|
![]() |
|
|
Yuko wapi Rais Kikwete?
26 03 2009Comments : Leave a Comment »
Categories : Haki za Binaadamu
‘Ombwe la uongozi sasa liko wazi’
26 03 2009Na Elias Msuya
Hivi karibuni kumekuwa na taharuki iliyoikumba dunia ya anguko la uchumi. Anguko hilo ambalo limeanzia nchini Marekani na kusambaa duniani kote limeshaanza kuonyesha athari zake kwa nchi za Afrika, Tanzania ikiwemo.
Sambamba na tatizo hilo, kumekuwepo pia mjadala wa kutatua tatizo la umeme ambapo wanasiasa mbali mbali wamekuwa wakilumbana kupinga au kuunga mkono ununuzi wa mitambo ya uzalishaji umeme.
Katika makala haya, Mwenyekiti wa chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba anaanza kueleza athari za anguko la uchumi wa dunia na suluhisho lake.
“Chanzo cha karibu cha mgogoro wa fedha wa Marekani ni puto katika bei za nyumba lililochochewa na upatikanaji rahisi wa mikopo ya kujengea na kununulia.
Mabenki yanayotoa yanayotoa mikopo ya kujengea na kununulia nyumba yalipunguza viwango na masharti ya kupata mikopo bila kuwa na ushahidi wa dhamana na uhakika wa kipato cha kulipia mikopo hiyo.
Sera ya kupunguza mikopo ya benki kuu ya Marekani baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001, ilipunguza gharama za mikopo katika sekta ya nyumba. Nchi za Asia na hata China, na wauzaji wa mafuta ya petroli wa Mashjariki ya kati wamekuwa na ziada kubwa katika urari wake katika urari wake wa malipo wa biashara na nchi za nje, Ziada hii iliwekwa katika amana za serikali ya Marekani na sekta binafsi.
Mabenki na taasisi za fedha zilianzisha amana zizsizoeleweka kwa urahisi ambazo kinga na dhamana yake ilikuwa ni mikopo ya nyumba kwa wateja wasiokuwa na uwezo wa uhakika wa kulipa mikopo hiyo” anasema profesa Lipumba.
Akieleza hali za maisha ya Watazania kama dalili za athari ya anguko la uchumi wa dunia, Profesa Lipumba anasema,
“Wakati wa hotuba ya bajeti na hotuba ya Rais Bungeni, Watanzania tulielezwa kuwa uchumi unakuwa vizuri kwa asilimia 7, na kwahiyo maisha ya Watanzania yanaboreka mwaka hadi mwaka .
Hata hivyo hali halisi ya wananchi wengi inazidi kuwa mbaya. Uchunguzi wa bajeti za Kaya (UBK) wa mwaka 2007, unaonyesha kwamba umasikini umepungua kidogo sana toka asilimia 35.7 mwaka 2001 mpaka asilimia 33.3 mwaka 2007.
kwakuwa idadi ya Watanzania inaongezeka kwa asilimia 2.6 kila mwaka, idadi ya watu masikini imeongezeka kwa watu milioni moja toka watu milioni 11.7 hadi watu milioni 12.7 mwaka 2007. Kutopungua kwa umasikini kunaashiria kwamba uchumi wa Tanzania kuwa unakuwa kwa asilimia 7 ni ngonjera. CCM na serikali yake inatufungia ngulai”
Vile vile mfumuko wa bei kati ya mwaka 2001 hadi 2007kwa kutumia bei za bidhaa zinazonunuliwa na Watanzania kama ulivyoainishwa na UBK ni asilimia 93 wakati takwimu za serikali zinaonyesha asilimia 42.
Kwa mwenendo unaoonekana katika uchunguzi wa Bajeti za kaya 2007, Tanzania haitafika malengo ya milenia ya kupunguza umasikini na kuboresha huduma za afya na elimu.” anasema Lipumba.
Hata hivyo Profesa Lipumba analo suluhisho la mgogoro huu,
“Watanzania tunahitaji tutafakari hali halisi tuliyonayo na tubuni sera na mikakati ya pamoja ya kujikwamua kutoka katika dimbwi la umasikini. Misingi muhimu ya sera na mikakati hiyo ni pamoja na kutumia vizuri maliasili ya Tanzania kwa manufaa ya wananchi wote huku tukilinda mazingira yetu.
Tuwekeze kwenye afya za watoto wa Tanzania toka wakiwa katika mimba za mama zao kwa kuhakikisha kina mama wajawazito na watoto wachanga wanapata lishe bora. Vile vile tuwekeze kwenye eilimu kwa watoto tangu wakiwa chekechea na kuendelea
Tuwekeze kwenye kilimo hasa cha chakula kama vile mahindi, mpunga maharage, jamii ya kunde, na mbegu za mafuta, ili kukidhi mahitaji ya ndani na kuuza katika masoko ya nje.
Tuimarishe viwanda vinavyotumia malighafi za ndani na kuajiri watu wengi kama vile viwanda vya nguo na mavazi, viatu na bidhaa za ngozi, vifaa vya matumizi ya nyumbani na vifaa vya umeme na elektroniki sambamba na kuimarisha miundombinu ya barabara, umeme, maji na mawasiliano.”
Licha ya hoja hizo, bado Profesa Lipumba anatoa wito kwa Rais Kikwete,
“Ni vyema Rais Kikwete akaitisha mkutano wa kitaifa wa wadau wote kutathmini hali yetu ya kiuchumi, tukizingatia mgogoro wa kiuchumi wa dunia na mabadiliko ya sera na mikakati ya sera na mikakati inayohitajika kuchukuliwa ili tuweze kujenga uchumi utakao kuwa na manufaa kwa wananchi wote kwa kuongeza ajira na kipato cha wananchi wa kawaida.
Ni wazi kuwa hotuba za kila mwezi siyo mjadala wa kitaifa wa kuchangia mawazo ya kuelewa nchi imetoka wapi, iko wapi na wapi inastahiki ielekee. Nini dira ya Taifa inayowaunganisha Watazania kutafuta maendeleo yenye kuleta neema kwa wananchi wote katika ulimwengu wa utandawazi uliomo katika mgogoro.
Mjadala wa kitaifa ufanye tathmini ya njia bora ya kusimamia asasi nyeti kama vile Benki kuu, TANESCO na usimamizi wa Bandari Tanzania. Benki kuu imevunjiwa heshima yake na ufisadi wa EPA, minara pacha, kampuni ya Meremeta na Mwananchi Gold.
Benki kuu inapaswa kuwa na watu mashuhuri walio huru na makini ambao hivi sasa hawapo katika shughuli za siasa lakini wanauelewa wa shughuli za Benki kuu kama vile Mzee Edwin Mtei na Bob Makani. Watu hawa wanaweza kuimarisha Bodi ya Benki kuu isifanye mambo ya aibu na yakuitia hasara nchi.” anasema
Akizungumzia tatizo la umeme na malumbano ya ununuzi wa mitambo ya Dowans, Lipumba anasema,
“Ukosefu wa uongozi (Ombwe la uongozi) unajidhihirisha wazi katika sakata la hivi sasa la TANESCO ambapo mapande ya CCM yanalipotosha na kuliyumbisha Taifa katika masuala mazito ya kutokuwa na mpango mahsusi wa taifa unaotekelezwa na TANESCO wa kuzalisha na kusambaza umeme.
Badala ya kujadili mbinu za muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu wa kuongeza uzalishaji wa umeme, makundi ya CCM yanaendeleza vita vyao vya kugombania madaraka na maslahi ya kibiashara.
Watanzania wamefikishwa mahala ambapo hawawezi kumwamini kiongozi yeyote wa CCM kuwa na maadili ya kutetea maslahi ya nchi. Mbunge wa CCM unamsikia anashambulia ufisadi unafikiri labda bado wapo wanaotetea maslahi ya taifa, kumbe nayeye ana maslahi binafsi anayoyaficha.
Kwa hiyo ni muhimu kuwa na mjadala wa kitaifa utakaochanganua dira na mikakati yetu ya maendeleo ya taifa letu na utaratibu wa kuitekeleza na kuweka misingi imara ya maadili ya uongozi.
Tuutumie mjadala huo kuweka dira mpya ya maendeleo ya nchi yetu itakayowahakikishia wananchi ulinzi wa haki zao za msingi na kutumia rasilimali za nchi kujenga uchumi imara utakaoleta neema kwa wananchi wote,” anasema Profesa Lipumba.
Chanzo: http://mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=10902
Comments : Leave a Comment »
Categories : Haki za Binaadamu
Shaaban Mloo: Shina la CUF lisilosahaulika
19 03 2009• Alifananishwa na kuchi aliyeikaa kooni CCM
• Ni kutokana na alivyokijua chama ndani, nje
• Alifukuzwa CCM na kuanzisah KAMAHURU
Na Sarah Mossi
“NAKUACHIENI Chama wajumbe wote wa Mkutano Mkuu huu wa leo mkiwa na jukumu moja kubwa sana. Ingawa sisi tunastaafu, lakini tutaangalia kwa macho mawili utendaji wenu katika kata, matawi, majimbo, wilaya na taifa. Nakuachieni Chama kilichokamilisha theluthi mbili ya mtandao wake katika mikoa 26 ya Tanzania . CUF imeenea kila mkoa. Katika wilaya 130, CUF iko wilaya 117, katika vitongoji 38,000, CUF ina asilimia 20, katika vijiji 11,600, CUF ina asilimia 15. Mitaa yote 3,080, CUF ina asilimia 20.”
Hiyo ni kauli ya mwisho ya Shaban Khamis Mloo ‘Kuchi’ aliyoitoa kwa wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) akiwa kama kiongozi wa chama hicho, akistaafu rasmi uongozi wa chama hicho. Kwa wale wenye kumbukumbu, watakumbuka kwamba kauli hiyo aliitoa mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Tatu wa CUF. Hiyo ilikuwa ni Februari, 2004. Ilikuwa ni kauli yake ya mwisho akiwa kiongozi wa chama hicho, akistaafu nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho.
Nilimfahamu Mzee Mloo na kumzoea zaidi kwa jina moja tu la ‘Babu’. Hakika jina hili nilizoea kumwita kila mara ninapokutana naye kwenye maeneo ya Mkunazini, mjini Zanzibar. Mkunazini ndio nyumbani kwake Mloo.
Lakini wengi walizoea kumwita kwa jina lake maarufu la ‘Kuchi’. Kwa nini aliitwa Kuchi? Jina hili alipewa na wanamageuzi wa visiwa vya Unguja na Pemba kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao wa kupambana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika kutetea usawa wa kisiasa na kijamii kwa wananchi wa Zanzibar.
Kwa wale wajuzi wa kiswahili ‘kuchi’ ni aina ya kuku, jogoo mkubwa mwenye uwezo mkubwa wa kupigana, hata ikibidi na binadamu. Jogoo huyu hutumiwa mara nyingi kwenye mapambano ya ngumi kama kikolezo kwa hadhira.
Mloo akaitwa kuchi kwa maana ya kwamba angeweza kuwakaba CCM kooni, ikizingatiwa kwamba naye kabla hajaanza mageuzi nje ya CCM, alikuwamo ndani kama kada wa siku nyingi. Mloo alikuwa na uwezo huo wa kupambana na viongozi wa CCM ambao kwa namna moja au nyingine walionekana dhahiri hawataki mageuzi katika visiwa hivyo.
Hawa waliwaona kina Mloo na wenzake kama Maalim Seif Sharif Hamad sawa na wasaliti, hasa baada ya kuamua kuingia kwenye mchakato wa mageuzi ya kisiasa kwenye miaka ya ’80 na hatimaye kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi ya siasa mwaka 1992.
Wapo waliojiuliza ujasiri wa mzee huyu ulitokana na nini, hasa kwa kuzingatia mazingira ya wakati ule. Lakini jibu likawa jepesi; ni kwa sababu alikuwa anaijua CCM na serikali yake kinagaubaga, au kwa maneno mengine ndani nje.
Katika uhai wake, mzee Mloo alipata kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali na katika CCM, ambapo aliwahi kuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Pwani, Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Hata katika michezo, Mloo hakuwa nyuma, kwa sababu alipata kuwa kocha wa timu maarufu ya Everton iliyokuwa na maskani yake Mtaa wa Kikwajuni.
Mzee Mloo alifariki asubuhi ya Machi 14, katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja mjini Zanzibar, akiwa na umri wa miaka 75. Katika uhai wake, mzee Mloo alikuwa miongoni mwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi Zanzibar kabla ya Mapinduzi na baada ya kuanza kwa Baraza la Wawakilishi, akaja kuwa mjumbe wa Baraza hilo.
Mwanasiasa huyo mkongwe wa Zanzibar, akiwa na wenzake aliongoza harakati za kudai mageuzi ya kisiasa, wakati huo akiwa na Ali Haji Pandu, Maulid Makame, Soud Yusuf Mgeni waliounda Kamati Huru ya Mageuzi ya kisiasa iliyokuwa ikijulikana kwa jina la KAMAHURU, lengo likiwa ni kuishinikiza SMZ ikubali mabadiliko ya kisiasa na kufuta mfumo wa chama kimoja kushika hatamu.
Hata hivyo, chama hicho baadaye kiliungana na Chama Cha Wananchi Tanzania (CCWT) kilichokuwa kikiongozwa na Mwenyekiti wake, James Mapalala na kuzaliwa CUF. Hayati mzee Mloo alikuwa Katibu Mkuu wa Kwanza wa CUF na alishika nafasi hiyo kwa miaka minane, kuanzia 1992 hadi 2000 alipochukua nafasi ya umakamo mwenyekiti hadi alipoamua kustaafu mwaka 2004.
Mloo ni miongoni mwa wanachama waliofukuzwa na CCM mwaka 1988 baada ya kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar, kwa namna ya pekee ndani ya CCM.
Wengine waliofukuzwa ni Maalim Seif, Ali Haji Pandu, Khatib Hassan, Hamad Rashid, Soud Yussuf Mgeni, Masoud Omar, Maulid Makame na Machano Khamis Ali. Baadhi yao pia waliwekwa gerezani kama watuhumiwa wa uhalifu.
Ingawa hatunaye tena, marehemu Mloo ataendelea kukumbukwa na CUF pamoja na wamageuzi wote nchini kama mfano kwa wanamageuzi wasioyumba, ambaye wakati wote alitetea haki na usawa mbele ya jamii.
Kwa sisi tulio hai tutamkumbuka ‘Kuchi’, si tu kama kiongozi mstaafu wa chama, bali zaidi kama mwasisi, mwanzilishi na mwanachama imara na shupavu katika siku zote za uhai wake. Atakumbukwa daima ndani na nje ya CUF kama mjuzi wa siasa za Zanzibar na za Tanzania na ni mchapa kazi na mtu aliyekuwa na ujasiri wa kupigiwa mfano.
Hata baada ya kustaafu umakamo mwenyekiti, mzee Mloo aliendelea kuwa sehemu muhimu ya CUF kwa kujitolea katika mashauri mbalimbali.
Kila alipokuwa na uwezo, hakuacha kuhudhuria mikutano ya hadhara au vikao vyovyote alivyoalikwa au kuchangia jambo aliloona pana umuhimu.
Kikao cha mwisho ‘Kuchi’ kuhudhuria ni Mkutano Mkuu wa Nne wa CUF uliofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, kuanzia Februari 23 hadi 27 mwaka huu, ambao pia ulikuwa mkutano wa uchaguzi. Kwa hivyo, hadi siku za mwisho mwisho wa uhai wake, mzee Mloo alisimama imara kuijenga na kuihuisha CUF na alibahatika kuiona safu mpya ya viongozi wa CUF inayoendelea kukiongoza chama hicho.
Katika kumwenzi ‘Kuchi’, lazima waliobaki ndani ya CUF watimize dhamira na azma ya waasisi wao, akiwamo mzee Mloo, kwa manufaa ya nchi na vizazi vijavyo, ili CUF aliyoiasisi, kuijenga na kuisimamia siku zote za uhai wake iendelee kuwa taasisi imara ya kisiasa kwa manufaa ya nchi na watu wake.
Mwenyezi Mungu ampokee mja wake akiwa ameshamsamehe makosa yake na aufanye mwema ujira wake. Amin.
Source: Gazeti la Rai la tarehe 19 Machi, 2009
Comments : Leave a Comment »
Categories : Haki za Binaadamu
Seif: Lipumba lazima agombee urais 2010
16 03 2009
2009-03-16 10:27:54
Na Muhibu Said
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, amempigia debe Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, kuwa lazima agombee urais wa Jamhuri ya Muungano katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
Maalim Seif alitoa kauli hiyo jana jioni katika Viwanja vya Temeke Mwisho, jijini Dar es Salaam wakati akihutubia mkutano wa hadhara.
Katika mkutano huo ambao lengo lake lilikuwa ni kutambulisha safu mpya ya uongozi wa CUF uliochaguliwa katika Mkutano Mkuu uliofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Hamad alisema kuwa Profesa Lipumba anapaswa kugombea urais kwa kuwa katika chama hicho hakuna mtu ambaye kwa sasa ana uwezo wa kukabiliana na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katibu Mkuu huyo alisema kuwa hivi sasa nchi inakabiliwa na matatizo ya uchumi, hivyo Profesa Lipumba ndiye wananchi wanayemhitaji kwa kuwa ni daktari wa uchumi.
“Mwakani, Inshallah, Profesa Lipumba atagombea,“ alisema Hamad, ambaye aliwatambulisha wajumbe wa Baraza Kuu, manaibu makatibu wakuu wa Bara na Visiwani na wakuu wa kurugenzi zote za chama hicho.
Ingawa hakufafanua, Hamad alisema kuwa CCM hivi sasa wanapigana wenyewe kwa wenyewe na kuongeza kuwa Watanzania wanataka kiongozi kama Profesa Lipumba.
Hivi karibuni, Profesa Lipumba alisema hivi sasa ni mapema kwake kutangaza kama ana nia ya kugombea tena urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
Alisema kuwa jukumu lake ni kutekeleza mambo waliyoafikiana katika mkutano mkuu uliopita na vile vile kukijenga chama.
Kama CUF kitampitisha Profesa Lipumba kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2010, itakuwa mara yake ya nne kugombea kiti hicho.
Kwa mara ya kwanza, aligombea kiti hicho mwaka 1995 na kushinda nafasi ya tatu nyuma ya Benjamin Mkapa wa CCM na Augustine Mrema, aliyegombea kupitia NCCR-Mageuzi. Hata hivyo, alimuacha nyuma John Cheyo wa UDP.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, Profesa Lipumba alipanda chati kwa kushika nafasi ya pili, akimfuatia Benjamin Mkapa wa CCM na kuwaacha nyuma Augustine Mrema wa TLP na John Cheyo wa UDP.
Profesa Lipumba alitetea nafasi yake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 baada ya kuibuka mshindi wa pili nyuma ya Rais Jakaya Kikwete wa CCM na kuwaacha nyuma Freeman Mbowe (Chadema), Augustine Mrema (TLP), Dk. Sengodo Mvungi (NCCR-Mageuzi), Mchungaji Christopher Mtikila (DP), Profesa Leonard Shayo (Demokrasia Makini), Paul Kyara, (Sau), Anna Senkoro (PPT-Maendeleo na Dk. Emmanuel Makaidi (NLD).
- SOURCE: Nipashe (http://ippmedia.com/ipp/nipashe/2009/03/16/133443.html)
Comments : Leave a Comment »
Categories : Haki za Binaadamu
Mzee Mloo afariki dunia
14 03 2009
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 14 Machi, 2009
TANZIA: MZEE SHAABAN KHAMIS MLOO
Wapendwa Wanahabari,

Marehemu Mzee Shaaban Khamis Mloo
The Civic United Front (CUF – Chama cha Wananchi) kinasikitika kuwaarifuni kwamba, leo asubuhi mwasisi wa chama hiki, Mhe. Shaaban Khamis Mloo, amefariki dunia, katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja, mjini Zanzibar, alikokuwa amelazwa kwa wiki moja sasa akisumbuliwa na maradhi ya moyo na shinikizo la damu. Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika leo leo saa 10.00 alasiri huko huko Zanzibar.
Marehemu Mzee Mloo, ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 75, alikuwa ndiye katibu mkuu wa kwanza wa CUF kwa miaka nane, kutoka 1992 hadi 1999 alipochukua nafasi ya umakamo mwenyekiti hadi alistaafu mwaka 2004. Yeye ndiye miongoni mwa waasisi wa Chama hiki, kwa kuanzia na vuguvugu la KAMAHURU. Ni yeye ndiye aliyeongoza mazungumzo ya kwanza na aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CCW), Mhe. James Mapalala, na hatimaye kuungana na kuzaliwa kwa CUF tuliyonayo sasa.
Kwa hivyo, CUF inamtambua Mzee Mloo sio tu kama kiongozi mstaafu wa Chama, bali zaidi kama mwasisi, mwanzilishi na mwanachama imara na shupavu katika siku zote za uhai wake. Atakumbukwa daima ndani na nje ya CUF kama mjuzi wa siasa za Zanzibar na za Tanzania kwa ujumla, mchapakazi na mtu aliyekuwa na ujasiri wa kupigiwa mfano.
Historia yake ya kisiasa inarudi nyuma sana, tangu enzi za kupigania uhuru wa Zanzibar katika miaka ya ’50 alipojiunga na Afro Shirazi Party (ASP) akiwa mwanaharakati wa vyama vya wafanyakazi. Baada ya Mapinduzi ya 1964, Mzee Abeid Karume alimteua kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi. Alikuwa pia mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia Jumuiya ya Wazazi (JUWATA) na pia mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC – CCM) na Katibu wa CCM wa Mkoa wa Pwani. Baadaye, kutokana na harakati zake za kudai demokrasia zaidi ndani ya CCM, akawa miongoni mwa watu saba waliofukuzwa na Mwalimu Julius Nyerere kutoka CCM, pamoja na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, hapo Mei 13, 1988.
Kwa hivyo, Marehemu Mzee Mloo alikuwa mwanasiasa wa kuheshimika tangu zamani; na aliendelea kuwa mwanasiasa hata baada ya kustaafu rasmi uongozi wa kisiasa. Kwa mfano, hata baada ya kustaafu umakamo mwenyekiti wa CUF, aliendelea kuwa sehemu muhimu ya CUF kwa kujitolea katika mashauri mbali mbali. Kila alipokuwa na uwezo, hakuacha kuhudhuria mikutano ya hadhara au vikao vyovyote ambavyo alialikwa. Kikao cha mwisho kuhudhuria ni Mkutano Mkuu wa Nne wa chama chetu uliofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, kuanzia 23 hadi 27 Februari, mwaka huu. Kwa hivyo, hadi siku za mwisho mwisho wa uhai wake, Mzee Mloo alisimama imara kuijenga na kuihuisha CUF.
Wakati akiwaaga wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Tatu, Februari 2004, Mzee Mloo alitoa waraka, ambao pamoja na mengine ulikuwa na kauli ifuatayo:
“Nakuachieni Chama wjaumbe wote wa Mkutano Mkuu huu wa leo mukiwa na jukumu moja kubwa sana. Ingawa sisi tunastaafu, lakini tutaangalia kwa macho mawili utendaji wenu katika kata, matawi, majimbo, wilaya na taifa. Nakuachieni Chama kilichokamilisha theluthi mbili ya mtandao wake katika mikoa 26 ya Tanzania. CUF imeenea kila mkoa. Katika wilaya 130, CUF iko wilaya 117, katika vitongoji 38,000, CUF ina 20%, katika vijiji 11,600, CUF ina 15%. Mitaa yote 3,080, CUF ina 20%.”
Kwa hivyo, CUF iliyosimama leo hii kama taasisi imara ya kisiasa, imewezekana kuwa hivi kwa sababu ya juhudi kubwa zilizofanywa na Mzee Mloo na wenzake. Hakuna chochote tunachoweza kukifanya kukumbuka mchango uliotukuka wa Mzee wetu huyu, zaidi ya kutimiza ile ndoto yake ambayo daima aliishi nayo, yaani kuiona CUF kikiwa kinaongoza Serikali za Muungano na Zanzibar, kikitekeleza sera yake ya neema na haki sawa kwa wote.
Sisi tuliobakia nyuma yake, tunaahidi kwamba tutaitimiza dhamira na azma hiyo ya waasisi wa Chama hiki, akiwemo Mzee Mloo, kwa manufaa ya nchi na vizazi vijavyo. Tunaahidi kuwa CUF aliyoiasisi, kuijenga na kuisimamia kwa siku zote za uhai wake itaendelea kuwa taasisi imara ya kisiasa.
Katika wakati huu mgumu, tunaunganika na familia ya Mzee Mloo – hasa Mama yetu, Mama Mloo, na watoto wake – kumuombea dua. Mwenyezi Mungu ampokee mja wake akiwa ameshamsamehe makosa yake na aufanye mwema ujira wake. Amin.
Kwa heshima ya Mzee wetu huyu, mwasisi wa Chama chetu na kiongozi wetu mstaafu, Marehemu Shaaban Khamis Mloo, bendera zote za CUF nchi nzima zitapepea nusu mlingoti kwa siku tatu kuomboleza kifo chake.
HAKI SAWA KWA WOTE
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba,
Mwenyekiti
Comments : Leave a Comment »
Categories : Haki za Binaadamu

Maoni