Wapinzani wautikisa Muungano bungeni
• Wadai ofisi za Pinda, Vuai hazina mamlaka sawia
Na Martin Malera, Dodoma
CHOKOCHOKO za kuutikisa Muungano zimeanza tena baada ya wabunge wa kambi ya upinzani kutaka kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika pamoja na kutaka mkataba wa uanzishwaji wake upelekwe bungeni ujadiliwe ili kuondoa kero zilizopo.
Msimamo huo wa kambi ya upinzani ulitangazwa bungeni jana na msemaji wa kambi hiyo, Riziki Omar Juma (CUF), wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), kwa mwaka wa fedha 2009/2010.
Kambi hiyo ilisema, inajua kuna vikao vya kutatua kero za Muungano, lakini hawaoni uhalali wake pamoja na utayari wa kulitatua tatizo lenyewe kwa kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Kiongozi wa Zanzibar hazina mamlaka ya kulizungumzia.
“Tungependa mkataba wa makubaliano ya waasisi wa Muungano uletwe bungeni ili tuanze kuujadili kwa lengo la kutatua kero za Muungano kwa nia ya dhati kuliko kuendelea na vikao ambavyo hatuvioni kama vina uhalali,” alisema Riziki.
Aidha, kambi hiyo pia imeliomba Bunge kuiagiza serikali isitishe mara moja vikao hivyo na badala yake mkataba wa Muungano upelekwe bungeni kama mwanzo mkuu wa kutekeleza kwa vitendo dhamira ya kutatua kero za Muungano.
Kwa mujibu wa kambi hiyo, tatizo la Muungano si mgawo wa asilimia 4.5 kutoka Serikali ya Muungano kwenda kwa Zanzibar; si Zanzibar kuwa na au kutokuwa nchi ndani ya Muungano; si nishati za gesi na mafuta kuwa au kutokuwa za Muungano; si Zanzibar kujiunga na au kutokujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu Duniani (OIC).
Aliongeza kuwa, tatizo si Wazanzibari kushikilia nafasi katika Serikali ya Muungano katika mambo ambayo si ya Muungano wakati ambapo Watanganyika hawawezi kufanya hivyo katika Serikali ya Zanzibar, bali ni kutoheshimiwa kwa mkataba wa Muungano tangu mwanzo.
Riziki alisema namna Serikali ya Muungano inavyofanya kazi kushughulikia matatizo ya Muungano, ni kama haitaki kusikia upande mwengine wa mawazo, kwani inapenda kujifungia chumbani na kujisikiliza yenyewe ndani ya viambaza vinne.
“Mheshimiwa Spika, tunasema hivi kwa kuwa zile hoja za msingi tunazozitoa kuhusu matatizo ya Muungano, hazionekani kabisa kupewa nafasi katika maamuzi ya vipi Muungano huu uendeshwe,” alisema Riziki.
Alibainisha kuwa, mara kadhaa huko nyuma wameshawahi kueleza kuwa, tatizo kubwa la Muungano huu ni kutokuheshimiwa kwa mkataba wake uliouunda, Katiba ya Jamhuri ya Muungano kukiuka kwa kiasi kikubwa, makubaliano hayo, hivyo ni katiba iliyokwenda kinyume na msingi iliyoiunda.
“Muungano huu haukuundwa, na wala hautakiwi uongozwe na katiba zote mbili – ya Muungano na ya Zanzibar, zilichotakiwa kukifanya, ni kuutafsiri mkataba ule tu, na si vinginevyo,” alisema Riziki.
Kwa mujibu wa kambi hiyo, asili ya Muungano ilitokana na sababu tatu kuu, ambazo ni udugu wa kihistoria baina ya watu wa Tanganyika na Zanzibar, vuguvugu la kulileta pamoja Bara la Afrika, maarufu kama ‘Pan-Africanism Spirit’, na zile hisia kwamba umoja ni nguvu (United We Stand), na sababu nyingine inayotajwa ni kuipatia ulinzi Zanzibar, ambayo siku 100 tu kabla ya Aprili 26, 1964 ilikuwa imefanya mabadiliko ya utawala kwa njia ya mapinduzi.
Aliongeza kuwa, mkataba wa Muungano ulisainiwa na mwakilishi wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Marehemu Rais Abeid Karume na wa Jamhuri ya Tanganyika, Marehemu Rais Julius Nyerere ambapo walioutia saini ni wawakilishi wa Tanganyika na Zanzibar na ndiyo unaojenga hoja ya ukosefu wa uhalali kwa kikao chochote cha kuujadili Muungano ambacho hakihusishi pande husika za mkataba wenyewe.
“Sisi wa kambi ya upinzani tunaamini kwamba, ni kosa kubwa dhidi ya sheria zinazolinda mikataba ya kimataifa na kwa hakika, ni hatua ya hatari kwa hatma njema ya Muungano huu, kwa ofisi za Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (ambayo Zanzibar ni sehemu yake) na Waziri Kiongozi (ambayo ni ya Zanzibar tu) kama mwasisi wa Muungano wenyewe, kujadili mustakbali wa Muungano.
“Tunajenga hoja hii kuhusiana na hili: kwanza, wanaostahili kuujadili na kuutolea maamuzi Muungano ni Serikali ya Zanzibar na mwenzake aliyetiliana saini mkataba wa Muungano, ambayo ni Serikali ya Tanganyika. Uongozi wa serikali hizo ndio waliokuwa washiriki wa mazungumzo ya kuunda Muungano kwa niaba ya nchi zao.
“Pili, kilichotokea mwaka 1964 ni Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika kukubaliana kuanzisha ushirika wao unaoitwa Muungano.
“Katika kulinda heshima za mataifa yao, viongozi hao waliweka saini mkataba wa makubaliano yao, ambao una kila sifa ya kuwa mkataba wa kimataifa unaostahiki kuheshimiwa na pande husika na, tatu, kutokana na kwanza na pili hapo juu, kwa hivyo, ni upotoshaji wa makusudi kuuchukua mjadala wa nchi mbili zilizoungana na kuukabidhisha mikononi mwa vyombo visivyohusika na kuvipa vyombo hivyo mamlaka ya kufanya maamuzi yote,” alisema Riziki.
Alisisitiza kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu haina sifa ya kuuwakilisha upande wa pili wa Muungano, maana hii ni Ofisi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo Zanzibar ni sehemu yake.
Alisema kambi yao inasema haya ikijua wazi kwamba, kumekuwa na kisingizio kutoka upande wa Serikali ya Muungano, kwamba hakuna Serikali ya Tanganyika, hivyo, haiwezekani kwa Serikali ya Zanzibar kufanya mazungumzo na serikali isiyokuwepo.
“Kwa hivyo, kilichofanywa na Bunge la Tanganyika tarehe 25 Aprili 1964, siku moja kabla ya Muungano, ‘kuifuta’ Serikali ya Tanganyika kwa kutumia Sheria Na. 22 iliyoitwa ‘Union of Tanganyika and Zanzibar’, kilikuwa kinyume na makubaliano ya Muungano. Bahati mbaya, kitendo kile mpaka leo kimebakia kikiongeza shaka, kwamba Tanganyika ilijiingiza kwenye Serikali ya Muungano na kujifanya nchi mpya yenye jina jipya la Tanzania na yenye mipaka mipya ya kijiografia,” alisema.
“Tunasema haya tukijua uzito na uchungu wake. Ni vigumu kukiri kwamba tulifanya makosa, ikiwa kosa hilo linaonekana kuwa na maslahi. Lakini ukweli ni kuwa, kosa haliwezi kuwa na maslahi ya kudumu, hata kama linajaribiwa kufifilishwa kila mara. Kufuta Katiba ya Tanganyika kulikofanywa na vifungu vya sheria hii kulikuwa ni kosa.
“Kuifuta Serikali ya Tanganyika kulikuwa ni kosa. Na kosa hilo ndilo leo hii lililozaa kosa jengine la kiumbe kuzungumza na mmoja wa waumbaji kuhusiana na hatima ya kiumbe hicho. Na hivi ndivyo tunavyohoji uhalali wa vikao baina ya Ofisi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano (ambayo inawakilisha kiumbe, Muungano) na Ofisi ya Waziri Kiongozi (ambayo inawakilisha Muumba, Zanzibar),” alisema msemaji huyo.
Alibainisha kuwa, kutekelezwa kwa azimio lile ndiko ambako kungetoa maana kwa vikao vinavyofanyika hivi sasa baina ya Ofisi za Waziri Mkuu na ile ya Waziri Kiongozi, lakini bila ya kuwapo kwa Serikali ya Tanganyika iliyo hai na inayotambulika, vikao hivi vya mazungumzo vinabakia kuwa vya mazungumzo tu na katiba inasema, matatizo ya Muungano yatatatuliwa kwa kupitia Mahakama ya Katiba na si vikao.
Msemaji huyo pia alizungumzia umuhimu wa kuitumia Mahakama ya Katiba, kumesababisha kushindwa kuanzishwa kwa Mfuko wa Pamoja wa Fedha wa Muungano, kuwa na chombo kinachoshughulikia michezo, mgawano wa mapato ya Muungano, kuondolewa kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar kuwa Makamo wa Rais au mbadala wake na mambo mengine.
“Sisi wa kambi ya upinzani tumekuwa wazi sana katika hili. Hatutafuni maneno kusema kwamba tatizo kubwa na la msingi ni kutokuheshimiwa kwa mkataba wa Muungano, ambako kunatokana na ukosefu wa dhamira njema. Tulilisema hilo mwaka juzi, mwaka jana, na mwaka huu tunalirudia. Kwamba wa kujadiliwa ni Mkataba wa Muungano tu (Article of Union),” alisema msemaji huyo.
Aliongeza kuwa, mjadala wa kina juu ya mkataba wa Muungano ndiyo utakaothibitisha kuwa Serikali ya Tanganyika haikutakiwa kufa na kama imekufa iliuliwa kimakosa, na kosa hilo linaweza kurekebishwa kwa kutangazwa rasmi kuwapo kwa Serikali ya Tanganyika kama yalivyokuwa maamuzi ya Bunge hili tukufu mwaka 1992.
“Naliomba Bunge hili tukufu na Watanzania waniwie radhi kwa kusema kwamba, wakubwa wetu wameufanya Muungano huu ushabihiane sana na kile kisa cha Mfalme Jeta aliyemo kwenye riwaya ya Kusadikika ya Marehemu Sheikh Shaaban Robert. Mfalme huyu alikutwa na mjumbe wa Kusadikika akiwa amekaa katika eneo ambapo mto uliokuwa unakokozoa kila kitu – mawe, magogo, majengo, n.k. – unatiririkia kinywani na kuishia tumboni mwake, lakini kila mara alisikikana akilia: “Njaa! Njaa! Kiu! Kiu!
“Hivyo ndivyo Muungano wetu ulivyofanywa, kwamba uwe unakula na kunywa kila kitu na bado kila siku uwe unalalamika kufa njaa na kiu. Na ili kuufanya usife, wakubwa wanaamua kuulisha kila cha Zanzibar na kila cha Tanzania Bara.
“Ikiwa hali ni hii, je, si sawa kusema kwamba tunatoka kwenye serikali mbili zilizopo sasa kuelekea serikali moja? Je, jukumu la vikao hivi vya Ofisi za Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi ni kuratibu na kusimamia mchakato wa kubadilisha muundo wa Muungano? Na je, hivyo ndivyo Wazanzibari na Watanganyika walivyotaka yawe matokeo ya vikao hivi vya kunywa chai na kahawa?” alihoji.
“Kambi ya upinzani iliweka bayana kuwa, kutokana na kupuuzwa na kudharauliwa kwa makusudi kwa matatizo ya Muungano huu, hakujawahi kupita muongo ambapo Muungano hautikiswi na kutikisika na kila unapotikisika, machoni mwa wakubwa huonekana kama kwamba unatikisika kwa kuwa hauna mambo ya kutosha.
“Hilo ni kosa kubwa katika sayansi ya utatuzi wa migogoro. Wahenga husema: ‘Ganga shina, matawi hayagangika!’ Kwa maana ya kuwa, kutibu maradhi ni kukitibu chanzo chake na sio dalili zake. Ni kosa kutokujiuliza kwa nini Muungano huu unatikisika na kujiuliza tu vipi unatikisika?” alihoji Riziki.
“Tumekuwa tukionesha mara zote kwamba chanzo cha matatizo ya Muungano huu ni kutokuheshimiwa kwa mkataba wake uliouunda. Tunarejea tena kusema hapa kwamba Muungano huu hauongozwi na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, bali unaongozwa na Mkataba wa Muungano wa mwaka 1964. Katiba ya Muungano na ile ya Zanzibar zinatakiwa zitafsiri tu yale yaliyomo kwenye mkataba na sio kuongeza wala kupunguza.
“Kwa hivyo, basi kama ni suluhisho, sisi wa kambi ya upinzani tunatoa jibu kama lile alilowahi kulitoa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, mwaka 1985, alipoulizwa ni kipi kipaumbele chake katika kuijenga Tanzania. Mzee Mwinyi alijibu: ‘Barabara!’ Alipoulizwa kipi chengine, akajibu: ‘Ni barabara!’, na alipoulizwa kipi chengine akasema: ‘Ni barabara!’
“Ikiwa Bunge lako hili tukufu litataka kujua ni kipi ambacho sisi wa kambi ya upinzani tunaamini kuwa ni suluhisho la matatizo yote ya Muungano huu, tutajibu kuwa ni ‘kurudi kwenye Mkataba wa Muungano!’ Tukiulizwa ni kipi chengine, tutasema ‘ni kurudi kwenye Mkataba wa Muungano!’ Na hata tukiulizwa mara ya tatu, tutasema ‘ni kurudi kwenye Mkataba wa Muungano!’” alisema.
Chanzo: http://freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=6331
Maoni