Ripoti ya Awali: Uchaguzi Mdogo wa Magogoni

26 05 2009

Ripoti ya Awali Kuhusu Matukio Yasiyo ya Kawaida Katika Zoezi la Upigaji Kura kwa Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Magogoni, tarehe 23 Mei, 2009

Wapendwa Wanahabari,

Wakati upigaji kura kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa jimbo la Magogoni, lililo kwenye Wilaya ya Magharibi, Unguja, ukiendelea hivi sasa, tunatoa tarifa ya mwanzo inayohusu matukio yasiyo ya kawaida yanayohusiana na uchaguzi huu.

I. KITUO CHA WELEZO SKULI

1. Aliyekuwa OCD wa wilaya ya Mjini, Bwana Nurdin, amewapeleka watu ambao si wakaazi halali wa jimbo la Magogoni kwa sheha wa shehia ya Welezo, Bi Mgeni, kwa ajili ya kupatiwa shahada za kupigia kura.
2. Sheha, Bi Mgeni, anapeleka watu wasiokuwa na shahada za kupiga kura na anasimamia kuwapigisha kura. Angalau watu watatu (miongoni mwa hao waliopelekwa) wamesharipoti katika ofisi zetu kuthibitisha hili.
3. Katika Chumba Na. 4, wapiga kura wanapewa shahada mbili za kupigia kura. Kwa uchache, watu wanne wamesharipoti kwetu kwamba wamepewa shahada mbili mbili.
4. Katika Chumba Na. 5, wapiga kura wamegundua kwamba karatasi zao za kupigia kura haziandikiki. Ni baada ya kujaribu mara zaidi ya tatu, ndipo kwa mbali alama waliyoweka imejitokeza
5. Saumu Kitwana Mussa mwenye shahada halali Na. 630003322 iliyoandikishwa kupigiwa kwenye kituo cha Welezo Skuli, Chumba Na. 6 amekataliwa kwa madai kwamba jina lake halimo kwenye Orodha ya Wapiga Kura

II. KITUO CHA KINUNI

1. Kundi la Janjaweed likiongozwa na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) limezunguka maeneo ya kituo kwa ajili ya kushinikiza kupiga kura

III. KITUO CHA VIWANDA VIDOGO VIDOGO

1. Magari Land Cruiser ZNZ 45948, Double Cabin ZNZ 25039, gari ya abiria ya njia ya Mkokotoni ZNZ 66364 zinatumika kupakia vijana kutoka ofisi ya CCM Mkoa na ambao si wakaazi wa jimbo la Magogoni, iliyopo Amani, kupeleka kituo cha Viwanda Vidogo Vidogo kwa ajili ya kupiga kura
2. PT 059 kwenye kituo cha Magogoni

IV. KITUO CHA WELEZO HOSPITALI

1. Kijana mwenye kipande kilichoandikwa jina la Omar Hashim Mohammed, chenye namba ya usajili 620 001 358, amekutwa na shahada ya kupiga kura ambayo ni feki. Wenzake wenye shahada kama hiyo wameweza kupiga kura katika kituo hicho cha Welezo Hospitali.

V. KITUO CHA MAGOGONI

1. Watu wanapelekwa kwenye kituo kupiga kura, ambao si wakaazi wa jimbo la Magogoni na wala hawakuandikishwa kuwa wapiga kura

Wapendwa Wanahabari,

Hii ni taarifa ya awali juu ya matukio yanayoendelea sasa na ambayo hadi sasa yameripotiwa kwenye ofisi yetu kwa ushahidi kamili. Tutawatumia taarifa nyengine kadiri zitakavyokuwa zinatufikia.

Pamoja na salamu za Chama,

Dawati la Habari na Mahusiano,
Civic United Front
(CUF – Chama cha Wananchi)





Madudu ya polisi Z’bar yabainika

23 05 2009

Na Asha Bani

IMEBAINIKA kuwa, baadhi ya askari polisi visiwani Zanzibar, walipiga kura zaidi ya mara moja katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.
Taarifa za uhakika zilizolifikia Tanzania Daima Jumatano kutoka kwa viongozi mbalimbali wa kambi ya upinzani visiwani Zanzibar, zinaeleza kuwa, wamenasa ushahidi wa shahada za kupigia kura za polisi waliopiga kura zaidi ya mara moja katika uchaguzi mkuu uliopita.

Taarifa hizo ambazo kwa mara ya kwanza zinaonyesha ushahidi wa polisi kujihusisha na vitendo vya udanganyifu na kuvuruga uchaguzi visiwani humo, zinaeleza kuwa katika Jimbo la Magogoni, wanasiasa wa kambi ya upinzani wamenasa vielelezo vya vitambulisho vya kupigia kura zaidi ya 210 ambavyo vina upungufu, ukiwamo ule wa mpiga kura mmoja kujiandikisha mara tatu katika vituo tofauti pamoja na wapiga kura wapya kuandikishwa wakiwa na umri chini ya miaka 18.

Baadhi ya wanasiasa wa visiwani humo wameeleza kuwa, kubainika kwa njama hizo za polisi ndicho chanzo cha kuibuka kwa mgogoro wa hivi karibuni baina ya Chama cha Wananchi (CUF) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Wanasiasa hao walilieleza gazeti hili kuwa, baada ya tume kubaini kuwa baadhi ya shahada zilizotumiwa na polisi kupiga kura zaidi ya mara moja zimetua mikononi mwa wapinzani, maofisa wa tume hiyo walikataa kutoa daftari la wapiga kura ili kuhakiki majina ya wapiga kura kama sheria ya uchaguzi namba 64 ya Zanzibar inavyoeleza.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Juma Duni Haji, akizungumzia hali hiyo, alieleza kuwa chama chake kimenasa majina ya askakri hao na vipande vya nakala ya vitambulisho vyao kwenye daftari la kupiga kura baada ya kuitilia shaka ZEC ilipokataa kutoa madaftari ya wapiga kura kabla ya zoezi la upigaji kura kuanza.

Duni alisema majina yaliyoonekana kuwa na makosa, ambayo kwa juhudi zao walifanikiwa kuyanasa ni zaidi ya 210 na 24 kati ya hayo ni ya askari wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) ambao wamejiandikisha mara tatu.

“Inashangaza sana kuona askari wa JKU ndio walioongoza katika kujiandikisha mara tatu, na kwamba aibu hii ndiyo imekifanya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwatuma ZEC kutunyima daftari hilo ingawa sheria ya Zanzibar inaruhusu kufanya hivyo,” alisema Duni.

Alisema kuwa, anamshangaa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha kwa kuwaita wao ni wakorofi, huku uhalali na ukweli wa uozo wa ZEC ukiwa unajulikana na kuwa wametumwa na CCM kufanya njama hizo ili waweze kuiba kura katika chaguzi mbalimbali.

Duni alisema kuwa, kuna sheria katika kifungu cha 64 ambayo inaruhusu wakala wa chama chochote kinachoshiriki uchaguzi aweze kumuona mpiga kura ili aweze kulinganisha kama aliyekuwamo kwenye daftari ndiye ambaye ana kadi ya kupigia kura ya kudumu katika uchaguzi.

“Hii sheria sasa inadharaulika, lakini ni kwamba wanashindwa kufahamu utakapomnyima daftari wakala au chama chake, atawezaje kujua wapiga kura? Buku la ZEC ni bovu na ZEC wanaona aibu kulionesha, kwani limejaa uchafu wa uharamia walioufanya mwaka 2005 katika wizi wa kura na wanaoufanya sasa katika uandikishaji huo,” alisema Duni.

Alisema katika uandikishaji wa sasa wa kura hizo katika Jimbo la Magogoni, wapiga kura 20 (majina tunayo) wamenyimwa shahada mpya ya kupiga kura huku wakiwa na cheti kinachoonyesha kuwa ni wazawa wa jimbo hilo.

Alisisitiza kwa kupinga kauli ya Waziri Kiongozi kwa kuwaita kuwa wao ni watu wenye vurugu, na kwamba kama wakihitaji wajitoe katika uchaguzi, alisema kuwa wao wanafuata sheria na kwamba si watu wenye vurugu huku akihoji ni sababu ipi inayowafanya ZEC washindwe kuwapatia daftari hilo kama si kuficha maovu yao wanayofanya na waliyozoea kuyafanya katika chaguzi mbalimbali zilizopita.

“Hayo ndiyo mambo ambayo ZEC wanatufanyia, hatuna vurugu wala nini, sasa sijui hii serikali yetu itakuwa lini na demokrasia, kila kukicha ni dhuluma katika chaguzi zetu mbalimbali, ndiyo maana tunataka tume huru ya uchaguzi, ama uchaguzi uweze kusimamiwa na Umoja wa Mataifa na si ZEC kwa kuwa ni wezi na wamejaa maovu,” alisema Duni.

Jimbo la Magogoni lipo katika kipindi cha uchaguzi mdogo ambapo vyama vitatu vimejitokeza kusimamisha wagombea.

Wakati CUF imemsimamisha Ahmad Ally Ahmad, CCM inawakilishwa na Asha Mohamed na Hamis Mselemu wa Sauti ya Umma amesimamishwa na SAU kugombea kiti cha jimbo hilo.

Chanzo: freemedia.co.tz





Zanzibar: Chaguzi za vurugu hadi lini?

23 05 2009

Na Issa Hussein

Leo Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) inasimamia uchaguzi mdogo katika jimbo la Magogoni kwa nafasi ya Uwakilishi iliyowachwa wazi kufuatia kufariki kwa aliyekuwa Muwakilishi wa jimbo hilo Mh. Daudi Hassan Daudi.

Kwa wale wasiojuwa hali halisi ya kisiasa ya Jimbo hilo, ninawaomba wafahamu kuwa Jimbo la Magogoni ni moja kati ya majimbo mapya yaliyoundwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar mwaka 2000 katika mpango wake wa kuhamisha majimbo kutoka Pemba na kuyahamishiya Unguja kwa kile CUF tulichokitafsiri kuwa ni njama za Tume hiyo kwa kushirikiana na CCM kuipunguzia CUF idadi ya majimbo. Jimbo hilo lipo wilaya ya Magharibi katika Mkoa wa Mjini Magharibi

Jimbo la Magogoni ni moja ya majimbo yenye upinzani mkali kati ya vyama vya CCM na CUF. Kwa hakika panapohusika uchaguzi katika jimbo la Magogoni, kama ilivyo katika majimbo mengi ya Unguja, hasa yaliyo katika Mkoa wa Mjini Magharibi, huwepo kinyang’anyiro cha “ kukata na shoka” kati ya vyama vya CCM na CUF. Na kwa upande wetu CUF, tunaamini kwa kiasi kikubwa kwamba kama chaguzi za Zanzibar zingekuwa huru na za haki basi aina ya majimbo ya Magogoni yengekuwa yanawakilishwa na CUF tokea mwaka 1995. Mwandishi wa makala haya anashauri kupitia kumbukumbu za Uchaguzi wa mwaka 2000 ambapo uchaguzi wa Mkoa wa Mjini Magharibi ulighairishwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar mara tu baada ya kubaini kuwa CUF ilikuwa imeshanyakuwa sahemu kubwa ya majimbo ya Mkoa huo likiwemo jimbo la Mwera ambalo Magogoni ilikuwa ni sehemu ya jimbo hilo.

Ukirejea Uchaguzi wa mwaka 2005 huna budi kupata taswira ya uchaguzi uliojaa vurugu. Ma-elfu ya watu wanaostahiki kupiga kura hawakupata haki yao kutokana na vipingamizi vilivyowekwa na masheha (mawakala wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar) wakati ambapo maelfu ya vijana wa Janjaweed na wale wa vikosi vya SMZ wakiandikishwa zaidi ya mara moja kuisaidia CCM. Wananchi wengi walipigwa na kuharibiwa mali zao. Vitendo ambavyo vilipangwa kwa kushirikiana kati ya CCM, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, vyombo vya usalama na kutekelezwa na vijana wa Janjaweed. Wakati unayaangalia haya, suala la msingi litakalokujia ni: Jee, CCM ilifaidika kiasi gani ?

Hebu sasa chunguza takwimu hizi kwa makini sana: katika jimbo la Magogoni watu waliojiandikisha kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar mwaka 2005 walikuwa ni 9,210 ambapo waliopiga kura ni 7,364. Kinachoweza kuonekana hapo ni tofauti ya watu 1,846 sawa na asilimia 20.04 ya watu wote waliojiandikisha kupiga kura, ambao ama hawakupata fursa ya kupiga kura kutokana na mizengwe iliyozuka baadae ya watu kutoshuhudia majina yao katika daftari la kudumu au ndio kusema kura zao zimeharibika. Hii ni idadi kubwa sana kwa mazingira ya Zanzibar ya watu kukosa kupiga kura burebure. Mashaka yanaanza kwamba chini ya mpango wa makusudi kabisa watu hao walinyimwa haki yao ya kuchagua.

Matokeo ni mgombea wa CCM kutangazwa mshindi kwa kupata kura 4,174 dhidi ya 3,154 za CUF na 36 za UPDP kukiwepo tofauti ya kura 1,020 kati ya CCM na CUF (Ripoti ya TUZ:2005). Matokeo hayo ni baada ya juhudi kubwa zilizofanywa na CCM kuhakikisha kuwa askari wa Vikosi vya SMZ na vijana wa Janjaweed wanapiga kura zaidi ya mara moja. Sasa ninatumai msomaji wa makala haya umepata picha halisi ya ushindani wa kisiasa ulivyo katika jimbo hilo la Magogoni.

CUF, kwa hakika haina matumaini kuwa uchaguzi mdogo wa jimbo la Magogoni kuwa unaweza kuwa huru na wa haki. Imani hii inajengeka kutokana na dalili zilizoanza kuonekana mapema sana. Ni pale tu, SMZ kupitia spika wa Baraza la wawakilishi iliposema kuwa baraza haliathiriki na chochote katika utekelezaji wa shughuli zake kwa kukosekana kwa muwakilishi wa Magogoni. Alisahau kuwa ni wananchi wa Magogoni ambao wanalipa kodi ndio wanaohitaji uwakilishi katika baraza, na hivyo wao ndio watakaoathirika wakiukosa uwakilihsi huo. Kwa mujibu wa spika, uchaguzi wa Magogoni haukuwa muhimu sana kufanyika wakati huu. Sisi CUF tulitafsiri kauli hizi kuwa ni woga wa CCM kuikabili CUF katika chaguzi.

Uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa jimbo la Magogoni haukukosa misukosuko, vituko na vioja. Wakati CCM wakipania kucheza mchezo wa faulu waliouzoea, CUF ilijipanga kuhakikisha inazuia faulu hizo. Pamoja na yote yaliyojiri, uandikishaji huo ulimalizika kwa jumla ya wananchi………… kuandikishwa kuwa ni wapiga kura katika uchaguzi huo mdogo unaotarajiwa.

Kama utarejea tena takwimu za Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar kwa mwaka wa 2005, utagundua tofauti kubwa iliyopo kwa watu waliojiandikisha. Ni kinyume kabisa na matarajio na uhalisia. Kwamba badala ya kuwepo ongezeko la wapiga kura, Tume inatupatia upungufu wa asilimia……….kutoka wale waliojiandikisha mwaka 2005.

Yaweza kuelezwa kuwa watu wengi hawakujitokeza kujioandikisha kama vile Tume inavyodai, bali hatushawishiki hata kidogo kuamini hivyo kwani wako wananchi wengi waliojitokeza na kupingwa bila ya sababu zozote za msingi. Wananchi wengi wa jimbo hilo wamenyimwa haki hiyo ambapo wengine zaidi ya 200 wamekwenda mahakamani kudai. Sisi CUF hatutaki kuamini kwamba kesi zao bado zinaendelea kusikilizwa na Mahakama. Na hata kama zinaendelea kusikilizwa, hatuoni dalili yoyote kwamba uamuzi unaweza kutolewa mapema ili madai yao kuleta maana.

Tukiwa tunajitayarisha kuingia katika kampeni za uchaguzi huo, kuna kila dalili zinazoashiria kuwa chaguzi za kistaarabu chini ya Serikali ya CCM ni ndoto Zanzibar. Tunajuwa kuwa vitisho vimeshaanza kutolewa kwa wananchi wa jimbo hilo na maeneo jirani. Lengo likiwa ni kuwahofisha wananchi wasijitokeze kutumia haki yao ya kuchagua. Na pengine kuna dhamira kubwa ya kuwakatisha tamaa kwa dhana kuwa “ CCM haitoondoka madarakani kwa vikaratasi vya kura.”

Wakati hayo yanatokea sasa kuelekea katika Uchaguzi mdogo wa jimbo la Magogoni, kuna taarifa kuwa masheha na viongozi wa CCM wanahaha kuwatishia wananchi ili kutoa taarifa za nani kaandikishwa kuwa mpiga kura na kufahamu ufuasi wake nyumba hadi nyumba. Kuna kubwa zaidi nalo ni mkakati wa vitisho unaofanywa na vikosi vya SMZ kwa kushirikiana na JWTZ.

Vikosi hivi sasa vina zoezi kubwa la kupita mitaani na gwaride kwa jina la “Route March. ” “Route March” hizi zimepangwa kufanyika kwa muda wa mwezi mmoja na nusu na kwamba kila siku kuwe na kikosi kimoja kinapita barabarani. Haya kwa Wa-Zanzibari si mageni hasa panapohusika vikosi vya SMZ- JKU, KMKM, KVZ, na hata KZU.

Kile kinachotusikitisha zaidi ni kuona kuwa zoezi hili limepata baraka kutoka Serikali ya Jamuhuri ya Muuungano wa Tanzania kwa kule kuruhusu JWTZ kushiriki katika uhalifu huu. Sisi CUF tunajiuliza, vipi JWTZ linakubali kutumiwa vibaya na wanasiasa? Hata hivyo tunapata picha kamili ya mwenendo wa Amiri Jeshi Mkuu wetu, Rais Jakaya Mrisho Kikwete pale panapohusika kulinda maslahi ya CCM. Mashaka yetu ni yale yatakayojiri katika uchaguzi mkuu mwakani, 2010, “If a start is like this, how about the real course?”

Pamoja na yote haya nimeamua kuandika makala haya kuufahamisha umma wa Tanzania juu ya hali inavyoendelea Zanzibar. Pengine watawala wetu ndivyo wanavyotaka iwe na ndio maana muafaka wa kisiasa ukapigwa mweleka katika staili ile ile ya usanii wa kisiasa ili Zanzibar iendelee kukosa utengamano wa kisiasa kwa maslahi ya wachache, wenye uchu wa madaraka usio kikomo. Sisi katika CUF tanaamini kuwa iko siku haki itasimama. Maneno ya wanafalsafa hivi sasa yako ukutani yanasomeka na mmoja “The absolute power, the absolute collapse.” Watanzania wakae tayari kushuhudia kumalizika kwa utawala kandamizi wa CCM.





CUF Zanzibar yataka ZEC itende haki

23 05 2009

Date::5/20/2009

Na Salma Said, Zanzibar

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimeitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuendesha uchaguzi kwa uhuru, haki na uwazi ili kila chama kiridhike na matokeo yatakayotangazwa katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Magogoni unaotarajiwa kufanyika Mei 23 mwaka huu.

Hayo yalielezwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad alipokuwa akihutubia katika mkutano wa kampeni za kumnadi mgombea wa jimbo la Magogoni mkoa wa Mjini Magahribi uliofanyika katika viwanja wa Daraja Bovu.

“Mizengwe imeshafanyika wakati wa uandikishaji, sasa nasema katika uchaguzi huu, sitarajii kufanyika kwa mizengwe yeyote tena, tunaomba uchaguzi huu, ufanyike kwa haki, ili kila mmoja aridhike kama ameshinda au ameshindwa, kila mmoja afurahi na kukubali matokeo, tunaomba sana sana,” alisisitiza Maalim Seif.

Maalim Seif alisema bado ZEC inayo nafasi ya kuuonyesha ulimwengu kwamba wanaweza kuendesha uchaguzi huru na wa haki, licha ya kasoro zote zilizojitokeza huko nyuma ambazo tume zilizotangulia zilikuwa zikilalamikiwa kuendesha uchaguzi kwa usiri mkubwa na kusababisha vyama kutokubaliana na matokeo yanayotolewa na tume hiyo.

Alisema matarajio ya wananchi wengi akiwemo yeye mwenyewe ni kufanyika kwa uchaguzi wa haki, lakini alionyesha wasi wasi wake katika uchaguzi huo mdogo, ambapo alidai kwamba tayari kuna tetesi za baadhi ya maafisa wa tume hiyo, kuanza kuchezea takwimu kwa kutumia mtandao na kubadilisha majina ya wapiga kura kwa lengo la kuwahangaisha wapiga kura wasiyaone majina yao kwa urahisi wanapofika katika vituo vya kupigia kura.

“Tunakuomba Mwinyichande (Mwenyekiti wa ZEC) mdhibiti meneja wako wa IT kuna tetesi kuwa anachezea daftari la wapiga kura kwa kubadilisha majina, mfano mimi ni Seif Sharif Hamad, lakini linaandikwa Hamad Seif Sharif, kusudi halafu uambiwe jina lako halionekani kaa pembeni, huwezi kumuweka mtu tangu asubuhi hadi saa 10 anasubiri kituoni halafu useme uchaguzi huo umefanyika huru, tunakuomba sana,” alisema Maalim Seif.

Maalim Seif alisema jukumu lote la kuharibika uchaguzi huo mdogo lipo juu ya kichwa cha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, hivyo ni vyema akachukua tahadhari na kujisahihisha ili asije kujitia kasoro hasa katika uchaguzi huo mdogo, kwani, makosa yaliofanyika huko nyuma ni vyema kujisahihisha kwa kutumia uchaguzi huo.

Hata hivyo aliwataka wana CUF kuheshimu sheria na kanuni za uchaguzi kwa kupiga kura kwa amani na utulivu na kudhibiti kura zao bila ya vurugu huku akisisitiza uchaguzi mdogo uwe ni mfano mzuri kwa Zanzibar ili kuionesha dunia kuwa Zanzibar ikikusudia inaweza kuendesha uchaguzi bila ya mizengwe na kufuata taratibu za uchaguzi kama inavyofanyika nchi nyingine duniani.

Akizungumzia suala la Muungano Maalim Seif, alisisitiza kuwa CUF haitaki kuvunja muungano, lakini inataka muungano wa usawa na wenye kuheshimiana kwa pande zote mbili bila ya kuonekana kama mkataba wa muungano uliobainisha na kukubalika kwa waasisi wawili wa muungano huo Mwalimu Nyerere na Mzee Karume.

Kwa upande wake, mgombea wa jimbo hilo, Hamad Ali Hamad aliwaomba wananchi wa Magogoni wampe kura zao kwani CCM imeshindwa kuwapelekea huduma katika jimbo hilo.

Awali, akizungumza katika mkutano huo mbunge wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ibrahim Sanya alisema CCM ni sawa na mnazi ulioparama hivyo lililobaki ni kuangushwa na kupasuliwa mbao tu.

Alisema hali ngumu ya maisha imekuwa ikizidi kila kukicha, huku huduma mbovu zinazotolewa zinawakera wananchi, lakini hawana pahala pa kupelekea malalamiko yao.

Aliwataka wananchi kuikataa CCM na kuiangusha kama mnazi ili waichague CUF ichukue serikali kwa kuwahudumia wananchi wote wa Zanzibar.

Sanya alisema Jimbo la Mji Mkongwe lilifanyiwa kazi kubwa hivyo aliwataka wananchi wa Magogoni kujitahidi kuikataa CCM na kuipa CUF kwa kura nyingi kwani ndio chama pekee chenye kuleta mabadiliko ya kimaendeleo na kiuchumi Zanzibar.

Chanzo: mwananchi.co.tz





Uchaguzi Magogoni leo, Mwakilishi Wawi afariki

23 05 2009

Wakati wananchi wa Magogoni leo wanachagua mwakilishi wa kuziba pengo lililoachwa kwa kifo cha Mwakilishi wa CCM, Daud Hassan Daud, Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani katika Baraza la Wawakilishi, Mwakilishi wa Wawi, Soud Yussuf Mgeni, 61 (CUF), naye amefariki dunia. Mgeni alifariki dunia jana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam, wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).

Taarifa ya Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Umma wa CUF, Salim Bimani, ilithibitisha kutokea kwa kifo hicho lakini haikutaja Mgeni alikuwa akisumbuliwa na maradhi gani. “Kwa sasa Soud hatunaye katika dunia hii na ndiyo kazi ya Mwenyezi Mungu…amefariki dunia katika Hospitali ya Muhimbili Dar es Salaam,” alisema Bimani.

Hata hivyo, Naibu Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Ashura Mustapha, alisema baadaye kuwa walipata taarifa juu ya kifo cha Mgeni jana asubuhi kutoka kwa ndugu wa marehemu na kwamba alikuwa akisumbuliwa kwa muda mrefu na saratani ya ini.

Bimani naye alikiri kuwa kifo cha Mgeni kimeacha pengo kubwa katika CUF kutokana na uzoefu wake mkubwa wa masuala ya siasa. Mustapha alisema marehemu ameacha mke na watoto kadhaa na mipango ya mazishi ilifanywa jana hospitalini hapo kabla ya mwili kusafirishwa.

Alisema Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba, ambaye yuko katika jimbo la Busanda kwenye kampeni za chama hicho na Katibu Mkuu, Maalimu Seif Sharif Hamad wametaarifiwa kuhusu kifo hicho na kupokea taarifa kwa masikitiko makubwa.

Mgeni aliingia katika Baraza la Wawakilishi mwaka 1980 akiwa Mwakilishi wa jimbo la Vitongoji. Pia alipata kuwa Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi na baadaye Waziri wa Kilimo na Mifugo, huku akiwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM.

Alifukuzwa CCM baada ya kuchafuka kwa hali ya kisiasa, sambamba na viongozi watendaji wakuu wa serikali na CCM wapatao wanane akiwamo Hamad. Mwili wa marehemu ulisafirishwa jana kwa ndege hadi Pemba kwa maziko kwa mujibu wa taarifa ya CUF. Kifo cha Mgeni kinakuwa cha pili katika Baraza la Wawakilishi, baada ya kile cha Daud, aliyefariki dunia mwishoni mwa mwaka jana.

Ofisa wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, alikiri kupata taarifa ya kifo hicho na kwamba sasa wanasubiri taarifa kamili kutoka ofisi ya Baraza la Wawakilishi. Wakati huohuo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, ametoa salamu za rambirambi kwa msiba huo.

Rais alieleza masikitiko yake na kushtushwa na kifo cha Mgeni na kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Zanzibar alitoa mkono wa rambirambi kwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, wajumbe na wafanyakazi wa Baraza, familia ya marehemu, ndugu, marafiki na jamaa zake wote.

Karume alisema kifo cha Mgeni ni msiba kwa wananchi wote wa Zanzibar na atakumbukwa kwa utumishi wake kwa wananchi wa Wawi, Pemba na wa Zanzibar kwa jumla. “Namwombea rehema za Mwenyezi Mungu na malazi mema peponi. Aidha, nawatakia subira na ustahamilivu wafiwa wote. Amina.” alisema Karume.