Maalim Seif, Karume wakutana Ikulu

6 11 2009

Thursday, 05 November 2009 17:06
Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Zanzibar Bw. Amani Abeid Karume jana alikutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Chama cha CUF, Maalim Seif Sharif Hamad Ikulu, mjini Zanzibar ambayo chama hicho cha upinzani kimesema ni ya ‘maelewano makubwa’.

Mazungumzo hayo, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Zanzibar, yaligusia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na haja ya kudumisha amani na utulivu nchini na maelewano na ushirikiano kati ya wananchi wote.

Viongozi hao wamezingatia haja ya kuzika tofauti zilizopo ambazo zinachangia kuwatenganisha Wazanzibari na kutoa wito kwa viongozi wa vyama vyote vya siasa na wananchi kwa jumla, kushirikiana katika kujenga nchi bila ya kujali itikadi zao za kisiasa.

Viongozi hao walifafanua kuwa wananchi wakishirikiana na kujenga nchi kwa pamoja, watapiga hatua kubwa zaidi za maendeleo.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao walihusisha umuhimu wa mchakato wa mazungumzo endelevu baina yao na vyama vyao kwa jumla.

Akizungumza na gazeti hili jioni jana, Msaidizi wa Maalim Seif, Bw. Ismail Jusa alisema mazungumzo yamekuwa ya mafanikio makubwa na wameahidi kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta umoja na ushirikiano kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar.

Chanzo: http://www.btl.co.tz/