Na Ally Saleh
Leo Jumatano itakuwa ni wiki mbili tokea Rais Amani Karume na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF ambao wamekuwa mahasimu wakuu wa kisiasa walipokutana katika tukio ambalo kwa wengi wetu halikuwa likitarajiwa kabisa. Na ukweli ni kuwa hadi sasa jambo hilo bado halijatulia katika akili za wengi.
Sababu ya kutotarajiwa kukutana kwao huko ni kwa vile juhudi za kuwakutanisha huko nyuma zilishindwa na hata sababu ya kuwakutanisha ambayo ilikuwa ni kuzungumzia maafikiano ya kisiasa ilikuwa imeshapigwa kumbo na Mkutano Mkuu Maalum wa Chama cha Mapinduzi CCM.
CCM ilisema wazi wazi kuwa maamuzi yoyote yale ya hatma ya kisiasa ya Zanzibar lazima yapelekwe kwa wananchi kwa njia ya kura ya maoni na wazo la kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama vile ya mpito kuelekea Uchaguzi wa 2010 si jambo linalokubalika.
Na kwa hivyo juhudi za miezi 14 za mazungumzo ya vyama hivyo viwili zikawa zimezikwa katika kaburi, lakini kumbe inavyoelekea hazikubali jambo hilo, na ndipo likatokea hili lilotokea la Wazanzibari wenyewe kwa wenyewe kuona kuwa ni lao na ni wao ndio walipe nguvu na kulifufua.
Kila Mtanzania na kila Mzanzibari na hata marafiki na washirika wa nchi hizo walikuwa wakiamini kuwa hakuna litalofanyika kwa kipindi hiki cha chini ya mwaka mmoja zaidi ya kusubiri Uchaguzi Mkuu wa 2010 ambao pia kila mtu ana kila imani kuwa utakuwa wa kupimana nguvu mno kwa vyama vikuu kinzani CUF na CCM.
Dalili za kuwa tumekuwa tukielekea katika Uchaguzi wa Damu ( Bloody Elections) zilikuwa zimeshakuwapo. Kukataliwa kuandikishwa watu, kukataliwa watu kupewa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, madai ya kuandikishwa vikosi katika sehemu ambazo wana vikosi wanapelekwa kwa madhumuni hayo na si kwa uhamisho wa kawaida wa kikazi, kuwepo kwa madai ya watu kuandikishwa zaidi ya jimbo moja, kuandikishwa watu wa chini ya umri wa kisheria kuchomewa nyumba watu, kuharibiana mali na kadhalika na kadhalika.
Kwa hivyo kuja ghafla kwa kile ambacho sasa Maalim Seif amekuwa akikipa jina la “maridhiano ya Wazanzibari” kumekuwa na upepo na mwanga mwiki kiasi ambacho kinaweza kutilika shaka. Waingereza wanasema usemao “ It is too good to be true” kwa maana yake ni kuwa uzuri wake ni mno kiasi cha kutilia shaka.
Inawezekana sisi tutapigwa muhuri au kunyooshewa kidole kuwa ni watu wenye shaka au tena tuazime msemo wa Kiingereza kuwa ni “Doubing Thomases” lakini tunahisi ni vyema kuwa na shaka sasa hivi kabla ya kuja kujiuliza masuala yasiojibika hapo baadae.
Ninachokiogopa mimi ni kile ninachokiona na kukisikia hivi sasa na ambacho kinanikerereketa akili yangu ni kule kuongezeka kwa matumaini ya watu kwa kuamini kauli za viongozi wao wa kisiasa, ambazo si ngeni na wala si za mara ya kwanza.
Kumekuwa na msemo wa kuwa “ Sasa ni wakati wa kujenga Zanzibar Mpya” na nyuma ya msemo huo watu wamekuwa wakisema mambo kadhaa kama vile kuamini kuwa kila kitu kimekubaliwa na mambo yataenda vizuri na kwa maridhiano ya Wazanzibar ( Zanzibari consensus).
Kumekuwa na tafsiri nyingi ya hiyo dhana ya Zanzibar Mpya. Nyingi ya hizo ni zile ambazo zinaamini kuondolewa kwa vikwazo ambavyo vimekuwa vikikwaza mfumo wa demokrasia na upigaji kura hapa Zanzibar na ambapo vikwazo hivyo pia vimepelekea kumwagika kwa damu.
Pia wengi wameanza kujenga matumaini kuwa ujenzi wa Zanzibar Mpya utakuwa na maana iwapo matokeo ya kura yataheshimiwa na kwamba uenedeshaji wa Serikali utajali ushirikishwaji wa umma na kila mmoja atapata fursa kwa mujibu wa uwezo wake na si kwa kujali mtizamo wake wa kisiasa.
Tumeambiwa kuwa mazungumzo ya Karume na Seif yalilenga kuhakikisha suala la amani na usalama katika nchi ambalo kwa tafsiri ni pana na kwa kweli linaweza kumeza mambo yote ambayo tumeyataja hapo juu yanayotiwa katika vunge la mtizamo wa kujenga Zanzibar Mpya.
Viongozi wakuu hao wa kisiasa wanataraji tuunge mkono na kubariki kile walichokizungumza bila ya kujua undani wake, misingi yake na hata mipaka yake. Tunatakiwa tushuhudie kitu ambacho hatuwezi kukisoma popote pale. Hivi sasa imekuwa ukihoji juu ya hilo unapigwa muhuri wa “Doubting Thomas.”
Ni wiki mbili sasa tokea tukio hilo kutokea kama nilivyotangulia kusema na hatuna mwanga wowote wala popote pale pa kushika juu ya kile kilichojiri chini ya paa la Ikulu lakini wakati huo huo tukitakiwa kuwa Wazanzibari wazuri tunaoitakia mema Zanzibar na kwa hivyo kuamini kuwa walikubaliana yalio na kheri na sisi.
Ni wiki mbili ambapo hatujaona hatua yoyote ile ya kuelekea katika kutatua kero za kisiasa na kidemokrasia ambazo kwa sasa ndio kabili na ambazo kama hazijakabiliwa sasa basi utatuzi wake unazidi kuwa mgumu kila siku moja inayokwenda. Kero hizo mbili ni uandikishaji wapiga kura na vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.
Sisi “Doubting Thomas” tupo kwa sababu tunajua wakati huu upande wenye uwezo wa kupenyeza wapiga kura, unafanya kila bidii kuifanya kazi hiyo ili ikija ikitoka kauli ya kusimamishwa au kurekebishwa iwe wamefika mbali. Hatari iliopo ni kuwa huko mbali watakako kuwa wamefika, inaweza ikatokea upande ambao ulisusia kuandikisha ukashindwa kuridhi.
Tungetaraji kwa nia njema ya maridhiano hayo, ndani ya muda huu wa wiki mbili kungekuwa na matamshi mazito kutokea upande wa Serikali kuhusiana na mambo hayo mawili, ingawa Rais Karume aliwaambia waandishi wa habari kuwa Uchaguzi Mkuu wa 2010 iwapo utawaacha watu wenye sifa, utakuwa si uchaguzi kitu, lakini hiyo si kauli ngeni, hata ndani ya mwaka huu.
Kwa hakika, ingawa baadhi ya watu watasema hilo si la muhimu, lakini inaonekana kuwa ni upande wa CUF peke yake ndio uliokwenda kwa umma kuelezea kilichotokea na kuwataka wanachama wake waunge mkono maridhiano hayo, lakini bado hatujaona upande wa CCM kufanya hivyo.
Najua hoja itakuja kuwa CCM haina haja ya kufanya hivyo kwa sababu wao ndio wenye Serikali na wao ndio waliotambuliwa na walikuwa wakiitaka CUF ifanye hivyo kwa muda mrefu, lakini tatizo langu ni ile picha ninayoiona sasa hivi ya baadhi ya watu ndani ya CCM kuona kuwa hayo hayawahusu wanachama, bali ni ya Serikali.
Hatari ninayoiona mimi hapa ni kuwa iwapo umma wa wanachama wa CCM haujatayarishwa, na tunavyowajua wanachama hao kwa misimamo yao ya asili, kuna uwezekano mkubwa wa kutofika mbali pamoja na kuwa na nia nzuri.
Maana ukweli ni kuwa hivi sasa kumekuwa na kauli kadhaa wa kadhaa za pembeni, ambazo mimi sitaki kuwa zionekane ni za mlango na hazimughasi aliyelala, ila zichukuliwe kwa umuhimu wake kwa CCM Zanzibar kuzitolea kauli za wazi wazi. Bahati mbaya kauli nyengine ni za watu wenye madaraka.
Kwa fikra zangu, kuendelea kuwataka watu washikilie kamba ya matumaini bila ya kuwaonyesha wanachotarajiwa kukitumaini, ni kujenga matumaini ambayo yana shaka katika kile kinachotumainiwa. Isichukue muda tena, kama hatuambiwi kilichomo kwenye furushi la maridhiano, basi angalau tuone vitendo vyenye ishara za wazi, na ikibidi kuwepo na maandishi juu ya kilichoridhiwa.
Tunataka kauli thabiti au maandishi ili tujue tunapimaje utekelezaji wa udhati wa maridhiano haya. La sivyo, tutajuaje kuwa tunasonga mbele na sio dangaya toto na kupoteza muda?
Chanzo: Mwananchi, 18 Nov 2009
Maoni