CUF kuongelea Daftari Jumapili

28 08 2009

Taarifa ya Mkutano na Vyombo vya Habari

Wapendwa Wanahabari,

The Civic United Front (CUF – Chama cha Wananchi) kinawaalika katika mkutano wake na waandishi wa habari utakaofanyika katika ofisi za Chama zilizoko Vuja, mjini Zanzibar, siku ya Jumapili ya tarehe 31 Agosti, 2009, saa 4.00 asubuhi. Mkurugenzi wa Uenezi na Mahusiano na Umma, Mhe. Salim Bimani atatoa taarifa maalum ya Chama kuhusu Uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura pamoja na hali ya jumla ya kisiasa nchini.

Kwa mwaliko, munaombwa nyinyi wenyewe ama wawakilishi wenu kuhudhuria katika mkutano huu ili kujua mtazamo na msimamo wa CUF katika masuala haya.

Pamoja na salaam za Chama

Umetolewa na kusambazwa na:

Dawati la Uchambuzi na Mahusiano na Vyombo vya Habari
Kurugenzi ya Uenezi na Mahusiano na Umma, CUF





SMZ iwache kushabikia na kuendeleza ubaguzi dhidi ya raia

28 08 2009

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 29 Agosti 2009

“SMZ iwache kushabikia na kuendeleza ubaguzi dhidi ya raia”

Kufuatia taarifa iliyochapishwa jana na gazeti la The Guardian juu ya hatua ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuwalazimisha Wazanzibari wenye asili ya Kingazija kwenda kujisajili rasmi kama raia wa Watanzania, Chama cha Wananchi (CUF) kinatoa tamko lifuatalo:

“Kwanza ni kiwango cha juu cha ubaguzi na upotofu kwa SMZ kuendeleza sera zake za kibaguzi dhidi ya Wazanzibari wa makundi tafauti. Misingi hii ya kibaguzi ilianza kujengwa dhidi ya Wazanzibari wenye asili ya Pemba kwa kuwanyima fursa na haki kadhaa za msingi zikiwemo za kielimu, kiuchumi na kisiasa; na sasa baada ya kwisha kuwabagua Wapemba, SMZ inawageukia Wangazija. Serikali ya kweli ya watu haisimamii ubaguzi na utengano, bali mapenzi baina ya watu wake na mshikamano.

“Pili, kisingizio kinachotolea na SMZ kwamba huko ni kufuata sheria iliyotolewa kwa njia ya Dikrii ya Rais tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Zanzibar na kwamba eti kwa kuwa hiyo ni sheria ambayo haijafutwa kwa hivyo haijatanguka, ni upotofu mwengine wa hali ya juu. Kwanza ilikuwa ni kosa kwa Rais Abeid Karume kutoa tamko hilo ambalo lilikuja kuwa dikrii, kwani aliingiza ugomvi wake binafsi na baadhi ya Wazanzibari waliokuwa na asili ya Kingazija katika masuala ya utawala na khatima ya wananchi. Pili, inasemwa kuwa Mapinduzi yalifanywa kwa lengo la kuwaunganisha Wazanzibari na kufuta misingi ya kibaguzi; kwa hivyo hiyo ilikuwa ni Dikrii iliyokwenda kinyume na misingi ya Mapinduzi na basi ilikosa uhalali tangu mwanzoni.

“Tatu, inaonekana uongozi wa SMZ hauijui hata hiyo jamii ya Wazanzibari unayoitawala. Haijifunzi ukweli kwamba ni mchanganyiko wa asili, makabila, mataifa na historia tafauti ndio ulioifanya Zanzibar kuwa Zanzibar waliyoipata wao (SMZ) kuitawala. Wanapowabagua watu ambao wameleta mchango mkubwa wa kuijenga Zanzibar kijamii, kielimu, kiutamaduni na kisiasa, inafaa Wazanzibari wajiulize tena na tena juu ya aina ya uongozi uliopo madarakani. Ni lazima serikali hii iwache kushabikia na kuendeleza ubaguzi dhidi ya raia.”

Imetolewa na:

Salim Bimani
Mkurugenzi wa Uenezi na Mahusiano na Umma, CUF





CCM Zanzibar washtushwa na matokeo ya utafiti

12 08 2009

Salma Said, Zanzibar

BAADHI ya wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM Zanzibar, wameshtushwa na matokeo ya utafiti wa masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi yanayoonyesha kuwa katibu mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad anapewa nafasi kubwa ya kushinda kiti cha urais wa visiwa hivyo mwakani.

Ripoti hiyo iliyotolewa juzi na kampuni ya Synovate, pia inaonyesha kuwa waziri kiongozi wa zamani wa Zanzibar, Gharib Mohammed Bilal wa CCM ndiye anayefuatia kwa karibu Maalim Seif kumrithi Rais Amani Abeid Karume, ambaye anamalizia muda wake wa miaka 10.

Ingawa kamati hiyo kuu ya CCM upande wa Zanzibar ilikuwa ikiendelea na kikao chake cha kawaida jana, ripoti ya matokeo ya utafiti huo haikujadiliwa, lakini wajumbe walioongea na Mwananchi nje ya ukumbi wa mkutano wa ofisi kuu ya CCM Kisiwandui, walionekana kutofautiana.

Wengi walionyesha kushtushwa na matokeo yanayompa nafasi kubwa Bilal kwa upande wa CCM, wakisema chama hicho hakiwezi kumteua mtu kwa sababu ya umaarufu wake.

“Kwanza mimi ni maarufu kuliko yeye kwa sababu mimi nimeshawahi kushika nyadhifa mbalimbali katika chama chetu nikianzia chini hadi juu,” alisema mjumbe mmoja nje ya ukumbi wa mikutano wa chama hicho ulio Kisiwandui.

“Nimeanza siasa tangu nikiwa mdogo. Tumuulize yeye (Bilal) anatoka wapi na amefanya nini katika chama,” alihoji mjumbe huyo ambaye yeye pia anatajwa kutaka kuwania urais Zanzibar.

Alisema licha ya Bilal kuwahi kuwa waziri kiongozi na kwa sasa kuwa mjumbe wa NEC, uzoefu wake katika siasa ni mdogo na pia hana jambo kubwa aliloifanyia CCM.

Mjumbe mwingine wa NEC ambaye ni waziri katika Serikali ya Muungano alisema haiwezekani utafiti umpe nafasi kubwa Dk. Bilal, ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma.

“Wewe ngoja huo uchaguzi uje utashangaa kitakachotokea,” alisema waziri huyo ambaye kama wengine aliomba jina lake lihifadhiwe.

Katika utafiti huo, Synovate walihoji ni kiongozi gani ambaye wananchi wa Zanzibar wanampa nafasi ya urais baada ya Karume kustaafu mwakani na asilimia 28 ilionyesha kuwa ni Maalim Seif, wakati asilimia 24 ilionyesha ni Bilal. Waziri kiongozi wa sasa, Shamsi Vuai Nahodha alipata asilimia 10 na Makamu wa Rais Mohamed Shein alipata asilimia 2.

“Sidhani kama huo utafiti upo sawa kwa sababu kwanza umefanywa wapi, katika mazingira gani na akina nani waliohojiwa maana inawezekana ukaenda sehemu moja; ukawauliza watu 1,000 kuhusu mtu mmoja ambaye ni wa kwao na ana nafasi kubwa. Unategemea watu hao wakuambie nini, hawamtaki,” alihoji mmoja wa wajumbe wa NEC Zanzibar.

Mjumbe mwingine alisema kuwa, suala la umaarufu halina nafasi katika siasa za Tanzania kwa kuwa huko nyuma imeshawahi kutokea mtu asiyekuwa maarufu kushinda na kuchaguliwa kuwa rais kuliko aliyekuwa maarufu.

“Ngoja nikuambie unakumbuka mgombea wa urais wa Zanzibar mwaka 2000 alikuwa nani? Unakumbuka kama Dk Bilal ndiye alikuwa maarufu, je, alipata?” alihoji mjumbe huyo.

“Na je, nani alitarajia kama Amani Karume atakuwa rais? Yeye si aliangushwa kwa kura nyingi sana na watu pia hawakumtaka, lakini je, hakuwa rais? Kwa hivyo kigezo cha kuwa maarufu kisitumike kabisa!”

Bilal pia alichukua fomu za kuwania urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM mwaka 2005, lakini alienguliwa katika uteuzi wa mwisho mjini Dodoma kutokana na utamaduni wa chama hicho wa kumwachia mshindi wa kiti cha urais amalizie kipindi chake cha miaka 10.

Mwenyekiti wa Vijana wa CCM, Hamad Masauni Yusuf alisema ingawa hajui vigezo vilivyotumika katika utafiti, anaamini kuwa wananchi wengi bado wana kasumba kwamba CUF bado ina ngome kubwa kisiwani Pemba wakati hali sasa ni kinyume.

Alisema sio kweli kwamba, CUF wana nafasi kubwa ya kushinda urais kwa Zanzibar na pia huko Pemba na kwamba hali imebadilika kwa sasa akidai kuwa, wananchi wengi wamekata tamaa na viongozi wao na hivyo, CCM ina nafasi kubwa ya kushinda.

“Nimetoka Pemba hivi karibuni na hali ilivyo sasa sivyo kama ilivyokuwa awali,” alisema Masauni.

Hata hivyo, Masauni alisema CCM haiwezi kumteua mtu asiyekuwa safi na kwamba lazima awe na sifa zinazokubalika.

Aliyekuwa Afisa katika ubalozi wa Tanzania nchini Geneva, Mohammed Yusuf alisema tafiti zinazofanywa katika nchi za Afrika huwa zinatumia vigezo vya nchi za Magharibi, jambo ambalo alisema halitoi picha halisi ya kile kinachokusudiwa.

Jijini Dar es salaam, wasomi na wanasiasa walikuwa na maoni tofauti kuhusu utafiti huo wakizungumzia sababu za Rais Jakaya Kikwete kukubalika huku watendaji wake wakionekana hawafai.

“Katika siasa, hili ni tatizo kubwa na linatakiwa litafutiwe ufumbuzi kwani hatuwezi kuangalia uzuri wa mtu mmoja katika taasisi nzima. Taasisi ni muhimu kuliko mtu mmoja kwani mtu huyo anaweza kuondoka na kuiacha taasisi,” alisema mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Audax Kweyamba.

Lakini alisema inashangaza kuwa mfumo mzima wa uongozi kuanzia bunge na baraza la mawaziri wanakabana koo, isipokuwa pale inapofikia suala linalomhusu rais ambalo hufanya pande zote kumtetea, jambo linalomfanya awe maarufu.

“Haiwezekani wabunge na mawaziri wakabane koo, lakini inapofikia suala linalomhusu rais, wanamlinda na kumfanya kama malaika wakiwa na lengo maalumu na sio kufichua uovu wake,” alisema Kweyamba.

Mhadhiri mwingine wa UDSM, John Jingu alisema matokeo ya utafiti huo yanategemeana na watu waliohojiwa.

Hata hivyo, utafiti huo katika kipengele cha viongozi wa kisiasa uliangalia umaarufu wa viongozi na ulihoji watu 2,000 walio Bara na Visiwani, wakati katika kipengele cha urais wa Zanzibar uliangalia nani mwenye nafasi kubwa ya kumrithi Rais Karume.

Aidha, baadhi ya wahadhiri ambao hawakutaka kutajwa majina yao walisema upande wa upinzani, hasa Chadema, umepata asilimia kubwa kutokana na kuibua kashfa nyingi za mikataba mibovu bungeni na kuwataja mafisadi.

Nao viongozi waandamizi wa vyama vya CCM, Chadema, TLP na CUF wameeleza wazi kwamba, hawakubaliani na mfumo uliotumika katika kupata matokeo ya utafiti huo.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM- Itikadi na Uenezi, John Chiligati alisema anakubaliana na utafiti huo kuonyesha kwamba, Rais Kikwete anaongoza kwa umaarufu, lakini akasema watafiti wamepotoka upande wa Zanzibar, ambako katibu mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad ameonekana ndiye anayeweza kushinda uchaguzi wa mwaka 2010.

Chiligati, ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema ni sahihi kwa utafiti huo kuonyesha kuwa Rais Kikwete anaongoza kwa kukubalika, lakini akapingana na kipengele cha mrithi wa Rais Karume akisema CCM imefanya makubwa visiwani humo.

“CCM imefanya mengi mazuri Unguja na Pemba na ukienda kumuuliza Mzanzibari yeyote, atakueleza safari hii CCM wameleta mabadiliko,” alisema Chiligati ambaye ni mbunge wa Manyoni Mashariki.

Alitaja miongoni mwa mambo ambayo anafikiri yanampa nafasi kubwa ya ushindi mgombea yeyote watakayemsimamisha kuwa ni ujenzi wa barabara, usambazaji wa maji safi na umeme.

Mwenyekiti wa vijana Chadema, John Mnyika, alisema utafiti huo haukuzingatia suala la ufisadi wala rushwa na kwamba kama ungezingatia masuala hayo, CCM isingepata kura za juu.

“Hii taasisi haikutenda haki kwani maswali mengi katika utafiti wao yalikuwa yanahusu elimu, jambo ambalo lazima CCM ipate kura nyingi, lakini ingegusia masuala ya rushwa na ufisadi, hali ingekuwa nzuri zaidi kwa vyama vya upinzani na haki ingeonekana kutendeka pia,” alisema.

Alisema taasisi zinatakiwa kujitokeza kwa wingi ili kufanya utafiti wa kina wa kura za maoni, na sio kutegemea zile zinazotumiwa na serikali ambazo zinaipandisha juu bila ya kuzingatia ukweli uliopo.

Mkurugenzi wa uenezi na mawasiliano wa CUF, Ashura Mustafa alisema matokeo hayo yanalenga kuifanya jamii ya Kitanzania iamini kuwa, CUF ina nguvu upande wa Zanzibar pekee na pia kuwafanya wananchi wa visiwa hivyo wasiwe na imani na Prof Lipumba.

“Wameonyesha kuwa, Maalim Seif ndiye anayekubalika kwa upande wa Zanzibar ili wananchi wasiwe na imani na rais wetu mtarajiwa Lipumba, lakini pia wanataka kuonyesha kuwa CUF inakubalika Zanzibar tu ili hata wananchi wasimchangue mgombea wetu kwa upande wa urais,” alisema Mustafa.

Alisema CUF ina nguvu kubwa ya kisiasa kwa upande wa Tanzania Bara kutokana na kuwa na uongozi kuanzia ngazi ya mtaa mpaka taifa tofauti na Chadema ambayo alisema haina uwakilishi kuanzia ngazi za chini.

Pia alipinga ripoti hiyo akidai kuwa idadi ya watu 2,000 waliohojiwa haiwezi kuwakilisha idadi ya Watanzania zaidi ya milioni 40.

Naye mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alichukulia matokeo hayo ya umaarufu kuwa ni kielelezo cha wanasiasa watakaogombea urais mwaka 2010 na hivyo kuielezea kampuni hiyo ya utafiti kuwa si wakweli kwa kuwa ameshatangaza kuwa hatagombea urais mwakani.

“Kwanza wamenidhalilisha kwa kuwa nimeshatangaza kutokugombea tena urais na hata chama changu kinajua hilo, sasa inakuwaje tena leo utafiti umhusishe Mrema?” alisema na kuunga mkono asilimia za Kikwete akisema kuwa amejitahidi kupambana na ufisadi.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz





Maalim Seif yuko juu urais wa Zanzibar

12 08 2009

Na Kizitto Noya na Hadija Jumanne

KATIBU Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, anapewa nafasi kubwa ya kushinda kiti cha urais visiwani Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani, kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa kampuni ya Synovate.

Synovate, ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kama Steadman Group Tanzania, imesema katika matokeo ya utafiti huo uliofanyika miezi mitatu iliyopita kwa kuwahoji wananchi wa Zanzibar pekee kuhusu urais wa visiwa hivyo, mtu anayeweza kumfuatia Maalim Seif ni aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Gharib Mohammed Bilal.

“Watu wanaotarajiwa kumrithi Rais Karume baada ya kustaafu mwaka 2010 ni Maalim Seif anayepewa asilimia 28 na Gharib Mohammed Bilal asilimia 24,” alisema meneja msaidizi wa kampuni hiyo, Aggrey Orio.

Utafiti huo pia umeonyesha kwamba, Waziri Kiongozi wa sasa, Shamsi Vuai Nahodha, amepata asilimia 10 wakati anayeshika nafasi ya nne ni Makamu wa Rais, Dk Mohamed Shein, aliyepata asilimia 2.

Maalim Seif, ambaye alikuwa waziri kiongozi kabla ya kupata misukosuko iliyomfanya awekwe kizuizini, amekuwa akigombea urais wa visiwa hivyo tangu mwaka 1995 wakati uchaguzi wa vyama vingi uliporejeshwa, lakini amekuwa akishindwa kwa asilimia chache.

Tofauti hizo ndogo za ushindi ambao umekuwa ukienda kwa mgombea wa CCM, zimekuwa zikisababisha CUF kukataa matokeo na wakati mwingine kusababisha vurugu kama za mwaka 2001 zilizosababisha watu zaidi ya 26 kupoteza maisha.

Bilal amekuwa akipanda chati katika siasa za Zanzibar na mwaka 2005 alichukua fomu kupambana na rais wa sasa wa Zanzibar, Amani Abeid Karume lakini jina lake likaondolewa kwenye vikao vya juu vya CCM, ambayo ina utamaduni wa kumwachia mshindi wa kiti cha urais kutetea kipindi kingine cha miaka mitano.

Nahodha na Dk Shein hawatajwi sana kwenye kinyang’anyiro cha urais wa visiwa hivyo ambao huwa na upinzani mkali baina ya CCM na CUF.

Hata hivyo, katika utafiti huo idadi kubwa ya watu walioulizwa swali kuhusu mtu maarufu baada ya kustaafu kwa Rais Karume, hawakuwa na jibu.

Utafiti huo wa Synovate unaonyesha kuwa, asilimia 24 ya watu waliohojiwa, hawakuwa na jibu katika swali hilo.

Kwa kuangalia umaarufu wa viongozi wa kisiasa, utafiti huo uliofanywa nchi nzima ukiwashirikisha watu 2,000, unaonyesha kuwa Rais Jakaya Kikwete anaongoza kwa asilimia 66 akifuatiwa kwa mbali na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye amepata asilimia 11.

Mwenyekiti huyo wa Chadema amempiku kwa umaarufu mwenyekiti wa CUF, Ibrahim Lipumba, ambaye katika Uchaguzi Mkuu uliopita alishika nafasi ya pili.

Prof Lipumba, ambaye atakuwa akigombea urais kwa mara ya tatu iwapo atapitishwa na chama chake, ameshika nafasi ya tatu kwa umaarufu akiwa amepata asilimia tisa, huku mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema akiambulia asilimia moja sawa na mwenyekiti wa UDP, John Cheyo.

Utafiti huo umebaini kuwa kiwango cha demokrasia nchini kimeongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na Watanzania kujua majimbo yao ya uchaguzi na wawakilishi wao bungeni, huku CCM ikiongoza vyama vingine kwa kufahamika zaidi kwa wananchi.

“Asilimia 67 wanaifahamu na kuipenda CCM kutokana na sera, uongozi wake na imani kwamba ni chama cha kidemokrasia,” alisema Orio na kutaja vyama vinavyoifuatia CCM kuwa ni Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na TLP.

Utafiti huo uliofanywa kupata maoni ya watu kuhusu masuala ya jamii, siasa na uchumi, umebaini kuwa rushwa nchini imeongezeka na kwamba maofisa wa Jeshi la Polisi na Idara ya Mahakama, ndio wanaoongoza kwa kuomba na kupokea rushwa.

“Taasisi za dini, vyombo vya habari, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na Bunge, ndiyo yanayofuatia kwa utaratibu huu,” alisema Orio.

Alisema katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, takriban mtu mmoja kati ya watu kumi waliopata huduma kwenye taasisi za serikali ambayo ni sawa na theluthi mbili, walihonga na rushwa ilifikia hadi Sh10,000.

Alisema utafiti umebaini kuwa asilimia 13 ya wananchi walieleza katika utafiti huo kuwa, hawana imani na Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), kutokana na wizi wa mitihani huku asilimia 12 wakisema kuwa hawana imani na taasisi za fedha kutokana na riba kubwa.

Taasisi nyingine zilizonyoshewa kidole katika utafiti huo ni vyama vya upinzani, Tume ya Uchaguzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

“Watanzania wengi vijijini wanamuunga mkono Rais Kikwete kuliko mjini, lakini hawajaridhika na jinsi ambavyo serikali inashughulikia mambo mbalimbali,” alisema.

Katika kuangalia masuala ya jinsia katika kinyang’anyiro cha urais, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk Asha Rose Migiro ndiye aliyepewa nafasi kubwa ya kuwa rais akifuatiwa na mbunge wa jimbo la Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, wakati mwanasiasa mkongwe, Getrude Mongella na Waziri Hawa Ghasia wamepewa nafasi ndogo.

Watu waliulizwa swali kwamba, “kwa kuangalia wanawake na demokrasia, kama Tanzania ingetakiwa kuwa na rais mwanamke, ni nani kati ya viongozi wa kitaifa anaweza kuchaguliwa kuiongoza Tanzania.

Asilimia 36 ya walioulizwa walimtaja Migiro, wakati asilimia 20 walimtaja Kilango, asilimia 10 walimtaja Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Margareth Sitta. Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa, Anna Tibaijuka alipewa asilimia 5, akifuatiwa na Sofia Simba, huku Mongella, Salma Kikwete na Ghasia wakiambulia asilimia 2.

Katika swali hilo, asilimia 19 ya waliohojiwa, hawakuwa na jibu.

Asilimia 71 ya watu walioulizwa kama wanawake nchini wana uwakilishi mzuri kwenye uongozi wa kitaifa, walikubali wakati asilimia 25 walikataa na asilimia 12 haikuwa na jibu.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz





Mafuta ya Zanzibar yampalia Khatib

12 08 2009

Exuper Kachenje

WAZIRI wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Muhammed Seif Khatib, amesema hatazungumzia tena uamuzi wa Zanzibar kuliondoa suala la mafuta na gesi katika Muungano.

Waziri Khatib alitoa kauli hiyo jana alipoombwa kuzungumzia kama hatua hiyo iliyofikiwa wiki iliyopita si ya kuchokonoa muungano wa Tanzania.

“Suala hilo sitaki kulinzungumzia, sitazungumzia tena kwa sasa, wewe andika hivyo hivyo,” alisema Khatib.

Hata baada ya kuulizwa kuwa haoni kutolitolea maelezo suala ni kuwanyima Watanzania haki ya kupata taarifa muhimu na msimamo wake akiwa waziri mwenye dhamana na Muungano, Khatib aliendelea kusisitiza kuwa hatalizungumzia suala hilo.

“Nimesema sitaki, nimeamua hivyo, ndo nishasema basi,” alisema Waziri Khatib.

Wiki iliyopita, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ilitangaza kuliondoa rasmi suala la mafuta na gesi katika orodha ya mambo ya Muungano, hatua iliyoibua mjadala kutoka kwa watu wa kada mbalimbali wakiwemo wabunge na wanasiasa.

Uamuzi huo wa SMZ, ulitangazwa katika kikao cha Bajeti cha Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kinachoendelea mjini Zanzibar.

Msimamo huo ulitangazwa na Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi wa serikali hiyo Mansour Yussuf Himid.

Katika maelezo yake, waziri huyo alisema uamuzi huo ni kauli halali ya SMZ kwa kuwa umeafikiwa na Baraza la Mapinduzi katika kikao chake cha Juni 9 mwaka huu.

Mansour aliwaambia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa suala hilo, kuingizwa katika mambo ya Muungano mwaka 1968 haikuwa muafaka na kuwa Katiba ya Zanzibar Ibara ya 2 (1) inaeleza kuwa suala la usimamizi wa mafuta na gesi asilia, linapaswa kusimamiwa na SMZ.

Alifafanua kuwa uamuzi huo ulifikiwa ili kulinda alichokiita maslahi ya wananchi wa Zanzibar, jambo ambalo hata hivyo, linapingana na agizo la Rais Jakaya Kikwete la Aprili mwaka huu, katika salamu zake miaka 45 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Katika hotuba hiyo Kikwete alisema,”sioni mantiki ya kubishania kitu ambacho hivi sasa hatunacho na huenda tusikipate. Nawaomba viongozi wenzangu tusilizungumzie suala hili kana kwamba kuna uhakika wa kupatikana mafuta au yameshapatikana na kwamba kilichobakia mbele yetu ni kuzungumzia namna ya kugawana papato yake.”

Wakati hayo yakiendelea Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Samuel Sitta alikaririwa na vyombo vya habari akisema Bunge la Jamhuri ya Muungano ndilo lenye mamlaka ya kuondoa vifungu vya katiba Jamhuri ya Muungano na siyo chombo kingine chochote.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz