Na Muhibu Said
Imekuwa ni kawaida sasa, kila unapofanyika mchakato wa uchaguzi wananchi wa visiwa vya Pemba, vinavyojumuisha Pemba yenyewe, Kojani na Panza kuishi kwa hofu.
Januari 26 na 27, 2001 bado iko vichwani mwa wananchi hawa kutokana na mauaji ya zaidi ya watu 30, huku wengine wakipata vilema vya maisha wakati wakipinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2000.
Matukio hayo ya kusikitisha, yalitokea miezi michache baada ya hali tete visiwani humo iliyotokana na matokeo ya chaguzi mbalimbali zinazotulizwa kwa miafaka butu.
Muafaka wa kwanza ulisainiwa mwaka 1999 na vyama vya CCM na CUF chini ya uenyekiti wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Emeka Anyauko, aliyewakilishwa na mjumbe wa jumuiya hiyo, Dk. Moses Anaf.
Hivi sasa, tunapoelekea Uchaguzi Mkuu wa mwakani, tayari hofu inayoashiria kurejea vurugu na kuvunjika amani, imeanza kujitokeza visiwani humo.
Hofu hiyo inajengwa kwa ushirikiano wa mamlaka za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), ikiwemo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Masheha ambao ni watendaji wa SMZ wa ngazi ya chini na Idara ya Vitambulisho Zanzibar.
Zinajenga hofu hiyo kupitia zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura linaloendelea hivi sasa kisiwani Pemba.
Masheha wanashiriki kujenga hofu hiyo wakiwa mawakala wa ZEC kwenye vituo vya uandikishaji.
Nilikuwa miongoni mwa wanahabari walioshuhudia zoezi hilo majimbo ya Konde na Mgogoni, yaliyoko Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Julai 12 hadi 15, mwaka huu.
Matukio ya uporaji haki za raia za Kikatiba, yamejitokeza kwenye zoezi hilo, ambayo sasa yanaonekana kukithiri.
Kulingana na utaratibu uliowekwa na ZEC, zoezi hilo ambalo limegubikwa na dosari nyingi za msingi, ikiwemo uduni wa elimu kwa wapiga kura, kufanywa kila jimbo.
Hata hivyo, mamia ya wananchi hasa vijana ambao wengi wao ambao mwaka huu wametimiza miaka 18, wamekuwa wakikataliwa kuandikishwa kwa kukosa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi (Zan ID).
Pia, wale wenye Zan ID wamekuwa wakikataliwa kuandikishwa kwa sababu hawana kadi za kupiga kura za mwaka 2005, wakati wenye kadi hizo wamekuwa wakikataliwa kuandikishwa kwa kuwa hawana Zan ID.
Mwongozo unaotolewa na Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 kuhusu Mzanzibari anayestahili kuwa mpiga kura, unapingana na Sheria ya Uchaguzi Zanzibar.
Linalosikitisha zaidi, masheha ambao walitegemewa kutoa msaada, pia wako kazini kukwamisha wananchi kuandikishwa. Wanakataa kuwapa barua wasiokuwa na Zan ID ili kuthibitisha kwenye Idara ya Vitambulisho ya Zanzibar kuwatambua wapatiwe kitambulisho hicho, wakidai wameelekezwa na wakuu wao.
Katika mlolongo huo, Idara ya Vitambulisho Zanzibar, nayo kwa upande wake imejipanga sawa kuhakikisha inawakomoa wananchi.
Yenyewe sasa inawataka wananchi kupeleka cheti cha kuzaliwa, badala ya barua ya sheha peke yake ili kupatiwa Zan ID kama ilivyokuwa ikifanyika huko nyuma.
Mkuu wa Idara ya Vitambulisho Wilaya ya Micheweni, Hamad Shamata, anasema wamepewa maelekezo na mkurugenzi.
Kwa uchache, hili ndilo ‘bomu’ ninalolihofiwa kwamba linatengenezwa na SMZ ili ‘kuvilipua’ visiwa vya Pemba.
Nionavyo, viongozi wa kitaifa wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete, wanawajibika kutatua suala hii mapema.
Vinginevyo, kuna hatari ya kutokea matatizo mengine Uchaguzi Mkuu wa mwakani, ambayo pengine inawezekana yakawa makubwa zaidi.
Mungu aepushe mbali kabisa.
CHANZO: NIPASHE
Maoni