Zanzibar Daima, yasema risala ya wanawake wa CUF

15 11 2009

RISALA YA JUMUIYA YA WANAWAKE WA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – CHAMA CHA WANANCHI) KWA MAKAMO MWENYEKITI WA CHAMA, MHE. MACHANO KHAMIS ALI, KWENYE MAANDAMANO YA KUUNGA MKONO HATUA ZA KATIBU MKUU WA CUF NA RAIS WA ZANZIBAR KUWALETA WAZANZIBARI PAMOJA

15 Novemba 2009,
Viwanja vya Demokrasia,
Zanzibar

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Makamo Mwenyekiti wa The Civic United Front (CUF – Chama cha Wananchi), Mhe. Machano Khamis Ali,

Mheshimiwa Katibu Mkuu wa The Civic United Front (CUF – Chama cha Wananchi), Maalim Seif Sharif Hamad,

Waheshimiwa wajumbe wa Baraza Kuu la Taifa la CUF, Wakurugenzi na Manaibu Wakurugenzi, wanachama na wanawake wenzangu na, juu ya yote, waheshimiwa Wazanzibari, Asalaam Alaykum!

Awali ya yote naomba niitambulishe salamu mpya ambayo sisi wa Jumuiya ya Wanawake wa CUF tumeamua iwe inatumika kusalimiana baina yetu kila tunapokutana, hasa katika muktadha wa shughuli kama hizi na wakati tulionao. Kuanzia sasa, tungelipenda Wazanzibari wenzetu wote, baada ya kuamkiana maakizi yetu ya kawaida ya Asalaam Alaykum – Alaykum Salaam, basi waongeze na Zanzibar na mwengine aitikie Daima! Kwa hivyo, iwe Zanzibar Daima!

Kwa heshima, naomba tusalimiane hivi sasa:

Zanzibaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaar! Daimaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa!

Zanzibaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaar! Daimaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa!

Zanzibaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaar! Daimaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa!

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, waheshimiwa Wazanzibari wenzangu, waheshimiwa waalikwa,

Jumuiya ya Wanawake wa CUF inaichukulia hii kuwa ni siku ya aina yake kwa Zanzibar. Ni siku ambayo wanawake wa Zanzibar wameamua kufanya maandamano ya kuwaunga mkono viongozi wakuu wa Chama chetu kwa maamuzi makubwa na mazito waliyoyachukua, ambayo maslahi yake kwa nchi yetu hayana mithali.

Ni jambo la fakhari kwamba, sisi wanawake ndio ambao tumekuwa jumuiya ya mwanzo kuuona umuhimu wa maamuzi hayo yaliyofanywa na uongozi wetu na, hivyo, tukaamua kuingia barabarani kuthibitisha uungaji mkono na utayarifu wetu wa kufanya kila lililo ndani ya uwezo wetu, kusudi dhamira ya pamoja tunayoisimamia iweze kutimia.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, waheshimiwa Wazanzibari wenzangu, waheshimiwa waalikwa,

Kuna ambao wanajiuliza kwa nini wanawake hawa hawa ambao wiki iliyopita kwenye viwanja hivi hivi walilia kwa uchungu na hasira pale Katibu Mkuu wao alipowafahamisha msimamo mpya wa Chama chao wa kumtambua Rais Amani Karume, na leo ndio hawa hawa ambao wanaandamana kumuunga mkono! Ndiyo, tulilia kwa mengi. Kumbukumbu za mateso na madhila, za unyanyasaji na dhuluma, za kupoteza na kudhalilishwa ndani ya nchi yetu wenyewe. Tulilia pia kwa upya wa habari yenyewe na wingi wa maswali ambayo kwa muda ule mchache hayakuwa na majibu. Tulilia tukijiuliza, hivi sasa Habibi Kipenzi Chetu, Maalim Seif Sharif Hamad, anatupeleka wapi mama zake, dada na shangazi zake, binti na wakwe zake?

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, waheshimiwa Wazanzibari wenzangu, waheshimiwa waalikwa,

Leo hii tuna jawabu kwa kila swali tulilojiuliza na tunaona fakhari kwamba uongozi wa Chama chetu ulikuwa wa mwanzo kuja hadharani kunyoosha mkono wa ushirikiano, umoja na mshikamano kwa ajili ya nchi yetu ya Zanzibar, Tanzania, Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla. Tunaona fakhari kwamba sisi sasa ni sehemu ya kuibadilisha nchi hii, na kwa hilo hatuna la kujutia wala hatuna la kupoteza. Wanawake wa Zanzibar hatuna cha kupoteza zaidi ya minyororo ambayo nchi yetu ilikuwa imefungwa kwa zaidi ya miaka 50 sasa!

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, waheshimiwa Wazanzibari wenzangu, waheshimiwa waalikwa,

Ni sisi wanawake ndio ambao tumekuwa tukibeba sehemu kubwa ya machungu yanayosababishwa na kufeli kwa mfumo wa siasa za Zanzibar kwa miaka yote hii 50. Hatukusudii kuwalaumu wanaume, ambao kwa miaka yote hiyo wamekuwa ndio vinara wa siasa zetu, lakini tunakusudia kusema kwamba sifa zetu za kuwa mama, dada, wazazi na walezi, ndizo zinazotufanya tuumie zaidi pale maafa yanayosababishwa na kufeli kwa siasa zetu yanapotokea.

Hapana shaka, huu si wakati wa kukumbushana wapi na vipi yalitupata yaliyotupata, lakini itoshe kunukulu msemo wa wenzetu Wanyarwanda, ambao baada ya kuangamizana kwenye mauaji ya kutisha ya miaka ya ’90, sasa wenyewe wameinuka na kusema ”NO MORE!” Basi tena! Nasi kwa pamoja, tunasema NO MORE. Basi tena!

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, waheshimiwa Wazanzibari wenzangu, waheshimiwa waalikwa,

Tunasema basi, basi tena! Basi tena kugawanywa na tugawanyika kwa misingi ya asili zetu. Basi tena kugombanishwa na tukagombana kwa misingi ya vyama vyetu. Basi tena kupiganishwa na tukapigana kutetea itikadi zetu. Basi tena kutishwa na tukaogopana kwa misingi ya visiwa vyetu. Basi tena kumpa nafasi mtu wa kando asimame baina yetu. Basi kwa kila jicho la adui na la hasidi dhidi ya nchi yetu. Basi tena kwa yote hayo, na mengine maovu zaidi ya hayo, dhidi ya nchi yetu.

Sasa, tunachokitaka sisi wanawake wa Zanzibar ni nchi yetu tu. Zanzibar hii ambayo kwa miaka 50 sasa imekuwa ikichinjwa na kukatwa vipande vipande, tuna jukumu leo hii la kuikusanyakusanya na kuileta pamoja. Na tafauti wanavyosema watu kwamba La Kuvunda Halina Ubani, Zanzibar yetu haijavunda. Bado inawezekana kuiunda tena, ikasimama kuchukua nafasi yake iliyokuwa imeshikilia kwa karne kadhaa huko nyuma, yaani kitovu cha elimu, ustaarabu na maendeleo. Na kama alivyokuwa akinadi kampeni zake Barack Obama, ambaye hata babu yake Bwana Onyango Hussein Obama, alipitia Zanzibar na kufaidika na ustaarabu wa watu wa nchi hii, YES WE CAN! Ndiyo, na sisi Wazanzibari tunaweza, na lazima tuweze.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, waheshimiwa Wazanzibari wenzangu, waheshimiwa waalikwa,

Wewe ni mtu mzima. Umeishi na kuona mengi na inshallah utaendelea kuishi na kuyashuhudia mengine tele yanayokuja. Waswahili husema Mtu Mzima Dawa, na kwamba penye Wazee hapaharibiki Jambo. Kwa hivyo, kwa kutumia utu uzima wako, nafasi yako kama kiongozi mkubwa wa Chama na nchi yetu ya Zanzibar, na juu ya yote Uzanzibari wako, tungekuomba tutumie nafasi hii tukiwa mbele yako kufikisha salamu hizi zifuatazo:

Kwa Mwenyekiti wa Chama chetu, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, tuna wingi wa shukrani na heshima ya hali ya juu. Ni unahodha wake imara kwa Chombo chetu ndio ambao umetuwezesha kuvuuka dhoruba na mawimbi ya kutisha katika safari yetu. Prof. Lipumba amekuwa akithibitisha uprofesa wake na kila mmoja wetu ni shahidi ya vile anavyolitimiza jukumu lake la kuwa kiongozi kwetu. Tunampongeza sana kwa kulisimamia hili hasa la kuwaona ndugu zake Wazanzibari wanakuwa kitu kimoja na kwa kujitolea kwake daima kwa ajili ya Chama na nchi yetu. Ushindi wa karibuni katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa huko Tanzania Bara usingelipatikana ikiwa si uimara wa uongozi wake.

Kwa Katibu Mkuu wa Chama chetu, Kipenzi chetu, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye Chama kilikupa jukumu zito la kuja hadharani kutangaza msimamo mpya kwa maslahi ya nchi yetu, tunakwambia kwamba sisi wanawake wa Zanzibar tuko pamoja nawe. Tuko pamoja na uongozi wa Chama chetu katika kuizamua Zanzibar kutoka miaka 50 ya siasa za mgawanyiko ambazo hazijawahi kuwa na faida kwa yeyote kati yetu. Tunakuomba utusamehe kwa hisia kali tulizozionesha wiki iliyopita katika viwanja hivi hivi. Tulikuwa hatujakuelewa. Sasa tumekuelewa na kutoka kwetu tegemea mashirikiano yasiyo masharti katika hili. Kwako ujumbe wetu ni mmoja tu, nao ni kwamba TULIKUPENDA, TUNAKUPENDA NA TUTAENDELEA KUKUPENDA MAANA NAWE DAIMA UMEKUWA UKITUPENDA!

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, waheshimiwa Wazanzibari wenzangu, waheshimiwa waalikwa,

Kupitia hadhara hii ya leo pia, tunamuomba Katibu Mkuu wetu, Maalim Seif, atufikishie salamu zatu kwa Rais wa Zanzibar, Mhe. Amani Karume. Uongozi wa Chama chetu umetutaka tumtambue kama rais halali wa Zanzibar. Mwanzoni tuliupinga uongozi wetu si kwa kuwa tu hatukufahamu, lakini pia kwa sababu ya kutokuiamini dhamira ya Mhe. Karume na wenzake panapohusika khatima ya Zanzibar. Tumefahamishwa na sasa tunaelekea kufahamu na kwa hivyo, sisi wanawake wa Zanzibar tunamtambua Mhe. Karume kwamba ndiye Rais wetu. Kwamba yeye ndiye mwenye jukumu la kuikoa nchi hii. Lakini tungeomba ujumbe wetu kwake uwe mfupi na wa moja kwa moja, nao ni kwamba SISI MAMA, DADA, BINTI NA WAKWE ZAKO WA ZANZIBAR TUNAKUPA IMANI YETU, TAFADHALI USIJE UKAIBWAGA CHINI!

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, waheshimiwa Wazanzibari wenzangu, waheshimiwa waalikwa,

Kwa viongozi wote wa Zanzibar kutoka pande zote mbili kuu, tupelekee ujumbe wetu kwao kwamba Waingereza husema IT TAKES TWO TANGO, na Waswahili husema kuwa KIDOLE KIMOJA HAKIVUNJI CHAWA. Ikiwa kuna sehemu yoyote duniani ambayo imethibitisha misemo hii ya Wahenga, basi ni Zanzibar. Licha ya viongozi hao kuongoza siasa za nchi hii kwa miaka yote hiyo 50, kwa kuwa kila mmoja alisimama kivyake, basi ndiyo maana Zanzibar imekwama. Kwao ujumbe wetu ni wa wazi, nao ni kwamba HESHIMA YAO KAMA VIONGOZI ITATAFSIRIWA TU KWA KUJITOLEA KWAO KWA AJILI YA ZANZIBAR. Nasi tutawaheshimu kwa kuiheshimu kwao Zanzibar, Wazanzibari na Uzanzibari!

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, waheshimiwa Wazanzibari wenzangu, waheshimiwa waalikwa,

Kwa wenzetu wa Tanzania Bara, katika wakati kama huu ambapo Wazanzibari wanatafuta njia za kuwaleta pamoja, wao ni ndugu ambao msaada wao unahitajika. Zanzibar iliyo pamoja na inayoshirikiana ina maslahi zaidi kuwa nayo kwenye Muungano kuliko Zanzibar iliyogawika. Zanzibar imara ni kwa Muungano imara na Zanzibar dhaifu ni kwa Muungano dhaifu. Kwa hivyo, ndugu zetu hawa wa damu wawe ni sehemu ya utatuzi wa matatizo yetu na wasiwe sehemu ya tatizo. Ujumbe wetu kwao ni mfupi tu, nao ni kwamba UDUGU NI KUFAANA, UDUGU SI KUFANANA!

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, waheshimiwa Wazanzibari wenzangu, waheshimiwa waalikwa,

Salamu zetu za mwisho, lakini za muhimu na za lazima ziende kwa Wazanzibari wote walio ndani na nje ya nchi. Tunakuomba Mgeni Rasmi pamoja na viongozi wenzako wote, popote mutakapokutana nao, muwape ujumbe wa wanawake wa Zanzibar kwamba milango ya nchi yao inafunguka. Ombi letu kwao ni kuwa tushirikiane ili kuhakikisha kuwa hivyo vinavyoingia ndani wakati milango hii ikifunguka, ndivyo vile vyenye kheri kwa nchi yetu. Kwa pamoja tuwe mawakala wa kuibadilisha Zanzibar na sio mawakala wa kuibakisha Zanzibar hapa ilipo au kuirudisha nyuma zaidi. TUSHIRIKIANE KUIJENGA ZANZIBAR MPYA.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, waheshimiwa Wazanzibari wenzangu, waheshimiwa waalikwa,

Sisi wanawake wa The Civic United Front (CUF – Chama cha Wananchi), kwa kusema haya tunatarajia kwamba tumemsemea kila mwenye kuitakia mema Zanzibar, Wazanzibari na Uzanzibari. Kwa hivyo, tunataka tukuhakikishie tena na tena kwamba TUNAIUNGA MKONO KAMATI YA ULINZI YA TAIFA AMBAYO KWA NIABA NA BARAKA ZA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA LA CHAMA CHETU LIMEFANYA MAAMUZI HAYA MAZITO YA KUUTAMBUA RASMI URAISI WA MHE. AMANI KARUME. Tunaahidi kwamba tuko tayari kuyafanyia kazi maamuzi haya kwa kadiri ambavyo inatustahikia.

Zanzibaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaar! Daimaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa!

Zanzibaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaar! Daimaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa!

Zanzibaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaar! Daimaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa!


Actions

Information

One response

15 11 2009
Mwiba

Nimefarijika na risala hii na INSHAALLAH yawe kama yalivyotarajiwa na kubwa zaidi pale wanawake hao walipotanabahi na kumtaka samahani Maalim Seif ingawa mjumbe hauwawi naona walitaka kumgeukia ,nawapongeza sana sana kwa hilo na matarajio yangu Maalim nae ataipokea na kuwasamehe INSHA’ALLAH nayo ataijibu kwenye mkutano wa hadhara.

Leave a comment