Ref: CUF/HQ/ZEC/O37/016 Tarehe: 01/10/2009 28/9/2009
Your Ref
Mwenyekiti,
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar,
Zanzibar.
Mheshimiwa,
YAH: UKOSEFU WA UADILIFU WA TUME YAKO
Tafadhali husika na mada ya hapo juu.
Kwa mara nyengine tunakuandikia kwa lengo la kukutanabahisha kwamba Tume yako unayoiongoza inajihusisha na uchafuzi wa uchaguzi na sio usimamizi wa uchaguzi kama ambavyo ingetakiwa ifanye. Lengo la kufanya hivi ni kukukumbusha kama mwananchi mwenzetu ambaye umekabidhiwa ofisi ya umma na ambaye ungetakiwa usimamie vyema wajibu wako ili kesho na keshokutwa usije ukapaswa kuwajibika kwa njia ambayo siyo.
Tatizo la msingi limebakia na linaendelea kuwa matumizi ya kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi katika uandikishaji wapiga kura. Tumegundua kwamba pana tafauti kubwa sana kati ya wale ambao Tume yako imewaandikisha kuwa wapiga kura katika sehemu ambazo tayari uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura umeshafanyika na au unaendelea na wale ambao Idara ya Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi imewapa vitambulisho hivyo hadi tarehe 29 Septemba 2009.
Angalia jadweli hili hapa chini kuona tafauti hiyo:
| Jimbo | Shehia | Waliopatiwa ZAN ID | Walioandikishwa na ZEC | Tafauti |
| Nungwi | Bwereu | 17 | 398 | 381 |
| Tumbatu | Pale | 611 | 949 | 338 |
| Mto wa Pwani | 352 | 447 | 95 | |
| Uvuvini | 84 | 1,109 | 1,025 | |
| *Mkwajuni | Kidombo | 32 | 411 | 379 |
| Tumbe | Magharibi | 40 | 1,208 | 1,168 |
| S/Vyamboni B | 1 | 146 | 145 | |
| Mihogoni | 58 | 92 | 34 | |
| Chimba | 29 | 863 | 834 | |
| Konde | Msuka Magh. | 81 | 1,056 | 975 |
| Tondooni | 23 | 842 | 819 | |
| Mgogoni | Mjananza | 3 | 430 | 427 |
| Mlindo | 27 | 580 | 553 | |
| Micheweni | Majenzi | 181 | 783 | 602 |
| JUMLA | 1,539 | 9,314 | 7,775 | |
* Uandikishaji unaendelea katika jimbo la Mkwajuni, kwa hivyo kuna uwezekano wa wapiga kura kuongezeka
Kwa ugunduzi huu, moja kati ya matatu linadhihirika. Aidha, la kwanza, Tume yako haitumii ZAN ID kama kigezo cha mtu kuandikishwa kuwa mpiga kura, vyenginevyo idadi ya waliopewa ZAN ID na wale walioandikishwa na Tume yako ingelikuwa sawa, au, la pili, moja kati ya taasisi zenu mbili (ZEC na Idara ya ZAN ID) inasema uongo kwenye data zake na au, la tatu, kuna uwezekano mkubwa kwamba watu wanapandikizwa kutoka majimbo mengine na masheha, ambao ni mawakala wenu wanaridhia kwa vile ni njama ya kukibeba Chama cha Mapinduzi (CCM). Kama hili linatokea, hakuna uhakika kwamba waliopandikizwa kuandikishwa katika majimbo ambayo si yao hawataandikishwa tena katika majimbo yao muda utapofikia. Kwa hivyo, mnaandaa mazingira yatakayowaruhusu baadhi ya watu kupiga kura zaidi ya mara moja wakati wengine wananyimwa haki ya kujiandikisha.
Lolote lililo ndilo kati ya matatu hayo linamaanisha kwamba zoezi hili limekosa uhalali. Kwa hivyo, unapaswa kuifahamu hoja yetu kwamba wananchi wanapolikataa zoezi hili ambalo Tume yako imelipa jina la ’Uboreshaji Daftari la Kudumu la Wapiga Kura’ ni kwa sababu wanafahamu kwamba zoezi hili ni muendelezo wa uchafuzi na kwamba wewe na Tume yako munasimamia uchafuzi wa haki ya Wazanzibari.
Sisi, CUF, hatuwezi kuwa sehemu ya uchafu huu na tungeliishauri Tume yako nayo ijisafishe kwa kujitoa kwenye uandikishaji huu mchafu.
HAKI SAWA KWA WOTE
Seif Sharif Hamad
KATIBU MKUU
Nakala kwa:
- Mkurugenzi wa Idara ya Vitambulisho
- Makamishna wa ZEC
- Mwakilishi wa United Nations Development Program (UNDP), Tanzania
- Kiongozi wa Upinzani Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
- Kiongozi wa Upinzani Baraza la Wawakilishi
- Vyombo vya Habari
lazima muwe up – to – date habari muhimu ya Maalim Seif au CUF kuitambua serikali ya Karume hakuna humu sasa faida gani ya kuwa na mtandao huu wa chama? muwe watu wa kisasa jamani.
Nawashangaa mbona hii web haina vitu vya maana wakati huu wa sakata la CUF kuitambua serikali ya Mapinduzi ya zanzibar au CCM?