Spika Sitta, Pinda wametupotosha

31 01 2009

JANA Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akijibu swali bungeni lililotaka kujua ni lini viongozi wa kiserikali kama rais wataacha kutumia ziara za kiserikali kufanya shughuli za kichama, kama alivyofanya Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni huko Pemba, alisema rais ni mkubwa wake wa kazi na yeye asingeweza kutoa kauli ya kile kinachodaiwa kuwa alikisema, kwa sababu hakuwepo, na hajui ni nini rais alisema, zaidi ya kusoma tu kwenye vyombo vya habari.

Zaidi ya majibu hayo ya Pinda, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, aliingilia kati kumsaidia waziri mkuu na kusema kwamba hakukuwa na haja ya swali hilo kujibiwa, kwani liko wazi.

Kwamba haiwezekani kutenganisha kofia mbili alizonazo rais, yaani ile ya urais na ile ya kuwa mwenyekiti wa chama chake, na kusisitiza kuwa hata katika nchi zilizoendelea sana kama Marekani, rais wao hutumia ndege ya serikali ‘Air Force One’ kufanya ziara ya kichama.

Kwanza, sisi tunasisitiza tena kuwa si sahihi kwa rais wala kiongozi yeyote wa serikali kutumia ziara za kiserikali ambazo kimsingi zimegharamiwa na kodi za Watanzania wote kutoa hotuba, kauli, kufanya shughuli au jambo lolote kwa masilahi ya chama chake cha siasa.

Si sahihi, kwa sababu mtu anapokuwa kiongozi wa kiserikali, wajibu wake ni kuwatumikia Watanzania wote bila kujali chama chake.

Pili, kiongozi wa kiserikali kufanya shughuli kwa masilahi ya chama chake cha siasa wakati akiwa kwenye ziara ya kiserikali, ni kuruhusu mgongano wa kimasilahi kati ya masilahi ya chama chake na masilahi ya taifa, ambayo ndiyo hasa anayopaswa kuyasimamia wakati huo akiwa kwenye ziara hizo za kiserikali.

Tatu, hatukubaliani na upotoshaji wa Spika Sitta kuwa haiwezekani kwa rais kutenganisha majukumu yake kama rais na kama mwenyekiti wa CCM, kwani sisi tunaamini kuwa inawezekana, kinachotakiwa ni kwa mhusika (Rais Kikwete) kuwa na utashi na utayari wa kutodharau misingi ya utawala bora wala kuwa mwepesi wa kubagua wafuasi wa vyama vingine vya siasa pindi awapo kwenye ziara za kiserikali.

Nne, Rais Kikwete anapaswa kupanga muda wa kufanya ziara za kichama ambao utakuwa ni tofauti na ule wa ziara za kiserikali, na anapaswa kutumia ruzuku ya CCM kwa ziara za kichama, badala ya kudoea usafiri wa kiserikali halafu anakwenda kuzungumzia mambo ya CCM kama alivyofanya Pemba hivi karibuni.

Akiona ni vigumu, basi aache ziara zake za kichama zifanywe na Makamu Mwenyekiti wake, Pius Msekwa, au Katibu Mkuu wake, Yusufu Makamba, pale inapolazimu.

Tano, kauli ya Pinda kuwa hawezi kutoa kauli kuhusu kile alichokisema Rais Kikwete, eti kwa sababu ni mkuu wake wa kazi, ni ya upotoshaji.

Pinda kwa nafasi yake kama Waziri Mkuu, ndiye mtu wa mwisho anayepaswa kujibu au kutoa ufafanuzi wa jambo lolote linalohusu serikali na maadili ya viongozi wake, akiwemo rais.

Kwa nini Pinda anasema hakuwepo na hajui alichokisema rais? Kama vyombo vya habari viliandika uongo kuhusu kile alichokisema Kikwete kule Pemba, serikali iliyo chini ya Pinda kama Waziri Mkuu, ilishindwa vipi kutoa taarifa ya kukanusha kile kilichoripotiwa kupitia mwandishi wake, Salva Rweyemamu?

Kwa nini Pinda anaviamini tu vyombo vya habari pale vinaporipoti mambo mazuri ya viongozi lakini haviamini pale vinaporipoti kauli zisizofaa za rais?

Tunautaka umma wa Watanzania uelewe kuwa majibu yaliyotolewa bungeni na viongozi hawa ni ya upotoshaji, ni wajibu wa kila mwananchi kutochoka kuwarudisha kwenye mstari viongozi wetu pale wanapofanya ndivyo sivyo.

Chanzo: http://freemedia.co.tz





CUF kufuta nyayo za JK Zanzibar

31 01 2009

Na Exuper Kachenje
CHAMA Cha Wananchi (CUF) kimeandaa mkutano wa hadhara utakaofanyika kesho mjini Zanzibar kujibu hoja za Rais Jakaya Kikwete alizotoa alipokuwa kwenye ziara visiwani humo.

Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma, Salim Biman alisema jana kuwa mkutano huo, utafanyika katika viwanja vya Kibandamaiti ambapo mgeni rasmi atakuwa Mwenyekiti wa chama hicho , Profesa Ibrahim Lipumba.

Biman alisema katika mkutano huo, Profesa Lipumba atajibu hoja mbalimbali za Rais Jakaya Kikwete, zikiwemo za, CUF kufuta ndoto ya kuiongoza Zanzibar, wanaobeza maendeleo ya CCM ni walevi tende na kuzungumzia uchaguzi mdogo wa ubunge jimboni Mbeya vijijini.

“Pia atazungumzia kauli ya Pinda kutaka wanaoua walemavu wa ngozi, wauawe na kujibu hoja mbalimbali alizotoa Rais kuikejeli CUF,” alisema Bimani.

Hivi karibuni akiwa ziarani Zanzibar, Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Chama Cha Mapinduzi (CCM), alitoa kauli mbalimbali zinazotafsiriwa na CUF kuwa kejeli na dharau dhidi yake.

Katika moja ya mikutano yake ya hadhara visiwani humo, aliyoifanya baada ya kufungua mradi wa maji wa Kengeja, Mkoa wa Kusini Pemba, Rais Kikwete alinukuliwa akisema “Ni muhimu kwa watu kukubali kuwa ipo serikali iliyoko madarakani hata kama wanaikataa jinsi ilivyoingia madarakani:

“Ukweli ni kwamba ipo na ni muhimu kwa watu wote kushirikiana nayo, katika kuleta maendeleo. Maana ukisubiri hiyo serikali yako, inaweza ikachelewa sana ama pengine isije kabisa katika uhai wako,” alisema Mwenyekiti Rais Kikwete.

Kuhusu kauli za wapinzani kubeza na kukejeli kuwa CCM wala SMZ haijaleta maendeleo yoyote kwa wananchi, Rais Kikwete aliwaambia wananchi hao wa Kengeja kuwa “Wananchi, hizi ni fitina tu. Unajua midomo kazi yake ni kusema. Unaweza kusema lolote hasa inapokuwa kwenye kufitini, kudanganya watu ili wakuchague,” alisema na kuongeza,

“Ujumbe wetu kwa wapinzani wetu ni rahisi kabisa, kuwa nyie endeleeni kuwachagua mnaowataka, lakini endeleeni kutukabidhi sisi serikali na dhamana ya kuleta maendeleo.
Wao wache waendelee kutia fitina, kubeza maendeleo, lakini maji safi, wanaendelea kunywa; barabara wanaendelea kupita wakipeperusha bendera zao kwa sababu zinateleza kama mgongo wa ngisi.”

Katika mkutano wake mwingine visiwani humo, Kikwete alisema watu hao wanaobeza maendeleo na serikazi ya Mapinduzi Visiwani humo ni walevi wa pombe ya kienyeji aina ya tende inayotengezwa na kunywewa Zanzibar.

“Watu wengine sijui wanakunywa tende, maana mtu mzima na akili yake anadiriki kusema hakuna maendeleo, wakati anapanda gari hatikisiki kwa sababu ya barabara zilizojengwa na CCM, manawe haugui na hafi kwa kuwa hakuna malaria, lakini mtu huyo anasemaaa, mpaka mapovu ya mdomo yanamtoka kulia na kushoto, wee sema, mfereji unatoa maji, wao watasema mfereji utatoa maziwa, na kila siku wanashangaa, kwa nini hawashindi, jibu ni kwamba hawasemi ukweli,” alisema

Biman alisema Profesa Lipumba atazungumzia kauli hizo kwenye mkutano huo ambao utafanyika kuanzia saa 8:00 mchana ambapo pia atazungumzia chaguzi mdogo wa Jimbo la Mbeya Vijijini uliofanyika hivi karibuni na mgombea wa CCM kuibuka kidedea.

Aidha katika siku za karibuni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akiwa katika ziara mikoa ya kanda ya Ziwa alinukuliwa akisema “Mkimuona mtu akamkata mwingine shingo naye amueni cha kumfanya kwani sasa viongozi wote tumechoka… no more, I can’t tolerate anymore (imetosha, siwezi kuvumilia tena).”

Kuhusu uchaguzi huo, mgombea wa CUF aliishia kupata nafasi ya pili huku chama hicho na vingine vya upinzani walitoa madai mbalimbali kuulalamikia uchaguzi huo, ambao idadi ya watu waliopiga kura ilikuwa chini ya asilimia 45 ya watu waliojiandikisha kupiga kura.

Kwa mujibu wa Biman, Jeshi la Polisi Zanzibar limeridhia na kutoa kibali cha kufanyika Mkutano huo akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuhudhuria mkutano muhimu.
Hata hivyo Pinda aliviomba vyama vya siasa kushirikiana na wananchi kuhakikisha suala la mauji linakwisha kwa kuwa ni rahisi kulimaliza tatizo hilo iwapo watakuwa kitu kimoja katika kuondoa kashifa.

Chanzo: http://mwananchi.co.tz





Profesa Lipumba amtaka Jaji Makame ajiuzulu

31 01 2009

Na Kizitto Noya

SIKU chache baada ya Chama cha Wananchi (CUF), kushindwa katika uchaguzi wa Mbeya Vijijini, mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, ameibua shutuma nzito dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na kumtaka mwenyekiti wake, Jaji Lewis Makame, ajiuzulu.

Profesa Lipumba aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, akiwa Mtendaji wa tume,Jaji Makame, anapaswa kujiuzulu na tume hiyo kuvunjwa na kuundwa upya, kwa sababu imeshindwa kusimamia chaguzi huru na haki.

Alisema kushindwa kwa chama chake katika uchaguzi wa Mbeya Vijijini na wapigakura wengi kutojitokeza kupiga kura, kumetokana na udhaifu wa tume hiyo, katika kusimamia uhuru na haki katika chaguzi.

“Kampeni zilitawaliwa na vituko vya mashabiki kupigwa, bendera za CUF kuchanwa, masunduku ya kura kukutwa kwa watendaji wa CCM, FFU kuwatisha wananchi na kasoro nyingine nyingi ambazo CUF imeziripoti kwa msimamizi wa uchaguzi na polisi,” alisema Profesa Lipumba.

Akitoa mfano wa tukio moja baada ya jingine, Profesa Lipumba alisema, katika kata ya Ikukwa, CCM iliingilia kampeni za CUF, kubandua mabango ya mgombea wa chama hicho na kuchana bendera zake huku baadhi ya makada wake, wakinunua kadi za wapigakura kwa fedha taslimu.

Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, Daftari la wapigakura lilikuwa na udhaifu mkubwa uliojitokeza kwa majina ya watu waliofariki dunia kuendelea kuwepo na wengine kujiandikisha zaidi ya mara moja.

Akizungumzia suala hilo, Jaji Makame alimpuuza Profesa Lipumba akisema, anongea asichokijua.

Jaji Makame aliliambia gazeti hili jana kuwa tume yake haihusiki na matukio yote aliyoyaeleza Profesa Lipumba na kwamba uchaguzi huo ulifanyika chini ya msimamizi maalum.

“Hivi ni kweli Lipumba hajui kama kama tume imeshatoa masanduku, anayepaswa kuyatunza ni msamamizi wa uchaguzi,” alihoji na kuendelea, “Hata kama masanduku yalikutwa kwa balozi, baada ya kuyakagua polisi walikuta nini ndani yake.”

Kwa mujibu wa Jaji Makame, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ilijitahidi kadiri ilivyoweza kufanya uchaguzi wa Mbeya Vijijini, kuwa huru na wa haki, lakini kilichovuruga ni kuondolewa kwa mgombea wa Chadema katika suala la kisheria.

“Sababu za matatizo hayo sio Tume kwani imefanya kila liwezalo ikiwamo kutoa elimu ya uchaguzi katika vijiji vyote vya Mbeya ambako huenda Lipumba hakufika. Hapa kuna sababu nyingine, na sisi tunaungana na watu wanaosema kuwa uchache wa wapigakura umetokana na Chadema kuenguliwa kwenye uchaguzi huo,” alisema.

Alisema ingawa hiyo ndiyo sababu ya msingi, halalamiki kwani Chadema iliondolewa kwa mujibu wa sheria za uchaguzi na wala isingekuwa vyema tume kukiuka sheria hiyo kwa sababu ya kuuhamasisha uchaguzi huo.

Uchaguzi mdogo wa ubunge Mbeya Vijijini ulifanyika Januari 25 mwaka huu ambapo watu waliopiga kura walikuwa 44,855 kati ya 127780 waliojiandikisha. Kura halali zilikuwa 4394, na kura zilizokataliwa zilikuwa 914.

Mgombea wa CCM Mchungaji Lackson Mwanjali alishinda kwa kura 32867 sawa na asilimia 73, CUF ilipata kura 10,578 ambazo ni asilimia 23 na Chama Cha Sauti ya Umma (SAU) kiliambulia kura 496 sawa na asilimia moja hivyo kura zote zilizopigwa ni sawa na asilimia 35.

Siku moja baada ya Tume ya Uchaguzi kutangaza matokeo hayo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimejigamba kwamba asilimia 65 ya watu ambao hawakujitokeza kupiga kura, ni watu waliotaka kikipigia kura chama hicho.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zitto Kabwe aliliambia gazeti hili jana kuwa watu hao ni wapenzi na wanachama wake ambao wameamua kutojitokeza kwa sababu ya chama hicho kuenguliwa.

Kabwe alitoa kauli hiyo baada ya Mwananchi kumtaka asema endapo anadhani kuwa idadi ya wapigakura ambao hawakujitokeza, ni wapenzi na wanachama wa Chadema.

“Unachosema ni kweli ni hii ni kwa sababu Tume imemwengua mgombea wetu ambaye alikuwa chaguo la wengi,” alijibu kwa ufupi Kabwe na kuongeza kuwa wapiga kura hao waligoma kupiga kura kwa sababu walimkosa yule waliyetarajia kumchagua ambaye ni mgombea wa chama hicho alienguliwa katika kinyang’anyiro hicho Sambwee Shitambala.

Chanzo: http://mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=9638





Kikwete aambiwa hajui maana ya maendeleo

27 01 2009

Date::1/26/2009

Na Salim Said

BAADA ya Rais Jakaya Kikwete kusema kuwa, wanaobeza maendeleo yaliyoletwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ni walevi wa pombe ya kienyeji aina ya tende, Chama cha Wananchi (CUF), kimesema amekikejeli kwa wananchi na kumtaka asipime maendeleo kwa kuangalia barabara, bali maisha ya watu.

Wakizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana, viongozi wa ngazi za juu wa CUF walisema, Rais Kikwete hajui maana ya maendeleo kwa kuwa anayapima kwa kutumia barabara badala ya kuangalia maisha ya watu.

Walisema inaonekana Rais Kikwete amefanya ziara hiyo kwenda kuwakejeli kwamba ni walevi wa pombe aina ya tende.

Juzi Rais Kikwete alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa wanaobeza maendeleo yaliyoletwa na SMZ na Serikali ya Muungano kuwa ni walevi wa pombe ya kienyeji aina ya tende.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Juma Duni Haji, alihoji kama maendeleo yanapimwa kwa kuangalia barabara na kuvalishwa kofia ya kiua (maua) na wananchi wa Nungwi basi wanampongeza rais.

“Kama maendeleo yanapimwa kwa kuangalia barabara za kwenda uchochoroni na kuvalishwa kofia ya kiua na wananchi wa Nungwi, basi tunampongeza rais wetu,” alibeza na kuongeza. “Barabara zote zilizopo Zanzibar ambazo Rais anasema kuwa ni maendeleo, kwa ubora hazikaribii hata barabara moja tu ya kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.”

Alikumbusha kuwa, ahadi ya hayati Mzee Abeid Amani Karume kwa Wazanzibari kuhusu kupata elimu, maji na afya bila ya malipo ilikufa pamoja naye, kwani mpaka sasa hakuna hata kimoja kati ya hivyo kinachotolewa bila ya malipo.

“Karume alienda Pemba miaka ya 60 wakati kuna njaa kali na watu wanakula machochoni, akawakejeli kwa kusema: ‘Angalia watu mambo yao, wanang’ara hadi nyuso zao’. Wananchi wakakasirika na yeye (Kikwete) leo anakuja kutukejeli!” alisema Duni.

Aliishutumu kauli za Kikwete kuwa ni za kilaghai na kwamba, zinalenga kujipendekeza kwa SMZ na Rais Amani Karume ili petroli ambayo ipo Zanzibar iweze kunyonywa na upande mmoja wa Muungano.

“Lakini sisi tumeshazishtukia kauli hizi ni za kilaghai, zinalenga na kujipendekeza kwa SMZ na Rais Amani ili wanyonye petroli yetu, hatukubali,” alidai Duni.

Aliponda kwamba, serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar haijafanya chochote kwa fedha zao na kwamba hata barabara zinazosemwa zimejengwa kwa fedha za wahisani.

Duni alisema Januari 30, mwaka huu watafanya mkutano mkubwa katika viwanja vya Kibanda Maiti, Zanzibar ambako wanakusudia kumwelewesha Rais Kikwete maana ya maendeleo.

Hata hivyo, alidokeza kuwa maendeleo ni ajira, elimu nzuri, miundombinu ya kutosha, afya zuri na maji safi ya kunywa, lakini leo ni miaka 49 ya Mapinduzi, wananchi wa Pemba wanatumia umeme wa jenereta, umeme wa Kivunge asubuhi upo jioni haupo,” aliponda na kuongeza:
“Huko Nungwi alikopewa kofia ya kiua juzi kaulizwa swali mbele ya wananchi kwamba, kuna hoteli nyingi za kitalii, lakini mbona wafanyakazi wote wanatoka Kenya na Uganda kwa sababu ya elimu? Lakini hakujibu. Je, haya ndio maendeleo?

Naye Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alisema, malengo ya ziara ya Kikwete visiwani humo mwaka huu ni kuwakejeli wananchi na si vinginevyo.

“Yeye ni rais wa wote, kwa hiyo anapaswa kusikiliza kero za wananchi na kuzifanyia kazi na si kutoa kauli za kejeli kama hizi, au hajui maana ya tende? Sasa ukiona kiongozi anasema kuna maendeleo na walengwa wanasema hakuna, ujue kuna tatizo hapo,” alisisitiza Maalimu Seif.

Alisema Rais kapotoka na anapaswa kujirekebisha kwa kuwa yeye kama kiongozi wa Watanzania wote, hapaswi kutoa kauli za kejeli na kinafiki kama hizo.

Alidai kuwa, mara ya kwanza Rais Kikwete alifika Zanzibar mwaka 1977 kwa hiyo haijui Zanzibar, vinginevyo kama angefika miaka ya 1960 kabla ya Mapinduzi angekuwa anaijua vizuri na asingethubutu kutoa kauli za kejeli kama anazotoa sasa.

“Kabla ya Mapinduzi Zanzibar kulikuwa na maendeleo, lakini yote wameyafuja na sasa wanaanza alfa kwa ujiti (mwanzo), halafu wanatumia ushabiki wa kisiasa na kutumia vibaya majukwaa kujisifu. Wajisifu kwa lipi kubwa walilofanya zaidi ya kuharibu?” alihoji Maalim.

“Wito wangu, namwomba rais wangu Kikwete akija Zanzibar, aje kwa nia ya kujua kero za wananchi na kuzifanyia kazi na huo ushabiki wake wa CCM auache huko huko Dar es Salaam,” alisema Seif.

Katika ziara yake ya wiki mbili Unguja na Pemba, Rais Kikwete amejikuta akipandisha hasira na chuki za wananchi wa visiwa hivyo kutokana na kauli zake, ambazo zimetafsiriwa kuwa ni za kuwakejeli wananchi na kuongeza mpasuko wa kisiasa visiwani humo.

Chanzo: http://mwananchi.co.tz kama ilivyochukuliwa 27 Januari 2009





CUF haiyatambui matokeo ya Ubunge Mbeya Vijijini

27 01 2009

Brandy Nelson, Mbeya

WAKATI Tume ya Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbeya Vijijini ikimtangaza mgombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mchungaji Luckson Mwanjali kuwa mshindi, Chama cha Wananchi (CUF), kimeyakataa matokeo hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya matokeo ya awali kutangazwa, Mwenyekiti wa CUF, Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba alisema chama chake hakiyatambui matokeo hayo kutokana na kuwepo kwa kasoro nyingi kuanzia wakati wa kampeni na siku ya upigaji kura.

Alisema matatizo ya awali ni pamoja na kampeni za CUF kuingiliwa na viongozi wa kampeni na kutoa mfano kuwa, katika kata ya Ikukwa baada ya chama hicho kufanya mkutano wao, CCM walitumia watu hao hao waliokuwa katika mkutano huo, jambo ambalo ni kinyume na utaratibu wa kampeni za uchaguzi.

“Kwa mfano katika kijiji cha Ikukwa ilikuwa ni siku ya chama chetu kufanya mkutano hapo na CCM ikawa na ratiba katika eneo hilo. Lakini cha kushangaza tulipomaliza mkutano wetu na wao wakaingia na kufanya mkutano katika eneo hilo hilo ambalo sisi tulikuwa tumewakusanya watu,” alilalamika Lipumba.

Alisema kuwa matatizo mengine ni pamoja na kupigwa kwa mwanachama wao na wafuasi wa CCM, kushushiwa bendera pamoja na kuchana picha ya mgombea wao.

Hata hivyo, alisema CCM waliomba msamaha baada ya suala hilo kufikishwa Tume ya Uchaguzi na kuzikutanisha pande zote mbili.

Profesa Ibrahim alisema kuwa, tatizo kubwa ambalo ndilo lililochangia watu wachache kutojitokeza kupiga kura ni watendaji wa vijiji na kata kuzuia shahada za wapigakura kwa kisingizio cha kuwapa vocha za mbolea ya ruzuku.

“Tatizo kubwa ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa wananchi kutopata haki ya kupiga kura, ni watendaji wa baadhi ya vijiji waliohodhi shahada za kupigia kura za wananchi kwa madai kuwa watapata vocha ya mbolea ya ruzuku,” alisema na kuongeza:

“Mwananchi wa Kijiji cha Msituni, Kata ya Iwindi, Ezekieli John alituambia kwamba hawezi kupiga kura kwa sababu shahada yake ilichukuliwa na balozi wa nyumba kumi na taarifa hiyo tumeipeleka polisi,” alilalamika Profesa Lipumba.

Mwenyekiti huyo alibainisha matatizo yaliyojitokeza siku ya kupiga kura kuwa ni pamoja na vituo vingi kutokuwa na majina ya wapigakura na kwamba, hata sehemu ambayo yalibandikwa hayakuwa sahihi.

Aliongeza kuwa, katika baadhi ya vijijini vya kata za Ilembo na Santilya vituo vilikuwa na umbali wa kilomita saba hadi kumi kutoka maeneo wanayoishi wananchi, hivyo kusababisha baadhi yao kushindwa kupiga kura.

“Siku ya kupiga kura tulifanikiwa kuwakamata vijana wakiwa na masanduku ya kupigia kura, hivyo hayo yote ni mlolongo wa kasoro ambazo zimejitokeza na kutufanya sisi tusiyakubali matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi,” alisema.

Alisema kuwa kwa sasa wanaandaa utaratibu wa kuwasiliana na wanasheria wa chama chao ili kupata ushauri wa hatua za kuchukuliwa.

Alalamika kuwa, kuna tatizo kubwa la kiutendaji ndani ya tume, kwani watendaji wake waandamizi wako Dar es Salaam badala ya kuwepo maeneo yote ya wapigakura ili kubaini matatizo hayo mapema.

“Unajua, tume haiwezi kumwadhibu mkurugenzi wa wilaya ambaye ndiye msimamizi wa uchaguzi kwa kuwa yeye si mwajiriwa wa tume, bali ni mkubwa wake wa kisiasa ambaye ni mkuu wa Wilaya ambaye ana uwezo kumshawishi atakavyo, ikiwamo kuhakikisha CCM inapata ushindi,” alisema.

Profesa Lipumba alisema kuwa, kuna umuhimu mkubwa wa kuwepo kwa tume huru ambayo itaweza kufanya kazi kwa kuhakikisha inafika maeneo ya vijijini ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya uraia ili wananchi wote wapate haki ya kupiga kura.