Taarifa ya Awali Zoezi la Uandikishaji Wilaya ya Micheweni – Siku ya 3
Julai 8, 2009
“Kasi ndogo ya uandikishaji”
Katika muendelezo wa taarifa hizi za namna zoezi la uandikishaji wa wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Zanzibar lililoanza tarehe 6 Julai, 2009 wilaya ya Micheweni, leo tunawatumieni yaliyojiri jana, ambayo ilikuwa ni siku ya tatu ya uandikishaji na siku ya mwanzo ya kuanza kubadilisha shahada za wapiga kura, kutoka kongwe na kupata mpya.
Jumla ya watu waliokubaliwa shahada zao ni 1,115 na waliokataliwa ni 48. Sababu za waliokataliwa kubadilishiwa zinalingana na sababu za wale waliokataliwa kuandikishwa kabisa katika siku ya kwanza na ya pili, hasa ile ya kutokuwa na kitambulisho cha Mzanzibari, ambapo limefanywa kuwa ni suala la lazima na Tume ya Uchaguzi (ZEC) kwa Mzanzibari kupewa haki yake ya kupiga kura hata kama atakuwa na vielelezo vyengine. Wengi wa waliokataliwa jana ni wale waliokuwa na shahada za kupiga kura za mwaka 2005 lakini hawana vitambulisho. Itakumbukwa kwamba sharti la kuwa na kitambulisho ili kuwa mpiga kura halikuwekwa mwaka 2005 kwa hivyo kuna uwezekano mkubwa kwamba watu wengi walikwenda kupiga kura bila ya kwanza kupatiwa vitambulisho hivyo vya Mzanzibari.
Tatizo jengine ni la kasi ndogo ya uandikishaji kwa siku ya jana na leo. Maafisa wa ZEC wanatoa sababu kwamba kompyuta zao hazina chaji, yumkini kutokana na tatizo sugu la umeme kisiwani Pemba, lakini sisi katika CUF tunaamini hiyo ni njama nyengine inayolenga kuhakikisha kuwa siku tatu za kubadilisha shahada zinamalizika huku maelfu ya wapiga kura ikiwa imetengwa kando kutokana na sababu ya muda.
Haingii akilini kwamba ZEC haikuwa ikijua kuhusu tatizo la umeme Pemba na ikawa haikujitayarisha kukabiliana nalo.
Tutaendelea kuwatumieni taarifa kadiri zinavyojitokeza na kutufikia.
Imesambazwa na:
Salim Bimani
Mkurugenzi
Uenezi na Mahusiano na Umma
CUF
Kwa maelezo zaidi, tafadhali pia 0777 414112 au tembelea http://hakinaumma.wordpress.com
Maoni