JK amebebeshwa mzigo wa Mkapa – Lipumba

28 11 2008

2008-11-27 12:05:44
Na Mashaka Mgeta Dar na Thobias Mwanakatwe, Mbeya

Katika kauli nadra kutolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesifu ujasiri uliounyeshwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wa kuthubutu kuwafikisha mahakamani vigogo wa serikali ya Awamu ya Tatu kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Sambamba na pongezi hizo, Lipumba pia alimshukukia Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, kuwa ni chimbuko la matatizo makubwa ya kiufisadi yanayoshughulikiwa na serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete kwa sasa.

Profesa Lipumba alisema Rais Mstaafu Mkapa anapaswa kuunganishwa katika kesi zinazowakabili waliokuwa mawaziri wake wawili, Basil Mramba na Daniel Yona.

Mramba ambaye ni Mbunge wa Rombo (CCM) na Yona, waliwahi kuwa mawaziri wa wizara tofauti, katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu.

Mramba aliteuliwa tena na Rais Jakaya Kikwete kuwa Waziri wa Miundombinu katika Serikali ya Awamu ya Nne.

Wote wawili (Mramba na Yona), wanashitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar e s Salaam, kwa makosa 13 yanayohusu matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7.

Akitoa maoni yake kuhusiana na hatua hiyo, Profesa Lipumba alisema kwa kuwa mawaziri wanafanya kazi ya maelekezo ya Rais, kuna haja ya kufanya uchunguzi ili kama kutakuwa na ushahidi unaomuhusisha Mkapa, aunganishwe katika kesi hiyo.

“Tunajua mtu aliyekuwa Rais ana kinga, lakini kinga hiyo ni kwa maslahi ya Taifa, kwa kuwa hili limeonekana ni suala la kufanya makosa, akibainika kuhusika kutumia vibaya mamlaka ya nchi, aunganishwe na kuwajibishwa,“ alisema.

Hata hivyo, Profesa Lipumba alisema ushahidi uliokusanywa, unastahili kutumika ipasavyo, ili kulifikisha shauri hilo katika hatua ya kutolewa hukumu dhidi ya washitakiwa hao.

Pia alisema Mkapa ana kila sababu ya kuwaomba radhi Watanzania kutokana na mawaziri na viongozi wengine wakati wa kipindi chake kujiingiza katika vitendo vya rushwa na ufisadi ambavyo vimesababisha nchi kuyumba kiuchumi na maisha ya wananchi kuwa magumu.

Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na mamia ya wananchi wa jiji la Mbeya kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Ruanda Nzovwe.

Alisema vitendo vya rushwa kwa mawaziri na watendaji wakuu wa serikali, vilishamiri wakati wa uongozi wa Mkapa.

“Ununuzi wa rada ambao umeleta utata mkubwa kutokana na gharama kubwa zilizotumika, masuala ya wizi wa fedha za EPA pamoja na kuingia mikataba feki yenye utata, imetokea kipindi cha uongozi wake,“ alisema.

Alitolea mfano wa mgodi wa makaa wa Kiwira kwamba thamani yake ni zaidi ya Sh. bilioni tano, lakini uliuzwa kwa kampuni moja ya binafsi kwa Sh. milioni 700 tu.

Aliongeza kuwa, mikataba mibovu ya madini ambayo serikali yake iliingia na wawekezaji, pia imeiingiza nchi katika umaskini mkubwa.

Mwenyekiti huyo alisema utaratibu wa sasa wa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa EPA ni mzuri, lakini akataka serikali ianze pia kuwakamata na kuwafikisha kortini mafisadi wa Richmond.

Katika mkutano huo, wananchi wa jiji la Mbeya walimweleza Prof. Lipumba kuwa, wanashangazwa kuona serikali imekazana kuwakamata mafisadi wa EPA huku wale walioingiza serikali katika mkataba wenye utata wa Richmond wakiendelea kupeta.

Chanzo: http://www.ippmedia.com/ipp/nipashe/2008/11/27/127196.html





Mnyaa aishangaa Serikali kuhusu Richmond

27 11 2008

MJUMBE wa Kamati ya Bunge iliyochunguza zabuni ya kufua umeme wa dharura iliyoipa ushindi Kampuni ya Richmond, Habib Mnyaa, amesema haridhiki na kasi ya serikali katika kutekeleza mapendekezo ya Bunge kuhusu suala la Richmond

Mnyaa ambaye ni Mbunge wa Mkanyageni (CUF) aliliambia gazeti hili katika mahojiano maalum kwamba, kinachomkera zaidi ni serikali kukwepa kutekeleza pendekezo namba tatu la Bunge lililoitaka ipitie upya mikataba ya makampuni ya IPTL, Songas, Aggreko na Alston, ili kupunguza mzigo wa kuyalipa makampuni hayo zaidi ya Sh244bilioni kila mwaka, kama gharama za uwezo wa mitambo (Capacity charge).

Alisema tangu kutolewa pendekezo hilo Februari mwaka huu, serikali bado inaendelea kuyalipa makampuni hayo kiasi hicho cha fedha jambo ambalo ni hatari kwa uchumi wa taifa.

“Mimi kama mmoja wa wajumbe wa kamati ya Richmond, siridhiki na jinsi serikali inavyoshughulikia maagizo ya Bunge kuhusu Richmond kwa sababu baadhi ya vipengele muhimu havijatekelezwa,” alisema.

ALisema mbali na serikali kushindwa kutekeleza pendekezo hilo pia imekwama kutekeleza pendekezo namba 20 linaloitaka kuendesha uchunguzi wenye lengo la kubaini ukweli kwamba, taarifa ya awali ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhusu suala hilo ilichezewa ili kuficha ukweli.

“Bunge lilipendekezo utekelezaji wa suala hilo ufanyike ndani ya miezi mitatu kuanzia Februari mwaka huu, lakini serikali ilianza kuzungumzia utekelezaji Agosti na imeanza utekelezaji kwa kuchagua vipengele rahisi na kuacha vipengele vigumu ambavyo ndivyo msingi wa matatizo,” alisema.

Alisema uzembe huo wa serikali ndio unaochochea umaskini katika jamii hasa baada ya taifa kuendelea kupoteza mabilioni ya shilingi kuyalipa makampuni yanayozalisha umeme wa dharura, badala ya fedha hizo kutumika katika nyanja zingine za maendeleo.

Akichambua malipo ya kampuni moja hadi nyingine, Mnyaa alisema: “Richomond ilikuwa inalipwa Sh54.8bilioni kwa mwaka, IPTL inaendelea kulipwa Sh40.5 bilioni, Songas Sh99.6, Aggreko Sh 21.8 na kampuni ya Alston inalipwa Sh27.4,” alisema.

ALisema fedha hizo ambazo jumla yake ni Sh244.1bilioni zingeweza kutumika katika mambo mengine ya maendeleo ili kulinusuru taifa na umaskini.

Akichambua matumizi mbadala ya fedha hizo aliyosema kuwa ndiyo yangechangia maendeleo, Mnyaa alisema Sh244.1bilioni zingiweza kununua matrekta 5424 na kuyagawa katika kila jimbo la uchaguzi matrekta 23.

Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=8306





Lipumba ataka Mkapa naye apandishwe kizimbani

27 11 2008

Na Mwandishi Wetu

KUKAMATWA kwa vigogo wawili katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Bw. Basil Mramba (aliyekuwa Waziri wa Fedha) na Bw. Daniel Yona (aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini) kumeanza kuibua tafsiri mpya huku jinamizi la vigogo hao likionekana kuhamia kwa bosi wao wakati huo, Rais mstaafu, Mzee Benjmain Mkapa, Majira limebaini.

Vigogo hao walikamatwa na kufikishwa kortini juzi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makosa mbalimbali yanayohusu kuiingia Serikali hasara kutokana na uamuzi wao katika masuala mbalimbali walipokuwa mawaziri hususani mkataba kwa kampuni ya ukaguzi wa kampuni ya Alex Stewart.

Wakati wananchi wakifurahia kuanza kuonekana kwa makucha yaliyokuwa yamejificha ya Serikali ya Awamu ya Nne, wataalamu wa masuala ya siasa na utawala, wameanza kulitazama suala hilo kwa mtazamo mpana zaidi wakisema kashifa dhidi ya mawaziri Mramba na Yona ni wazi kuwa inakwenda mbali zaidi na kumgusa mkuu wao wa kazi.

Miongoni mwa watu wa kwanza kuvunja ukimya juu ya kufikishwa mahakamani vigogo hao na kusisitiza kuwa kunamgusa pia Mzee Mkapa ni Profesa Ibrahim Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na mchumi anayeheshimika kwenye Benki ya Dunia.

Profesa Lipumba amezidi ‘kumshikia bango’ Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP), Bw. Eliezer Feleshi, atangaze haraka yamuzi wa kumfungulia mashitaka Rais Mkapa.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa Shule ya Msingi Ruanda Nzovwe mkoani Mbeya, alisema Rais Mkapa ndiye anayejua masuala yote kuhusu upotevu wa fedha nyingi za umma ikiwemo katika masuala ambayo Mramba na Yona wametuhumiwa.

‘’Mkapa naye awekwe ndani, alikuwepo wakati wa mchakato…yeye ndiye alikuwa Rais, bila kuwekwa ndani, hakutakuwa na haki iliyotendeka…wahusika wote pia wa EPA wawekwe ndani kuanzia mdogo hadi mkubwa,’’ alisema Prof. Lipumba.

Hata hivyo kauli hiyo ya Profesa Lipumba ni sawa na mzigo mzito kwa DPP ambaye huenda akawa na wakati mgumu kuamua iwapo kuna hoja na haja ya kufikia kumshitaki Rais Mkapa hasa wakati huu ambapo Rais Jakaya Kikwete alikwishaweka bayana zaidi ya mara mbili kuwa hafikirii kuwashitaki Marais waliomtangulia.

Mara ya kwanza Rais Kikwete aliweka msimamo huo alipokuwa kwenye ziara yake ndefu ya nchi za Skandinavia na kusisitiza msimamo wake huo alipokuwa akijibu swali la Mhariri wa MwanaHALISI, Bw. Saed Kubenea wakati Rais alipohutubia taifa kupitia kwa wahariri wa vyomnbo vya habari.

Mtoto wa miaka 11

Katika mkutano huo kiliibuka kituko kufuatia mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mwakibete aliyejitambulisha kwa jina la Rupia Chaula (11) kumuuliza swali Profesa Lipumba sababu za watuhumiwa wa Richmond kutofikishwa mahakamani wakati wale wa EPA wameshaanza kuchukuliwa hatua hizo.

“Kwa nini watuhumiwa wa EPA wamepelekwa mahakamani na wa Richmond hawajapelekwa mahakamani?” aliuliza mwanafunzi huyo huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo.

Akijibu swali hilo Prof. Lipumba alisema anakubaliana na hoja zilizotolewa na kijana huyo na kusema kuwa huo ndio ukweli wa kinachotendeka katika utawala uliogubikwa na tuhuma za ufisadi kwa kuwakumbatia vigogo bila kuwafikisha katika mikono ya sheria.

“Wezi wa fedha za EPA ni wezi kama walivyo watuhumiwa wa Richmond, wachukuliwe hatua za kisheria na kufikishwa mahakamani kama wengine …Wao ndio wanahusika na mikataba mibovu…mikataba ya kifisadi ivunjwe iingiwe mikataba mipya yenye maslahi kwa wananchi,’’ alisema Prof. Lipumba.

Hata hivyo, kauli ya Profesa Lipumba ya kutaka Rais Mkapa ashitakiwe, huenda ikakumbana na utata wa kinga aliyonayo kiongozi huyo kikatiba, kinga amabayo hata hivyo rejea ya kisheria na kesi mbalimbali za mfano kutoka sehemu mbalimbali duniani, ina acha maswali mengi zaidi kuliko majibu.

Utafiti wa Majira umeonesha kuwa kwa mujibu wa ibara ya 46 ya Katiba ya Muungano Rais amepewa kinga dhidi ya kushitakiwa kwa makosa ya jinai au madai kwa kipindi akiwa madarakani na hata baada ya kuacha madaraka iwapo aliyoyatenda (akiwa madarakani) yamo katika mambo anayopaswa kuyafanya kwa mujibu wa kiapo chake.

Ibara hiyo imekuwa ikiibua utata wa tafsiri hapa nchini hasa juu ya ni wakati gani Rais aliyeko madrakani au mstaafu atachukuliwa kuwa ametenda jambo lililo nje ya kiapo chake au utekelezaji wake wa kawaida kisheria.

Katika ripoti za Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu hapa nchini bado hakujafikishwa shauri ambalo lingeweza kuifanya mahakama kutoa tafsiri kamili na ya moja kwa moja juu ya ukomo wa kinga ya Rais kwa mujibu wa ibara hiyo.

Shauri pekee ambalo walau lilijaribu kugusa nguvu za kiutendaji za Rais juu ya maamuzi yake lakini si moja kwa moja kinga ya kushitakiwa ni lile la Mwalimu Peter Mhozya V AG (Civil Case no 206, 1993) ambapo mlalamikaji alitaka Rais Alli Hassan Mwinyi aondolewe madarakani kwa kushindwa kulinda katiba ya nchi kwa ‘kunyamazia’ Zanzibar kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC).

Jaji Barnabas Samatta wakati huo, pamoja na kulitupa shauri hilo kwa kuwa kikatiba Mahakama haina nguvu za kumwondoa madarakani Rais, bali Bunge, hakujadili suala la kama Rais anaweza kushitakiwa au la kama ambavyo mwalimu huyo alivyokuwa amejaribu kufanya..

Hata hivyo maoni ya wanasheria jadidi waliobobea katika masuala ya katiba kama Profesa Issa Shivji, Profesa Jwan Mwaikusa na Dkt. Sengondo Mvungi katika maandiko yao na wanapopata nafasi ya kutoa maoni yao, yamekuwa yakionesha kuwa kinga ya kikatiba ya Rais ina ukomo.

Nchini Marekani, walau suala la kinga ya Rais limeshawekwa bayana kuwa lina ukomo awapo madarakani na hata anapokuwa ameshamaliza madaraka yake.

Awali katika shauri maarufu la Nixon v. Fitzgerald (1982), katika uamuzi wake wa majaji watano dhidi ya wanne, Mahakama ya Rufaa ya nchi hiyo iliamua kuwa katika shauri la Rais Richard Nixon kutakiwa kuunganishwa katika mashitaka kutokana na uamuzi wa kumfukuza kazi ofisa wa umma kuidhinishwa naye, ilihukumiwa kuwa Rais alikuwa na kinga ya kutoshtakiwa kwani hapo alikuwa ametekeleza nguvu zake za kisheria.

Lakini mtazamo huo ulibadilishwa katika shauri jingine mashuhuri la Jones V Clinton, Mahakama ya Rufani ya nchi hiyo ilipokubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu kuwa Rais Bill Clinton wakati huo akikabiliwa na kashfa ya ngono, hakuwa juu ya sheria kwa sababu alilolifanya ni suala binafsi lisilohusu miiko ya ofisi yake.

Katika shauri la kwanza Rais Nixon alikuwa ameshtakiwa kwa kuhusishwa na uamuzi alioufanya kama Rais na ni tofauti na shauri la Clinton ambapo kesi ilihusu masuala yake binafsi yasiyo sehemu ya kiapo chake cha Urais na aliyoyafanya kabla hajawa Rais.

Tofauti baina ya kesi hizi mbili zinaweza kuipa nguvu nadharia ya wasomi wa hapa nchini kuwa baadhi ya vitendo vya marais vina kinga iwapo tu vilifanywa kwa mujibu wa sheria na viapo vyao na si pale ambapo wamehusika kufanya ‘madudu.’

Chanzo: http://majira.co.tz/kurasa.php?soma=tanzania&habariNamba=9023





Lipumba `amkandia` Makamba

26 11 2008

2008-11-25 13:58:44
Na Thobias Mwanakatwe, Mbeya

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amempigilia msumari wa moto Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, kwamba iwapo ataendelea kushikilia wadhifa huo, CCM kitaendelea kuwa cha kisanii.

Akihutubia wananchi wa Kijiji cha Igoma, Kata ya Ulenje wilayani Mbeya Vijijini juzi, Profesa Lipumba alisema CCM kuendelea kumkumbatia Makamba, kitaendelea kukumbwa na migogoro isiyoisha.


”Chama makini kinatakiwa kuwa na viongozi makini wanaoweza kuleta maendeleo, lakini kama Makamba ataendelea kuwa Katibu Mkuu, ni usanii mtupu viongozi badala ya kuangalia shughuli za maendeleo watakuwa wanalumbana wao kwa wao,” alisema.

Alisema kutokana na mwenendo wa nchi, imefika wakati kwa Watanzania kuangalia nchi inakokwenda na kuacha ushabiki wa vyama.

Profesa Lipumba alisema viongozi wa CCM kuendelea kusuguana ni dalili mbaya kwamba, uongozi wa serikali ya chama hicho ni mbovu wananchi wanahitaji kuchukua uamuzi wa kufanya mabadiliko.


Kuhusu msafara wa Rais Jakaya Kikwete kupigwa mawe akiwa ziarani mkoani hapa Oktoba mwaka huu, alisema sio ufumbuzi wa matatizo yao wanachotakiwa ni kutochagua CCM.

Alisema iwapo tabia ya kupiga mawe viongozi itaendelea, nchi itapoteza viongozi suala ambalo baya kwa mustakbali wa nchi.

SOURCE: Nipashe





CUF yazoa wapiga kura 700 wa Karamagi

23 11 2008

Novemba 22, 2008

Na Kizitto Noya, Bukoba Vijijini

ALIYEKUWA Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi amepata pigo kwenye jimboni lake la Bukoba Vijijini, baada ya wapigakura wake 700 kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF).

Wapiga kura hao walifikia uamuzi huo baada ya wabunge wa CUF, Habib Mnyaa (Mkanyageni), Shoka Khamis Juma (Micheweni) na Severina Mwijage (viti Maalum) wakiongozwa na Katibu Mkuu wa CUF Seif Hamad kumchambua Karamagi katika mkutano wa hadhara kwa kumhusisha na kashfa ya kampuni ya Richmond.

Katika mkutano huo uliofanyika juzi jioni kwenye viwanja vya kata ya Ibwera, CUF ilichaumbua utendaji wa CCM na kumhusisha Karamagi na matukio ufisadi wa Richmond.

Shoka Khamis Shoka aliwauliza wananchi waliohudhuria mkutano huo sababu za kuendelea kumchagua Karamagi na CCM yake kuwaongoza wakati hajawahi kusema chochote bungeni kuwatetea tangu aingie madarakani mwaka 2003.

“Mimi na Karamagi tulichaguliwa pamoja kwa mara ya kwanza mwaka 2005, tangu niamfahamu bungeni sijasikia hata siku moja akichangia chochote kinachohusu jimbo lake zaidi ya kujitetea mwenyewe kwa kashfa zilizokuwa zikimkabili za Richmond na TICTS,” alidai Shoka.

Naye Savelina Mwijage aliwahoji wapigakura hao faida wanayoipa kwa kumchaugia baada ya kupata fulana na kofia za CCM kisha mbunge wao kutoweka mpaka uchaguzi mwingine.

Mbunge huyo ambaye mara nyingi alikuwa anazungumza kwa lugha la Kihaya, aliwataka wakazi wa jimbo kujiunga na chama hicho.

Akizungumza katika mkutano huo Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad, alisema Tanzania inatakiwa kufanya ya uongozi kwa kuwa CCM inachoka, inalewa madaraka na kuanza kuyumba.

Alisema migomo ya vyuo vikuu, walimu na kukithiri kwa vitendo vya ufisadi nchini ni dalili za CCM kushindwa kushughukia matatizo ya wananchi hivyo kutostahili kuendelea kupewa muda kuiongoza nchi.

“Nadhani Watanzania tunatakiwa tufikie mahali tufanye mabadiliko, tuiangalie CCM kwa makini na kutafakari inakopeleka kisha tufanye maamuzi mbadala ya kukiondoa madarakani,” alisema

Mkutano huo uliozoa wapigakura wa Karamagi, ilifuatiwa na mikutano kadhaa iliyofanyika katika jimbo la Bukoba Mjini Kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Khamis Kagasheki, ambako nako Seif aligawa kadi 1,900 kwa wanachama wapya wa CUF.

Maalim Seif yuko mkoani Kagera kwa ziara ya siku kumi ya ujenzi wa chama. Katika ziara hiyo anafungua matawi mapya ya CUF na kusimika viongozi wa matawi na kuwapa maelezo kadhaa ya kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani na Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=8231