CCM imedanganya – CUF

Iliyokuwa timu ya CUF katika mazungumzo yake na CCM ikiongozwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, kuelekea ukumbi wa mikutano wa CUF, Buguruni, Dar es salaam, kuzungumza na waandishi wa habari juu ya msimamo wa CUF baada ya CCM kukwamisha Muafaka kwa madaia yake mapya ya Kura ya Maoni, Aprili 1, 2008

Iliyokuwa timu ya CUF katika mazungumzo na CCM ikiongozwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, kuelekea ukumbi wa mikutano wa CUF, Buguruni, Dar es Salaam, kuzungumza na waandishi wa habari juu ya msimamo wa CUF baada ya CCM kukwamisha Muafaka kwa madai mapya ya Kura ya Maoni, Aprili 1, 2008

“Uzushi na upotoshaji hauwezi kuisaidia CCM ambayo inapoteza kwa kasi uhalali wa kisiasa kama chama chenye dira na mwelekeo hapa nchini. CCM inapaswa ijirudi na ijisahihishe kama inataka ikubalike kuwa ni chama makini mbele ya macho ya Watanzania na jumuiya ya kimataifa. Kujidanganya kwamba wataendelea kufanya mchezo wa kitoto wa mazungumzo yasiyokwisha na baadaye kufikia Miafaka ambayo hawana nia ya kuitekeleza sasa hakuwasaidii tena maana Watanzania wameamka. ..

Ufafanuzi wa CUF dhidi ya upotoshaji wa CCM

 

Ufafanuzi wa Chama Cha Wananchi (CUF) wenye Lengo la Kuweka Kumbukumbu Sahihi Kuhusiana na Mwenendo wa Mazungumzo ya Kutafuta Ufumbuzi wa Kudumu wa Mpasuko wa Kisiasa Zanzibar Kufuatia Upotoshaji Uliofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM)

 

<!–[if !supportLists]–>I. <!–[endif]–>Utangulizi

 

Chama Cha Wananchi (CUF) kimepata faraja kubwa baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Kamati yake ya Mazungumzo kutoa kile ilichokiita “Ukweli juu ya Mwenendo wa Mazungumzo kati ya CCM na CUF” katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumapili, tarehe 11 Mei, 2008. Tumepata faraja siyo kwa sababu CCM hatimaye imeeleza ukweli. Tunajua hilo liko nje ya utamaduni wa kisiasa wa CCM. Chama ambacho itikadi yake kuu ya kisiasa ni kuendesha propaganda zilizopitwa na wakati huku wakiwatumia wanasiasa waliochoka na ambao akili zao zimepoteza hata uwezo wa kuweka kumbukumbu za wanachokizungumza seuze kuweza kufikiri na kubuni sera mpya zitakazoweza kumpatia Mtanzania mahitaji yake ya wakati huu, hakiwezi kutegemewa kueleza ukweli. Ni bahati mbaya kwa Watanzania kwamba ukweli si sehemu ya kamusi la kisiasa la CCM.

 

Tumepata faraja kutokana na hatua hiyo ya CCM kwa sababu taarifa yao badala ya kuwasaidia (kama walivyotegemea) imezidi kuwaumbua na kuwafedhehesha mbele ya macho ya Watanzania na jumuiya ya kimataifa. Tumepata faraja kwa sababu hatua hiyo sasa imetupa nafasi ya kuyaeleza na kuyaweka hadharani mengi ambayo tulikuwa tumeyazuia kuhusiana na mwenendo wa mazungumzo kati ya CUF na CCM ili Watanzania na jumuiya ya kimataifa wajue nani anawaambia ukweli na nani anawapotosha. Tunafanya hivi, kwa sababu kama tulivyowahi kusema, kwetu sisi CUF, siasa si proaganda zilizopitwa na wakati bali ni utumishi wa dhati na uliotukuka kwa wananchi wanaowaamini viongozi wake. Kwa msingi huo, CUF inaamini katika ukweli na ukweli mtupu kuhusiana na mambo yanayohusu maisha ya Watanzania na hatima yao kama Taifa.

 

Katika kuweka kumbukumbu sahihi za mwenendo mzima wa mazungumzo, tumeona kuna haja ya kwenda nukta kwa nukta kati ya yale yaliyopotoshwa na CCM na pia maeneo mengine ambayo CCM kwa kuuogopa ukweli, kwa makusudi kabisa, wameamua kuyaficha. Tutatumia kumbukumbu za vikao ambazo zina saini za Wenyeviti Wenza na Makatibu Wenza wa CUF na CCM kuthibitisha yale tutakayosema.

 

 

<!–[if !supportLists]–>II. <!–[endif]–>KUHUSIANA NA KUKAMILIKA KWA MAZUNGUMZO

 

UPOTOSHAJI WA CCM:

Kamati ya Mazungumzo ya CCM inawapotosha wananchi na jumuiya ya kimataifa kwamba eti mazungumzo hayakuwa yamekamilika na kwamba agenda zilizojadiliwa ni nne (4) tu kati ya tano (5). Wanawapotosha wananchi kwamba eti agenda ya 5 inayohusu “Utaratibu wa Utekelezaji na Programu ya Utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa katika Mazungumzo” haijaanza kujadiliwa.

 

UKWELI WA CUF:

Katika kikao cha mazungumzo kilichowashirikisha Makatibu Wakuu wa CUF na CCM cha tarehe 21 Januari, 2008, pamoja na mambo mengine, wajumbe wa CUF waliwaeleza wenzao wa CCM kwamba kwa vile ridhaa waliyopewa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ilikuwa imemalizika mwishoni mwa mwezi Desemba 2007, hivyo hawana njia isipokuwa katika kikao cha Baraza Kuu hilo cha mwishoni mwa Januari 2008 ni lazima wapeleke taarifa ya mwisho ya mazungumzo hayo na kupatiwa maamuzi. Kumbukumbu za kikao kuhusiana na suala hilo zinasema:

 

“Ujumbe wa CUF ulishauriwa kwa sasa usitishe hatua ya kufikisha taarifa ya mazungumzo katika vikao vyake ili kusubiri mazungumzo yakamilike na baadaye vyama vyote viwili viwasilishe taarifa hiyo katika kipindi kimoja.”

 

Unapoyasoma maelezo hayo, utaona kwamba vyama vya CUF na CCM vilikubaliana kuwa taarifa za mazungumzo ziwasilishwe kwa pamoja katika vikao vyake vya juu baada ya mazungumzo kukamilika. Kwamba CUF na CCM viliwasilisha taarifa ya mazungumzo katika vikao vyao vya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na Halmashauri Kuu ya Taifa katika mwezi wa Machi 2008 ni ushahidi tosha kuwa mazungumzo yalishakamilika.

 

Ili kulielewa hilo, ni vizuri pia kuzisoma kumbukumbu za kikao hicho hicho kuhusiana na makubaliano ya kukamilisha mazungumzo (na hivyo kuwa ushahidi kuwa kinyume na upotoshaji wa CCM, mazungumzo yalishakamilika), katika uk. 5 kama ifuatavyo:

 

Mhe. Hamad Rashid Mohammed, aliyathibitisha yote yaliyosemwa na Mhe. Kingunge Ngombale-Mwiru. Kwa upande wake, aliongeza kuwa walikubaliana kuwa mazungumzo hayo yakifeli itakuwa fedheha kwa nchi na viongozi wake kutokana na matumaini yaliyojengwa kwa wananchi na jumuiya ya kimataifa. Pia alisema wamekubaliana kuwa mazungumzo yamechukua muda mrefu, hivyo hatua zichukuliwe kuyakamilisha ili ikifika Machi 2008 yawe yamemalizika.

 

Mazungumzo hayo yalikamilishwa katika kikao cha ishirini cha tarehe 24 – 29 Februari, 2008 ambapo agenda nam. 5 ilijadiliwa. Ni bahati mbaya kwamba kwa sababu hakujafanyika tena vikao vya mazungumzo kutokana na ubabaishaji uliofanywa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM huko Butiama, hakujakuwa na kumbukumbu za kikao hicho zilizopitishwa rasmi. Hata hivyo, miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa na kufanyiwa maamuzi katika kikao hicho yanatajwa katika orodha ya shughuli zitakazofanywa kupitia kumbukumbu za kikao cha kumi na tisa cha tarehe 14 – 21 Januari, 2008 (uk. 11) kama ifuatavyo:

 

“Mwenyekiti wa kikao Mhe. Kingunge Ngombale-Mwiru aliwaarifu wajumbe kwamba katika kikao kilichowashirikisha Makatibu Wakuu na Wenyeviti wenza wa Kamati walikubaliana mambo yafuatayo yazungumzwe:-

 

<!–[if !supportLists]–>· <!–[endif]–>Njia za Kujengeana Imani:

<!–[if !supportLists]–>(i) <!–[endif]–>Hatua za Kikatiba na Kisheria

<!–[if !supportLists]–>(ii) <!–[endif]–>Hatua za Kisiasa na

<!–[if !supportLists]–>(iii) <!–[endif]–>Hatua za Kiutawala

 

<!–[if !supportLists]–>· <!–[endif]–>Chombo cha utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa

 

Mwenyekiti Mwenza Mhe. Hamad Rashid alipendekeza kikao pia kijadili Ratiba ya Utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa.

 

Mwenyekiti wa kikao alithibitisha yale yaliyokubaliwa katika kikao cha Makatibu Wakuu na Wenyeviti wenza wa Kamati lakini akasema ni vyema suala la Ratiba ya Utekelezaji lije mwisho baada ya mambo yote yaliyotajwa kukamilika.”

 

Kama inavyoonekana katka kumbukumbu hizo, masuala hayo yote yaliyotajwa hapo juu yanahusu “Utaratibu wa Utekelezaji na Programu ya Utekelezaji wa Makubaliano yatakayofikiwa katika Mazungumzo haya”.

 

Labda kama kuna agenda iliyobaki ambayo haijajadiliwa basi ni hiyo itakuwa ni agenda ya 6 iliyozushwa na CCM inayohusu kura ya maoni. Na hiyo haikuwamo katika orodha ya agenda za mazungumzo ya CUF na CCM.

 

<!–[if !supportLists]–>III. <!–[endif]–>KUHUSIANA NA KUWEPO KWA RASIMU YA MAKUBALIANO:

 

UPOTOSHAJI WA CCM:

Kamati ya Mazungumzo ya CCM inawapotosha wananchi na jumuiya ya kimataifa kwamba eti hakukuwa na rasimu ya makubaliano iliyokubaliwa na CUF na CCM katika mazungumzo.

 

UKWELI WA CUF:

Rasimu ya Makubaliano ipo na ilipitishwa kwa pamoja na Kamati ya Makatibu Wakuu wa CUF na CCM katika kikao cha mazungumzo cha kumi na nane cha tarehe 03 – 04 Januari, 2008. Kumbukumbu za kikao hicho (uk. 5) zinaeleza:

 

Kikao kilikubaliana kwanza kupokea rasimu ya makubaliano yaliyokwisha fikiwa na baadaye kujadili njia za kujengeana imani.

 

Kaimu Katibu wa Kamati kutoka upande wa CCM, Mhe. Dk. Masumbuko Lamwai, kwa niaba ya mwenzake kutoka CUF, aliwasilisha rasimu waliyoitayarisha.

 

Rasimu hiyo iliyokuwa na kichwa na maneno “Rasimu ya Makubaliano kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Wananchi (CUF) katika kuupatia Ufumbuzi wa Kudumu Mpasuko wa Kisiasa Zanzibar“ ikiwa na kurasa na 13 inaambatanishwa pamoja na kumbukumbu hizi.“

 

Kikao kilipitia rasimu hiyo na kuifanyia marekebisho na hatimaye rasimu mpya ikiwa na marekebisho yote ikapitishwa. Kumbukumbu za kikao hicho hicho cha tarehe 03 – 04 Januari, 2008 (uk. 12) zinabainisha:

 

“Baada ya hatua hiyo, Makatibu wa kikao walitayarisha rasimu mpya ya makubaliano iliyoingiza marekebisho yote yaliyofanywa na kikao kiliipitisha rasimu hiyo.”

 

 

<!–[if !supportLists]–>IV. <!–[endif]–>KUHUSIANA NA KUWEPO KWA NAFASI YA WAZIRI KIONGOZI KATIKA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA NA MUDA WA KUUNDWA SERIKALI HIYO.

UPOTOSHAJI WA CCM

Kwamba Katibu Mkuu wa CUF aliwapotosha wananchi kwamba katika Serikali Shirikishi kutakuwepo nafasi ya Waziri Kiongozi ambaye atatoka katika Chama kitakachopata ushindi wa pili. Kwamba jambo hilo halijakuwepo kabisa katika makubaliano. Pia Kamati ya CCM inadai kwamba hakujakuwa na makubaliano kuwa Serikali ya Pamoja itaanza mara baada ya kutiwa saini kwa makubaliano na inadai kwamba “ujumbe wa CUF uliendelea kutoa maombi kuwa katika kipindi hiki kabla ya mwaka 2010 wapatiwe angalau nafasi mbili, tatu za Uwaziri ili waingie Serikalini. Ombi hilo lilikataliwa na ujumbe wa CCM kwa kuwa jambo hilo halikuwa katika mamlaka yake. Hilo ni suala la Dola.”

 

UKWELI WA CUF

Wajumbe wa CCM wamepotosha kwa makusudi suala hili. Wangetaka kuwa wakweli wangesema kwamba nafasi ya Waziri Kiongozi ilikubaliwa ifutwe katika muundo wa Serikali Shirikishi ambayo ilikubaliwa itaanza mwaka 2010. Hata hivyo, katika mazungumzo ilikubaliwa kuwa CUF ishirikishwe katika Serikali ya Zanzibar katika kipindi hiki (mara baada ya kutiwa saini makubaliano ya Muafaka) ambapo Serikali itaendelea kuwa na muundo wake kama ulivyo sasa yaani Rais na Waziri Kiongozi pamoja na Mawaziri wengine. Kumbukumbu za Kikao cha tarehe 21 Januari, 2008 kilichoongozwa na Makatibu Wakuu (uk. 5) zinasema:

 

“Mhe. Kingunge Ngombale-Mwiru alianza kwa kusema kwamba wameelewana kuwa pande zote mbili zinataka ufumbuzi wa kudumu wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar na kwamba unahitajika mustakbali mpya wa kisiasa ambao utatokana na uchaguzi ulio huru na wa haki mwaka 2010. Hata hivyo, katika kipindi hiki cha kuelekea 2010, kuwe na njia za kujengeana imani ambazo katika hatua za kisiasa zitajumuisha na Rais wa Zanzibar aliyepo madarakani kuteua mawaziri kadhaa kutoka CUF ili waingie Serikalini. Lakini kwa kuwa hili la Rais kuteua mawaziri kutoka CUF ni la Dola na si la vyama, basi CUF watatayarisha mapendekezo yao na kisha watayawasilisha kwa CCM ili yaweze kufikishwa kwa viongozi wa juu.”

 

Kwamba CUF iingizwe Serikalini kabla ya 2010 yalikuwa ni makubaliano ya Kamati ya Makatibu Wakuu liko wazi hapo juu. Mapendekezo ya CUF yalihusu kiwango cha ushirikishwaji na yaliwasilishwa kwa Katibu Mkuu wa CCM tarehe 22 Januari, 2008 kupitia barua yenye Kumb. Nam. CUF/AKM/CCM.II/2008/001. Sehemu ya barua hiyo inasema:

 

Kama tulivyokubaliana, nakuletea mapendekezo ya Chama Cha Wananchi (CUF) kuhusu kuingizwa kwa CUF katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mara baada ya kutiwa saini Makubaliano kati ya CCM na CUF kwa ajili ya kuyawasilisha kwa viongozi wakuu wa CCM. Mapendekezo haya yanajadilika.”

 

Mapendekezo hayo ya CUF yalikuwa kama ifuatavyo:

 

<!–[if !supportLists]–>1. <!–[endif]–>Rais wa Zanzibar na Waziri Kiongozi watoke upande tofauti kati ya CCM na CUF ili kujenga kuaminiana kwa kweli na kuendesha Serikali kwa mashirikiano ya pamoja.

<!–[if !supportLists]–>2. <!–[endif]–>Mawaziri (ikijumuishwa na nafasi ya Mwanasheria Mkuu) wagawiwe kwa idadi ambapo wanane (8) watoke CCM na saba (7) watoke CUF.

<!–[if !supportLists]–>3. <!–[endif]–>Upande mmoja ukipewa Waziri wa Wizara moja katika ule mlinganisho basi upande wa pili uachiwe Waziri wa Wizara iliyolinganishwa nayo.

<!–[if !supportLists]–>4. <!–[endif]–>Manaibu Waziri wanne (4) watoke CCM na watatu (3) watoke CUF kwa utaratibu kwamba Waziri na Naibu Waziri wa Wizara watatoka vyama tofafuti.

 

Pande zetu mbili zilikubaliana kuwa iwapo mapendekezo ya CUF yataonekana yamekwenda mbali mno basi viongozi wa CCM watarudi kwa wenzao wa CUF kuyazungumza kabla ya kuyafikisha kwa viongozi wa dola. Pamoja na barua ya Katibu Mkuu wa CUF kutamka wazi pia kwamba “Mapendekezo haya yanajadilika”, hakuna barua au mawasiliano yoyote mengine yaliyowasilishwa kwa CUF yaliyoashiria kutokubalika au kutaka marekebisho.

 

Hata katika barua ya Katibu Mkuu wa CCM ya tarehe 05 Mei, 2008 yenye Kumb. Nam. CMM/OND/804/C/5 ambayo ilikuwa inawasilisha maamuzi ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuhusu rasimu ya makubaliano, hamkuwa na chochote kilichoonyesha CCM kutokubaliana na mapendekezo ya CUF kuhusiana na Serikali ya Umoja wa Kitaifa kabla ya mwaka 2010. Kutokana na hatua hiyo, ndiyo maana katika majibu yake kwa barua hiyo, (barua Kumb. Nam. CUF/AKM/CCM.II/2008/009 ya tarehe 08 Mei, 2008), Katibu Mkuu wa CUF alimueleza kama ifuatavyo:

 

“Nimefurahi pia kwamba katika maamuzi ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM uliyotuandikia hakukuwa na mapendekezo yoyote ya marekebisho kuhusiana na hoja ya kushirikishwa kwa CUF katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mara baada ya kutiwa saini kwa Makubaliano ya Muafaka (transitional arrangement) kama tulivyokuwa tumekubaliana. (Rejea Kumbukumbu za kikao cha Kamati ya Makatibu Wakuu cha tarehe 21/01/2008 kilichofanyika Courtyard Protea Hotel, Dar es Salaam chini ya uwenyekiti wa Makatibu Wakuu wenyewe, uk. 4/5; na pia barua yangu Kumb. Nam. CUF/AKM/CCM.II/2008/001 ya tarehe 22 Januari, 2008). Kwa msingi huo, tunachukulia kuwa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM haikuwa na pingamizi kuhusiana na suala hilo na hivyo limekubalika.”

 

 

Ni kwa sababu suala hilo lilikwisha kubaliwa ndiyo maana lilikuwa sehemu ya rasimu ya makubaliano iliyofikishwa kwenye vikao vya juu vya vyama vyetu.

 

<!–[if !supportLists]–>V. <!–[endif]–>KUHUSIANA NA MAZUNGUMZO YA KUTAFUTA UFUMBUZI WA KUDUMU WA MPASUKO WA KISIASA KUTOHUSIKA NA UCHAGUZI MKUU WA 2005

 

UPOTOSHAJI WA CCM

Pamoja na hili kutokuwemo katika taarifa ya maandishi ya CCM, lakini katika kujibu maswali ya waandishi wa habari, wajumbe wa CCM walisema si sahihi kulinganisha mchakato wa makubaliano ya ufumbuzi wa mgogoro wa Kenya na yale yanayohusu mgogoro wa Zanzibar kwa sababu haya ya Zanzibar hayahusu kuhoji Uchaguzi Mkuu wa 2005.

 

UKWELI WA CUF

Kama kuna pahala, wajumbe wa CCM wameonyesha hawajui hata wanachokizungumza ni hapa. Bila hata ya kutumia Kumbukumbu za Vikao, taarifa yao wenyewe imeorodhesha agenda za mazungumzo na agenda ya kwanza waliyoitaja ilikuwa:

 

1. Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 30, 2005 na Taathira zake.

 

Hivi ujumbe wa CUF unahitaji kueleza zaidi kuhusu hili? Kama mazungumzo hayakuhusu uchaguzi huo wa 2005 na matokeo yake, na kwamba lengo lilikuwa kutazama mgogoro wa kihistoria wa ubwana, utwana, utumwa na usultani, mbona katika agenda zilizotajwa, hamna agenda inayohusisha masuala hayo ya kihistoria? Na kama chaguzi zote ni kielelezo tu cha mpasuko wa kisiasa na siyo tatizo lenyewe, basi ni kwa nini agenda ikajumuisha uchaguzi mkuu wa 2005 tu? Lakini mbali na hayo, ni vizuri sasa kuwaambia wananchi kuwa kichwa cha maneno cha agenda hii hasa kilikuwa ni “Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 30, 2005: Uhalali na Taathira zake”. Ni baada ya upande wa CCM kuomba baadaye kwamba neno hilo “UHALALI” lifutwe ili kujenga mazingira ya kuaminiana hasa kutoka kwa Mheshimiwa Amani Karume, ndipo CUF kwa nia njema ilipokubali. (Rejea Kumbukumbu za Kikao cha Tatu cha tarehe 22 – 25 Februari, 2007, uk. 2).

 

Suala la kuwauliza CCM ni kwa nini walikubali kuhojiwa uhalali wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa 2005 iwapo wao wanaamini ulikuwa huru na wa haki na hivyo haupaswi kuwa na mjadala?

 

Katika hoja zao wakati wanajibu maswali ya waandishi wa habari, wajumbe hao wa CCM pia walisema kuwa uchaguzi huo ni huru na wa haki kwa vigezo vya waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje. Hayo si kweli na ujumbe huo ulishindwa kutetea hoja hiyo pale CUF ilipotoa nukuu nzito nzito za ripoti za waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje zilizoonyesha kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki. (Waraka huo wa CUF unaambatanishwa hapa).

 

Labda kwa msingi wa hoja tu, tuulize kama ripoti za waangalizi wa uchaguzi ndiyo msingi wa kukubalika au kutokubalika kwa uchaguzi, mbona CCM ilikataa madai ya waangalizi WOTE wa uchaguzi wa ndani na nje waliotaka uchaguzi mkuu mwaka 2000 urudiwe upya chini ya Tume mpya ya Uchaguzi? Na vipi kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu wa 1995 ambayo CCM yenyewe baada ya kushindwa iliandika barua kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kuyakataa? (Rejea barua ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Ali Ameir Mohamed yenye Kumb. CCM/AKZ/U.30/21 ya tarehe 25 Oktoba, 1995).

 

<!–[if !supportLists]–>VI. <!–[endif]–>HOJA KUHUSIANA NA KURA YA MAONI

 

UPOTOSHAJI WA CCM

CCM, chama ambacho siku zote kimebeza na hata kuitukana dhana ya kuwashirikisha wananchi kupitia kura ya maoni katika masuala mazito yaliyohitaji kufanyiwa maamuzi katika nchi yetu, ghafla sasa kimekuwa kinadai kuwathamini wananchi kwa kutaka wapige kura ya maoni kuhusiana na suala la kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

 

UKWELI WA CUF

CUF ambayo siku zote imekuwa mstari wa mbele kutetea haki za msingi za raia ikiwemo ile ya kushirikishwa katika maamuzi ya mambo mazito yanayowahusu, imeikataa hoja ya kiusanii ya CCM ya kura ya maoni kwa suala la utatuzi wa mgogoro wa kisiasa Zanzibar kwa sababu zifuatazo:

 

  1. Hoja ya kura ya maoni haijawahi kuwa miongoni mwa agenda zilizokubaliwa katika mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar. Kama ilikuwa na nia njema, CCM ilikuwa na miezi 14 ya mazungumzo kuwasilisha pendekezo la hoja hiyo lakini haikufanya hivyo. Kulizua sasa wakati mazungumzo yamekamilika, tena kwa lengo la “kuipiku CUF kisiasa” hakuashirii kuwepo kwa nia njema kwa upande wa CCM katika mazungumzo haya.

 

  1. Mgogoro wa kisiasa Zanzibar kimsingi ni mgogoro uliotokana na kuendeshwa vibaya na kuvurugika kwa chaguzi za 1995, 2000 na 2005. Katika hali hiyo, uchaguzi kwa njia ya kura ya maoni hauwezi kuwa ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi bila ya kwanza taasisi zote zinazohusika na masuala ya uchaguzi kufanyiwa marekebisho.

 

  1. CCM na CUF wote wanakubaliana kupitia rasimu ya makubaliano kuwa taasisi zote zinazohusika na uendeshaji na usimamizi wa uchaguzi, zikiwemo Tume ya Uchaguzi, Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, Vyombo vya Ulinzi na Usalama na vyombo vya habari vya Serikali zina kasoro kubwa ambazo zinahitaji kurekebishwa. Vipi unaweza ukafanya kura ya maoni iliyo huru na ya haki katika hali kama hiyo?

 

  1. Hakuna sheria wala kifungu cha katiba kwa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinachozungumzia kura ya maoni, jinsi inavyofanyika na nguvu ya maamuzi yake. Kwa hivyo, kutahitajika marekebisho ya Katiba kwanza kabla ya kufanyika kura ya maoni. Marekebisho hayo ya Katiba kwa ajili ya kuruhusu kura ya maoni yatasimamiwa na nani?

 

  1. Iwapo Katiba itabadilishwa na kuingiza suala la kura ya maoni, je itakuwa ya maamuzi ya mwisho au ya ushauri tu? Iwapo itakuwa ndiyo yenye uamuzi wa mwisho, je yale masharti ya kwamba Katiba inaweza kubadilishwa kwa theluthi mbili ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi yatakuwa yanaondoka?

 

  1. Maamuzi makubwa na mazito zaidi hapa nchini yamefanywa bila ya kupigiwa kura ya maoni. Mifano ni mingi lakini kwa kutaja michache: Muungano wa Tanganyika na Zanzibar 1964, kufutwa kwa mfumo wa vyama vingi Tanganyika 1965, Azimio la Arusha 1967, kuunganishwa kwa TANU na ASP 1977, kupitishwa kwa Katiba ya kudumu ya Muungano 1977 na marekebisho yake yote 14 hadi sasa, kupitishwa kwa Katiba ya Zanzibar ya 1979 na 1984, kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi 1992, Marekebisho ya 11 ya Katiba ya Muungano yaliyofanywa 1994 ambayo yalimuondolea Rais wa Zanzibar nafasi yake ya kuwa Makamu wa Rais wa Muungano, Muafaka I wa 1999 na Muafaka II wa 2001.

 

  1. Katika utatuzi wa migogoro, kuna njia tatu za kufikia maamuzi yanayozaa ufumbuzi au suluhisho. Njia hizo ni ya uchaguzi (voting), ya muafaka (consensus), na ya kidikteta (imposition). Unapoamua kutumia njia mojawapo, huwezi tena mwishowe ukataka kuchanganya na njia nyengine. CCM na CUF vilikubaliana kutafuta ufumbuzi wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar kwa njia ya muafaka. Sasa kutaka kurejea katika uchaguzi (kura ya maoni) ni kichekesho. Je, iwapo ikipigwa kura ya maoni, asilimia 51% wakasema hawataki Serikali ya Umoja wa Kitaifa na asilimia 49% wakasema wanaunga mkono. Ukifuata matokeo ya kura ya maoni, ndiyo mgogoro au mpasuko utakuwa umeondoka? Utawafanya nini hawa asilimia 49% wanaounga mkono?

 

  1. Kura ya maoni ni njia ya hadaa ya kupoteza muda tu hadi 2010 ili kutayarisha mazingira ya uchaguzi mkuu mwengine utakaotawaliwa na vurugu na fujo kwa sababu tu CCM inaogopa uchaguzi huru na wa haki.

 

<!–[if !supportLists]–>VII. <!–[endif]–>UPOTOSHAJI WA CCM KUHUSIANA NA MUDA WA KUKAMILISHA MAZUNGUMZO

 

Kama kuna kitu CCM wanakikwepa na hawataki kukitolea maelezo ni kuhusiana na utaratibu wa mazungumzo na hasa muda wa kuyakamilisha.

 

Awali kabisa katika kikao cha kwanza cha Kamati ya Mazungumzo kilichofanyika tarehe 1- 2 Februari, 2007 huko Dodoma ilikubaliwa kuwa kufanyike vikao tisa (9) vya mazungumzo na kuweza kukamilisha kazi iliyokusudiwa. Hayo yanaonekana katika bajeti iliyopitishwa na kikao hicho kwa shughuli hiyo. Ilipopelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete kama ilivyokubaliwa na kikao, maamuzi yakawa tofauti. Kumbukumbu za kikao cha pili cha tarehe 13 – 14 Februari, 2007 (uk. 2) zinafafanua kama ifuatavyo:

 

<!–[if !supportLists]–>(a) <!–[endif]–>Kikao kilifahamishwa kwamba kama ilivyoamuliwa, nakala ya bajeti ya iliyopitishwa ilisainiwa na Wenyeviti Wenza na baadaye kukabidhiwa Mhe. Kingunge Ngombale-Mwiru kwa ajili ya kuifikisha Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano.

 

<!–[if !supportLists]–>(b) <!–[endif]–>Mhe. Ngombale-Mwiru alikiarifu kikao kwamba bajeti hiyo aliiwasilisha kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye aliipokea na kutoa ushauri wake. Mhe. Rais alipendekeza kwamba idadi ya vikao vya mazungumzo ipunguzwe na badala yake viwe vichache vyenye siku nyingi zaidi ili kupunguza gharama na shughuli hiyo iweze kufanyika na kumalizika haraka. Alipendekeza kutafutwa mahala penye utulivu wa kutosha ambapo patakuwa nje kidogo lakini karibu na Dar es Salaam kusudi wajumbe wakihitaji kufanya mashauriano na viongozi wao iwe ni rahisi.

 

<!–[if !supportLists]–>(c) <!–[endif]–>Wajumbe waliupokea ushauri huo wa Mhe. Rais kupitia kwa Mhe. Ngombale-Mwiru na kumuomba amfikishie Mhe. Rais shukrani zao kwa kuwapa ushauri huo mzuri.

 

<!–[if !supportLists]–>(d) <!–[endif]–>Kikao kilipendekeza kupunguza vikao kutoka tisa hadi vitatu kwa utaratibu utakaopendekezwa na pia kuchagua Bagamoyo kama mahala pazuri pa kufanyia shughuli hiyo.

 

Hata hivyo, vikao viliendelea na kuzidi vile vitatu vilivyokadiriwa awali. Ujumbe wa CUF ulianza kugundua kwamba CCM haikuwa na nia ya kuona mazungumzo haya yanamalizika na hivyo ikasisitiza haja ya kuyakamilisha.

 

Katika kikao kilichowashirikisha Makatibu Wakuu wa CUF na CCM peke yao hapo Mei 25, 2007 hatimaye walikubaliana kuwa mazungumzo yamalizike si zaidi ya Agosti 15, 2007. Pamoja na makubaliano hayo kuwa wazi, ujumbe wa CCM ulikuja kumkanusha Katibu Mkuu wake kuwa hakuwa na uwezo wa kufikia makubaliano hayo na Katibu Mkuu mwenzake. Kumbukumbu za kikao cha kumi na mbili cha tarehe 23 – 24 Juni, 2007 (uk. 2) zinalifafanua vyema hilo:

 

Mwenyekiti wa kikao, Mhe. Hamad Rashid Mohammed, alieleza kwamba katika kumbukumbu za kikao cha kumi na moja zilizothibitishwa kumejitokeza suala la haja ya kuweka muda wa kukamilisha mazungumzo (time frame). Alieleza kwamba Makatibu Wakuu wa CCM na CUF walipokutana tarehe 25 Mei, 2007 walilijadili hilo na kukubaliana kuwa mazungumzo haya yakamilike si zaidi ya tarehe 15 Agosti, 2007. Hivyo, alilisitiza haja ya kulizingatia hilo.

 

Mwenyekiti mwenza, Mhe. Kingunge Ngombale-Mwiru, alikifahamisha kikao kwamba kwa kumbukumbu zake suala la tarehe 15 Agosti, 2007 kuwa tarehe ya mwisho ya kukamilisha mazungumzo halikuwa makubaliano bali lilikuwa pendekezo la Katibu Mkuu wa CUF kwa Katibu Mkuu wa CCM.

 

Kutokana na tafsiri hizo tofauti, iliamuliwa kuwa Muhtasari wa Mazungumzo ya Makatibu Wakuu wa CCM na CUF ya tarehe 25 Mei, 2007 usomwe ili kuelewa msingi wa suala hilo. Muhtasari ulisomwa na wajumbe walikubaliana kwamba tarehe 15 Agosti, 2007 ilitokana na makubaliano ya Makatibu Wakuu wote wawili. Hata hivyo, ujumbe wa CCM ulitanabahisha kwamba kwa utaratibu wa Chama Cha Mapinduzi suala kubwa kama hilo ni lazima lifikishwe kwenye vikao vya ngazi za juu vya Chama.”

 

Suala la muda wa kukamilisha mazungumzo liliendelea kuibuliwa na CUF katika kila kikao kilichofuata (rejea kumbukumbu za vikao hivyo) na CCM ikawa inapiga chenga kutamka lini mazungumzo hayo yatamalizika. Hatimaye katika Taarifa ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa kwa vyombo vya habari tarehe 14 Agosti, 2007, alisema:

 

“Ni kweli, mazungumzo ni lazima yawe na ukomo. Na sisi wote tungependa yafikie mwisho wake mapema inavyowezekana. Lakini, ukomo wa mazungumzo ni lazima utokane na ridhaa ya pamoja ya pande zote na hasa kwamba ajenda zote zimepata nafasi ya kujadiliwa kwa kina na maelewano yamefikiwa.”

 

Baada ya tamko hilo la Rais na baada ya yale mazingatio aliyoyataja kufikiwa, hatimaye Kamati ya Makatibu Wakuu wa CUF na CCM ilikubaliana katika kikao cha kumi na tisa cha tarehe 14 – 21 Januari, 2008 (kumbukumbu za kikao uk. 12) kama ifuatavyo:

 

“Mwisho kikao kimekubaliana kwamba kikao kijacho kifanyike Dodoma kuanzia tarehe 10/2/2008 na wajumbe wote wafike Dodoma tarehe 9/2/2008. Wajumbe walikubaliana kuwa kikao hicho kijitahidi kukamilisha mambo yote yaliyobaki katika mazungumzo.”

 

Na katika kikao cha tarehe 21 Januari, 2008 kilichowashirikisha Makatibu Wakuu, kikao kiliafikiana (rejea Kumbukumbu za kikao, uk. 5) kwamba:

 

Mhe. Hamad Rashid Mohammed, aliyathibitisha yote yaliyosemwa na Mhe. Kingunge Ngombale-Mwiru. Kwa upande wake, aliongeza kuwa walikubaliana kuwa mazungumzo hayo yakifeli itakuwa fedheha kwa nchi na viongozi wake kutokana na matumaini yaliyojengwa kwa wananchi na jumuiya ya kimataifa. Pia alisema wamekubaliana kuwa mazungumzo yamechukua muda mrefu, hivyo hatua zichukuliwe kuyakamilisha ili ikifika Machi 2008 yawe yamemalizika.

 

 

Tumechukua sehemu kubwa ya taarifa kulitolea ufafanuzi suala hili ili Watanzania waone ustahamilivu mkubwa uliyoonyeshwa na CUF katika kuendesha mazungumzo haya, huku CCM ikionekana mara zote lengo lake ni kuwa na mazungumzo yasiyo na mwisho ili hatimaye yafikie mwaka 2010 bila ya kuchukuliwa hatua zozote za maana za utekelezaji wa yale yanayokubaliwa.

 

 

<!–[if !supportLists]–>VIII. <!–[endif]–>UZUSHI WA CCM KWAMBA CUF INAKUBALI KUWA INATOKANA NA ‘HIZBU’:

 

Katika kilele cha propaganda zilizopitwa na wakati, Mwenyekiti wa Timu ya CCM Mhe. Kingunge Ngombale-Mwiru katika mkutano wao wa waandishi wa habari, wakati akijibu maswali, alisema CUF inatokana na ‘Hizbu’ na yenyewe imekiri hivyo. CCM inapofika mahala hata mtu kama Mheshimiwa Kingunge akawa anazungumza uzushi wa waziwazi, basi kweli imefikia mahala pagumu na imepoteza dira na mwelekeo. Tunampa changamoto (challenge) Mzee Kingunge atoe ushahidi wa kauli yake hiyo.

 

Lakini hoja hii inatumiwa sana kuwapotosha wananchi, hasa wa Tanzania Bara, kuhusiana na misingi ya CUF. Kwa hivyo, pengine si vibaya kulifanyia uchambuzi kidogo suala hili.

 

Hoja hii siyo tu kwamba ni dhaifu bali ni kichekesho kabisa. Tunasema hivyo kwa sababu unapotazama hasa muundo na mpangilio wa uongozi katika vyama hivi viwili vinavyohodhi siasa za Zanzibar, yaani CUF na CCM, basi utaona kuwa ni CCM ndiyo yenye sifa zote za mahusiano na Hizbu, na siyo CUF. Na kwa msingi huo, kama kuna hoja pia ya kurudisha Waarabu, hilo linapaswa kukhofiwa kutoka CCM, na siyo kutoka CUF.

 

Hebu tuziangalie safu za viongozi wa vyama hivi viwili na tuone historia na chimbuko la viongozi hao.

 

Chama Cha Wananchi (CUF) kiliasisiwa mwaka 1992 pale Tanzania iliporuhusu mfumo wa vyama vingi. Viongozi wake wanne wakuu kutoka Zanzibar ni Seif Sharif Hamad, Ali Haji Pandu, Shaaban Khamis Mloo na Machano Khamis Ali. Wote hao ni wana-ASP wasio na chembe ya shaka.

 

Seif Sharif Hamad ingawa hakujishughulisha na siasa moja kwa moja katika miaka ya 1957 – 1964, lakini anatokana na familia iliyokuwa nguzo imara ya ASP kisiwani Pemba. Ushahidi wa hayo ni kuwa wakati Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM inapitisha azimio la kumfukuza uanachama wa CCM yeye na wenzake saba hapo Mei 13, 1988, mjumbe mmoja anayeheshimika kutoka Zanzibar, Mzee Mohamed Mahmoud Jecha, alisimama na kukiomba kikao kusimama kwa dakika moja kwa heshima ya kaka yake Maalim Seif aitwaye Hamad Sharif Hamad ambaye alimueleza kama mtu aliyekuwa mwana-ASP asiyetetereka wala kuyumba.

 

Ali Haji Pandu kutoka Makunduchi kisiwani Unguja alikuwa mwanachama wa umoja wa vijana wa ASP Youth League na pia umoja wa vijana wasomi wa ASP uliokuwa ukiitwa YASU na ndiyo uliompeleka masomoni Yugoslavia alikopata shahada ya sheria. Aliporejea kutoka masomoni baada ya Mapinduzi akateuliwa na Rais wa Kwanza, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar. Shaaban Khamis Mloo, mwenyeji wa Kikwajuni, mjini Unguja alikuwa kiongozi katika Umoja wa Vyama vya Wafanyakazi vilivyojitambulisha na ASP, umoja uliokuwa ukiitwa Zanzibar and Pemba Federation of Labour (ZPFL) na baada ya Mapinduzi aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya , Njia, Kazi na Nguvu za Umeme. Machano Khamis Ali kutoka Donge na Bumbwini kisiwani Unguja alikuwa mmojawapo wa vijana wa ASPYL na baada ya Mapinduzi alifanya kazi katika Idara ya Usalama wa Taifa kabla ya kuhamishiwa katika Jeshi la Polisi. Hao ndiyo viongozi wakuu wanne wa CUF.

 

Lakini hata ukizitazama safu nyengine katika Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF utawakuta watu kama Mzee Juma Ngwali Kombo ambaye hakuna asiyemuelewa kama kiongozi wa ASP kisiwani Pemba aliyekuwa akitegemewa.

 

Mwengine ni Hamad Rashid Mohammed, Kiongozi wa Upinzani Bungeni na mjumbe wa Baraza Kuu ambaye baba yake, Sheikh Rashid Mohammed Khamis, alikuwa ndiye Mwenyekiti wa ASP wa kisiwa cha Pemba na pia alikuwa mgombea ubunge wa ASP wa jimbo la Pujini. Pia yumo Mussa Haji Kombo ambaye baba yake, Sheikh Haji Kombo, alikuwa ndiye Katibu wa ASP wa kisiwa cha Pemba.

 

Hiyo ni mifano michache tu ya viongozi wa ngazi za juu wa CUF ambao wote wana asili na mizizi ya ASP. Sasa hebu tuitazame hali ya CCM Zanzibar ikoje?

 

Katika Mawaziri wa Zanzibar wa hivi sasa, yupo Waziri ambaye anajulikana kuwa alikuwa mwanachama wa Hizbu.

 

Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansour Yusuf Himid, ambaye ni ndugu wa mama mmoja na Shadya Karume, mke wa Bwana Amani Karume, wote wawili ni wajukuu wa Sheikh Mohammed Salim Jinja ambaye alikuwa mwasisi wa Hizbu na ambaye wenyewe Hizbu wakimwita ‘Founding Father of Zanzibar Nationalism’ yaani Mwasisi wa Dhana ya Uzalendo wa Kizanzibari, uliokuwa ndiyo msingi wa itikadi ya Hizbu. Mohammed Salim Jinja ni wa kabila moja la Barwani na kwa hakika ni bin-ami na aliyekuwa kiongozi wa Hizbu, Sheikh Ali Muhsin Barwani. Ndiyo kusema Mansour na Shadya katika nasabu ni watoto wa familia ya Sheikh Ali Muhsin Barwani.

 

Yupo pia Waziri mmoja katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Zanzibar ambaye anafahamika kwa lugha kali za matusi na kejeli dhidi ya Maalim Seif na CUF kupitia makala zake katika magazeti alikuwa mwanachama wa umoja wa vijana wa Hizbu uliokuwa ukijulikana kama Youth Own Union (YOU).

 

Lakini mbali ya viongozi hawa wa sasa, hata katika viongozi wastaafu, utawakuta watu kama Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi na Spika mstaafu wa Baraza la Wawakilishi, Mzee Ali Khamis Abdalla, ambao mara baada ya Uhuru wa Disemba 1963, walikwisha teuliwa kuwa Makatibu wa Kwanza (First Secretaries) wa Ofisi za Kibalozi za Zanzibar huko Indonesia na Misri. Wakati Mapinduzi yanatokea, Mzee Ali Khamis Abdalla alishakuwa Cairo akiwa ameanza kazi na ndiyo sababu ilimchukua miaka mingi kurejea Zanzibar baada ya Mapinduzi. Sheikh Ali Hassan Mwinyi yeye alikuwa katika matayarisho ya kuelekea Indonesia. Mamlaka iliyowateua ilikuwa ni ya Serikali ya Hizbu.

 

Msomaji utaona dhahiri kuwa CCM Zanzibar ina viongozi wengi wenye asili ya HIZBU tofauti na ilivyo CUF.

 

Lakini pia ukiangalia katika upande wa pili wa hoja kwamba CUF itarudisha Waarabu, ni jambo la dhahiri kwamba viongozi wa ngazi za juu wengi wa CCM na kabla ya hapo ASP wameoa Waarabu baada ya Mapinduzi. Hawa ni pamoja na Mzee Abeid Amani Karume, Mzee Aboud Jumbe, Sheikh Ali Hassan Mwinyi, Dk. Salmin Amour, Ramadhani Haji Faki, Said Iddi Bavuai, Khamis Darweshi, Hamid Ameir, Hassan Nassor Moyo, na hata Mheshimiwa Amani Karume na ndugu yake Ali Karume. Watoto wa viongozi hawa wa CCM ni machotara kwa maana ya kuchanganya damu za Kiafrika na Kiarabu. Kwa vyovyote vile, hawawezi kuukwepa Uarabu. Je, na hawa watakuwa hawana haki ya kuja kuiongoza kwa sababu ya dhambi ya asili ya mama zao kuwa ni Waarabu?

 

Ni bahati mbaya sana kwamba lugha zinazochochea ubaguzi na kujidai kuwakataa Ma-Hizbu zilizotolewa katika Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM hazikukemewa hata na Mwenyekiti wa CCM mwenyewe. Ulitumiwa Uhizbu kukataa ufumbuzi wa kudumu wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar wakati hao waliokuwa wakiwakataa Ma-Hizbu ndiyo Ma-Hizbu wenyewe.

 

Zanzibar ni visiwa vya watu mchanganyiko wenye asili za maeneo mbali mbali ya ndani na nje ya bara la Afrika. Zanzibar imekuwa Zanzibar kwa sababu ya ukweli huo. Kuna hatari kwamba tukianza kupigana mafungu kuwa huyu anafaa na yule hafai kwa sababu ya asili ya mtu anapotoka, tutakuja kufika siku ambapo tutawakataa hata wajukuu wa waasisi wa Mapinduzi. Mfano mzuri unaonekana katika familia ya Mheshimiwa Amani Karume.

 

Mwandishi wa kitabu kiitwacho ZANZIBAR: The Rise and Fall of an Independent State 1895 – 1964, aitwaye Suleiman Said Bin Shahbal, ambaye ni rafiki wa karibu wa Mheshimiwa Amani Karume, anaeleza hatari hiyo na mikanganyiko yake katika siasa za Zanzibar kupitia ukurasa wa 460 wa kitabu hicho:

 

“Yet it is not Amani Karume who is interesting. It is his children who are more interesting. The grand children of Abeid Amani Karume are also the grand children of Ali Muhsin Barwani. The son of Karume married from Ali Muhsin Barwani family. Today, Karume’s children are typically Zanzibari – neither pure Arab nor pure African. The same identity that Ali Muhsin spoke so often about, the same identity that the Zanzibari newspaper of Zam Ali Abbas wrote of in 1930’s. The grand children of Abeid Karume and Ali Muhsin debate the future of Zanzibar, debating whether the Union created by their grandfather is beneficial to their country or whether Zanzibar should go its own way. Within the Karume familiy, this is a raging debate. The Revolution has come full circle again.”

 

“Lakini si Amani Karume mwenye kuvutia (katika hili la mchanganyiko wa makabila). Ni watoto wake ndiyo wenye kuvutia zaidi. Wajukuu wa Abeid Amani Karume ni wajukuu pia wa Ali Muhsin Barwani. Mtoto wa Karume ameoa katika familia ya Ali Muhsin Barwani. Leo hii watoto wa Karume ni Wazanzibari hasa – si Waarabu safi na wala si Waafrika safi. Utambulisho wao ni ule ule ambao Ali Muhsin akiuzungumzia sana, na ndiyo ule ule ambao gazeti lililokuwa likiitwa ‘Zanzibari’ la Zaim Ali Abbas lilikuwa likiuandikia katika miaka ya 1930. Wajukuu wa Abeid Karume na Ali Muhsin wanajadiliana kuhusu mustakbali wa Zanzibar, wanajadiliana endapo Muungano ulioasisiwa na babu yao una manufaa kwa nchi yao au Zanzibar inapaswa kujitoa katika Muungano huo. Ndani ya familia ya Amani Karume, huu ni mjadala unaoendelea. Mapinduzi yamejidhihirisha tena upya.”

 

Hii ndivyo Zanzibar ilivyo. Hata tukitaka kulazimisha, haiwezi kuwa vyenginevyo.

 

 

<!–[if !supportLists]–>IX. <!–[endif]–>HITIMISHO:

 

Uzushi na upotoshaji hauwezi kuisaidia CCM ambayo inapoteza kwa kasi uhalali wa kisiasa kama chama chenye dira na mwelekeo hapa nchini. CCM inapaswa ijirudi na ijisahihishe kama inataka ikubalike kuwa ni chama makini mbele ya macho ya Watanzania na jumuiya ya kimataifa.

 

Kujidanganya kwamba wataendelea kufanya mchezo wa kitoto wa mazungumzo yasiyokwisha na baadaye kufikia Miafaka ambayo hawana nia ya kuitekeleza sasa hakuwasaidii tena maana Watanzania wameamka. Zanzibar kuna tatizo kubwa la kisiasa ambalo linahitaji kupatiwa ufumbuzi wa kweli, makini, wa dhati na wa haki.

 

Ni lazima pia tuseme tumesikitishwa sana na kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kukaa kimya wakati chama chake kikichezea shere suala zito linalohusu mustakbali wa taifa kama hili linalohusu mpasuko wa kisiasa Zanzibar. Kwa hatua iliyofikia sasa, yeye ndiye mtu pekee anayeweza kuyanusuru mazungumzo haya. Watanzania wanahitaji kumuona kama anavyojishughulisha na masuala ya Kenya, Comoroes, Zimbabwe na hivi majuzi tu mgogoro wa DRC Congo na Uganda, basi kwa uzito mkubwa zaidi ashughulikie suala hilo la mpasuko wa kisiasa Zanzibar. Wahenga wamesema sadaka huanzia nyumbani.

 

Mwisho, tunaendelea kuwasisitiza CCM kwamba njia za kutufikisha huko kwa sasa ni mojawapo kati ya hizi zifuatazo:

 

  1. CCM kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa na Kamati ya Mazungumzo ya vyama vyetu viwili na endapo kweli Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho “imeyakubali kimsingi” makubaliano yaliyofikishwa kwake kama ilivyosema taarifa yake, basi kikubali kutia saini makubaliano hayo na utekelezaji wa yaliyokubaliwa uanze mara moja.

 

  1. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete achukue hatua za haraka kuitisha mkutano wa pamoja utakaomshirikisha yeye pamoja na wadau wakuu wa masuala haya kwa Zanzibar ambao ni Mheshimiwa Amani Karume na Maalim Seif Sharif Hamad kujadili na kukubaliana juu ya mapendekezo yaliyotolewa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na kisha kuhitimisha makubaliano hayo kati ya vyama vyetu viwili.

 

Kama hayo hayafanyiki, CUF inatoa wito kwa marafiki wa Tanzania na jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti, za uhakika na za haraka kuingilia kati suala hili ili kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa yanatiwa saini. Baada ya Tanzania yenyewe kushindwa katika utatuzi wa mgogoro wake huu wa muda mrefu, sasa ni wakati muafaka kwa Jumuiya ya Kimataifa kuingilia kati kwa kuhakikisha makubaliano ya dhati yanafikiwa yatakayotoa ufumbuzi wa kweli na wa haki wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar.

 

CUF inatoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuepuka fedheha iliyoipata katika nchi nyengine za Kiafrika ambazo iliziachia hadi hali ikachafuka na ndipo ikaingilia kati. Hali ya Zanzibar ni mbaya. Ilitulia kwa sababu ya matumaini ya Wazanzibari na Watanzania kwamba mazungumzo ya CCM na CUF yataleta suluhisho la utulivu na umoja. Makubaliano yaliyofikiwa yanapokosa uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuyakamilisha, yanahitaji kuona jumuiya ya kimataifa inaingilia kati kwa hatua za wazi na madhubuti kuinusuru Zanzibar na Tanzania isitumbukie kule nchi nyengine za Kiafrika zilipotumbukia.

 

Wakati tunawashukuru kwa dhati viongozi wa vyama vyengine vya siasa, viongozi wa dini, taasisi na jumuiya za kijamii, mabalozi wa nchi za nje wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania na vyombo vya habari hususan magazeti huru kwa mchango wao mkubwa walioutoa na ambao ulisaidia kuyafikisha mazungumzo hadi hatua ya kukamilishwa, CUF tunatoa wito tena kwao kuendelea kutoa ushirikiano wao na kutimiza wajibu wao kuona mgogoro huu unamalizwa kwa njia za amani na za haki.

 

CUF inawataka wanachama na wapenzi wake pamoja na Wazanzibari na Watanzania wote kwa ujumla kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hiki wakijua kuwa CUF iko upande wa amani, ukweli na haki na siku zote upande wa amani, ukweli na haki utashinda.

 

 

HAKI SAWA KWA WOTE

 

 

Dar es Salaam

13 Mei, 2008

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s