Dk. Karume: Hakuna masharti tuliyowekeana na Seif

14 11 2009

Na Mwanajuma Abdi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, amesema hakuna masharti waliyowekea na Katibu Mkuu wa Chama cha CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, walipokutaka hivi karibuni, Ikulu ya Zanzibar.

Amesema hakuna masharti isipokuwa sharti lao kubwa ni kusameheana na kusahau yalitopita kwa kurejesha udugu katika kudumisha utulivu na amani kwa ajili ya kuwaletea maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.

Rais Karume aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar mara baada ya kuwasili akitokea Dar es Salaam, kwa ajili ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Falsafa ya Udaktari wa Sayansi na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki, shehere zilizofanyika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Aidha alimpongeza Maalim Seif Sharif kwa ujasiri mkubwa wa kwenda kuwatangazia wanachama wake katika mkutano wa Jumamosi iliyopita uliofanyika Kibandamaiti ya kumtambua Rais Karume.

Alifahamisha kuwa Seif baada ya kukaa na Baraza kuu la CUF, na kuona kuona Wazanzibari wote ni wamoja na inafaa washirikiane kuleta maendeleo na kulinda utulivu na amani nchini.

“Wazanzibar wote ni ndugu wasikubali kutofautishwa na visiwa vya Unguja na Pemba, na visiwa vidogo vidogo vya Tumbatu, Kojani, Fundo na Uzi, kwa vile kila mmoja anazunguka katika familia hizo hizo na wengine kuoana”, alisisitiza.

Dk. Karume alieleza siku zote anaomba dua nchi hii iendelee kuwa ya amani na utulivu, ambapo hadi sasa hakuna mtu anayebughudhiwa.

Alifahamisha kuwa, anaomba dua uchaguzi wa mwakani ufanyike kwa utulivu na amani, ambapo mtu atakayeshindwa au kushinda wapeane mikono kwa kupongezana kwa ajili ya maendeleo ya mustakabali wa Zanzibar.

Hata hivyo, aliongeza kuwa yupo tayari kuteuwa nafasi mbili za wajumbe wa CUF kuingia katika chombo cha kutunga sheria cha Baraza la Wawakilishi iwapo atapelekewa majina.

Rais Karume akiwa na mke wake, Mama Shadya Karume, walipokewa na viongozi mbali mbali wa serikali, Chama Cha Mapinduzi na vyama mbali mbali vya upinzani katika uwanja wa ndege wa Zanzibar.

CHANZO: ZANZIBAR LEO


Actions

Information

One response

17 11 2009
Paku

Tunakubali kusameheana ndio ubinadamu,lakini mbona kauli za Mhe. Karume hazina uzito,hivi ni kweli kuteua wajumbe wa Baaza La wawakilishi iwe ishu kubwa ya Rais wetu.

Leave a comment