CUF Bunge

“BILA NISHATI MBADALA, UHIFADHI WA MAZINGIRA NI NDOTO” 

“Asilimia kubwa sana ya wananchi wa nchi hii wanatumia nishati ya kuni na mkaa kwa kupikia. Ni dhahiri kabisa ukataji wa miti ili kukidhi haja hiyo ni mkubwa kila mwaka. Inabidi iwe hivyo kwa sababu Serikali haijakuwa na mkakati wa kuwa na nishati mbadala ya kupikia itakayotumiwa na wananchi wengi. Kusamehewa ushuru Moto Poa sio suluhu kuunusuru uharibifu wa mazingira kwa ukataji miti kwani wenye uwezo wa kutumia nishati hiyo ya kupikia ni wachache mno. Serikali bila ya kuwa makini kwa suala hilo la nishati mbadala ya kupikia badala ya mkaa au kuni, uhifadhi wa mazingira kwa kutokata miti utakuwa ni ndoto.”

 Endelea kusoma hotuba ya Msemaji wa Upinzani Bungeni kuhusu Mazingira…

“SERIKALI YA MUUNGANO HAISIKILIZI”

Tunapenda kurejea kauli yetu ya mwaka jana, kwamba pale mwaka 1992 Bunge hili tukufu lilipofanya maamuzi ya kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika, lilikuwa limepitisha uamuzi wa busara kama uliopitishwa na chama cha TANU mwaka 1958 kule Tabora kuingia kwenye mfumo wa kura tatu. Bali zaidi ya hapo, Bunge hili tukufu lilikuwa limefanya kitendo cha kisheria na cha kimantiki. Uamuzi ule ulikuwa sahihi wakati ule, ni sahihi leo hii na utakuwa sahihi kesho, maana sio tu kwamba uliakisi matakwa halisi ya Mkataba wa Muungano uliokuwa umetiwa saini zaidi ya nusu karne nyuma yake, bali pia ulikuwa ni kielelezo cha kujitathmini kulikofanywa na waheshimiwa wawakilishi wa Watanzania kupitia chombo chao hiki. Ni bahati mbaya sana kwamba, maamuzi yale ya Bunge yalikuja kuwekwa kando na kuufanya muda, fedha, na busara iliyotumika kuonekana kama si lolote si chochote!

 Endelea kusoma hotuba hii ya Msemaji wa Upinzani Bungeni kuhusu Muungano, Mhe. Riziki Omar Juma

UPINZANI BUNGENI WAJA NA BAJETI MBADALA

“Waziri wa Fedha na Uchumi alipowasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa katika kipindi cha mwaka 2008 alieleza kuwa pato la taifa linakadiriwa kukua kwa asilimia 7.4. Kwa kipindi cha miaka minane 2001-08, pato la taifa limekua kwa wastani wa asilimia 7.1 kwa mwaka. Ikiwa ongezeko la watu ni asilimia 2.9, wastani wa pato la kila mwananchi limeongezeka kwa wastani wa asilimia 4.2 kwa mwaka. Kutopungua kwa umaskini kwa kasi kunaashiria kwamba uchumi wa Tanzania haukui kwa wastani wa asilimia 7.1 kwa mwaka kama takwimu za serikali zinavyoeleza.” Bonyeza hapa kusoma bajeti mbadala ya 2009/2010 kama ilivyowasilishwa Bungeni na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Mhe. Hamad Rashid Mohammed.

KWA NINI SERIKALI IMEMILIKISHA ARDHI KWA MGENI?

Tembo, miongoni mwa wanyama wanaovutia watalii kutembelea mbuga za Tanzania

“…Kambi ya Upinzani inataka majibu kutoka kwa Serikali ni taratibu gani zilifuatwa kumilikisha ardhi ya wananchi wa mkoa wa Mara kwa mwekezaji huyo raia wa Marekani, Johnes Tudor? Kuna usiri mkubwa wa shughuli zinazofanywa kwenye eneo hili na mtu yeyote haruhusiwi kuuliza. Tuna wasiwasi hata mapato yanayokusanywa na serikali kutoka eneo hili siyo sahihi. Mwekezaji huyu amekuwa anawanyanyasa sana wananchi wanaozunguka eneo hilo. Amekuwa anatumia askari wake kuwapa kipigo kikali mwananchi yeyote anayekutwa hata jirani na eneo lake. Kumekuwepo na malalamiko kuwa askari hawa wanawalazimisha wananchi kula nyama mbichi pale wanapokamatwa na mnyama. Hii ni haki kwa nchi inayoendeshwa kisheria?” Magdalena Sakaya (Mb), Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni kuhusu Maliasili na Utalii

‘PUNGUZA MAKONGAMANO, HUDUMIA WAATHIRIKA WA UKIMWI’

Dkt. Ali Taarab, Mbunge wa Konde (CUF)

Dkt. Ali Taarab, Mbunge wa Konde (CUF)

“….ni jambo la kusikitisha sana kusikia ya kuwa 19% ya maambukizi ya VVU hapa nchini ni kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT+). Kiasi hicho cha watoto wachanga wasio na hatia, wanakuja duniani wakiwa tayari wameshaambukizwa VVU. Maambukizi haya yanatokea ikiwa virusi vitaingia katika mfumo wa damu wa mtoto kutoka katika damu ya mama wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua au wakati wa kunyonyesha.” – Dkt. Ali Taarab (Mb), Msemaji Mkuu wa Upinzani bungeni kuhusu Afya na Ustawi wa Jamii

UKUWAJI WA UCHUMI HAUJAMGUSA MWANANCHI WA KAWAIDA

Licha ya takwimu 'tamu' za serikali ya Rais Kikwete juu ya kukua kwa uchumi, ukweli ni kwamba ukuwaji huo hauonekani kuakisika katika maisha halisi ya Watanzania

Licha ya takwimu 'tamu' za serikali ya Rais Kikwete kwamba uchumi unakua, ukweli ni kwamba ukuwaji huo hauakisiki kwenye maisha halisi ya Watanzania

“…..Mtanzania wa kawaida haamini kuwa uchumi unakua kwa sababu haoni matunda ya kukua huko. Waheshimiwa Wabunge, ambao ndio wawakilishi wa wananchi na wako karibu nao, wanapata shida kupata picha halisi ya ukuaji huu kwa sababu maisha ya Mtanzania wa kawaida yameendelea kuwa duni siku hadi siku…..Ripoti ya Umaskini na Maendeleo ya Watu ya 2007 imebaini kuwa Watanzania wengi wanaona kuwa maisha yao yanazidi kuporomoka….Wananchi wengi hawaamini kuwa uchumi unakua na maisha ya mwananchi wa kawaida yanaboreka. Wananchi wengi wanaamini kuwa misaada ya nje inawanufaisha wakubwa wa Serikali huku wafanyakazi na wakulima wakiwa wanaambulia patupu…” - Hamad Rashid Mohammed (Mb), Kiongozi na Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni

ZIWAPI ZILE AJIRA MILIONI MOJA ZA KIKWETE?

Salim Abdallah Khalfan, Mbunge wa Tumbe (CUF)

Salim Abdallah Khalfan, Mbunge wa Tumbe (CUF)

“Serikali ya awamu ya nne iliahidi itaanzisha ajira mpya milioni moja katika kipindi cha miaka mitano wastani wa ajira laki mbili kila mwaka. Waziri ameeleza kwamba katika kipindi cha miezi 18 kuanzia mwezi Julai 2005 hadi Desemba 2007, ajira mpya 412,608 zilikuwa zimepatikana. Ajira 194,325 zimetokana na sekta rasmi na ajira 218,283 zimetokana na sekta isiyo rasmi. Hata hivyo Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2007 hakina jedwali linaloonyesha ajira hizo na sekta zake. Kitabu hicho kinaonyesha ajira viwandani imeongezeka toka watu 89,316 mwaka 2005 na kufikia watu 91,112, ongezeko la wafanyakazi 1,796 tu. Kwa kadri muundo wa uchumi unavyobadilika ndivyo sekta ya viwanda inavyotegemewa kutoa mchango mkubwa kwa ajira mpya. Aidha, Kambi ya Upinzani inamtaka Mhe. Waziri alieleze Bunge lako tukufu, hizo ajira zaidi ya laki nne ziko sekta gani? Au ajira hizo ni ajira hewa?”- Salim Abdallah Khalfan (Mb), Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Ajira, Kazi na Maendeleo ya Vijana

KWA NINI POLISI ILIWAVAMIA WAPEMBA USIKU WA MANANE?

Muhammad Ibrahim Sanya, Mbunge wa Mji Mkongwe (CUF)

“…Sote tunaelewa kuwa taratibu mahali pengi duniani ambapo heshima na haki za binadamu zinathamniwa, askari wanakuwa na mipaka katika kutekeleza majukumu yao. Mfano, askari hatakiwi kumpekuwa raia zaidi ya saa kumi na mbili jioni.  Kwa msingi huo, napenda Mhe. Waziri alieleze Bunge hili, ni mamlaka yapi yaliyotumika kuwavamia wakazi saba wa Pemba zaidi ya saa saba za usiku waliojiita askari walifanya fujo, wakatishia hata kuvunja milango ya nyumba za hao waliowaita watuhumiwa? Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inauliza je huu si uvunjifu wa haki za raia na kwenda kinyume na matakwa ya Umoja wa Mataifa wa kuheshimu haki za binadamu….?” – Muhammad Ibrahim Sanya (Mb), Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu Mambo ya Ndani

ILE REAL MADRID INAKUJA LINI HASA?

Kikosi cha Real Madrid ya Hispania

Kikosi cha Real Madrid ya Hispania

“…miongoni mwa mafanikio ambayo yalisemwa kuwa ni kutokana na ziara za Mheshimiwa Rais nje ya nchi, ni pamoja na ujio wa timu ya mpira wa miguu ya Real Madrid ya Hispania. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa tamko la kuthibitisha kuwa timu ya Real Madrid ingelifika Tanzania rasmi kwa michezo ya kirafiki Julai mwaka 2007 ikiwa na msafara wa watu wapatao 80. Hili ni tamko rasmi la Serikali ndani ya Bunge. Kambi ya Upinzani inauliza ujio wa timu hii ni lini? Je, Rais alipotoshwa? Kuna jambo gani hapo? Kama imeshindikana, ni kwanini Serikali inakosa ujasiri wa kulieleza Taifa kilichojiri kama ilivyotamka rasmi na kwa mbwembwe wakati wa kutangaza uwepo wa utaratibu huo?” Mwanawetu Said Zarafi (Mb), Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Habari, Utamaduni na Michezo

HAPA PANA MGOGORO WA KIKATIBA

Fatma Mussa Maghimbi, Mbunge wa Chake (CUF)

Fatma Mussa Maghimbi, Mbunge wa Chake (CUF)

“Kwa bahati nzuri siku ya Alkhamis ya tarehe 3 Julai, 2008, Waziri Mkuu alitamka ndani ya Bunge hili kwamba Zanzibar sio nchi. Tarehe 9 Julai, 2008, Mhe. Iddi Pandu Hassan, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alisema katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kwamba Zanzibar ni nchi. Je, huu sio mgogoro wa kutosha wa kuonyesha haja ya kuwepo Mahakama ya Katiba? Na hili sio jambo la kusema litatatuliwa na tafsiri ambayo itatolewa kwa mashirikiano ya wanasheria wakuu wawili, yaani yule wa Zanzibar na wa Jamhuri ya Muungano, kwa sababu ni mgogoro wa kikatiba ambapo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza litatuliwe na Mahakama ya Katiba ya Tanzania. Vile vile jambo hili sio swali la kujadiliwa na CCM kama alivyotamka Mheshimiwa Waziri Mkuu katika Bunge lako tukufu, ikizingatiwa kuwa Tanzania siyo mali ya CCM wala ya wana CCM pekee.” – Fatma Maghimbi (Mb), Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni kuhusu Sheria na Katiba

SERIKALI IMTAJE MMILIKI HALISI WA MEREMETA

Mohammed Habib Mnyaa, Mbunge wa Mkanyageni (CUF)

Mohammed Habib Mnyaa, Mbunge wa Mkanyageni (CUF)

“Kauli ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuwa MEREMETA ni ya jeshi na haiwezi kutolewa maelezo Bungeni kwani ni kutoa siri za Jeshi, hivyo kuhatarisha usalama wa nchi, ni majibu ya kushangaza. Wanahisa wa MEREMETA ni wageni na hivyo siri za jeshi ni salama kwa wageni kuliko wabunge au Bunge lako? Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe majibu sahihi na sio kutoa majibu ya kisiasa tu. Kambi ya Upinzani imekwisha kusema iwapo kuna jambo kweli la siri basi liwasilishwe kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge au Kamati ya Uongozi. Lakini kauli kuwa Serikali haiwezi kusema lolote haiwezi kamwe kukubalika na Bunge hili. Bunge linapaswa kusimamia hata jeshi kwa mambo yasiyohusu mikakati ya kijeshi. Dhahabu ni biashara na hakuna siri ya kibiashara kwa Bunge. Ni imani yetu kuwa serikali itatuelewa na, hivyo, kutoa majibu ya kuridhisha.” – Mohammed Habib Mnyaa (Mb), Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Nishati na Madini

UDUMAVU WA KILIMO NI HATARI KWA USALAMA WA NCHI

Hemed Khamis Salim, Mbunge wa Chambani (CUF)

Hemed Khamis Salim, Mbunge wa Chambani (CUF)

“Katika nchi kama yetu ambayo Watanzania walio wengi bado wanategemea sekta ya kilimo katika kujiendeleza kimaisha, udumavu huu wa ukuwaji na uchangiaji wake katika pato la taifa ni hatari kwa usalama wa nchi. Tukumbuke kuwa, katika dunia yetu hii ya sasa, suala la kilimo na chakula si suala la ustawi wa wananchi kijamii na kiuchumi tu, bali pia ni suala la kiusalama.” – Hemed Khamis Salim (Mb), Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni kuhusu Kilimo, Chakula na Ushirika

SASA NI WAKATI WA KUWA NA JESHI LA KISASA

“Kambi ya Upinzani, inalitaka jeshi letu lifikirie kwa   kina namna ya kuongeza kasi ya kuleta mapinduzi ya maendeleo katika nchi yetu kama wanavyofanya wenzetu kwa ajili ya kunyanyua uchumi wa nchi zao jambo litakalosaidia kupatikana kwa fedha za kutosha kwa bajeti ya jeshi letu…Kambi ya Upinzani ilikwishashauri jinsi ya kupata vijana wenye vipaji maalum ambao tunaamini kama vipaji hivyo vikitumiwa vizuri jeshi letu litakuwa ndiyo hazina kubwa ya chimbuko la teknolojia mpya na rahisi kwa maendeleo ya watanzania. Jeshi waanze kuwatafuta vijana wenye vipaji tangu wakiwa mashuleni…” - Masoud Abdalla Salim (Mb) Msemaji Mkuu Kambi ya Upinzani kuhusu Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MUUNGANO: TUME BASI, SASA KURA YA MAONI!

Riziki Omar Juma, Mbunge - CUF

Riziki Omar Juma, Mbunge - CUF

“Kwa mujibu wa taarifa tulizonazo, SMZ pekee na baadhi ya wakati kushirikiana na SMT imewahi kuunda takriban kamati 12 kutoa maoni juu ya kutatua kero za muungano, jee mapendekezo haya yalishughulikiwa kwa kiasi gani? Kana kwamba haitoshi, SMZ na SMT kwa pamoja, zimeunda takriban kamati 8 na kufanya vikao vya pamoja takriban 80 kuzungumzia kero za Muungano, lakini hadi leo hakuna mafanikio yoyote katika kero za msingi. Je, Wizara ya Muungano inaweza kulieleza Bunge hili na Watanzania kwa ujumla tatizo la kutofanikiwa hasa ni nini?…Kambi ya Upinzani inaona kwamba njia ya kutumia vikao baina ya serikali ya SMZ na SMT vinavyoongozwa na Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi wa Zanzibar kama sehemu au mkakati wa kutatua kero au matatizo ya Muungano si muafaka na hazina ufanisi. Hivyo basi, Kambi ya Upinzani inashauri kuwa kura ya maoni na mjadala wa wazi wa kitaifa juu ya muundo na mfumo wa muungano utakaozingatia na kuhakikisha maslahi ya pande zote mbili za Muungano na unaohitajika uitishwe nchi nzima.” Riziki Omar Juma (Mb), Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Muungano

IWEJE MILIONI 551 KWA PICHA ZA BALLALI TU?

Hamad Rashid Mohammed, Mbunge wa Wawi (CUF)

“Taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Benki Kuu uliofanywa mwaka 2006/07 umebainisha matumizi ya shilingi milioni 551 kwa ajili ya kununua picha zenye sura ya marehemu Daudi Ballali kwa ajili ya kutundikwa katika jengo jipya la ghorofa pacha (BoT twin tower) na majengo mengine yenye ofisi za Benki Kuu. Uchunguzi unaonesha kwamba picha hizi zote zilikuwa na ukubwa sawa na hazikuwa na tofauti yoyote na zile picha zilizonunuliwa kwa kiasi cha shilingi milioni 4.76 kwa kila moja na vile vile ripoti inaeleza kwamba ni picha 43 tu zilizo katika hifadhi ya Benki Kuu ndizo zilizolipiwa na Benki Kuu kwa kampuni iliotengeneza picha hizo ambayo ni Zahr Ramj of Mediapix International.” – Hamad Rashid Mohammed (Mb) Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Fedha na Uchumi

AIBU YA TANZANIA KUTATUA MIGOGORO YA WENGINE IKASHINDWA NA WA ZANZIBAR

Khalifa Suleiman Khalifa, Mbunge wa Gando (CUF)

Khalifa Suleiman Khalifa, Mbunge wa Gando (CUF)

“Kilichotokea nchini Kenya na kupelekea ghasia na mauaji ya zaidi ya watu alfu moja na wengine wengi kukosa makazi, kinashabihiana kabisa na yaliyotokea katika chaguzi mbalimbali zilizowahi kutokea hapa nchini mwetu hasa katika chaguzi za Zanzibar za mwaka 2000 na mwaka 2005. Ni vyema kutambua kuwa, kuendelea kuchezea juhudi za kusuluhisha mgogoro wa Zanzibar kwa kisingizio chochote; na kushindwa kuanzisha mchakato wa katiba mpya utakaoshirikisha Watanzania wote kutengeneza mfumo halali wa kisasa na kiuchumi utakaotoa nafasi sawa kwa makundi yote kisiasa, kijamii na kiuchumi ni sawa na kuchochea mazingira ya machafuko makubwa zaidi hapa nchini mwetu. Hivi hatuoni haya manung’uniko mbalimbali yaliopo?” – Khalifa Suleiman Khalifa (Mb), Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa