CCM yafikiria mseto Zanzibar

29 09 2009

Friday, 25 September 2009 16:58
* Msekwa ahofia yaliyotokea Kenya, Zimbabwe
* CUF yasema hatudanganyiki, huo ni usanii

Na Reuben Kagaruki

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezinduka na kutangaza kuwa hakitasubiri machafuko yaliyotokea Kenya na Zimbabwe yatokee Zanzibar ndipo kiunde Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo.

Kauli hiyo ya CCM imetolewa huku zikiripotiwa vurugu za mara kwa mara visiwani humo za kupinga utaratibu wa uandikishaji wananchi kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura kutokana na vikwazo katika utoaaji wa vitambulisho vya ukaazi, kiasi cha kusababisha Jeshi la Polisi kutumia mabomu kutuliza hali hiyo.

Akihojiwa katika kipindi cha Jambo Tanzania kilichotangazwa Dar es Salaam jana na Televisheni ya Taifa (TBC1), Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Bw. Pius Msekwa alisema kuwa chama chake kinatambua kuwa Zanzibar kuna tatizo.

“Tunafikiria kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Tatizo ni mfumo tulionao mtu akishindwa kwa kura chache anabaki nje ya Serikali,” alisema Bw. Msekwa na kutahadharisha kuwa;

“Msingojee matatizo yatokee kama ya Zimbabwe na Kenya ndipo iundwe Serikali ya kitaifa…hayo ndiyo tunayozungumzia.”

Alitolea mfano uchaguzi wa mwaka 1995 ambapo mgombea wa CCM, Dk Salmin Amour (Komandoo) ilipata ushindi wa asilimia 50.2 na chama kilichofuatia (CUF) kilichoapata asilimia 49.8 kikawa nje ya Serikali. “Hii siyo hali nzuri,” alionya Bw. Msekwa.

Bw. Msekwa lizidi kutolea mfano tofauti iliyokuwepo kwa upande wa Baraza la Wawakilishi akisema chama kimoja (CCM) kilikuwa na wawakilishi 29 na kingine (CUF) 24.

Hata hivyo, alisema matatizo ya Zanzibar hayakuanza leo bali ni ya tangu nchi hiyo inatawaliwa Uingereza ambapo kwenye uchaguzi wa kwanza zilitokea vurugu na kwa kumbukumbu zake watu 30 walikufa.

Bw. Msekwa alisema hali ya kutokubali matokeo iliendelea na utulivu uliokuwepo uliletwa na mfumo wa chama kimoja uliokuwa umeanzishwa.

“Mfumo huu wa vyama vingi ulipoanzishwa matatizo ndipo yalipoanzia, mwaka 1995 tukapata muafaka lakini haukuleta mafanikio, mwaka 2005 muafaka haukutusaidia, tunaendelea,” alisema Bw. Msekwa.

Lakini kauli hiyo ya Bw. Msekwa ilipokewa kwa shingo upande na chama cha CUF na kuibatiza kuwa ni usanii wa kisiasa.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma wa CUF, Bw. Salim Biman, alisema, “Mpango huo ni usanii wa kisiasa, kwanza hatuwezi kumwamini (Msekwa) kwa kuwa anatofautiana na mwenyekiti wake.”

Bw. Biman alisema CUF haiwezi kukaa kwenye mazungumzo tena kwa kuwa muafaka ulishafikiwa na kinachosubiriwa ni utekelezaji. “Tulishakubaliana muundo wa Serikali ya umoja utakavyokuwa, wao (CCM) walienda Butiama wakarudi na pendekezo la kura za maoni, kama wanataka wakutane makatibu wakuu wa vyama kwa ajili ya utekelezaji,” alisema Bw. Biman

Muafaka ulitolewa na chama cha CUF kikidai ndiyo makubaliano ya kamati ya muafaka na CCM, unaitaka katiba ya Zanzibar iwe na kifungu kinachoainisha kuwa Naibu wa Kwanza wa Rais ni Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi/Baraza la Mawaziri.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, ambayo CCM iliyakana, kutakuwa na Msaidizi Mkuu wa Rais kuhusu mambo yote ya Zanzibar ambaye atamsaidia Rais kufuatilia utekelezaji wa siku hadi siku wa Mambo ya Muungano katika Zanzibar.

Pia, kikatiba, ndiye atafanya kazi zote atakazoagizwa na Rais, na atakaimu urais wakati Rais hayupo nchini.

Pia kutakuwa na Manaibu wawili wa rais, Naibu wa Kwanza anakayetoka chama cha pili katika uchaguzi na Naibu wa Pili atakayetoka chama sawa na kilichomtoa rais.

Pia iliainishwa kuwa Rais atashirikiana na Naibu wa Kwanza wa Rais katika uundaji wa Baraza la Mawaziri, Baraza la Mapinduzi na nafasi zipi chama chake kinazostahiki kupata.

Muda wa kushika madaraka wa mtu aliyechaguliwa kuwa Naibu wa Kwanza wa Rais utakuwa sawa na ule wa Rais na mazingira ya kuacha madaraka yatakuwa sawa na yale yanayomhusu Rais.

Ikitokezea kwamba kiti cha Naibu wa Kwanza wa Rais kikawa wazi kutokana na masharti hayo ya kikatiba, Rais atamteua mtu mwingine atakayependekezwa na chama cha siasa alichotoka Naibu wa Kwanza wa Rais aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo kuwa Naibu wa Kwanza wa Rais kwa muda uliobakia.

Mbali na kuzungumzia umuhimu ya serikali ya umoja wa kitaifa, Bw. Msekwa alisema malumbano ambayo yamekuwa yakiendelea ndani ya Baraza la Wawakilishi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yanadhohofisha nguvu za chama na kukifanya kishindwe kuelekea kinapotaka kwenda.

“Malumbano yanadhohofisha nguvu ya pamoja ya kutaka kuelekea kule tunapotaka kuelekea,” alisema Bw.Msekwa.

Alisema kutokana na hali hiyo, ndiyo maana Mwenyekiti wa CCM (Rais Jakaya Kikwete) kwa kutumia busara zake aliamua kuunda kamati ili kufuatilia hali hiyo na kutoa mapendekezo ya kuiondoa.

Aliongeza kuwa hatua ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kukutana na kuunda kamati ambayo yeye ni mjumbe ni utaratibu wa kawaida ndani ya chama. Wengine wanaounda kamati hiyo ni Bw.Abdulrahaman Kinana na Rais Mstaafu, Mzee Ali Hassan Mwinyi anayeiongoza.

“Hii siyo kwamba imetokea mara ya kwanza kwenye NEC, miaka yote tumekuwa tukizungumzia hali ya siasa, katika kikao kilichopita tukaelekeza macho yetu katika malumbano yaliyotokea katika Baraza la Wawakilishi na Bungeni,” alisema

Chanzo: Majira





IGP Mwema aonja siasa za CUF, CCM

29 09 2009

Juhudi za Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, kutaka kuhakikisha amani inakuwepo visiwani Zanzibar, zimekutana na kigingi.

Mwema alikutana na hali hiyo katika kongamano la kujadili demokrasia na mchakato wa uandikishaji wapiga kura Zanzibar, baada ya kumalizika bila ya kupatikana muafaka pale suala la vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi lilipowagawa washiriki.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi wa vyama vya siasa pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Wazanzibari Wakaazi, Mohammed Juma Ame. Wakichangia mada kuhusu demokrasia, uandikishaji wapigakura na vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, baadhi ya washiriki walisema chanzo cha vurugu zinazojitokeza Zanzibar ni baadhi ya wananchi kukoseshwa vitambulisho hivyo.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Juma Duni Haji, alisema vurugu hizo zitaendelea kujitokeza iwapo wananchi hawatapewa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.

Alisema tangu kuanza kwa uandikishaji wapigakura, kumekuwepo na malalamiko mengi kuwa wananchi wananyimwa vitambulisho vya Mzanzibar Mkaazi, kinyume cha misingi ya demokrasia.

“Zoezi la uandikishaji wapigakura limekuwa gumu kwa vile nia njema haipo,” alisema Mbunge wa Mji Mkongwe, Ibrahim Sanya.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz, alilaumu mada iliyowasilishwa katika mkutano kwamba ililenga kutoa lawama kwa upande mmoja.

Mada hiyo iliyotolewa na mwandishi wa habari maarufu Zanzibar, Salim Said Salim, ilisema baadhi ya wananchi kunyimwa vitambulisho vya ukaazi Zanzibar ndio chanzo cha vurugu zinazojitokeza Pemba na Unguja.

Mwakilishi wa Kwahani (CCM), Ali Suleiman Ali, alisema chama cha CUF ndicho cha kubeba lawama kutokana na vurugu zinazojitokeza kwa vile wanawazuia watu wasiende kujiandikisha.

Alisema ni vyema viongozi wa vyama vya siasa wakaacha vitendo hivyo ili wananchi waweze kupata fursa ya kuandikishwa.

“CUF ndio wamekuwa wakizuia watu wasiende kujiandikisha, ni vyema wakaacha vitendo hivyo ili malengo ya kweli ya demokrasia yaweze kufikiwa,” alisema.

Wawakilishi wa vyama vya PPT Maendeleo na TLP, walisema chimbuko la matatizo yote yanayojitokeza Zanzibar ni vitambulisho vya ukaazi kutokana na urasimu mkubwa wa watendaji.

Mwakilishi wa PPT Maendeleo, Khamis Suleiman Khamis, alisema viongozi wa serikali za mitaa (masheha) wamekuwa vikwazo zaidi katika utoaji vitambulisho hivyo.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Wazanzibari Wakaazi, Mohammed Juma Ame, alikanusha madai ya wananchi kunyimwa vitambulisho kwa maelezo kuwa kinachoonekana kuna watu wameanza kuficha vitambulisho na kudai hawajapewa kwa malengo yao ya kisiasa.

Mkurugenzi huyo alisema kwamba Idara yake imekuwa ikitoa vitambulisho kwa wananchi wote ambao hawana, na hadi ifapo Jumapili karibu Wazanzibari wote watakuwa wamepewa vitambulisho hivyo (ZAN ID).

Akizungumza katika mkutano huo, Mwema alisema ameamua kufika Zanzibar kuhimiza suala la amani na usalama.

Alisema viongozi wa vyama vya siasa na dini wana wajibu wa kuzingatia suala la kudumishwa kwa usalama katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwakani.

“Mimi nimekuja hapa kuhimiza usalama, amani na utulivu, sote tuna jukumu la kuhakikisha hilo, hivyo viongozi wa dini na vyama vya siasa ni nafasi yenu ya kuzungumzia amani,” alisema IGP Mwema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu TDEA, Juma Ali Khatibu, alisema suala la elimu ya uraia lina umuhimu mkubwa Zanzibar ili kuepusha vurugu zinazojitokeza.

Kutokana na tofauti zilizojitokeza kwenye mkutano huo uliisha bila ya maazimio yoyote katika kumaliza matatizo yaliyojitokeza, likiwemo la vitambulisho.

Mwema alishiriki katika kongamano lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) katika hoteli ya Manson na pia kukutana na viongozi wa vyama vya siasa na madhehebu ya dini katika Hoteli ya Bwawani.

Mchakato wa uandikishaji wapigakura katika daftari la kudumu linaendelea Unguja na Pemba huku likitawaliwa na matukio ya vurugu. Baadhi ya wananchi wanadai wamenyimwa vitambulisho hivyo na kukataliwa kuandikishwa kwa makusudi.

CHANZO: NIPASHE





Mwandishi wa The Guardian akamatwa Z`bar

29 09 2009

Mwandishi wa habari wa magazeti ya kampuni ya Guardian Ltd ofisi ya Zanzibar, Mwinyi Sadallah amekamatwa na maofisa wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na kupelekwa kituo cha polisi wakati akiwa kazini.
Mwinyi alikamatwa wakati akiwa katika kambi ya wagonjwa wa kipindupindu iliyofunguliwa kimyakimya eneo la Karakana, mjini hapa, baada ya ugonjwa huo kulipuka bila ya serikali kutoa taarifa rasmi kwa wananchi hadi jana.
Maofisa hao walimpeleka Mwinyi kituo cha Polisi cha Chumbuni, eneo ilipo kambi hiyo baada ya mwandishi huyo kukataa kukabidhi kamera yake anayoitumia kupigia picha za matukio mbalimbali ya habari anayoyafuatilia kila siku.
Kabla ya kumpeleka kituoni, maofisa hao wakishirikiana na Sheha wa Shehia ya Chumbuni ambaye jina lake halijapatikana, walimlazimisha mwandishi kuitoa kamera na kuwakabidhi lakini mwandishi alikataa ndipo mvutano ulipozidi.
Walipofika kituo cha Polisi, maofisa hao pamoja na sheha walitoa maelezo kwa uongozi wa kituo yaliyomtuhumu mwandishi kwa kosa la kupiga picha bila ya ridhaa ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Kuona hivyo, mmoja wa askari waliokuwepo kituoni alimwamuru mwandishi akabidhi kamera kwa kituo hicho amri ambayo mwandishi alitii baada ya kuhakikishiwa na polisi kuwa iko kwenye mikono salama.
Maofisa wa wizara waliandikisha maelezo ya tuhuma dhidi ya Mwinyi kwamba alitenda kosa na hivyo tuhuma hizo kusajiliwa kwa kumbukumbu namba CH/RB 1774/09 ya Septemba 26, mwaka huu.
Baada ya maelezo hayo, Mwinyi aliachiwa na kutakiwa kuacha nambari yake ya simu ya mkononi hadi Polisi watakapopata maelekezo baada ya kuwasiliana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Bakari Khatibu Shaaban alipoulizwa kama ana taarifa za kukamatwa kwa mwandishi huyo, alisema alikuwa anawasiliana na Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ili kujua kilichotokea kuhusu suala hilo.
Mwandishi wa habari wa Guardian jana alijipangia kazi ya kufuatilia taarifa za kufunguliwa kwa kambi ya wagonjwa wa kipindupindu baada ya kupata habari kuwa ugonjwa huo umeibuka ghafla na tayari kuna watu wamefariki dunia.
Baada ya kukusanya taarifa kutoka ndani ya wizara, alikwenda Chumbuni ambako kumekuwa kukiwekwa kambi kila ugonjwa huo unapotokea.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, watu watatu wamefariki na kuna wagonjwa wapatao 40 wanapatiwa huduma kutokana na ugonjwa huo ambao bado serikali haijatoa taarifa za kulipuka kwake.
Mkurugenzi wa Kinga katika wizara hiyo, Juma Rajab alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema ni kweli ipo kambi imefunguliwa lakini bado hawajathibitisha kama wagonjwa waliopo ni wa kipindupindu.
Hakutoa taarifa zaidi lakini baadaye jana wizara ilitoa taarifa na kuipeleka kwenye vyombo vya serikali pekee iliyoeleza kuwa wananchi wawe na tahadhari na mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha hivi karibuni kwa vile zinaweza kusababisha kulipuka kwa magonjwa ya mlipuko ukiwemo kipindupindu.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa kamati ya uongozi ya wizara hiyo inayojumuisha wataalamu wa fani mbalimbali za afya, ilikutana juzi chini ya Waziri Sultan Mugheiry na kujadili kwa kina mlipuko wa kipindupindu lakini ulitoka uamuzi kuwa kusitolewe taarifa hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Mohamed Jidawi mara kadhaa jana alieleza waandishi kwamba hana nafasi ya kuzungumza nao kwani yuko katika kikao.
Uchunguzi wa mwandishi wa habari hizi umebaini kwamba wagonjwa wengi wametoka maeneo ya Kihinani na Chumbuni ambako kumekuwa na shida ya maji ya kutumia majumbani na ni maeneo maarufu kwa kukumbwa na mazingira machafu.
Maofisa wa wizara ya afya waliozungumza na mwandishi wa habari hizi wanasisitiza kuwa kuna haja ya serikali kutoa taarifa rasmi ya mlipuko wa kipindupindu ili wananchi wachukue hatua za kujilinda na hatari za kupata ugonjwa huo.
Ni kawaida kwa maeneo mbalimbali ya mji wa Zanzibar kukumbwa na kipindupindu kila wakati wa msimu wa mvua lakini safari hii maofisa wa afya wanasema mazingira machafu na matumizi ya maji yasiyokuwa salama, yamechangia kujitokeza kwake.
Waandishi wawili wa habari hapa, Zeudi Muano na Salha Hamadi wamezuiwa kuingia ndani na kutakiwa kuondoka kwani hapakuwa na mwenye uwezo wa kuwapata taarifa zozote kuhusu wagonjwa waliomo ndani.
Walitakiwa kuwasiliana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kwa taarifa zaidi na waliondoka kwenye kambi hiyo ambayo kwa ndani yalionekana mahema yenye alama ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Zanzibar (JWTZ).

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI





Tunajiandaa kuivuruga amani ya Z’bar?

29 09 2009

Na Salim Said Salim

NI nani anayesema ukweli na yupi anadanganya? mkurugenzi wa Idara ya Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi au maelfu ya wananchi ambao hawajandikishwa?
Mkurugenzi anasema, tena kwa kujiamini kuwa maelfu ya watu na hasa katika kisiwa cha Pemba wameshapatiwa vitambulisho, lakini idadi kubwa wakiwemo wazee, wanalalamika na kula kiapo kwamba wamenyimwa hivyo vitambulisho.

Ni kawaida unapokwenda kila pembe ya kisiwa cha Pemba watu wanalalamika kwamba hawajapatiwa vitambulisho hivyo hawawezi kujiandikisha kuwa wapiga kura katika uchaguzi wa mwaka 2010 si kwa sababu nyingine bali isipokuwa ni Wapemba na hasa baada ya kutambulika kuwa ni wapinzani.

Kwa mujibu wa takwimu za mkurugenzi, zaidi ya theluthi mbili ya watu wa Pemba wanaostahiki kupewa vitambulisho wameshapatiwa. Kwa maana hiyo malalamiko yao ni uzushi, unafiki na uzandiki.

Kwa upande mwingine takwimu za uandikishaji zilizotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) zilionyesha kuwa hadi mwishoni mwa wiki iliyopita ni watu 852 tu ndio walioandikishwa katika jimbo la Ole ukilinganisha na watu wapatao 10,000 wanaotarajiwa kuandikishwa katika jimbo hilo.

Hivyo kweli inaingia akilini kwa watu wawe na vitambulisho na baadaye waamue kuhangaika na kuhimili kupigwa mabomu ya machozi wakati wanachokitaka wanacho majumbani mwao? Kama ni hivyo Wapemba watakuwa watu wa ajabu na kama tunatakiwa tuamini dhana kwamba Wapemba wana matatizo ya akili ni vyema kuambiwa wazi wazi na si kwenye mabano.

Lakini je ni watu wa kisiwa cha Tumbatu ambacho ni miongoni mwa ngome ya Chama cha Wananchi (CUF) nao akili zao zina mushkeli kama za Wapemba?

Nimejaribu kulifuatilia suala hili kwa undani na umakini. Nimefanya utafiti mitaani, majumbani na hata ndani ya daladala. Nimezipitia nyumba zaidi ya 50 katika miji ya Chake, Wete na vijiji vya jimbo la Ole.

Nilichokigundua ni kuwa zaidi ya theluthi mbili ya watu wenye umri wa zaidi ya miaka 18 hawana vitambulisho na wengi wamenieleza kuwa juhudi zao za kuvipata zimegonga ukuta, kama vile hawana haki hiyo.

Hizi ni zama za ukweli na uwazi na hapa kuna upande hausemi ukweli kati ya hizi mbili, ofisi ya Mkurugenzi wa Vitambulisho au mamia ya wananchi walioniambia wamenyimwa vitambulisho.

Ni hatari kwa jamii kuivumilia hali hii ambayo imechangia kuwapo kwa vurugu za kisiasa, hasa kisiwani Pemba na kusababisha baadhi ya nchi kutaka raia zao wasiende huko kwa vile si salama na hasa baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kueleza kwamba imegundua kuwepo magaidi kisiwani Pemba na kwa hiyo inaimarisha usalama, huku helikopta za polisi zikiranda randa katika anga ya kisiwa cha Pemba.

Kama mkurugenzi anataka jamii iamini anayosema basi atoe orodha ya watu na anwani za hao anaotuambia wamepatiwa vitambulisho na hapo ndipo tutajua mbivu na mbichi.

Zipo habari juu ya uwezekano wa watu kuandikishwa mara mbili au tatu ili wapige kura zaidi ya mara moja na kama orodha ya waliopatiwa vitambulisho ingewekwa hadharani ndipo tutaamini hakuna njama hizo.

Jambo jingine muhimu na linalofaa kutiliwa maanani ni kwamba kwa vile mtu haandikishwi kupiga kura bila ya kuwa na kitambulisho na wakati vinapotolewa hakuna wawakilishi wa vyama vya siasa hii inasababisha mchakato wa uandikishaji uchaguzi kuchukua sura ya kutekwa nyara na Idara ya Vitambulisho.

Ninasema hivi kwa sababu mwenye kitambulisho ndiye anayeandikishwa kuwa mpiga kura na kama kungetokea shaka au mizengwe basi mawakala wa vyama wangetarajiwa kuwepo katika vituo vinavyoandikisha watu wanaopatiwa vitambulisho ili watu wasiostahili au wanaotiliwa shaka kuwekewa pingamizi.

Lakini usiri uliopo katika utoaji wa vitambulisho unazusha shaka kubwa.

Hizi si zama za kuaminiana kwamba jambo fulani limefanywa kwa nia njema na kuitaka jamii ikubali. Kinachotakiwa ni uwazi kwa mambo yenye kutiliwa shaka, kama ilivyo katika hili zoezi la utoaji wa vitambulisho.

Kutokana na kisiwa cha Pemba kuwa ngome madhubuti na isiyotetereka ya chama cha CUF na CCM katika chaguzi zote za vyama vingi kupata chini ya asilimia 10 ya kura na chini asilimia nne katika baadhi ya majimbo, kumezusha shaka kwamba idadi ya Wapemba wanaoshiriki katika uchaguzi ujao inapunguzwa kwa zaidi ya 100,000.

Ili kuachana na dhana hii ni vema wahusika kuliweka hadharani daftari la vitambulisho na lile la wapiga kura.

Inawezekana usiri ndio mfumo ndani ya CCM, hasa yanapokuja mambo ya uchaguzi, lakini ni kosa na halikubaliki kwa uchaguzi wa kitaifa.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Salum Kassim, anasema sheria ya uchaguzi haiwalazimishi kuliweka hadharani daftari, lakini sheria hiyo pia haisemi daftari hilo linatakiwa liwe siri ya tume.

Kama hakuna mchezo mchafu kwa nini pawepo na usiri?

Wapemba wamekuwa wakidai wanabaguliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) katika kupewa nafasi za uongozi, elimu na ajira. Sasa kuwanyima haki ya kupiga kura kutaipa nguvu hoja yao kwamba SMZ inawabagua.

Huu usiri na uwongo, sijui kama ni wa Idara ya Vitambulisho au wa mamia ya watu wanaosema hawapewi vitambulisho, ndio utaozaa balaa ambalo dalili zake zimeanza kuonekana katika kisiwa cha Pemba.

Njia pekee ya kuhakikisha inapatikana amani ni kuufanya mchakato na utoaji wa vitambulisho na uandikishaji wapiga kura kuwa wazi na kila mwenye haki ya kupiga kura anashiriki katika uchaguzi.

Kama mambo hayo hayawezi kufanyika ni vema SMZ itangaze rasmi kuwa uchaguzi wa mwaka 2010 ni wa CCM na sio wa watu wote wa Visiwani.

Jamani, ninarudia, Wapemba nao ni watu. Wanachotaka si upendeleo au msaada bali haki yao ya kupiga kura. Wapeni au kuikataa kwao CCM ndio imekuwa nongwa?





Dk Bilal ahofia Zanzibar inaelekea kubaya

29 09 2009

Boniface Meena na Salma Said, Pemba

Waziri Kiongozi wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kipindi cha Dk Salmin Amour, Dk Garib Bilal amesema haelewi siasa za Zanzibar sasa zinaelekea wapi. Dk Bilal alisema hayo juzi katika mahojiano maalumu na Mwananchi Jumapili alipokuwa ametakiwa kuzungumzia vurugu zinazoendelea visiwani Zanzibar katika zoezi la uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la Kudumu. Alisema asingependa kusema lolote kuhusu jambo hilo kwa kuwa haelewi siasa za Zanzibar sasa zinaelekea wapi lakini, akashauri mamlaka husika kufanya kila liwezekanalo kudhibiti mambo yanayotokea sasa na kuharibu taswira ya Zanzibar. ”Sielewi siasa hizi zinaelekea wapi na siko katika nafasi nzuri kuzungumzia hilo kwa undani lakini, kwa kuwa kuna mamlaka za kisheria hali iliyopo inapaswa kushughulikiwa na mamlaka hizo,” alisema Dk Bilal.

Dk Bilal pia alisita kuzugumzia ripoti ya utafiti wa kampuni ya Synovate iliyomtaja kuwa miongoni mwa watu wachache wanaoweza kumrithi Karume kiti cha urais baada ya kumaliza muda wake mwakani akisema “hii ni ripoti ya wataalamu na ni maoni yao. Hiyo ni ripoti ya wataalamu na ni maoni yao, siyo wakati wa kuzungumzia hilo la urais ila ukifika wakati nitafanya hivyo”, alisema Dk Bilal.

Kauli ya Dk Bilal imekuja siku moja baada ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Pius Msekwa, kusema kwamba suluhisho la matatizo ya Zanzibar ni kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Msekwa aliyasema hayo alipokuwa akijibu swali aliloulizwa na kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC 1) kuhusu msimamo wa CCM kwa matatizo ya kisiasa visiwani Zanzibar. “Matatizo hayo yamekuwepo tangu wakati uliporudishwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, na kabla ya hapo yalikuwepo tangu Zanzibar ikitawaliwa na Mwingereza. Kwa mfano katika uchaguzi wa mwaka 1957, kulizuka vurugu kubwa na kusababisha mauaji ya watu 30 kwa hesabu ninayokumbuka,”alisema. Alisema ikichunguzwa kiini cha matatizo haya ni upande mmoja kutoridhishwa na ushindi wa mwenzake. Alisema kwamba mfumo wa utawala uliopo nao ni kikwazo cha amani.

“Mfumo wa mshindi kuchukua madaraka yote (winners take all) nao una matatizo. Ndiyo maana upande mmoja unabaki na malalamiko. Kwa hiyo cha msingi ni kugawana madaraka kwa pande hizo ili kupunguza jazba za watu. Tusingoje matatizo yatokee kama ilivyokuwa Kenya, tusingoje yafikie kama ilivyokuwa Zimbabwe, tuchukue tahadhari mapema,” alisema Msekwa.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Msekwa ilipokelewa kwa hisia tofauti na wananchi wa Zanzibar ambao kwa nyakati tofauti baadhi yao walionyesha kufurahishwa na wengine kuchukizwa nayo. Wasomi kadhaa, viongozi wa dini, wanasiasa na wananchi waliozungumza na Mwananchi Jumapili kwa nyakati tofauti katika visiwa vya Unguja na Pemba walisema Msekwa anachekesha kutambua hilo sasa. “Zanzibar mie nakwambia hawana ukweli hasa hawa CCM kwa sababu CUF wao wameshasema miaka mingi kwamba suluhisho na hatima ya siasa za hapa ni serikali ya umoja, lakini nakwambia hebu ajitokeze kiongozi mmoja tu wa SMZ tumsikie aseme kama alivyosema Msekwa itakuwaje au aunge mkono hoja hiyo…hakuna hata mmoja atakayethubutu kujitokeza” alisema kiongozi mmoja wa SMZ ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini.

Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) Azzan Khali Hamdan amesema sio kweli kama CCM ina nia ya kutaka kuundwa serikali ya mseto lakini, wamekuwa wakitoa kauli hizo kwa kujifurahisha. “CCM ni wanafiki wakubwa hawana ukweli juu ya kuundwa kwa serikali ya mseto kwa sababu kauli hiyo haikuanza leo, imeanza miaka mingi sana wao wanazungumza tu, lakini ukija utekelezaji kila mmoja huwa anatoa sababu zake kwa hiyo wanawafurahisha wahisani tu hawana ukweli hata kidogo” alisema Sheikh Azan.

Muumini wa kanisa la Kianglikana, Mabula Richard alisema kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, kutaiongezea nchi baraka kwani umoja ni agizo la Mungu. “Sisi katika dini yetu tunahimiza sana upendo na umoja na mimi nadhani wakati umefika katika visiwa vya Unguja na Pemba kufanywa maamuzi sahihi, ambayo yataleta umoja, lakini bahati mbaya sana viongozi wetu wamekuwa wasemaji sana hawana utekelezaji wa dhati” amesema kwa masikitiko makubwa.

Masoud Said Masoud ni Mkaazi wa Mwera Meli Sita anasema serikali ya mseto ni wimbo wa taifa na usanii wa kupindukia kwa kuwa maneno hayo yamezungumzwa miaka mingi bila ya serikali hiyo kuundwa. “Mie naona hao CCM kama wasanii wa kimataifa maana suala hilo mbona ni la muda mrefu linasemwa wala halitekelezwi, hebu siku moja wajaribu kufanya vitendo waache hayo maneno mengi imekuwa usanii kila siku ndio maana hatwendi mbele kimaendeleo kwa usanii wetu” amesema Masoud.

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa CUF, Ismail Jussa Ladhu amesema suala hilo linafahamika na sio geni katika chama chao na ndio maana kutokana na ushindani uliopo kati ya CCM na CUF katika visiwa vya Unguja na Pemba, CUF katika katiba yake tokea mwaka 1995 wameeleza suala la kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Amesema kwa kujua hilo CUF iliona suala hilo libakie katika katiba yake kwa kuwa hali ya visiwa vya Unguja na Pemba ina nguvu sawa, na chaguzi zote zinaonesha kuwa ushindani wa kisiasa ni mkubwa na hivyo chama kitakachoshinda lazima kiunde serikali ya umoja, ili kuleta umoja na mshikamano katika nchi. “Sisi tuseme nini kwa sababu wao CCM ndio waliokuwa hawataki umoja na kama wao wanataka ni wao watekeleze tu kazi rahisi sisi tumelisema hilo tokea 1995 na katika manifesto(ilani) yetu tumesema atakayeshinda katika uchaguzi aunde serikali ya umoja” amesema Jussa kwa njia ya simu ya mkononi.

Mwanasheria wa Kujitegemea Khaleed Said Masoud amesema serikali ya mseto sio hoja, muhimu ni mgao wa serikali yenyewe itakayoundwa, kwani nchini Kenya wameunda serikali ya umoja baada ya kutokea vurugu za uchaguzi, lakini matokeo yake imekuwa kugombeana madaraka jambo ambalo limesababisha baadhi ya viongozi kuachia ngazi kwa maslahi ya kitaifa.

Viongozi wa vyama vingi vya siasa Zanzibar wameunga mkono wazo la kuundwa kwa Serikali ya Mseto, lakini wamesisitiza uundaji huo uwe umevishirikisha vyama vingine vya kitaifa na sio CCM na CUF peke yake kwa kuwa migogoro inayotokea katika visiwa vya Unguja na Pemba husababishwa na vyama hivyo, kwa kuwa wanashauriana peke yao bila ya kupata nguvu ya tatu. “Tatizo kubwa linaloonekana hapa ni hivi vyama viwili na hasa hawa CCM, wao ndio wenye madaraka kwa hiyo wanawakandamiza wenzao na hawa CUF kwa kuwa wapo peke yao katika vikao, wanakuwa hawana nguvu kwa sababu si unajua CCM wababe na wataalamu wa ujanja? Lakini wakipata upinzani wa vyama vingine watatulia, lakini CUF peke yao hawawezi hawa ni wababe mno” amesema Mwanachama wa Chadema.

Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa CCM waliozungumza na Mwananchi Jumapili ambao wamekataa kutaja majina yao gazetini wamesema, wazo ni zuri, lakini kuunda Serikali ya Mseto itamlazimu Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad arejee madarakani na hilo kwa viongozi wa CCM Zanzibar haliwezi kukubalika. “Sisi bwana kama kutakuwa na kiongozi mwingine atakayeweza kuingizwa madarakani sawa, lakini kwa huyu Seif hatutaki kabisa apewe nafasi yoyote ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,”alisema mmoja wa wajumbe wa NEC huku akicheka.
Kiongozi wa Zamani wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar alisema kama kuna jambo muhimu kuliko yote lililobaki katika visiwa vya Unguja na Pemba ni kuundwa kwa Serikali ya Mseto na hakuna jambo jingine lolote ambalo litaweza kuinusuru na machafuko yanayokaribia katika uchaguzi mkuu ujao.

Siasa za Zanzibar zimechafuka hasa katika siku za hivi karibuni, baada ya kuanza kwa kazi ya kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura. Tayari Umoja wa Nchi za Ulaya (AU) kwa kushirikiana na balozi mbalimbali barani Ulaya na Marekani umeelezwa kusikitishwa na matatizo hayo yanayojitokeza kwenye zoezi hilo na kuiomba serikali iwe madhubuti katika kulisimamia.

EU imeeleza kuwa imesikitishwa na taarifa kuwa raia wengi wa Tanzania Bara, waliopo Pemba wanakabiliwa na vikwazo katika kupata vitambulisho vya ukaazi wa Zanzibar, ambavyo vimekuwa ni sharti muhimu kuweza kuandikishwa kama mpiga kura visiwani humo. Kwa upande wake Marekani ilienda mbali zaidi kwa kuwazuia raia wake kufanya safari zisizokuwa za lazima visiwani humo kwa usalama wao.

Hata hivyo alipotakiwa kuzungumzia vurugu hizo, mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) Jaji Lewis Makame alisema Nec haipaswi kulaumiwa bali lawama kama zipo zielekezwe kwa Zec. Alisema Zec inapaswa kubeba lawama zote kuhusu vurugu hizo kwa kuwa ina mamlaka kamili kiutendaji. Zoezi la uandikishaji wapiga kura visiwani Zanzibar limekumbwa na vurugu kubwa baada ya wananchi kudai kuwa, masharti ya kujiandikisha yaliyowekwa na Zec yanakiuka katiba ya visiwa hivyo. Sharti linalolalamikiwa na baadhi ya wananchi hao ni kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi kinachowafanya wasiokuwa nacho wanyimwe fursa ya kuandikishwa.