoa hiyo. Na ndio sababu nchi zilizo makini na maendeleo bajeti ya RESEARCH AND DEVELOPMENT inakuwa ni kubwa na inakuwepo miaka yote.

49. Mheshimiwa Spika, Wakati akitoa hotuba ya kuliahirisha Bunge mwezi wa nane 2006, Waziri Mkuu wa wakati huo aliunda kamati ambayo ingeshughulikia utaratibu wa kutoa mikopo hiyo. Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri alieleze Bunge lako Tukufu ni kazi gani imefanywa na kamati hiyo kwani hadi sasa walengwa wamekosa mikopo hiyo japokuwa vigezo vyote vilivyohitajiwa walivitimiza.

IX. UHITAJI WA KIGEZO CHA UZOEFU KATIKA AJIRA

50. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inalileta tena suala la uhitaji wa uzoefu katika ajira kwa ajili ya mjadala. Tujiulize na kujadili tukikumbuka matangazo mbalimbali ya ajira. Ni asilimia ngapi ya matangazo hayo hayana kigezo cha uzoefu? Tena mengine yanataja miaka mingi mpaka pengine ingeitwa uzeefu badala ya uzoefu.

51. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inatambua na kuthamini mchango wa uzoefu katika utumishi na kazi. Hivyo, kambi haina tatizo uzoefu kuendelea kuwa kigezo cha MUHIMU katika kuajiri. Lakini, Kambi ya Upinzani haioni umaana wa uzoefu kutumika kama kigezo cha LAZIMA. Utaratibu wa sasa wa asasi nyingi za serikali na sekta binafsi kutumia uzoefu kama kigezo cha lazima unawazuia vijana wahitimu ambao hawajafanya kazi bado, hata kupata nafasi ya kusailiwa na kupimwa uelewa na vipaji vyao kuhusiana na kazi husika ni kuwanyima haki yao ya msingi. Watapata lini uzoefu bila kupata fursa ya kupata uzoefu?

52.  Mheshimiwa Spika, Wizara iweke utaratibu wa kuishawishi sekta ya umma na binafsi kupenyeza mabadiliko katika utaratibu wao kuhusiana na suala hili la uzoefu kwa kutoa motisha ya vyeti vya punguzo kidogo la kodi kwa makampuni yatakayochukua wanafunzi toka vyuoni moja kwa moja (graduate tax relief certificate).

53. Mheshimiwa Spika, Idara yetu ya kazi haifanyi kazi yake ipasavyo ya kuwaunganisha waajiri na wanaotafuta kazi. Ili kurahisisha kazi ya kupata ajira na kuwa na mikakati ya kuwasaidia wazalendo ni muhimu mambo yafuatayo yafanyike:

A. Tuwe na upendeleo wa makusudi kwa wazawa katika kutoa fursa za biashara na uwekezaji nchini kila mwekezaji lazima awe na mshirika mtanzania katika uwekezaji huo. Hii iambatane na kuwapunguzia ugumu        wowote unaoweza kujitokeza wakati wa utoaji wa fursa hizo za biashara na uwekezaji.

B. Tuwe na vigezo tofauti vya kutoa mikopo na vivutio vya biashara ili tuwasaidie wazawa kutengeneza fursa nyingi za kazi na kuajiri watu wengi zaidi.

C. Tuwe makini katika kutoa vibali vya kazi kwa wageni ili kuhakikisha wawekezaji wanafuata sheria na masharti ya ajira katika kuwekeza nchini kwetu kwani sheria ziko wazi kuhusu mgawanyo wa ajira kati ya wageni na wazawa.

IDARA YA VIJANA

54. Mheshimiwa Spika, Vijana ni sehemu muhimu sana ya nchi yetu. Ni muhimu kwa sababu ya nafasi yao katika uchumi wa taifa na uhai wa taifa kwa siku za usoni. Kiuchumi, hii ndiyo nguvu kazi ya taifa ambayo inatarajiwa kuzalisha na kuleta tija. Ili waweze kushiriki vizuri lazima wawekewe fursa katika uchumi ili waweze kujiajiri na wengine kuajiriwa na kuajiri wengine. Taarifa za tafiti na takwimu mathalani, MKUKUTA zinatuonyesha kuwa suala la vijana kutokushirikishwa katika uchumi wa nchi ni suala mtambuka.

SERA YA MAENDELEO YA VIJANA

55. Mheshimiwa spika, Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002 vijana wa kati ya miaka 15 mpaka 35 ni takribani 11,775,259. Hivyo hili ni kundi ambalo halipaswi kupuuziwa. Na zaidi ukitazama hali ya vijana nchini; wengi wao hawana ajira, wengi wao wamekata tamaa, wao ndio waathirika zaidi wa UKIMWI na mambo mengine. Kwa vyovyote vile, tusipoweka kipaumbele kwa kundi hili taifa lipo katika bomu la wakati.

56. Mheshimiwa Spika, tunapaswa kubadili mtizamo wetu kuhusu vijana na kuwatazama kama suluhisho badala ya tatizo. Kwa asili vijana ni kundi muhimu kiuchumi kama wazalishaji wakuu, ndio wenye uwezo wa kulisukuma taifa mbele kutokana na nguvu na ubunifu wao.  Ndio maana maendeleo ya vijana inapaswa kuwa ajenda mtambuka (cross cutting agenda) kwa sekta zote. Kwa kuwawezesha wazee tunajenga taifa lipitalo, kwa kuwalea watoto tunajenga taifa la kesho, kwa kuwezesha vijana tunawekeza katika Tanzania ya leo na kesho.

Mheshimiwa Spika, ili tufike huko tunahitaji sera mwafaka ya maendeleo ya vijana. Kwa muda mrefu tumekuwa tukitumia sera ya maendeleo ya vijana ya mwaka 1996. Kwa vyovyote vile sera hii imepitwa na wakati. Kwa miaka kadhaa sasa serikali imekuwa ikitoa matamko kwamba iko katika mchakato wa kuibadili sera hii. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni lini Sera ya maendeleo ya vijana itakuwa tayari?

57. Mheshimiwa Spika, Baada ya kuyasema hayo, ninawashukuru wabunge wote na Watanzania kwa ujumla kwa kunisikiliza na naomba kuwasilisha.

……………………………….

Salim Abdallah Khalfani (Mb)

MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI- WIZARA YA KAZI, AJIRA NA MAENDELEO YA VIJANA

18.07.2008

Advertisements

One thought on “Zi wapi zile ajira milioni moja za Kikwete?

 1. Siku njema,

  Hali yako ni nini? Need 100% fedha? Je, nimechoka kutafuta Mikopo na rehani, “Je, imekuwa daima akageuka chini na benki na

  taasisi za fedha, i am Mr Albert Sheriff mmiliki wa Albert Sheriff mkopo, Sisi kutoa mikopo kwa makampuni, makampuni, viwanda

  nk nia ya mtu yeyote lazima Wasiliana nasi sasa Via hii Email: ivor.loanfund@gmail.com na maelezo yafuatayo:

  TAARIFA wakopaji

  majina yako ……….
  Inahitajika kiasi ………
  Muda :………….
  Nchi yako ………
  anwani yako ……..
  Simu Idadi ……….
  Mapato kwa mwezi ……..
  Sex ……………….
  Fax wako Idadi …….
  Umri wako …………..

  Email: ivor.loanfund@gmail.com
  Regards,

  Mr Albert Sheriff

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s