Muungano kama nyenzo ya kuwagawa Wazanzibari

Mhe. Juma Duni Haji, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Zanzibar

Mhe. Juma Duni Haji, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Zanzibar

“Kwa hivyo suala la kuuliza ni kwa nini kila baada ya miaka mitano kunatokea mgogoro wa kisiasa Zanzibar? Mgogoro wa kisiasa unatokea kwa sababu hakuna utashi wa kufanyika uchaguzi huru na wa haki huko Zanzibar. Mimi ninaamini kwamba na huku Bara hali ni kama hiyo. Matatizo ya huku yanafichika kutokana na ukubwa wa nchi na wala si usafi wa chaguzi zenyewe. Vurugu za kuharibu uchaguzi kila baada ya miaka mitano, mara zote, husindikizwa na viongozi wa CCM na vyombo vya Serikali ya Muungano hasa vyombo vya ulinzi: jeshi la polisi, majeshi ya ndani na hata ya kuazimwa, majeshi kutoka nchi jirani, pamoja na kutumiwa Usalama wa Taifa kuendesha chaguzi hizo. Kila ikifika uchaguzi, vyombo vya Serikali ya Muungano ndivyo husindikiza na kulinda makundi haramia ya vijana wa CCM maarufu kwa jina la Janjaweed wanaosaidiwa na vikosi vya SMZ, kuhujumu utaratibu mzima wa kuendesha uchaguzi huru na wa haki.”

Hotuba ya Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Mhe. Juma Duni Haji, katika Kongamano la Kuadhimisha Miaka 44 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tarehe 26 Aprili, 2008

UTANGULIZI

Nashukuru kualikwa kushiriki mjadala wa Kustahiki kuwepo au kutokuwepo Muungano wetu (feasibility of the Union). Nimetakiwa nizungumze juu ya vipi ‘Siasa za Muwafaka wa Zanzibar zinavyo au zitavyoathiri kuwepo kwa Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar.

Miaka miwili iliyopita, nilialikwa katika maadhimisho kama haya ili nije kutoa maoni yangu juu matatizo ya Muungano ambayo wenzetu huyadogoza na kuyaita ‘Kero za Muungano’. Leo nimepata tena nafasi kama ile. Hoja ya leo inahusiana sana na mjadala uliopita, kwani kama ninakumbuka vyema nilisisitiza sana hapa kwamba tatizo linalouponza Muungano ni tabia ya kujiona Serikali ya Muungano ndiyo yenye nguvu kwa Zanzibar na kwamba uendeshaji wa siasa za Zanzibar huamuliwa kwa maslahi ya upande mmoja wa Muungano bila kujali athari za upande wa pili.

Hivi ninavyozungumza, tumo kwenye kukwama kwa kusainiwa kwa Muwafaka wa Tatu wa Zanzibar ambao ulitegemewa utoe suluhisho la kudumu la Mgogoro wa Kisiasa Zanzibar na, pengine, kupunguza hizo ‘Kero za Muungano.’

Ni vizuri kuzingatia kwamba Muwafaka wa Tatu umekuja kwa sababu miafaka miwili mengine ya 1999 na ule wa 2001 haijasaidia kumaliza mgogoro wa Zanzibar, kwa sababu wale waliopo kwenye madaraka wamekataa kuitekeleza kwa makusudi. Kwa mfano, katika Muwafaka wa 2001, kwa mujibu wa sheria iliyotungwa baada ya kutiwa saini muwafaka huo, Mhe. Amani Karume alitakiwa kuteuwa wawakilishi wawili tu kuingia katika Baraza la Wawakilishi kutoka CUF. Hili lilimshinda. Sisi mpaka leo tunajiuliza: je, kuteua wawakilishi  nako kunahitaji  fedha za nje za msaada wa wafadhili?

Kuvurugwa kwa chaguzi kwa kutumia Vyombo vya Dola

Kwa hivyo suala la kuuliza ni kwa nini kila baada ya miaka mitano kunatokea mgogoro wa kisiasa Zanzibar? Mgogoro wa kisiasa unatokea kwa sababu hakuna utashi wa kufanyika uchaguzi huru na wa haki huko Zanzibar. Mimi ninaamini kwamba na huku Bara hali ni kama hiyo. Matatizo ya huku yanafichika kutokana na ukubwa wa nchi na wala si usafi wa chaguzi zenyewe.

Mhe. Juma Duni Haji

Mhe. Juma Duni Haji

Vurugu za kuharibu uchaguzi kila baada ya miaka mitano, mara zote, husindikizwa na viongozi wa CCM na vyombo vya Serikali ya Muungano hasa vyombo vya ulinzi: jeshi la polisi, majeshi ya ndani na hata ya kuazimwa, majeshi kutoka nchi jirani, pamoja na kutumiwa Usalama wa Taifa kuendesha chaguzi hizo.

Kila ikifika uchaguzi, vyombo vya Serikali ya Muungano ndivyo husindikiza na kulinda makundi haramia ya vijana wa CCM maarufu kwa jina la Janjaweed wanaosaidiwa na vikosi vya SMZ, kuhujumu utaratibu mzima wa kuendesha uchaguzi huru na wa haki. Tafadhalini angalieni takwimu nilizozileta kwenu juu ya mwendo wa uchaguzi wa 2005 zenye kuthibitisha maelezo haya. Vurugu huanza tangu wakati wa kufanya makisio ya uandikishaji kama ilivyooneshwa hapa chini:

Jimbo

Pop. 2005

48 %  as Voters

ZEC Estimate.

Registered voters

Uzini

19,049

9,144

10,117

14,101

Muyuni

17522

8,411

11,506

9,785

Makunduchi

16,501

7,921

7,269

10,839

Donge

18,584

8,920

9,561

11,634

Bumbwini

17,856

8,571

9,314

10,904

Chwaka

21,785

10,457

11,620

13,773

Kojani

25,575

12,276

9,556

10,469

Mgogoni

21,560

10,349

6,689

8,329

Chambani

17,741

8,516

8,356

6,404

Mkoani

19,484

9,352

9,487

8,319

Chanzo: ZEC 2005

Mfano mzuri wa vurugu za uandikishaji zinaonekana katika vituo vya jimbo la Uzini, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, ambalo ni moja kati ya majimbo makubwa ya CCM.  

VITUO

Name of the Camps

Estimates

Registered

%  Registration

UBAGO SCHOOL

UBAGO TPDF

441

1402

317.91

MACHUI SCHOOL

MACHUI JKU&FFU

696

1060

152.3

POSTA KAE PWANI

UNGUJA UKUU NAVY

1268

2076

163.72

TUNGUU SCHOOL

TUNGUU FIRE BRIGADE

520

556

106.92

MARUMBI SCHOOL

MARUMBI NAVY

561

876

156.15

DUNGA BWENI SCHOOL

DUNGA JKU&FPDF

1520

2106

138.55

JENDELE SCHOOL

JENDELE JKU

907

1366

152.81

CHEJU SCHOOL

CHEJU PRISON

971

1163

119.77

BAMBI SEC. SCHOOL

BAMBI JKU

1336

2125

159.06

JUMLA

8220

12730

154.87

Uandikishaji wa aina hii huanza kulalamikiwa mapema hata kabla kupigwa kura. Haya hufanyika chini ya ulinzi wa polisi wa Muungano na vikosi vya SMZ.

Kuvurugwa kwa Daftari la Kudumu la Kupigia Kura

Hali ya Daftari la Wapiga Kura la Zanzibar haliwezi kuitwa daftari, maana kuna watu waliozaliwa mwaka 2005 wamepewa vipande vya kupigia kura.

Majina ya mitaa kama Forodhani, Muembeladu na Mbuyuni pia yamepewa vipande vya kupigia kura. Kuna majina yaliyorudiwa mara mbili mbili na kuna majina yasiyo baba wala babu kama vile ni majina ya Adama na Hawa – manabii wa Mungu, na baadhi ya majina kukosa tarehe ya kuzaliwa. Mengi ya majina haya ni ya watoto wadogo.

Daftari la aina hii haliwezi kutoa matokeo yenye kukubalika. Kuongeza wapiga kura hewa kumeongeza nafasi ya kuzifanya kura za Karume kuonekana nyingi, kumbe sehemu kubwa si kura za watu isipokua ni nambari zilizoandaliwa kwa lengo la kutoa ushindi bandia kama inavyonekana hapa chini katika baadhi ya matokeo ya majimbo ya uchaguzi:

Jimbo

Watu/005

(a)

48%  watu (b)

Makisio / ZEC

(c)

Registered

(d)

Kura / Karume

(e)

% (e)/(d)

% (e)/(b)

Bumbwini

17,856

8,571

9,314

10,904

6,189

57

89

Kitope

20,210

9,701

10,714

10,378

8,099

78

83

Donge

18,584

8,920

9,561

11,634

10,124

87

106*

W/Kas’B’

56,650

27,192

29,589

32,916

24,412

74

90

Chwaka

21,785

10,457

11,620

13,773

11,161

81

107*

Koani

25,726

12,348

13,167

15,639

10,664

68

86

Uzini

19,049

9,144

10,117

14,101

12,486

89

137*

W /Kati

66,560

31,949

34,904

45,513

34,311

79

107.4*

Muyuni

17,522

8,411

11,506

9,785

7,741

79

92

Makunduchi

16,501

7,921

7269

10,839

8,659

80

109*

W/Kusini

34,024

16,331

18,776

20,624

16,400

80

100.4*

Chanzo: Takwimu za ZEC 2005

Matokeo ya Uchaguzi 2005

Pamoja na kuvurugwa kwa utaratibu mzima wa uchaguzi na nguvu nyingi  kutumika, bado matokeo yaliyotolewa na ZEC yamezaa ulalamishi. Maana katika kipindi cha mwezi mmoja, yametolewa matokeo aina mbili tafauti kwa upande wa nafasi ya uraisi:

MAELEZO

MATOKEO

CCM

CUF

Kama Yalivyotangazwa na

ZEC baada ya uchaguzi

ZEC 1

239,832

53.2%

207733

46.1%

Baada ya kurekebishwa

Mwezi mmoja baadae

ZEC 2

241,899

53.6%

205,872

45.6%

TAFAUTI

+2067

-1861

Ushindi huo wa Mhe. Karume uliambatana na kufichwa fomu za uchaguzi kura kuonekana tafauti katika vituo na ulisukumwa na nguvu za dola zilizojumuisha Tume ya Uchaguzi (ZEC), Masheha, Polisi, Jeshi la Wananchi (JWTZ), KMKM, JKU,  Jeshi la Magereza, Zima moto, Volantia, Usalama wa taifa, Janjaweed, TVZ, Redio Zanzibar na vyombo vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Baada ya nguvu zote hizi, mtu angetegemea kwamba, ushindi wa Mhe. Amani upindukie asilimia zaidi ya 80. Lakini bado matokeo yaliyotolewa na ZEC hayajaonesha tafauti kubwa kati ya washindani hao wawili. Kwa maelezo mengine, ushindi huu wa CCM usingewezekana kama nguvu zisingetumika na utaratibu wa uchaguzi ungefuatwa. Kwa ufupi, hivyo ndivyo chaguzi za Zanzibar zinavyokua.

Historia ya mauaji Zanzibar na mchango wa CCM na SMT katika mauaji hayo

Mhe. Kikwete anajua kwamba CUF ilishinda chaguzi zote tatu za 1995, 2000, na 2005. Anajua kwamba wafuasi wa CUF wameuliwa na polisi wa Muungano, na kwa mara ya kwanza Tanzania kuzaa janga la wakimbizi. Lakini bado viongozi wa CUF wamerudi na kukaa na wauaji hao kuzungumza ili kumaliza uhasama wa siasa wa Zanzibar.

Kinachosikitisha ni kwamba viongozi wa CCM na wa Serikali ya Muungano hawapendi kuona Wazanzibari wanasikilizana. Wanafurahia tuendelee kugombana kwa kutumia siasa za wagawe ili uwatawale (Divide and Rule).

Kiongozi mmoja mkubwa  wa CCM kutoka Bara wakati tukianza mazungumzo, alifika hadi kutwambia kwamba: “Nyinyi CUF mara hii hamna uzito wa hoja kwenye mazungumzo, kwa sababu hakuna Wazanzibari waliokufa. Bora mazungumzo ya 2001 mulikua na hoja ya msingi.”

Sisi tulishangaa sana kusikia kauli ya kiongozi wa Muungano akisema hivyo. Baada ya NEC ya CCM kuyakataa makubaliano tuliyofikia, ndipo tulipozinduka na kuelewa kiongozi yule alikusudia nini.

Ushahidi wa kueleza haya ni jinsi Mhe. Kiwkete na CCM walivyolichukulia maskhara suala hili la Muwafaka. Mhe. Kikwete  ndiye kiongozi wa nchi , na pia kiongozi wa chama chake, vipi anashindwa kufanya maamuzi ya kuona amani inapatikana Zanzibar?

Badala yake anakuja na lugha ya kisanii na kuepuka hoja ya msingi ya kukamilisha makubaliano yaliyofikiwa yatakayoandaa mazingira mazuri ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki hapo 2010

Pendekezo la CCM la ‘Kura ya Maoni’

Kura ya maoni inayopendekezwa na CCM inatafuta jibu moja kati ya mawili yafautayo: aidha watu wengi kukubali mfumo mpya wa serikali shirikishi au watu wengi kukataa serikali shirikishi.

CUF wanauliza kama wengi watasema wanataka, je kuna uhakika gani wa Mhe. Karume kutekeleza maamuzi hayo akiachiwa peke yake? Maana Muwafaka wa 2001 alishindwa kuteua wajumbe wawili wa Baraza la  uwakilishi kutoka CUF, vipi atakubali kutekeleza kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa hivi sasa kabla kupiga kura ya maoni?

Na kama watu wengi watasema hawataki serikali ya umoja wa kitaifa, je hali hiyo itakua imetoa jibu la ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huo wa Zanzibar? Maana chanzo cha mgogoro imetokana na SMZ kubaki washindani na wasimamizi wa chaguzi na hivyo kuvuruga utaratibu mzima wa uchaguzi huo.

Katika hali zote mbili, kura ya maoni haiwezi kusaidia chochote kati ya hayo mawili kwenye mazingira ya sasa ya CCM kubaki peke yao katika serikali.

Ufumbuzi wa kudumu utapatikana vipi?

Mhe. Kikwete anajua kwamba bila uchaguzi huru na wa haki 2010 Zanzibar, ni kurudia vurugu na mauaji mengine Visiwani humo. Hiyo Serikali ya Umoja wa Kitaifa hapo 2010 haiwezi kupatikana bila uchaguzi huru na wa haki 2010. lakini ni vipi utapata uchaguzi huru 2010 bila kutekeleza muwafaka kwa kushirikiana pamoja hivi sasa?

Mhe. Kikwete anajua kwamba Karume hakushinda uchaguzi wa 2005 na hivyo serikali iliyopo madarakani hivi sasa siyo halali, vipi anakubali kufanya kura ya maoni kwa kutumia serikali isiyokubalika na wananchi, chini ya Tume ya Uchaguzi isiyokubalika na chini ya  Daftari lisilokubalika?

Mhe. Kikwete anajua kwamba bila CCM na CUF kufanya kazi pamoja kuanzia sasa katika serikali ya pamoja kwa kutekeleza Muwafaka huu, hakutakua na uchaguzi huru na wa haki 2010. Kwa hivyo, kizingiti cha muwafaka wa sasa kipo penye tatizo la utaratibu wa namna ya kupata uchaguzi huru na wa haki hapo 2010 ili tuepuke mgopgoro mpya.

Lakini, pamoja na kujua yote hayo, badala yake Mhe. Kikwete amekwenda Butiama kuzaa mgogoro ndani ya mgogoro. Eti ‘Kura ya Maoni.’ Aulizwe nani chini ya usimamizi wa nani ili upate jibu gani ambalo hivi sasa halipo?

Imani huzaa imani. CUF – Chama cha Wananchi kilionesha imani kwa kuiachia miwafaka miwili ya 1999 na ule wa 2001 itekelezwe na Serikali ya SMZ, bila sisi kushiriki, maana CUF hatuna nguvu za Dola. CCM na Serikali, kwa maksudi, walikejeli miafaka hiyo na matokeo yake kwa mara ya tatu tunazungumzia muwafaka mwengine.

Hivyo, chama chetu, CUF, kimesimama na kauli kwamba kama hakuna imani ya kufanya kazi pamoja hivi sasa, hakuna matumaini yoyote ya kutekelezwa muwafaka huu.

Na kama CCM inakataa kufanya kazi pamoja hivi sasa, hakuna matumaini ya kuwepo serikali ya pamoja hapo 2010.

Hiki kilikuwa ndicho kipimo kikubwa cha kuupima uongozi wa CCM kwa wao kuonesha kwamba wako tayari kumaliza mgogoro wa Zanzibar. Mhe. Kikwete na CCM wamefeli mtihani huu mdogo.

Usanii wa Kisiasa

Waraka wa CCM uliofikishwa kwenye NEC umethibitisha kwamba ajenda mpya kuhusu kufanywa kura ya maoni ameipeleka Mhe Kikwete kwenye NEC baada ya kujadliwa katika Kamati Kuu. Inashangaza baadae Rais anarudi kuwaambia wakazi wa Dar es Salaam kwamba hoja ilitokana na mjadala.

Mhe. Kikwete anafanya usanii wa kisiasa, na matokeo ya usanii wake ni janga kwa Wazanzibari waliochoka mateso kwa kutopewa nafasi ya kuchagua kwa hiari yao viongozi wanaowataka bila ya sindikizo la Serikali  ya Muungano

Kikwazo cha Migogoro ya Zanzibar

Kwa hivyo, Wazanzibari wote wanaamini kuwa viongozi wa Muungano ndiyo kikwazo cha ufumbuzi wa matatizo yao ya kutosikilizana ili kujenga nchi yao, kwa sababu kila unapofika wakati wa uchaguzi, huleta majeshi kulazimisha chama cha CCM kishinde.

Kwa mfano, wakati Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa akijitayarisha kwa uchaguzi wa 2005, alisema bila kificho kwamba atafanya kila lililo katika uwezo wake kuhakikisha kwamba CCM inashinda Zanzibar na Bara. Ndipo akatuletea vikosi vya polisi na majeshi kunajisi na kupiga wafuasi wa CUF, huku jeshi hilo chini ya Kamanda wa Mkoa wa Mjini Magharibi aitwae George Kizuguto, likivilinda vikundi kiharamia vya CCM vifanye vitakavyo.

Kabla ya hapo, pale mwaka 2001 wakati wa maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi, Mkapa alipeleka askari aliowaita Ngunguri kule Zanzibar na wakawaua Wazanzibari wasiopungua 45 na baadae Rais akarudi kujisifu kwamba: “Tusifanye mchezo maana hiyo ndiyo maana ya Mapinduzi daima.”

Baada ya kuwaua Wazanzibari wale, Mkapa alikuja kwenye mkutano wa hadhara pale Jangwani na kuwapa vyeo askari walioua. Hivyo ndivyo Serikali ya Muungano inavyowafanyia Wazanzibari.

Tulitegemea matukio yale yawe fundisho kwa Mhe. Kikwete. Hali iliyojidhihirisha kule Butiama ni kwamba yale yaliyotokea kule Zanzibar 2001 na 2005, hayajamshtua na wala hatajali yakitokea tena 2010.

Kwa miaka 15 sasa Chama cha Wananchi (CUF) kimeonesha uvumulivu mkubwa sana ili kuepusha Wazanzibari wasianze mapigano ya wenyewe kwa wenyewe. Viongozi wetu wa kitaifa wamefika kiwango cha kutukanwa hadharani na wafuasi wao pale walipowakataza  wasijibu fujo kwa fujo. Wamekua wakifanya hivyo kwa maslahi ya taifa. Kila mara tumekua tayari kuacha kudai hoja ya msingi ya kurejewa uchaguzi ulioharibiwa kwa maksudi ili kulinda Umoja wa Wazanzibari. Viongozi wa CCM na Muungano wao bado hushikilia misimamo ya chama chao.

Hivyo athari za siasa za Muwafaka wa Zanzibar kwa Muungano ni sawa na kuweka kijinga cha moto kwenye jaraha la mateso ya Wazanzibari, na kwa Wazanzibari ni ushahidi mwengine kwamba Muungano huu hauna faida kwao isipokua kuwakandamiza na  kwa kutumia nguvu.

Ahadi na malengo ya Mapinduzi ya 1964 na ubaguzi wa kihafidhina

Mapinduzi yalikua na lengo la kuwaunganisha Wazanzibari wawe kitu kimoja. Baada ya miaka 50, Wazanzibari wamegawika zaidi kuliko walivyokua kabla ya Mapinduzi. Huku ni kupotosha lengo la Mapinduzi ya 1964.

Wachunguzi wa kitaalamu wanabainisha kuwa iwapo historia ndiyo inayotizamwa katika kuueleza muundo wa kisiasa wa visiwa viwili vya Unguja na Pemba kwa kudhani kuwa kila kisiwa kimekuwa ngome ya chama kimojawapo peke yake, basi matokeo ya tafiti zinazotokana na hali halisi hayaneshi hivyo.

Huko Pemba ambako ndiko kisingizio kikubwa cha wahafidhina wa Zanzibar wanakokueleza kuwa CCM haiungwi mkono, ukweli ni kwamba katika uchaguzi mkuu wa Julai 1963 chama cha Afro-Shirazi(mzazi mmoja wa CCM) kilipata asilimia 44 ya kura zote za kisiwa hicho. Lakini leo, katika kipindi cha miaka takriban 50 ya utawala wa ASP/CCM, matokeo ya kura za urais yameshuka na kutoa sura mbaya sana ya kibaguzi kama inavyoonekana hapa chini. Kura za ASP/CCM kutoka Pemba zimeshuka kutoka asilimia 44 hapo 1963 na kufika asimia 16 tu 2005. Si hivyo tu, ila kilicho kibaya ni kwamba katika kila kura 100 za ushindi wa CCM, mchango wa kura za Pemba katika ushindi huo umeshuka mpaka kura 9 tu  katika uchaguzi wa 2005.

CHAMA/VYAMA

Oktoba 1995

Oktoba 2005

Unguja

Pemba

Unguja

Pemba

CHAMA CHA  MAPINDUZI (CCM)

144,408

20,863

217,209

22,413

69%

17%

72%

16%

Mchango/Kisiwa katika ushindi

87%

13%

91%

9%

Wahafidhina wa CCM walipaswa kujiuliza hali hii imesababishwa na nini. Si kingine isipokua siasa mbaya za kibaguzi na ukandamizaji, kama zinavyothibitika katika mfumo wa serikali ya SMZ hivi sasa. Hivi ninavyozungumza Serikali ya Zanzibar ina umbo lifuatalo:

Wadhifa

Unguja

Pemba

Jumla

Mawaziri

14

1

15

Naibu Waziri

5

1

6

Makatibu Wakuu

13

2

15

Naibu Makatibu Wakuu

12

0

12

Wakuu wa Mikoa

4

1

5

Wakuu wa Wilaya

7

3

10

Wakuu wa Idara

83

17

100

Wakuu wa Polisi

18

0

18

Wakuu wa Vikosi vya SMZ

5

0

5

Kamati za Baraza la Wawakilishi

5

1

6

Jumla

166

26

192

Nyote munaelewa kwamba hata Pemba wapo wanachama na viongozi wa CCM wenye uwezo na waliosoma kuweza kuteuliwa kushika nyadhifa hizo. Lakini kwa makusudi kabisa, viongozi wanaojidai kulinda Mapinduzi wamewaacha. Kweli haya ndiyo malengo ya Mapinduzi ya 1964?

Mapinduzi ya 1964 yalitegemewa kuwatoa watoto wa wakwezi na wakulima kutokana na mateso ya utumwa na maonevu: mateso ya kukosa elimu na pia mateso ya kubaguliwa. Leo watoto wa wakwezi na wakulima wanagombanishwa wenyewe kwa wenyewe. Wamefanywa watumwa wa hiari chini ya ulinzi wa Polisi.

Kwa mwenendo huu ile falsafa ya Mwalimu Julius Nyerere ya Pan-Africanism ni ndoto ya Alinacha, maana kama nchi mbili zinaendeleza ubaguzi mbaya kuliko ule wa Makaburu, vipi tutaweza kujenga umoja wa Waafrika. Ni aibu kwamba vijana waliokoseshwa elimu huchukuliwa katika makambi na kufundishwa chuki za kuwachukia ndugu zao. Vijana kutoka Makunduchi, vijana waliokata tamaa ya maisha, wakiongozwa na askari wa KMKM, JKU, Magereza na Polisi  walikwenda katika kisiwa cha Tumbatu au Pemba na kuwanajisi ndugu zao, kuvunja nyumba zao na kuwalazimisha wakimbie katika makazi yao. Kosa la Watumbatu na Wapemba wale ni kukipigia kura chama cha CUF.

Mateso haya yalifanywa chini ya usimamizi wa Polisi na mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, ambae pia ni mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM, Mhe. Haji Omar Kheri. Huyu si Mwarabu, huyu ni mtoto wa Kitumbatu, aliyezaliwa Tumbatu na kusoma Tumbatu. Baada ya kupata bahati ya kuwasaidia jamaa zake, amewageuka na kuwafanya vikaragosi, walokosa heshima. Hapo ndipo CCM na Serikali ya Muungano ilipowafikisha Wazanzibari. Haya ndiyo yanayotakiwa yaendelezwe hapo 2010 na Mhe. Kikwete anayafurahia na kuyakubali.

Siasa za Kurejeshwa Ardhi kwa Waarabu

Kuna wakati CCM ikitumia hoja ya kurejeshwa ardhi kwa Waarabu kama CUF itaingia madarakani. Hoja hii sasa haizungumzwi kwa sababu takribani ardhi yote imeshachukuliwa na familia ya viongozi wa CCM na inasemekana hasa Mhe. Karume na familia yake.

Siasa za Kihafidhina na Mgogoro wa Muungano

Ni vizuri kueleza pia kwamba hoja pekee inayosimama hivi sasa katika siasa za CCM Zanzibar na katika Serikali ya Muungano ni ubaguzi. Nusu ya Wazanzibari hubaguliwa kwamba wao asili yao ni Waarabu, au hubaguliwa kwa kuambiwa kwamba wao ni vibaraka wa chama cha Hizbu – Zanzibar Nationalist Party (ZNP).

Pale wanapotaka kututukana au kupinga kile wasichokitaka, viongozi wa CCM wanapenda sana kuitumia hoja hii hata kufikia kiwango hawajali kwamba huwa wanajitukana wenyewe. Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2005, Mhe. Salim Ahmed Salim, mwana-CCM wa kutegemewa, alibaguliwa kwa asili ya Uarabu mbele ya watoto na wake wa waheshimiwa hao ambao hata wenyewe ni Waarabu wakiwepo hapo kwenye mkutano.

Hoja hii ya ubaguzi huunganishwa na kunasibishwa na chama cha zamani cha ZNP ambacho ndicho kilichopinduliwa. Viongozi wa wahafidhina wanashindwa kujitambua kwamba wengi kati ya wale watetezi wakubwa wa sera hii ya kihafidhina, kama akina Muhamed Seif Khatib, inasemekana kwamba mwenyewe alikua kijana wa Umoja wa Vijana wa ZNP aliekua ni mpiga tarumbeta ya bendi ya vijana hao.

Matatizo y Kiuchumi ya Zanzibar

CCM inashindwa kueleza kwamba hali ya maisha ya wananchi hivi sasa ni mbaya sana. Ukosefu wa kazi haupungui asilimia 80, hali ambayo imefanya vijana wa Kizanzibari kushiriki katika vitendo vya kula madawa ya kulevya na wasichana kushiriki vitendo vya kuuza heshima zao, yaani umalaya mkubwa sana.

Sekta pekee inayotoa ajira Zanzibar ni uaskari. Aidha uwe askari wa JKU, askari wa KMKM, askari wa Fire Brigade (walokosa hata gari la kuzimia moto), askari wa Valantia, askari wa Usalama wa Taifa au Janjaweed. Hakuna sekata yoyote ya uzalishaji inayotoa ajira, labda udereva wa kutembeza watalii. Kwa hivyo, karibuni tutafikia hali ya one man one soldier– yaani mtu mmoja askari mmoja.

Hali ya ugumu wa maisha inaashiria kwamba uchaguzi wa 2010 utakua na maafa makubwa sana kama muwafaka huu haukutoa suluhisho lenye kuleta maelewano mapema. Vijana, bila kujali itikadi za vyama, wenye ukosefu mkubwa wa maisha ya maana watashindwa kusubiri mabadiliko yenye matumaini ya hali ya uchumi wa Zanzibar kubadilika.

Kila siku zinavyopita, hali inazidi kuwa ngumu na uonevu na ubaguzi uliokithiri unaendelea na kushamiri. Sasa pale mjini Zanzibar, mwenye kuomba naye anaombwa. Hakuna mwenye nacho isipokua wakubwa wa serikali na viongozi wachache wa CCM. Hata wafanyabiashara wamekimbizwa na serikali, eti kwa kisingizio kwamba wanakisaidia chama cha CUF.

Kwa hivyo kukwama kwa Muwafaka ni kuendelea kuwanyima Wazanzibari fursa ya kujipa nafasi ya kufanya kazi za maendeleo yao, kwani wengi wao wanaamini kwamba sababu kubwa ya hali mbaya ya uchumi ni kukosekana utulivu wa kisiasa, na kwamba hali hiyo inachochewa na Serikali ya Muungano.

Wazanzibari wanaamini kwamba hali hii ya kubaki na hali ngumu inafurahiwa na Serikali ya Muungano maana lengo ni kwamba Wazanzibari wafike mahali waseme hakuna haja ya kubaki na serikali isiyo manufaa nao.

Viongozi wa CUF watafika mahala hawatasikilizwa tena na vijana waliokosa haki na kuteswa kwa kudai haki yao ya kushiriki katika kuchagua viongozi wa nchi yao. Kuna kila kiashirio kwamba maafa yanaweza wakati wowote kutokea, maana njaa haina bwana wala haijui kiongozi na wala haina itikadi

Yote haya Mhe. Kikwete anayaelewa vyema. Kilicho cha   ajabu ni kwamba ameshindwa kusimama kama kiongozi wa nchi na amebaki kushabikia itikadi za kichama, za kibaguzi zinazowadhalilisha hata wao. Hii ni hatari kwa taifa.

Wazanzibari wanauona Muungano ni kikwazo kikubwa cha kupatikana suluhu ya kudumu na hivyo kuwasababishia hali ngumu ya maisha, ugomvi usiokwisha katika jamii na kukosa nafasi ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Kukosekana Uongozi Wenye Hekima

Kwa hivyo, katika kuhusisha kufeli kwa Muafaka na suala la kuwepo au kutokuwepo Muungano, tunaona sasa kwamba Watanzania wanahitaji kuzinduka kwamba taifa lao hivi sasa limekosa uongozi wenye hekima, wenye uwezo wa kusimamia masuala mazito ya kitaifa. Tafadhali tafautisheni JK ya Julius Kambarage na JK ya Jakaya Kikwete. Hizi ni tafauti ya mbingu na ardhi. Ni hatari sana. Tangu kuingia madarakani Mhe. Kikwete, inasemekana maamuzi yake mengi yamekua ya kusukumwa. Haonekani kabisa kwamba ana uwezo kama ule Watanzania walioaminishwa hapo 2005 wakati wa kampeni za uchaguzi, ingawa CUF tuliwatahadharisha Watanzania siku ya ufunguzi wa kampeni zetu kule Tabora 2005.

Mgogoro wa Zanzibar unaweza kusababisha kuvunjika kwa amani Tanzania nzima na ndiyo maana CUF inasisitiza Wazanzibari kufanya kazi pamoja hivi sasa ili kuandaa uchaguzi huru na wa haki wa 2010. Kama Mhe. Kikwete ataendelea kuona kwamba chama chake ni bora kuliko usalama wa taifa, basi wakati ndiyo utatoa jibu.

Mgogoro wa Afrika ya Kusini ulikwisha si kwa sababu ya ushupavu pekee wa Mzee Nelson Mandela, bali pia ujasiri wa mzee De’ Clerk kukubali  ukweli kwamba lile lenye faida kwa Wazungu ndilo lenye faida kwa Waafrika. Alimaliza uhasama wa Wazungu na Waafrika kwa kuzingatia faida ya taifa lao. Baada ya kumaliza mazungumzo Mzee De’ Clerk hakurudi nyuma, bali alisimama kwenye utekelezaji bila kusukumwa kwa sababu alikua na nia njema.

Makubaliano yaliyozika uhasama wa zaidi ya miaka 100 wa Afrika ya Kusini hayakupigiwa kura ya maoni. Msumbiji walikua na mgogoro wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka 18, makubaliano yao hayakupigiwa kura ya maoni. Kule Uingereza kumekua na mgogoro wa Nothern Ireland. Umemalizwa kwa kuundwa serikali ya pamoja bila kura ya maoni. Jirani zetu hapo Kenya, ambapo Mhe. Kikwete anajisifu kuhusika katika usuluhishi wake, yamemalizika kwa kuunda serikali ya pamoja bila kupigwa kura ya maoni.

Lengo kubwa katika nchi zote lilikua kuweka mbele mustakabali wa taifa. Kuna lipi la jabu lisilowezekana kwa mgogoro wa Zanzibar? Ni ukosefu wa utashi wa kisiasa kwa upande wa CCM na Mhe. Kikwete.

Inaelekea Mhe. Kikwete alitoa kauli ya kuumaliza mgogoro wa Zanzibar pale Bungeni, Disemba 30, 2005 si kwa nia njema, isipokua alikusudia kuiweka CUF katika matumaini (political engagement) huku akivuta muda hadi ifike 2010, kama maelezo ya kutaka kura ya maoni katika waraka wa NEC ya CCM unavyoeleza. Waraka huo umeeleza kwamba pendekezo la kura ya maoni ni kwa lengo la kuipiku CUF ili waache kushabikia kudai mambo madogo madogo. Madai haya madogo ni ile haja ya kutaka kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa hivi sasa kabla 2010.

Kama ni kiongozi kweli, basi Mhe. Kikwete alitakiwa asimame juu zaidi ya ushindani wa siasa za vyama na kuelekeza msimamo wake kwa hekima na kumaliza tatizo. Hilo limemshinda kwa sababu hakuwa na nia njema.

Kuwepo au kutokuwepo Muungano kunategemea jinsi viongozi waliopo madarakani wanavyotoa umuhimu wa kulinda umoja wa Wazanzibari na hivyo wa Watanzania. Huwezi kuwa na Zanzibar ilipasuka, kisha ukatarajia kuwa na Muungano ulioimarika. Huko, kwa hakika, ni kujidanganya hata kama kunaweza kuonekana katika mahisabu ya juu juu ya kisiasa kwamba ni kufanikiwa kwa CCM na Serikali ya Muungano. Kukataa Serikali ya Umoja wa Kitaifa hivi sasa ni kuongeza mgogoro Zanzibar na hivyo kupalilia vurugu hapo 2010. Vurugu hizo zikianza Zanzibar, hazitaacha kuingia na Tanzania Bara. Huu ndiyo mtihani wa Mhe. Kikwete na wahafidhina wake.

Kukosekana Viongozi wenye Hekima Barani Afrika

Lakini haishangazi sana, kwani hivyo ndivyo historia ya viongozi wa Kiafrika ilivyo. Kwa kawaida huwa hawajifunzi maharibiko yaliyotokea kwa wengine. Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, kwa mfano, anaongeza silaha kuua raia zake, wakati anajua ameshindwa hata kuwapatia mkate watu wake ambao anajigamba kwamba anawatetea. Vipi rais atatetea maiti ilhali alitakiwa kutetea walio hai?

Wazimbabwe sasa wanakufa njaa kwa ukosefu wa chakula. Yeye, baada ya kuuona ukweli wa kushindwa kwake, anagombana na mataifa makubwa. Sijui ili aweje. Hivyo kiburi chake kinaweza kushinda kile cha Sadam Hussein?

Kwa hivyo, mfano wa akina Mugabe unatwambia sisi Wafrika kuwa tuna tatizo. Watanzania tuna tatizo. Hatuna viongozi na hatupewi nafasi ya kuwachagua viongozi tunaowataka.

Nalo hili pia halishangazi sana, maana tunajua jinsi tulivyowapata viongozi wa aina ya Kikwete na akina Andrew Chenge. Hawa tumewaandaa sisi, hatuna sababu ya kumlaumu Mwaarabu hapa. Hawa tumewachagua sisi, hawa wametayarishwa na CCM. Hawa ndio vijana wa Mwalimu Nyerere waliouweka mwenge juu ya mlima wa Kilimanjaro ili umwilike pale penye dhuluma, uonevu na ukandamizaji. Tumewachagua wenyewe hawa baada ya kutupa kapero na fulana isiyo hata suruali ya kuficha sehemu zetu za siri.

Haishangazi, maana hawa ndio tuliowachagua kwa nyimbo za kwaya zilizoimbwa na Kapteni John Komba.

Haishangazi, maana hawa ndio tuliowachagua kwa harufu ya sahani ya pilau na jagi moja ya pombe ya kienyeji.

Haishangazi, maana hawa ndio tuliowachagua kutokana na sura zao nzuri na uso wenye bashasha bandia.

Watanzania tuna tatizo la ukosefu wa uongozi lakini pia tuna tatizo la kuelewa. Kiburi hiki walichonacho kina Kikwete na CCM tumewapa sisi. Walituahidi Tanzania yenye neema, wanatulipa Tanzania yenye njaa na ufisadi. Wanatunga sheria za uchaguzi halafu wao wenyewe ndio wanazivunja. Salama itatoka wapi? Muungano utanusurika vipi?

Khitimisho: Hatuna Viongozi wenye Hekima

Kwa kumalizia ni vyema nieleze kwamba Muungano umeendelea kuwa na matatizo kwa miaka 44 sasa na inaonekana bado hatujapata kiongozi wa Muungano aliye tayari kukabili ukweli wa matatizo yaliyopo na kufuata taratibu za kikatiba na kisheria kuelekea kwenye amani na demokrasia ya kweli.

Migogoro mingi ya siasa za Tanzania imetokana na aidha kuwadhbiti Wazanzibari mmoja mmoja au kuwadhibiti viongozi wao. Kila mara tafsiri hutolewa kwamba viongozi hao wanahatarisha Muungano. Ni ajabu kwamba maisha yote wenye kuhatarisha Muungano ni wale wanaodai haki zao za demokrasia. Na ndiyo maana muda wote CUF imesimama juu ya kupitiwa upya Muungano huu na kuundwa kwa Serikali Tatu: ya Zanzibar, ya Tanganyika na ya Muungano.

Hali ya kisasa iliyowakumba Mzee Aboud Jumbe, Mzee Idrissa Abduwakil na hata akina Maalim Seif Sharif na wenzake ni hali ya ukandamizi kwa kujaribu kukwepa ukweli wa mgogoro wa Muungano.

Tuna hitaji viongozi wapya na chama mbadala kutetea na kushughulikia hali hii. Viongozi waliopo sasa inaonekana hawana uwezo huo na huenda wakawa wao ndiyo chanzo cha tatizo na kuutia matatizo Muungano wetu. Hatuna sababu ya kuakhirisha tena suala hili. Demokrasia ya kweli Zanzibar itazaa demokrasia ya kweli Tanzania Bara na hivyo kuimarisha Muungano wa kweli wa Tanzania. Na ni hapo tu, ndipo ufisadi na wizi wa mali za Watanzania utakapomalizika, maana viongozi watatakiwa kujibu uharamia wao mbele ya wananchi.

HAKI SAWA KWA WOTE

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s