NEC ni sehemu ya uchafuzi wa ZEC

19 10 2009

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 18 Septemba 2009

”NEC NI SEHEMU YA UCHAFUZI UNAOFANYIKA Z’BAR”

Kufuatia habari iliyochapishwa katika gazeti la leo la Mwananchi ambayo imemnukuu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Lewis Makame, akisema kwamba Tume yake haihusiki na matatizo yanayojitokeza katika zoezi la uandikishaji wapiga kura kisiwani Pemba kwa kuwa jukumu hilo linasimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) peke yake, Chama cha Wananchi (CUF), kinatoa kauli ifuatayo:

Kwanza, Jaji Makame anaudanganya umma wa Tanzania na ulimwengu kwa ujumla kwa kuzitenganisha Tume hizi mbili (ZEC na NEC) kama vile ni taasisi zisizo na uhusiano wowote kikazi. Ukweli ni kuwa, NEC inaitumia ZEC kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano kama wakala wake kwa chaguzi za Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano zinazofanyika Zanzibar na, kwa hivyo, uchafu wowote unaofanywa na ZEC visiwani Zanzibar ni uchafu pia ni wa NEC.

Uandikishwaji unaofanywa na ZEC hivi sasa Pemba na Unguja, unafanywa pia kuwaandikisha wapiga kura kwa ajili ya chaguzi za Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano kinyemela, huku NEC ikifahamu hilo. Maana yake ni kwamba wanaoandikishwa na ZEC ndio watakaopiga kura kwenye uchaguzi unaosimamiwa na NEC. Inachofanya NEC baada ya kupokea data za wapiga kura kutoka ZEC ni kuwajazia wale wachache ambao ZEC haikuwaandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa Muungano. Kwa hivyo, kama kweli Jaji Makame anataka kuivua Tume yake na uchafu huu, afuate Katiba ya Jamhuri ya Muungano (Kif. Na. 5) kwa NEC yenyewe kuratibu uandikishaji na upigaji kura kwa ajili ya chaguzi za Muungano zinazofanyika Zanzibar. Bila ya kufanya hivyo, NEC itaendelea kuwa sehemu ya uharamia unaoratibiwa na ZEC na inabeba lawama zile zile ambazo ZEC inazibeba.

Pili, chini ya Jaji Makame, NEC imekuwa nyenzo kubwa ya kuvunja Katiba na kuwagawa Watanzania baina ya wale wa Tanzania Bara na wa Zanzibar kwani inatumia taratibu mbili tafauti inapowaandikisha kutumia haki yao ya kupiga kura. Ambapo mpiga kura wa Rais na Mbunge wa Jamhuri ya Muungano aliye upande wa Bara hatumii kitambulisho cha uraia wala cha ukaazi kujiandikisha, yule wa Zanzibar analazimishwa kuandikishwa kwa sheria iliyokwenda kinyume na Katiba ya Zanzibar ambayo inatambua kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi kama sharti la pekee la kuwa mpiga kura.

Matokeo yake ni kuwa Watanzania hawa wawili wanamchagua Rais na Mbunge wa Jamhuri katika uchaguzi mmoja lakini kwa kutumia taratibu tafauti. Huo ni upotofu wa kimakusudi ambao NEC inaujua, lakini inaufanya kwa kuwa imeamua kuwa sehemu ya uharamia unaofanyika Zanzibar.

Tatu, kutokana na kwanza na pili hapo juu, tunataka yafuatayo yafanyike:

i. Kama kweli Jaji Makame anakiamini anachokisema, basi Tume yake isitishe mara moja kuifanya ZEC kuwa wakala wake na pia iwache kutumia Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linaloratibiwa na ZEC, kwani kuendelea kufanya hivyo ni kuvuja Katiba zote mbili na kujipaka uchafu.

ii. Kwa kuwa hapa pana uvunjwaji wa wazi wa Katiba ya nchi, tunaiomba juumuiya ya wanasheria nchini wauone ukiukwaji huu na washirikiane nasi kulipatia tatizo hili ufumbuzi wa kisheria. Ni aibu kwa nchi yenye wasomi wa Sheria kama yetu na kwa taasisi inayoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu kama NEC kuendelea kuvumilia uvunjaji wa Katiba na ukiukwaji wa sheria.

iii. Kwa kuwa jumuiya ya kimataifa ndiyo ambayo inafadhili uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura pamoja na shughuli zote za chaguzi, tunaiomba ifikirie upya namna kodi za wananchi wao zinavyotumiwa na ushirikiano wa ZEC/NEC katika kuizika demokrasia nchini Tanzania.

iv. Kwa kiwango hiki cha udhaifu kinachooneshwa na NEC, msimamo wa Profesa Haruna Lipumba wa kwamba Tume hii ijiuzulu unaendelea kuthibiti.

Imetolewa na:

Salim Bimani,

Mkurugenzi wa Uenezi na Mahusiano na Umma, CUF

Simu: +255 777 414 112

E-mail: cufhabari@yahoo.co.uk

Weblog: www.hakinaumma.wordpress.com





CUF yalaani fujo na ubambikiziwaji kesi

19 10 2009

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 4/10/2009

“CUF YALAANI MATUMIZI YA FUJO NA RAIA KUBAMBIKIZIWA KESI”

Kumekuwepo ripoti za matukio ya kinachodaiwa kuwa ni miripuko ya mabomu kisiwani Pemba kwenye nyumba za wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (SMZ) na au viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Na kufuatia ‘miripuko’ hiyo, jeshi la Polisi hufanya hima kuwakamata na kuwanyanyasa wafuasi na viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa kisingizio kwamba wao ndio watuhumiwa wakubwa. Huko nyuma pia kumekuwepo matukio ya watu (hasa wafuasi wetu) kuvamiwa usiku majumbani mwao, kupigwa mbele ya Polisi, kuchomewa moto mali zao na hata kuvunjiwa nyumba zao, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na jeshi la Polisi.

Kutokana na haya yote, sisi CUF tunapenda kuweka wazi msimamo wetu. Kwamba, kwanza, hatuungi mkono na tunalaani matumizi yoyote ya fujo yawe yanafanywa na raia au na vyombo vya dola. Unapokuwa na dola ambayo inaandaa na kusimamia fujo na unyanyasaji dhidi ya raia inaowatawala (state-organized terrorism) na unapokuwa na raia ambao hawana uhakika na usalama wao chini ya dola hiyo (civilian instability), huko ni kuserereka kwa Taifa kuelekea kwenye machafuko makubwa; na hicho si kitu cha kukiunga mkono. CUF ni chama cha siasa kinachoamini katika matumizi ya njia za kistaarabu katika kutimiza malengo ya kisiasa, na hiyo ndiyo imani ya wananchi wanaotuunga mkono.

Pili, tunalitaka jeshi la Polisi lisifanye kazi yake kwa shinikizo la kisiasa. Tumekuwa tukiheshimu ufanyaji kazi wao kwa siku kadhaa sasa, nalo linapaswa kuizingatia heshima tunayolipa. Isijikubalishe kuelemewa na presha ya CCM, ambayo imewahi kusema kuwa haina imani nalo kwa kuwa eti lilikuwa halifanyi kazi yake kitaalamu na likiipendelea CUF. Kwa msamiati wa CCM, Polisi kufanya kazi kitaalamu ni kuwapiga, kuwaua, na kuwanyanyasa wananchi wasiokuwa na hatia madhali tu wananchi hao ni wapinzani. Tunalitaka jeshi hili lisiwe sehemu ya tatizo ambalo tayari lipo, bali sehemu ya utatuzi wa tatizo hilo.

Tatu, tunahitaji haki, uadilifu na usawa katika utendaji kazi. Haiwezekani kwamba kila linalopotokezea tukio baya, ni wana-CUF tu ndio wawe ndio wanahusika. Haiwezekani kwamba hata nyumba ya mwana-CUF inapovunjwa na kuchomwa moto na familia yake kudhalilishwa, Polisi isiwe na mtuhumiwa wa kumkamata lakini inapotokezea mali ya mwana-CCM kuharibiwa, Polisi iwapate watuhumiwa haraka kama kwamba ilishawajua tangu mwanzo. Huo si uadilifu, si utaalamu wala si utashi unaoendana na dhana ya Polisi Jamii, ambayo jeshi hili imekuwa ikijaribu kuijenga.

HAKI SAWA KWA WOTE

Imetolewa na:

Salim Bimani

Mkurugenzi wa Uenezi na Mahusiano na Umma, CUF

Simu: 0777 414 112

www.hakinaumma.wordpress.com





Mwakilishi akanusha uongo wa vyombo vya SMZ

19 10 2009

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 13 OKTOBA 2009

CUF YAKANUSHA UONGO WA VYOMBO VYA HABARI VYA CCM NA SMZ

Kufuatia matangazo ya Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ), kama yalivyosikikana kwenye taarifa yake ya habari ya leo ya saa 1.00 magharibi, ambayo yamedai mwakilishi wa jimbo la Gando (CUF), Mheshimiwa Said Ali Mbarouk, ameipongeza Idara ya Vitambulisho kwa utendaji kazi wake, Mhe. Mbarouk ametoa kauli ifuatayo kwa umma:

“Si kweli kabisa kwamba nimempongeza Mkurugenzi wa Vitambulisho, Bwana Mohammed Juma Ame, kwa kazi yake. Sijaona ikiwa anafanya kazi yake kwa uadilifu na kitaalamu, na hivyo hastahili pongezi za mtu mwenye heshima zake, ambaye ni mtunga sheria na ambaye anaona wazi sheria zikivunjwa na Idara inayoongozwa na Mkurugenzi Ame.

“Kile hasa nilichomwambia Mkurugenzi Ame, katika mkutano huo uliofanyika saa 4.00 asubuhi hadi saa 6.00 mchana katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Wete na kuhudhuriwa na wakuu wa wilaya za Wete na Micheweni, viongozi wa vyama vya CCM na CUF, mkuu wa Usalama wa Taifa wilaya ya Wete na yeye mwenyewe (Mkurugenzi Ame) akiwa na kundi la waandishi ‘wake’ wa habari, ni kuwa Idara yake inafanya kazi kinyume na sheria.

“Nilimpa mifano miwili kuthibitisha hilo : mmoja ni kuwatumia masheha katika utoaji wa vitambulisho vipya, ambao hawamo kwenye Sheria ya Vitambulisho. Nafasi pekee ya sheha katika suala hili ingelikuwa ni pale tu ambapo mkaazi wa shehia yake amepoteza kitambulisho hicho na akataka barua ya uthibitisho ili kuiwasilisha Polisi na Idarani. Mfano mwengine ni hatua ya upotoshaji wa Idara yake ya kulazimisha kwamba watu waende na vyeti virefu vya kuzaliwa.

“Katika mifano yote miwili, Idara yake inajua tatizo lilipo: kwenye nafasi ya masheha, inajua kuwa pamoja na kwamba si halali kisheria kuwatumia kudai kitambulisho kipya, lakini pia masheha hao hutumia ukereketwa wa kisiasa katika suala hili kama ambavyo mifano kadhaa imeendelea kuthibitisha. Kwenye suala la vyeti virefu, Idara yake inajuwa kuwa utaratibu wa kuvipata ni mrefu pia na una gharama kubwa ambazo wananchi wengi wa kawaida hawawezi kuulipia. Kwa hivyo, inapoweka vigingi hivi inafanya makusudi ili kuzuia Wazanzibari wengi wenye haki ya kuwa na vitambulisho wasiwe navyo!

“Kwa yote mawili, Mkurugenzi Ame alikiri kuwepo kwa kosa na tatizo, kwani kwa maneno yake mwenyewe ni kweli kwamba sheria haikumpa nafasi sheha wala idara yake haijapewa nguvu za kudai cheti cha kuzaliwa, lakini akasema hizo ni “kanuni za Waziri.”

“Nikiwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na, hivyo, mtunga sheria, nafahamu kuwa ‘Kanuni ya Waziri’ wa Mkurugenzi Ame haitakiwi ikiuke Katiba wala Sheria na kwamba inapofanya hivyo, huo unakuwa ni ubatili mtupu. Kwa hivyo, ni wazi kuwa Mkurugenzi Ame anasimamia ubatili, na hilo si jambo la kumsifia, bali ni lawama ya kumlaumu.

“Hayo niliyabainisha kwenye mkutano huo na, angalau kwa maneno, Mkurugenzi Ame alikubaliana na lawama nilizozitoa na kuahidi kwamba angelikaa na wenzake (labda alikusudia wenzake serikalini) na kuhakikisha kuwa gharama za upatikanaji cheti zinashuka na kwamba Mrajis aliyeko Pemba anapewa nguvu na mamlaka ya kusaini vyeti ili kupunguza urefu wa muda wa kupata cheti kirefu. Kuhusu masheha, ufafanuzi pekee alioutoa ni kwamba wao (masheha) ndio wanaowajua zaidi watu wanaokaa nao.

“Kwa hivyo, kwa umma, ningependa kueleza kwamba kilichotangazwa na STZ kilikuwa ni uongo mtupu, ambao lengo lake ni kunichafulia hadhi na heshima yangu. Watu wengi wamesumbuka kunipigia simu na kutaka uhakika kutoka mdomoni mwangu mwenyewe. Nami ingawa nimejitahidi kuwafahamisha, huenda kuna wengine ambao wamesikia na ambao wangetaka kujua ukweli lakini hawawezi kunipigia simu. Taarifa hii itosheleze kuwa hakikisho la msimamo wangu.

“Kwa STZ, nimempigia simu Juma Mohammed kutoka Idara ya Habari Maelezo kumtaka asahihishe makosa hayo na aeleze ukweli. Ninawaonya wafuate maadili ya taaluma yao ya uandishi wa habari ambayo yanawataka waseme ukweli na ukweli mtupu!

“Nirudie tena msimamo wangu kwamba Idara ya Vitambulisho inayoongozwa na Mkurugenzi Ame haijafanya chochote kinachostahiki kusifiwa katika hili, kwani bado kuna maelfu ya Wazanzibari wenye sifa ambao hawana vitambulisho na ambao mtandao wa Idara hiyo na masheha unawazuia kwa makusudi wasivipate.

“Siku Mkurugenzi Ame na Idara yake watakayostahiki sifa zangu, ni pale watakapowacha vituko vyao vya makusudi na wakampa kila Mzanzibari anayestahiki kitambulisho chake cha Mzanzibari. Na hadi siku hiyo ifike, yeye na idara yake wataendelea kubeba lawama zote zinazohusiana na Wazanzibari kunyimwa haki yao ya kimsingi, ya kiraia na ya kisheria.”

Imetolewa na:

Said Ali Mbarouk (Mwakilishi wa Gando)

Simu: +255 777 411 739

Imesambazwa na:

Kurugenzi ya Habari na Uenezi na Mahusiano na Umma, CUF

Simu: +255 777 414 112

cufhabari@yahoo.co.uk

www.hakinaumma.wordpress.com





Sasa CUF kumpeleka Mkurugenzi wa Vitambulisho mahakamani

19 10 2009

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 15 – 10 – 2009

CUF KUMPELEKA MKURUGENZI WA VITAMBULISHO MAHKAMANI

Tarehe 12 Oktoba 2009, Mkurugenzi wa Idara ya Vitambulisho, Mohammed Juma Ame, alitoa kitisho kwa Chama chetu cha Wananchi (CUF) mkoa wa Kusini Pemba, kwamba kimpelekee maelfu ya wananchi ambao hawajapatiwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ifikapo siku ya leo, Oktoba 15, 2009, vyenginevyo angeliwapeleka viongozi wa CUF mkoa huo mahkamani kwa kudanganya.

Kitisho hiki kilikuja baada ya Katibu wetu wa wilaya ya Chake, Maalim Saleh, kupingana na takwimu za Mkurugenzi Ame kwamba katika wilaya hiyo, Idara yake ilishavuuka lengo la kutoa vitambulisho. Katibu Maalim Saleh alihoji kwamba bado kuna maelfu ya wananchi ambao hawajapewa vitambulisho na kwamba hilo linafanywa kwa makusudi.

Leo ndiyo siku ambayo ilikubaliwa kwa pamoja kuthibitishika au kukanushika kwa hoja ya CUF kuhusu vitambulisho, na wananchi wapatao 10,000 walikusanyika katika Ofisi ya Vitambulisho, Chake, wakiwa na vielelezo vyote vinavyotakiwa ili wapatiwe vitambulisho, lakini Mkurugenzi Ame amekimbia ofisi. Matokeo yake, ni wasaidizi wake tu ndio walioshuhudia ukubwa na uzito wa tatizo lililopo, ambalo linapingana na takwimu alizozitoa yeye.

Kwa hivyo, CUF imeweza kuthibitisha kwamba:

• Kwanza, si kweli kuwa Idara ya Vitambulisho imevuuka lengo la kutoa vitambulisho katika wilaya ya Chake
• Pili, si kweli kwamba kila mkaazi wa Chake ameshapewa kitambulisho chake
• Tatu, kuna idadi kubwa ya watu ambao Idara ya Vitambulisho haijataka kuwapa vitambulisho
• Nne, kwamba Mkurugenzi wa Vitambulisho anadanganya

Kwa hili, sisi CUF, tunafikiria upya uhusiano na ushirikiano wetu na Mkurugenzi Ame, kwani imedhihirika kwamba si mwaminifu na hana uthubutu wa kukabiliana na ukweli. Tunashauriana pia kumpeleka mahakamani kwa udanganyifu na matumizi mabaya ya ofisi yake, ambapo matokeo ya yote mawili ni kuutia rehani (compromise) uadilifu wa Idara anayoisimamia. Zanzibar haiwezi tena kuwastahmilia watumishi wa umma wanaoutia rehani uadilifu wa ofisi zao.

HAKI SAWA KWA WOTE

Imetolewa na:

Salim Bimani,
Mkurugenzi wa Uenezi na Mahusiano na Umma, CUF
Simu: +255 777 414 112
E-mail: cufhabari@yahoo.co.uk
Weblog: www.hakinaumma.wordpress.com





Zanzibar: Tusipoziba ufa tutajenga ukuta

3 10 2009

Na Nizar Visram

HAKUNA anayeweza kukataa kuwa Zanzibar inaelekea kubaya, kuwa hali ya visiwani inatia wasiwasi. Zoezi linaloendelea la kujiandikisha katika daftari la wapigakura limetawaliwa na mabomu, risasi, helikopta, uchomaji moto, mapigano, ukamataji wa raia na vitisho vya kuua.

Hapo awali tuliambiwa Pemba ndiko kwenye vurugu. Tukasikia na Unguja nako katika kisiwa cha Tumbatu polisi wanamimina mabomu ya machozi kutoka helikopta. Tunaambiwa polisi inashindwa kuwatawanya wananchi kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi na ndipo risasi za moto zinafyatuliwa.

Vilio vya akinamama na watoto kutokana na hofu ya milio ya risasi na nyumba kuungua moto ni sehemu ya patashika lililoendelea katika uandikishaji katika jimbo la Tumbatu.

Askari polisi (FFU) na kikosi cha KMKM huacha eneo la uandikishaji na kuelekeza mabomu yao kwenye makazi ya wananchi na kusababisha baadhi yao kupoteza fahamu na wengine kupanda maboti na kukimbia. Mkazi mmoja wa Tumbatu mtu mzima alikimbizwa kituo cha afya baada ya kupoteza fahamu.

Akina mama wakiwa wamewabeba watoto wao migongoni pamoja na wazee wanaonekana kukimbilia vichakani ili kuokoa maisha yao kutokana na hofu ya mabomu na risasi za moto.

Tunaambiwa kundi la wafuasi wa CUF na CCM wanarushiana mawe, wanatwangana makonde na kupambana kwa silaha za kienyeji na kusababisha baadhi yao kujeruhiwa. Mwanamke mmoja aliyejeruhiwa na jiwe alikimbizwa hospitali.

Huko Pemba nako baadhi ya wakaazi tunaambiwa wamelazimika kuyakimbia makazi yao na kuhamia porini kwa vile polisi wanawavamia majumbani mwao usiku wa manane. Tunaambiwa katika kamata kamata hiyo polisi wanavamia nyumba za baadhi ya viongozi wa “chama kimoja cha siasa.”

Wakati wote huo magari ya polisi yaliyokuwa na vitambaa vyekundu na magari ya msalaba mwekundu yamekuwa yakiranda mitaani.

Yote haya yanafanyika wakati wa kuandikisha wapigakura. Uchaguzi wenyewe bado. Hata kampeni bado. Hii ni hatua ya mwanzo tu ya kuandikishwa kwa wapiga kura. Tufikirie kitakachotokea siku za usoni, hasa tukizingatia historia ya kisiasa visiwani Zanzibar.

Rais Jakaya Kikwete alikubali kuwa kuna mpasuko huko Zanzibar. Akaahidi kuwa atafanya kila juhudi kutafuta suluhisho. Akaanzisha mazungumzo ya Mwafaka. Wakati wa kutiliana saini ulipowadia chama chake ‘kikaruka kimanga.’

Vurugu hii ya sasa huko visiwani isingetokea kama Mwafaka ungetekelezwa. Hata hivyo kuna haja ya Rais Kikwete kuingilia kati na kutatua matatizo. Haya si mambo ya ndani kwani jeshi la polisi linalotumiwa huko Zanzibar ni la Muungano.

Wanaojiandikisha wanafanya hivyo ili wachague Wabunge na Rais wa Muungano.

Iweje sasa tatizo hilo aachiwe Rais Amani Karume peke yake? Yeye alipobanwa na wafadhili kama kawaida yao mara moja akawaalika Ikulu Zanzibar na akatoa amri kuwa vitambulisho vya ukaazi vitolewe bila ya usumbufu. Wafadhili wakanywa chai na kisha kuendelea kumwaga mabilioni.

Wanaotegemea kuwa wafadhili wataingilia kati wanajidanganya.

Hawakufanya hivyo tangu 1995 kwa sababu wao wanaangalia maslahi yao ya kitaifa. Wataingilia kati pale tu maslahi yao yatakapohatarishwa. Si Kenya, si Zimbabwe wala si Zanzibar

Sasa tunaona Waziri wa Mambo ya Ndani na Mkuu wa Polisi (IGP) wanatembelea Zanzibar na kukutana na makamanda wa polisi. Kisha wanatoa onyo kuwa polisi itajizatiti kuzuia vurugu.

Atakayevuruga amani atakiona kilichomtoa kanga manyoya!

Yaani tatizo la kisiasa linatatuliwa kipolisi. Watu wanataka kujua kwa nini kitambulisho cha Uzanzibari kiwe ni sifa ya uandikishaji wa wapigakura? Cheti cha kuzaliwa hakitoshi? Na hicho kitambulisho kwanini iwe balaa kukipata? Watu wanataka kujua kwa nini daftari la wapiga kura liwe siri?

Haya ni maswala ambayo hayawezi kujibiwa na IGP. Ilitakiwa Rais Kikwete aingilie kati na kuonana na wadau wote huko Zanzibar. Ilitakiwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itimize wajibu wake na kuisaidia Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Badala yake NEC inajivua lawama kutokana na matatizo yanayojitokeza Zanzibar na kuitupia mzigo huo ZEC.

Katika baadhi ya vituo hakuna hata mtu mmoja aliyejitokeza kuandikisha. Hata ZEC yenyewe imesema hairidhishwi na zoezi hilo kutokana na kasi ndogo ya uandikishaji. Imesema zoezi hilo katika Mikoa ya Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba, “halikutoa mafanikio” yaliyotarajiwa. Lakini CCM eti inaipongeza ZEC kwa “kazi nzuri.” Huo siyo utatuzi wa kisiasa tunaozungumzia.

Matatizo haya hayakuibuka ghafla. Yalibainika mapema. Julai mwaka huu tuliambiwa kuwa huko Zanzibar kumekuwao malalamiko kwamba kuna wananchi wananyimwa haki yao ya kujiandikisha. alalamiko haya yalifika hata bungeni ambako baadhi ya wabunge kutoka Zanzibar walilalamika kwamba watawala wa Zanzibar kuanzia sheha hadi wakuu wa wilaya wamejenga utaratibu mgumu kwa baadhi ya watu kupata vitambulisho vya ukaazi.

Zanzibar imekuwa na migogoro ya kisiasa hata kabla ya uhuru wa 1963 na Mapinduzi ya 1964 na kuendelea baada ya uchaguzi wa 1995, 2000 na 2005.

Kama mara hii tena uandikishwaji utatawaliwa na vurugu ni dhahiri kuwa visiwa hivyo vinaelekea kubaya.

Chanzo: Mwananchi la 30 Septemba 2009