Sasa CUF kumpeleka Mkurugenzi wa Vitambulisho mahakamani

19 10 2009

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 15 – 10 – 2009

CUF KUMPELEKA MKURUGENZI WA VITAMBULISHO MAHKAMANI

Tarehe 12 Oktoba 2009, Mkurugenzi wa Idara ya Vitambulisho, Mohammed Juma Ame, alitoa kitisho kwa Chama chetu cha Wananchi (CUF) mkoa wa Kusini Pemba, kwamba kimpelekee maelfu ya wananchi ambao hawajapatiwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ifikapo siku ya leo, Oktoba 15, 2009, vyenginevyo angeliwapeleka viongozi wa CUF mkoa huo mahkamani kwa kudanganya.

Kitisho hiki kilikuja baada ya Katibu wetu wa wilaya ya Chake, Maalim Saleh, kupingana na takwimu za Mkurugenzi Ame kwamba katika wilaya hiyo, Idara yake ilishavuuka lengo la kutoa vitambulisho. Katibu Maalim Saleh alihoji kwamba bado kuna maelfu ya wananchi ambao hawajapewa vitambulisho na kwamba hilo linafanywa kwa makusudi.

Leo ndiyo siku ambayo ilikubaliwa kwa pamoja kuthibitishika au kukanushika kwa hoja ya CUF kuhusu vitambulisho, na wananchi wapatao 10,000 walikusanyika katika Ofisi ya Vitambulisho, Chake, wakiwa na vielelezo vyote vinavyotakiwa ili wapatiwe vitambulisho, lakini Mkurugenzi Ame amekimbia ofisi. Matokeo yake, ni wasaidizi wake tu ndio walioshuhudia ukubwa na uzito wa tatizo lililopo, ambalo linapingana na takwimu alizozitoa yeye.

Kwa hivyo, CUF imeweza kuthibitisha kwamba:

• Kwanza, si kweli kuwa Idara ya Vitambulisho imevuuka lengo la kutoa vitambulisho katika wilaya ya Chake
• Pili, si kweli kwamba kila mkaazi wa Chake ameshapewa kitambulisho chake
• Tatu, kuna idadi kubwa ya watu ambao Idara ya Vitambulisho haijataka kuwapa vitambulisho
• Nne, kwamba Mkurugenzi wa Vitambulisho anadanganya

Kwa hili, sisi CUF, tunafikiria upya uhusiano na ushirikiano wetu na Mkurugenzi Ame, kwani imedhihirika kwamba si mwaminifu na hana uthubutu wa kukabiliana na ukweli. Tunashauriana pia kumpeleka mahakamani kwa udanganyifu na matumizi mabaya ya ofisi yake, ambapo matokeo ya yote mawili ni kuutia rehani (compromise) uadilifu wa Idara anayoisimamia. Zanzibar haiwezi tena kuwastahmilia watumishi wa umma wanaoutia rehani uadilifu wa ofisi zao.

HAKI SAWA KWA WOTE

Imetolewa na:

Salim Bimani,
Mkurugenzi wa Uenezi na Mahusiano na Umma, CUF
Simu: +255 777 414 112
E-mail: cufhabari@yahoo.co.uk
Weblog: www.hakinaumma.wordpress.com


Actions

Information

Leave a comment