WAKATI wananchi wa Pemba wakiwa ndiyo wanaandikishwa katika daftari la kudumu la wapigakura, kuna wasiwasi uliokwishaonyeshwa kwa baadhi ya wadau wa siasa.
Katika moja ya habari katika ukurasa wa tatu wa gazeti hili, toleo la jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, alinukuliwa akieleza wasiwasi wake juu ya kuanza kwa uandikishaji huo, huku kukiwa na malalamiko kuwa kuna watu karibu 50,000 hawajapewa vibali vya ukaazi, vinavyotolewa na viongozi wa Serikali za Mitaa (masheha).
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, urasimu wa masheha ndiyo unaowakwamisha wananchi kupata vitambulisho hivyo vya ukaazi, hivyo kukosa sifa ya kujiandikisha katika daftari hilo la kudumu.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Suleiman Othman Nyanga, alinukuliwa akisema kuwa hakuna wananchi walionyimwa vitambulisho na hadi sasa, ni mtu mmoja pekee aliyekata rufaa kwa kunyimwa vitambulisho vya ukaazi.
Lakini pamoja na malalamiko hayo, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Salum Kassim Ali, alinukuliwa na gazeti hili akisema kuwa, pamoja na malalamiko hayo, zoezi la uandikishaji litakwenda kama lilivyopangwa.
Sisi wa Tanzania Daima, tukijua nafasi yetu katika jamii, tunaamini kuwa kinga ni bora kuliko tiba, hasa katika suala hili ambalo ni ishara kuwa tuko katika maandalizi ya chaguzi za serikali za mitaa, udiwani, ubunge na urais.
Tunasema hivyo hasa tukifahamu kuwa, baada ya uchaguzi kufanyika na matokeo kutangazwa, si kelele za kuyapinga pekee zitakazotokea, bali hata uvunjifu wa amani kwa wafuasi wa vyama kupinga uonevu wanaofanyiwa.
Kutokana na hali ya kurushiana maneno ambayo imeanza kujitokeza, tunaamini kuwa hiyo ni ishara ya mgogoro utakaotokea mara baada ya kufanyika uchaguzi wowote kupitia majina yanayoandikishwa sasa na ZEC.
Tulidhani kuwa, kiongozi huyo wa ZEC asingepuuza tuhuma hizo na badala yake angewasiliana na wahusika kwa lengo la kujiridhisha kwanza iwapo kuna ukweli ama la.
Kwa kufanya hivyo, tunaamini kuwa, wasiwasi wa CUF utakuwa umeondoka hata kukosa sababu yoyote kuhusu kutoandikishwa kwa baadhi ya wapigakura kutokana na urasimu wa masheha.
Aidha, tunaamini kuwa endapo ZEC itakubali na kuyashughulikia madai hayo ya CUF, ni dhahiri kwamba imani itajengeka kwa vyama vya siasa na hata kuyapokea matokeo ya uchaguzi kwa moyo mweupe kwa kuwa wanajua idadi ya watu waliojiandikisha.
Ikumbukwe kuwa, pamoja na vyombo vya usalama kuwa nguzo muhimu ya kusimamia amani ya nchi, sisi tunaamini kuwa hata tume za uchaguzi, hasa kwa nchi za bara la Afrika, zina nafasi kubwa ya kuhakikisha kuwa amani inaendelea kuwepo na kudumu.
Tukichukua mfano wa karibu kwa nchi jirani ya Kenya, mtu anapotaja chanzo cha machafuko ya kisiasa yaliyoikumba, Tume ya Uchaguzi nchini humo huwa haikwepeki kutajwa. Kwa nafasi iliyopo, tume ya uchaguzi, tungetarajia kuwa ingekuwa na wepesi wa kufuatilia suala hilo.
Tunaitaka ZEC kutokaa kimya katika suala hili endapo inataka kujenga imani na kupunguza malalamiko mara baada ya uchaguzi kufanyika.
Kwa mantiki hiyo, kwa malalamiko ya Seif, mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa pamoja na chama chake, CUF, ZEC inatakiwa kuchukua hatua mara moja kuhakikisha kuwa kila mtu anapata haki yake ya msingi ya kuwepo katika daftari la kudumu.
*Chanzo: Tahriri ya Tanzania Daima, Julai 7, 2009
Maoni