Uandikishaji Wapiga Kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Wilaya ya Micheweni: Taarifa ya Awali – Siku ya Kwanza 7 Julai, 2009
“Watu 830 wanyimwa haki ya kuwa wapiga kura katika siku ya kwanza”
Zoezi la uandikishaji wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Zanzibar limeanza jana katika wilaya ya Micheweni. Hata hivyo, tayari kumeshaonekana dalili za wazi wazi kwamba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa kushirikiana na masheha na Idara ya Vitambulisho watatekeleza azma yao ya kuwazuia wapiga kura wengi kadiri watakavyoweza wasipate haki yao hiyo.
Tathmini ya jana inaonesha kwamba katika Jimbo la Konde, ambako uandikishaji huo umeanza, watu walioandikishwa kwenye vituo sita vya jimbo hilo ni 133 tu huku wengine 830 wakikataliwa kuandikishwa kwa sababu ya kutokuwa na vipande vya Mzanzibari Mkaazi. Wengi wa watu hao wana vielelezo vyengine vinavyothibitisha uzawa na ukaazi wao katika jimbo hilo na kwamba tayari wamefikisha umri wa miaka 18, vikiwemo vyeti vya kuzaliwa.
Zoezi la jana lilikuwa ni kutoa vipande vipya vya kura, ambalo linatarajiwa kuendelea leo. Na siku tano kuanzia kesho itakuwa ni kubadilisha shahada za wapiga kura. Lakini kwa muendelezo wa kile sisi tunachokiita ‘utatu usio mtakatifu’ (trinity of the demons) kati ya SMZ kupitia masheha wake, Idara ya Vitambulisho na ZEC, ni wazi kwamba lengo ni kuwakata wapiga kura wengi zaidi kila siku. Hali ikienda hivi ya kukata wapiga kura 830 kwa siku kwa siku 35 za uandikishaji katika wilaya ya Micheweni, basi mwisho wa uandikishaji jumla ya 29,050 watakuwa wamenyimwa haki yao wa kuwa wapiga kura.
Hesabu hii inaweza kushuka kutoka na mwenendo wa siku za uandikishaji, lakini haitashuka chini ya wapiga kura 20,000. Na kwa kuwa Pemba ina wilaya nne, kukata wapiga kura 20,000 kwa kila wilaya kuna lengo la kuwanyima kiasi ya Wazanzibari wa kisiwa hicho 80,000 kukosa haki hiyo hadi kumalizika kwa zoezi.
Tunatuma taarifa hii ikiwa ni indhari ya namna hali inavyoendelea na makisio ya hali inakoelekea. Tutakuwa tukituma taarifa kila siku hadi kumalizika kwa zoezi.
Imesambazwa na:
Kurugenzi ya Uenezi na Mahusiano na Umma
CUF
Maoni