CUF yalaani fujo na ubambikiziwaji kesi

19 10 2009

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 4/10/2009

“CUF YALAANI MATUMIZI YA FUJO NA RAIA KUBAMBIKIZIWA KESI”

Kumekuwepo ripoti za matukio ya kinachodaiwa kuwa ni miripuko ya mabomu kisiwani Pemba kwenye nyumba za wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (SMZ) na au viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Na kufuatia ‘miripuko’ hiyo, jeshi la Polisi hufanya hima kuwakamata na kuwanyanyasa wafuasi na viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa kisingizio kwamba wao ndio watuhumiwa wakubwa. Huko nyuma pia kumekuwepo matukio ya watu (hasa wafuasi wetu) kuvamiwa usiku majumbani mwao, kupigwa mbele ya Polisi, kuchomewa moto mali zao na hata kuvunjiwa nyumba zao, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na jeshi la Polisi.

Kutokana na haya yote, sisi CUF tunapenda kuweka wazi msimamo wetu. Kwamba, kwanza, hatuungi mkono na tunalaani matumizi yoyote ya fujo yawe yanafanywa na raia au na vyombo vya dola. Unapokuwa na dola ambayo inaandaa na kusimamia fujo na unyanyasaji dhidi ya raia inaowatawala (state-organized terrorism) na unapokuwa na raia ambao hawana uhakika na usalama wao chini ya dola hiyo (civilian instability), huko ni kuserereka kwa Taifa kuelekea kwenye machafuko makubwa; na hicho si kitu cha kukiunga mkono. CUF ni chama cha siasa kinachoamini katika matumizi ya njia za kistaarabu katika kutimiza malengo ya kisiasa, na hiyo ndiyo imani ya wananchi wanaotuunga mkono.

Pili, tunalitaka jeshi la Polisi lisifanye kazi yake kwa shinikizo la kisiasa. Tumekuwa tukiheshimu ufanyaji kazi wao kwa siku kadhaa sasa, nalo linapaswa kuizingatia heshima tunayolipa. Isijikubalishe kuelemewa na presha ya CCM, ambayo imewahi kusema kuwa haina imani nalo kwa kuwa eti lilikuwa halifanyi kazi yake kitaalamu na likiipendelea CUF. Kwa msamiati wa CCM, Polisi kufanya kazi kitaalamu ni kuwapiga, kuwaua, na kuwanyanyasa wananchi wasiokuwa na hatia madhali tu wananchi hao ni wapinzani. Tunalitaka jeshi hili lisiwe sehemu ya tatizo ambalo tayari lipo, bali sehemu ya utatuzi wa tatizo hilo.

Tatu, tunahitaji haki, uadilifu na usawa katika utendaji kazi. Haiwezekani kwamba kila linalopotokezea tukio baya, ni wana-CUF tu ndio wawe ndio wanahusika. Haiwezekani kwamba hata nyumba ya mwana-CUF inapovunjwa na kuchomwa moto na familia yake kudhalilishwa, Polisi isiwe na mtuhumiwa wa kumkamata lakini inapotokezea mali ya mwana-CCM kuharibiwa, Polisi iwapate watuhumiwa haraka kama kwamba ilishawajua tangu mwanzo. Huo si uadilifu, si utaalamu wala si utashi unaoendana na dhana ya Polisi Jamii, ambayo jeshi hili imekuwa ikijaribu kuijenga.

HAKI SAWA KWA WOTE

Imetolewa na:

Salim Bimani

Mkurugenzi wa Uenezi na Mahusiano na Umma, CUF

Simu: 0777 414 112

www.hakinaumma.wordpress.com


Actions

Information

Leave a comment