CUF yalaani wazee wa EAC kupigwa, kushtakiwa

31 10 2008
Na Salim Said

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimelaani vikali hatua ya serikali ya CCM kutumia nguvu kubwa kuwaondosha barabarani wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) na kuwafungulia mashtaka.

CUF pia imeitaka serikali kufuta mara moja mashtata waliofunguliwa wazee hao badala yake ifungue mashtaka kwa wezi wa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) leo kama Rais Jakaya alivyoahidi.

Akisoma Maazimio ya Baraza Kuu la CUF lililomaliza jana kikao chake cha siku tatu kwenye ofisi za makao yake makuu, Mwenyekiti Ibrahim Lipumba alisema baraza kuu linalaani vikali nguvu kubwa iliyotumika kuwaondoa wazee hao barabarani.

Wazee hao, ambao kwa miaka kadhaa wamekuwa wakidai stahili zao za mafao baada ya kuitumikia EAC iliyovunjika mwaka 1977, walizuia Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, eneo la Daraja la Salender, ikiwa ni njia kuu inayounganisha mjini na maeneo wanayoishi vigogo wa serikali, wafanyabiashara wakubwa, mabalozi na wafanyakazi wa kada za juu katika taasisi za kimataifa na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa.

Waliamua kufanya hivyo ili kuishinikiza serikali kuwalipa fedha zao, lakini polisi iliingilia kati na kuwaondoa eneo hilo kwa kuwapiga, kuwamwagia maji ya kuwasha na kuwafungulia mashtaka.

Jana mwenyekiti huyo wa CUF, Prof. Lipumba alielezea kitendo hicho kuwa hakikufuata utaratibu wala kutumia cha busara.

”Tunalaani vikali hatua ya serikali kuwamwagia maji ya kuwasha, kuwapiga, kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wazee wetu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki,” alisema Prof. Lipumba.

Alieleza kuwa Baraza Kuu la CUF linaitaka serikali kuwafutia mashtaka mara moja wastaafu hao na kumtaka Wazara wa Fedha na Uchumi kuwalipa mafao yao mara moja.

”Mafao ni haki yao kwa kuwa waliitumikia sana nchi hii na wamevumilia vya kutosha… kwa nini wapigwe na kufunguliwa mashtaka wakati wezi wa EPA wanadunda barabarani,” alihoji Prof. Lipumba.

Profesa Lipumba alisema kuwa Baraza linashangazwa sana na hatua ya serikali ya CCM kuwakingia kifua mafisadi wa EPA wakati mamilioni ya Watanzania wakiendelea kuishi katika dhiki.

Lipumba aliahidi kuwa kama serikali haitawafikisha mahakamani wezi wa EPA baada ya Novemba mosi, chama chake kitawataka Watanzania wafanye maamuzi ya pamoja kuiadhibu CCM.

Alisema adhabu hiyo itakuwa ni pamoja na kufanya maandamano makubwa nchi nzima na kuwataka Watanzania waiondoe CCM madarakani wakati wa uchaguzi wa mwaka 2010.

Alimtaka Rais Jakaya Kikwete kuacha mara moja tabia yake ya kupuuza ushauri unaotolewa na viongozi wa siasa na dini ambao wanaitakia mema Tanzania.

”Kuongezeka kwa migogoro katika kila sekta ya nchi hii kunasababishwa na tabia ya Rais Kikwete ya kupuuza ushauri anaopewa, kwa hiyo Baraza Kuu linamtaka aache mara moja tabia hiyo,” alisema Prof. Lipumba.

Alieleza kuwa baraza lao pia linapinga hatua ya serikali kuingilia mamlaka ya Bunge kwa kuwazuia wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kujadili hotuba ya Rais aliyoitoa bungeni Agosti 21 mwaka huu kwa kuwa ni ukandamizaji wa demokrasia.

”Baraza kuu linaamini serikali kwa kutumia uongozi wa Bunge kuzuia mjadala wa hotuba ya rais, ni kuzuia mjadala wa ufisadi wa EPA na hatua zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya wahusika,” alisema Prof. Lipumba.

Alisema kuwa Baraza Kuu la CUF linamtaka Spika wa Bunge, Samwel Sitta kuheshimu kauli yake na maamuzi ya bunge kwa kuruhusu mjadala huo uendelee katika kikao kinachoendelea.

Kuhusu hoja ya nchi kujiunga au kutojiunga na OIC, Lipumba alisema haoni tatizo la kutojiunga na jumuiya hiyo kwa kuwa nchi kama Marekani na Urusi zimeomba kuwa wanachama kutokana na faida kubwa za kiuchumi na kijamii.

“Kama Marekani ya (Rais George W.) Bush na Urusi zimeomba uanachama wa OIC, sisi tunasubiri nini,” alihoji Profesa Lipumba.

Alisema kuna kila asababu ya Tanzania kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo kwa kuwa hali na uduni wa maisha ya wananchi umezidi.

Prof. Lipumba pia alilaani vikali na kwa nguvu zote kufungiwa na vitisho vinavyotolewa na viongozi wa CCM dhidi ya gazeti la MwanaHalisi.

Alisema Baraza Kuu halikubaliani hata kidogo na uamuzi uliochukuliwa na serikali dhidi ya gazeti hilo kwa kuwa ni wa kidikteta na kwamba sera hizo hazina nafasi tena duniani.

Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=7824





Kashfa ya EPA:Warioba, Lipumba waijia juu serikali

31 10 2008

Na Peter Edson na Noya Kizito

WAZIRI Mkuu wa zamani, Joseph Warioba amesema anashangazwa na kitendo cha serikali kufanya mazungumzo na wezi fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) badala ya kuwafikisha mahakamani akisema kufanya hivyo ni kuligawa taifa katika matabaka, ikiwa ni siku moja kabla ya muda wa mwisho waliopewa kurejesha fedha hizo.

Warioba, ambaye amekuwa akikemea rushwa, ukosefu wa uadilifu kwa viongozi wa umma na kuunga mkono harakati za kutetea wanyonge, alikuwa akizungumza kwenye kongamano la Haki za Binadamu lililomalizika jana jijini Dar es salaam.

Wakati Warioba akisema hayo, mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Ibrahim Lipumba pia alizungumzia suala hilo alipoitaka serikali kuwafikisha mahakamani wote waliochota fedha hizo, badala ya kuwasamehe wale watakaokuwa wamezirejesha kabla ya siku ya mwisho iliyowekwa na Rais Jakaya Kikwete ambayo ni kesho.

Katika hotuba yake kwenye kikao cha Bunge katikati ya mwaka, Rais Kikwete aliwapa muda wote waliochota fedha hizo ambazo ni Sh133 bilioni, kuzirejesha kabla ya Oktoba 31 na kwamba wale watakaoshindwa kufanya hivyo wafikishwe mahakamani ifikapo Novemba mosi.

Kauli hiyo ilitafsiriwa kama huruma kwa mafisadi hao na Warioba jana alipingana kabisa na uamuzi huo wa Kikwete.

“Hata kama wakirudisha fedha, wanatakiwa kuwajibishwa kisheria ili liwe fundisho kwa wengine,” alisema waziri mkuu huyo wa zamani ambaye ana kitaaluma ni mwanasheria.

“Serikali haikupaswa hata kidogo kufanya mazungumzo na wezi, badala yake ilitakiwa kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili wahukumiwe kwa sheria na si kwa mahojiano.

“Anapokamatwa mwizi, kisheria anatakiwa kufikishwa mahakamani. Hivyo ndivyo ilivyowapasa wezi hao wa EPA kufikishwa bila kuonewa huruma ili liwe fundisho kwa wengine ambao wana mpango wa kuliangamiza taifa hili.

“Kama ilivyo kwa Watanzania wengine wanavyofikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuhukumiwa kwenda jela kwa miaka mingi kwa kosa la wizi wa fedha ndogo, kadhalika hawa mabwana iliwapasa kuwajibishwa hivyo hivyo kwani huo ndio usawa.”

Alisema sheria inakata pande zote kwa usawa, lakini kitendo cha serikali cha kutochukua hatua mapema dhidi ya mafisadi hao tangu sakata hilo lianze, ni kukiuka na kuvunja misingi ya utawala bora na haki za binadamu.

“Jambo hili ni ukiukwaji wa haki za msingi za binadamu na matokeo yake ni mgawanyiko wa kimatabaka, ni vyema serikali ikaliona hili na kulishughulikiwa sawasawa,” alisema mbunge huyo wa zamani wa Bunda.

Alisema suala la kurudisha fedha bila kuchukuliwa hatua za kisheria, baadaye linaweza kuleta madhara makubwa katika jamii ikiwa ni pamoja na wananchi kukosa imani kwa serikali yao.

Suala la wezi hao wa fedha za EPA pia lilikuwa hoja kuu kwa Prof. Lipumba wakati akifungua kikao cha Baraza Kuu la CUF jijini Dar es salaam alipoeleza kuwa kurudisha mali ya wizi, sio mwisho wa sheria za nchi katika kushughulikia wezi.

“Nchi hii inaongozwa kwa misingi na taratibu za kisheria ambazo kwa mujibu wa katiba, hakuna mtu aliye juu yake,” alisema Lipumba, ambaye ni mchumi.

“Kwa mujibu wa sheria, wizi ni kosa la jinai na kurudisha mali iliyoibwa si mwisho wa adhabu ya kosa hilo, bali sheria inaelekeza kuwa mtuhumiwa wa kosa la jinai lazima afikishwe mahakamani.

“Nashangaa kusikia kwamba (mkurugenzi wa mashtaka) DPP anasubiri maagizo ya mwisho kutoka kwa rais ili kuona atawafanye watuhumiwa wa EPA. Nashangaa kwa sababu si rais anayeelekeza nani afikishwe mahakamani kwa kosa gani. Sheria zipo na hii ni kazi ya polisi, Takukuru na mwendesha mashataka.”

Alisema kusubiri maelekezo ya rais, ni kupingana na sheria za nchi ambazo zimeweka mwongozo wa namna ya kuwashughulikia wahalifu na badala yake kitendo hicho kinamaanisha kuwa serikali inawalinda watuhumiwa hao.

“Hii inaonyesha dola inakwepa kutekeleza majukumu yake katika suala hili na kusubiri maelekezo ya rais ni ishara tosha kuwa nchi imekosa uongozi bora na inahitaji jitihada madhubuti kuinusuru.”

Wizi wa fedha hizo uligundulika katika ukaguzi uliofanywa na kampuni ya Ernst & Young katika mahesabu ya Benki Kuu ya mwaka 2005/06 baada ya kuona malipo ya fedha yasiyo ya kawaida kwa wafanyabiashara wa ndani badala ya makampuni ya nje yaliyokuwa yanaidai.

Fedha hizo zilitokana na serikali kudhamini makampuni ya ndani kununua bidhaa nje kwa mkopo baada ya kuwepo upungufu mkubwa wa fedha za kigeni. Lakini baada ya makampuni ya ndani kulipa madeni hayo kwa serikali, fedha hizo zilibakia zikizagaa BoT kutokana na baadhi ya makampuni ya nje yaliyokuwa yakidai, ama kufilisika, kulipwa fidia na serikali zao ama kufuta madai yao na ndipo mafisadi walipozing’amua na kuzitengenezea mpango huo wa wizi.

Hadi sasa serikali inadai kuwa tayari Sh61 bilioni zimesharejeshwa na kwamba baadhi ya wahusika wameshadhibitiwa, ikiwa ni pamoja na kushikilia mali zao, ikiwa ni pamoja na fedha zilizo kwenye akaunti zao, na kuzuiwa kusafiri nje.





Lipumba: Kikwete basi 2010

31 10 2008

Na Deogratius Temba

BARAZA Kuu la Chama cha Wananchi (CUF) limesema linajipanga kuweka mkakati wa kuhakikisha Rais Jakaya Kikwete harudi madarakani ifikapo mwaka 2010 kwa madai kuwa nchi imemshinda.

Kauli hiyo ilitolewa jana kwenye makao makuu ya CUF Buguruni jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alipokuwa akifungua mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho.

Alisema hivi sasa nchi imekumbwa na machafuko ya kijamii yanayotokana na migomo na maandamano yasiyoisha, inayosababishwa na serikali ya Rais Kikwete kukosa uongozi imara.

“Mheshimiwa Kikwete, nchi imemshinda Baraza Kuu litakaa tuweke mkakati mkali wa kuikomboa nchi yetu, kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani, na ule mkuu wa mwaka 2010,” alisema Lipumba.

Alisema wananchi wa Tarime wamefungua njia, kwa kuichagua CHADEMA kwa kuiangusha CCM na hiyo imeonyesha ukomavu wa kupambana na dola.

“Nchi yetu inapita katika kipindi kizito sana, ukosefu wa uongozi bora umeanza kujitokeza kwa kila nyanja, rais amekuwa kiguu na njia kwa kukimbia badala ya kukaa Ikulu asikilize shida za wananchi,” alisema Lipumba.

Alibainisha kuwa Watanzania wamechoka ni lazima kila mtu ahakikishe kwa dhamira moja kuwa mwisho wa Kikwete unafikia ifikapo mwaka 2010.

Alisema ni vema CCM wajue kuwa Kikwete, waliyempa nafasi ya kuongoza hawezi tena kukiongoza chama na nchi.

Alibainisha kuwa kamwe rasilimali za nchi haziwezi kusimamiwa na watu wasio na mbinu za kuongoza.

Kuhusu malipo ya wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC), ambao wamekuwa wakiidai serikali kwa zaidi ya miaka 31, alisema ni aibu kwa wazee hao kujipanga barabarani, tena baadhi yao wakiwa uchi.

Alisema serikali imekuwa ikiahidi kila mwaka na kila rais aliyepita alisema wastaafu hao watalipwa madai yao, lakini kila serikali inapita na ahadi hizo hazitekelezeki.

“Wastaafu walishaahidiwa pesa zao kwanini kila siku maandamano, pigo la jana linapaswa kuwa fundisho kwa taifa hili na jumuiya za kimataifa zichukue hatua sasa. Walimu nao waliahidiwa kulipwa kwa kipindi kirefu na serikali ilishakiri kudaiwa na walimu inapaswa kuwalipa…” alisema Lipumba.

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema nchi imechafuka, kila mtu anashangaa ni nchi ya wendawazimu au ni binadamu gani wasiosikia vilio vya watu.

“Uongozi wa nchi hii, umeshindwa kabisa, jana (juzi) waandishi wa habari, na wahariri wao leo (jana) ni wastaafu, kesho kundi lingine litajitokeza, tutafika wapi,” alisema Maalim Seif.





Lipumba amvaa Kikwete, Mwanyika

31 10 2008

Na Gaudence Massati

IKIWA leo ni Oktoba 30, siku ambayo Rais Jakaya Kikwete ndiyo aliyoitaja kuwa ya mwisho kwa mafisadi waliochota fedha kwenye akaunti ya EPA kuzirejesha, huku bado kukiwa hakuna taarifa yoyote ya Serikali, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amewajia juu Rais Jakaya Kikwete na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Johnson Mwanyika.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza Kuu la Taifa la chama hicho, Profesa Lipumba, mchumi aliyebobea, amesema Rais Kikwete ameshindwa kuliongoza Taifa na kwamba chama chake kitazindua mkakati wa kuhakikisha anashindwa katika uchaguzi wa 2010.


Aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa nchi inapita katika wakati mgumu ambapo chanzo kikubwa ni ukosefu wa uongozi bora na makini.


Kutokana na hali hiyo, Prof. Lipumba aliwataka wajumbe wa mkutano huo ulioanza jana kutafakari kwa kina mkakati wa kitaifa wa Chama hicho wa kuhakikisha kuwa Rais Kikwete anaishia mwaka 2010, kwa kile alichokiita “nchi imemshinda na anawaweka wananchi kwenye wakati mgumu.”


“Utendaji duni wa Serikali ndiyo chanzo cha matatizo yote haya, hivyo hakuna haja ya kuhukumu magazeti, yenyewe ni lazima yaandike kila wanachoona,” alisema Prof. Lipumba.

Aliongeza kuwa ufisadi unaimaliza nchi na kwamba Watanzania wasitarajie mambo mapya katika taarifa ya mafisadi wa EPA ambayo amri ya Rai ilitaka wafikishwe mahakamani ifikapo Novemba mosi kama wameshindwa kurejeshwa. Hata hivyo Novemba mosi ni Jumamosi, siku ambayo mahakama hazifanyi kazi.


Alieleza wasiwasi wake pia juu ya hali aliyoiita ya kugwayagwaya ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu mafisadi hao, kwa kutamka kuwa anasubiri ripoti ya Rais ili aweze kuchukua hatua juu ya watuhumiwa, wakati jukumu la kushughulikia wahalifu ni la kwake na Jeshi la Polisi.


“Hiyo siyo kazi ya Rais, mtu akiiba haihitaji Rais aamue, hii ni kazi ya polisi na Mwanasheria Mkuu,
kama kweli angekuwa imara mafisadi wa EPA wangekwisha fikishwa kwenye mikono ya sheria,” alisema.

Awali Katibu mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Hamad alisema kikao hicho cha kawaida kinahudhuriwa na wajumbe 39 kati ya 49, kitajadili masuala mbalimbali kuhusu hatima ya nchi, kikiwa kama chama kikuu cha upinzani.

Chanzo: freemedia.co.tz





Tanzania bila CCM inawezekana – CUF

31 10 2008

Maazimio ya Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi kilichofanyika Ofisi Kuu Buguruni, Dar es Salaam, tarehe 29 – 30 Oktoba, 2008

Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, akisoma maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi kwa waandishi wa habari, kwenye ukumbi wa Ofisi Kuu za CUF, Buguruni 31 Oktoba, 2008

Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, akisoma maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi kwa waandishi wa habari, kwenye ukumbi wa Ofisi Kuu za CUF, Buguruni 31 Oktoba, 2008. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma, Mbaralah Maharagande

UTANGULIZI

Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) limekutana chini ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama, Mheshimiwa Prof. Ibrahim Lipumba, katika kikao cha kawaida kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni, mjini Dar es Salaam, tarehe 29-30 Oktoba, 2008.

Kikao hicho kilitanguliwa na kikao cha siku tatu cha Kamati ya Utendaji ya Taifa inayoongozwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, ambacho kiliandaa agenda za kufikisha mbele ya Baraza Kuu.

Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lilipokea, kuzijadili na kuzifanyia maamuzi agenda kumi (10) ambazo ni pamoja na Taarifa ya Utekelezaji wa Kazi za Chama kwa kipindi cha Julai – Oktoba 2008, Taarifa za Kambi ya Upinzani Bungeni na Kambi ya Upinzani katika Baraza la Wawakilishi, Taarifa ya Kazi za Madiwani wa CUF katika sehemu mbali mbali za nchi, Taarifa ya Uchaguzi wa Chama ndani ya Chama kwa Kanda D, E na F, Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Taifa, Mapendekezo ya Marekebisho ya Katiba ya Chama, Mapendekezo ya Kanuni za Jumuiya mpya zinazoanzishwa katika Chama – Umoja wa Wanawake, Jumuiya ya Vijana na Jumuiya ya Wazee, Taarifa ya Hali ya Kisiasa Nchini, Tathmini ya Ushirikiano wa Vyama vya Siasa vya Upinzani na Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Chama kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Baada ya mjadala wa kina kuhusiana na agenda hizo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limefikia maazimio yafuatayo kuhusiana na masuala hayo:

KUHUSU TAARIFA ZA UTEKELEZAJI WA KAZI ZA CHAMA, KAMBI ZA UPINZANI BUNGENI NA BARAZA LA WAWAKILISHI, MADIWANI NA UTEKELEZAJI MPANGO MKAKATI WA CHAMA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU WA 2010

LIMERIDHISHWA na kazi nzuri ya kusimamia shughuli za kisiasa na kiutawala inayoendelea kufanywa na Kamati ya Utendaji ya Taifa chini ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, na linaipongeza Taarifa ya Kazi za Chama ambayo imeonyesha utekelezaji wa mikakati madhubuti yenye kukielekeza CUF katika kuongoza harakati za Watanzania kujipanga kuing’oa CCM madarakani kupitia Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Linawapongeza Wabunge wa CUF wakiongozwa na Mkuu wa Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Hamad Rashid Mohamed, na Wawakilishi wa CUF wakiongozwa na Mkuu wa Upinzani katika Baraza la Wawakilishi, Mheshimiwa Abubakar Khamis Bakary, kwa kazi kubwa na ya kupigiwa mfano ya kuongoza mapambano dhidi ya ufisadi uliokithiri, kutowajibika na tabia ya CCM na Serikali zake ya kuwacheza shere wananchi kwa kutotimiza ahadi zake ilizozitoa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2005. Baraza Kuu linawapongeza Wabunge na Wawakilishi hao wa CUF kwa kutekeleza vyema wajibu wao wa kuwatetea wananchi kwa kuyafikisha matatizo yao katika Bunge na Baraza la Wawakilishi na kutoa sera mbadala ambazo zikitekelezwa zitawaondoa Watanzania katika dimbwi la umasikini unaosababishwa na ufisadi wa CCM na Serikali zake zilizochoka na zisizo na mawazo mapya tena.

LiNAWAPONGEZA Madiwani wa CUF kwa taarifa zao za kazi wanazozifanya katika Kata na Wadi zao na ambazo zimeonyesha jinsi gani wanavyowatumikia Watanzania bila ya ubaguzi wa kiitikadi katika maeneo yao, kuwapa huduma bora na hivyo kutoa taswira safi ya sera mbadala za CUF.

KUHUSU MAANDALIZI YA MKUTANO MKUU WA TAIFA WA CHAMA

LIMERIDHIKA na taarifa ya hatua zilizokwisha chukuliwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa katika maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama utakaofanyika mjini Dar Es Salaam, tarehe 23 – 27 Februari, 2009 na limeagiza hatua zilizobaki ziendelee kutekelezwa ili kufanikisha Mkutano Mkuu huo ambao unatarajiwa kutoa mwelekeo mpya wa CUF katika uendeshaji wa siasa za nchi hii na uongozaji wa harakati za kuing’oa CCM madarakani mwaka 2010.

LIMEAGIZA Wilaya za Chama nchini kote kusimamia vyema na kufanikisha zoezi la utoaji fomu kwa wanachama wote wanaotaka kugombea nafasi za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama na kuhakikisha kuwa misingi ya demokrasia iliyo wazi inazingatiwa na kufuatwa kikamilifu. Baraza Kuu linatoa wito kwa wanachama wa CUF nchini kote waliotimiza sifa kwa mujibu wa Katiba ya CUF kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi hizo na kujenga misingi ya demokrasia ya ushindani ndani ya Chama.

KUHUSU MAPENDEKEZO YA MAREKEBISHO YA KATIBA YA CUF NA KANUNI ZA JUMUIYA MPYA ZINAZOANZISHWA KATIKA CHAMA – WANAWAKE, VIJANA NA WAZEE

limeyapitisha Mapendekezo ya Marekebisho ya Katiba ya CUF ambayo yatafikishwa mbele ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama utakaofanyika mwezi Februari mwakani ambayo yanalenga kuongeza demokrasia kwa wanachama wa CUF katika kuwapigia kura za maoni wagombea Ubunge na Uwakilishi wa Chama, kuongeza uwakilishi wa wanawake katika vyombo vikuu vya maamuzi ya Chama kufikia asilimia 30% kama yalivyo matakwa ya SADC, kuimarisha uteuzi wa Wakurugenzi na Manaibu Wakurugenzi wa Kurugenzi za Chama na uanzishwaji wa Jumuiya za Chama za Wanawake, Vijana na Wazee.

LIMEIDHINISHA rasmi Kanuni za Umoja wa Wanawake wa CUF na pia kupitisha miongozo ya Kanuni za Umoja wa Vijana wa CUF na Jumuiya ya Wazee wa CUF ambazo zitakuwa ndiyo msingi wa uendeshaji wa Jumuiya hizo tatu za Chama. Baraza Kuu linatoa wito kwa wanawake, vijana na wazee wa Tanzania kujiunga kwa wingi na Jumuiya hizi tatu huku wakitambua kwamba hiyo ni sehemu muhimu mojawapo ya Mkakati wa Chama wa kuongoza mapambano ya kisiasa ya Watanzania waliochoshwa na ufisadi na ubabaishaji wa CCM ili kuking’oa chama hicho madarakani mwaka 2010.

KUHUSU TATHMINI YA USHIRIKIANO WA VYAMA VYA SIASA VYA UPINZANI

limesikitishwa na vitendo vilivyoonyeshwa na washirika wake katika Ushirikiano wa Vyama vya Upinzani nchini vilivyojitokeza hivi karibuni hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mdogo wa jimbo la Tarime ambavyo vimevuruga dhamira njema ya Watanzania ya kutaka kuona vyama vyetu vinashirikiana ili kutimiza malengo ya kuwaletea mabadiliko ya kweli yanayohitajika mno hapa Tanzania.

LIMEVUNJWA MOYO sana na kauli za vyama hivyo katika vipindi tofauti kutangaza kuwa Ushirikiano huu umekufa bila ya kufuata taratibu ambazo vyama hivi vilijiwekea wakati vinasaini makubaliano ya ushirikiano. Baraza Kuu limemuagiza Katibu Mkuu wa CUF kuwaandikia barua rasmi Makatibu Wakuu wa vyama vya Chadema, NCCR na TLP ili kujua kama bado vina nia ya dhati ya kuendeleza ushirikiano huo au vimejiondoa ili Watanzania wanaopenda mabadiliko wajue jinsi ya kujipanga wakati wanaelekea katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.

KUHUSU HALI YA KISIASA, KIUCHUMI NA KIJAMII NCHINI

linashtushwa mno na ukosefu wa uongozi (Leadership Vacuum) unaoonekana kutawala Serikali ya CCM ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambao unajidhihirisha kutokana na Serikali hiyo kushindwa kuyashughulikia ipasavyo masuala ya ufisadi uliokithiri hasa ule wa EPA, Richmond, IPTL, Kiwira, ununuzi wa rada na ndege ya Rais, ujenzi wa majengo ya Benki Kuu, kampuni za Meremeta, Mwananchi Gold na Deep Green, kupanda kwa kasi kwa gharama za maisha na bei ya bidhaa, kuyumba kwa uchumi, migogoro na migomo ya wafanyakazi na wanafunzi, mgogoro wa wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutolipwa haki zao, hali ya wananchi kukata tamaa mpaka kufikia hatua ya kuupiga mawe msafara wa Rais, kwafungia viongozi maofisini na hata wazee kulala barabarani, mpasuko na mgawanyiko wa kidini kati ya Waislamu na Wakristo, kushindwa kukamilisha mazungumzo ya CCM na CUF ya kutafuta ufumbuzi wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar na kuzidi kwa nyufa katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

linampongeza Mwenyekiti wa CUF, Mheshimiwa Prof. Ibrahim Lipumba, kwa kuwa mtu wa kwanza kulitanabahisha Taifa juu ya ukosefu wa uongozi hapa nchini wakati alipozungumza na Jukwaa la Wahariri wa Vyombo vya Habari mwezi Mei 2008 na pia kupitia hotuba yake makini aliyoiita “UKOSEFU WA UONGOZI NA HATIMA YA TANZANIA” ambayo aliitoa kwenye Kongamano lililoandaliwa na CUF kwa madhumuni ya kuwataka Watanzania waungane kukabiliana na hali hiyo na kuipumzisha CCM ambayo inaonekana wazi imechoka na haina tena uwezo wa kuiongoza Tanzania ya leo.

LINAMTANABAHISHA Rais Jakaya Kikwete kutoendelea na tabia yake ya kupuuza ushauri unaotolewa na viongozi wa CUF na Watanzania wengine wanaoitakia mema nchi yetu wa kumtaka apunguze safari za nje ya nchi na badala yake ajipe muda wa kutafakari hali hii ya kuongezeka kwa migogoro katika kila sekta ya maisha ambayo sasa imefikia hatua ya kutishia amani na utulivu wa nchi yetu. Baraza Kuu linaunga mkono wito uliotolewa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, wa kumtaka Rais Kikwete aitishe Mkutano wa Kitaifa utakaoshirikisha wadau mbali mbali ili kujadili mwenendo wa mambo hapa nchini na kwa pamoja kutafuta ufumbuzi wa migogoro hii inayotishia umoja na uhai wa Taifa.

linamtaka Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua ya kuwafikisha mahakamani mafisadi wote walioiba fedha za EPA ifikapo Novemba 1, 2008 kama alivyoahidi kupitia hotuba yake Bungeni ya tarehe 21 Agosti, 2008. Baraza Kuu linashangazwa na hatua za Serikali ya CCM kuwakingia kifua na kuwaonea huruma mafisadi hawa huku mamilioni ya Watanzania wakiendelea kuishi katika dhiki na shida kubwa kutokana na sera mbovu za Serikali hiyo ya CCM.

LINATOA mkono wa pole kwa familia za watoto 19 waliopoteza maisha yao Mjini Tabora, katika tukio la maafa ya kujazwa ukumbi wa disko kupita kiasi wakati wa sikukuu ya Iddi. Baraza Kuu linaamini vifo hivyo vingeweza kuepukwa iwapo Serikali ya CCM ingepambana na ufisadi wa kuuza viwanja vya maeneo ya wazi ya kuchezea watoto na kuruhusu sehemu zinazouzwa pombe kutumiwa na watoto.

linalaani vikali na kwa nguvu zote mauaji ya kikatili ya Watanzania wenye ulemavu wa ngozi (Maalbino) kutokana na imani za kishirikina za baadhi ya watu wenye tamaa ya utajiri wa mali na vyeo ambao, badala ya kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na kujituma, wamejiingiza katika uharamia huu. Baraza Kuu linatoa wito kwa Watanzania wote kushirikiana kuwafichua wale wote wanaohusika na unyama huu, na pia kwa vyombo vya dola kufanya kazi ya ziada katika kukabiliana na uharamia huu na kuhakikisha Watanzania wenzetu hawa wanaishi bila ya wasiwasi wa kupotezewa maisha yao.

linalaani kitendo cha Serikali kupuuza madai ya walimu, wafanyakazi wengine na wastaafu nchini wanaodai haki zao kwa njia za migomo ambazo ni njia halali na za kistaarabu zinazokubaliwa na kutambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baraza Kuu linaitaka Serikali ya Rais Kikwete kuyashughulikia madai yao ipasavyo na kwa njia za uhakika badala ya ubabaishaji ambao unazidi kuwakatisha tamaa na kuiyumbisha nchi. Serikali inapaswa itambue kwamba Taifa linalowakera walimu linajenga jamii pofu.

LINALAANI vikali hatua ya Serikali ya CCM kuwapiga, kuwamwagia maji ya kuwasha, kuwakamata na kuwafungulia mashitaka wazee wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao wanadai malipo ya mafao kwa muda wa miaka 30 sasa. Baraza Kuu linaitaka Serikali kuwafutia mashitaka wale wote waliokamatwa katika tukio hilo, na pia linaitaka Wizara ya Fedha na Uchumi kuwalipa mafao yao hayo mara moja.

linalaani vikali na kwa nguvu zote hatua ya Serikali ya kulifungia kwa miezi mitatu gazeti la MWANAHALISI kwa kuandika habari za kuwapo mpango wa baadhi ya viongozi wa CCM kutaka kumpinga Rais Kikwete asigombee Urais mwaka 2010. Baraza Kuu halikubaliani na hatua hiyo ya kidikteta ambayo haina nafasi katika ulimwengu wa leo unaoheshimu demokrasia na uhuru wa habari na linaitaka Serikali kulifungulia gazeti hilo mara moja.

LINAUTAKA Uongozi wa EWURA kuwajibika kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kusimamia bei ya mafuta hapa nchini wakati ambapo bei hiyo katika soko la dunia imeteremka kutoka dola za kimarekani 147 kwa pipa mwezi Julai 2008 hadi dola 65 hivi sasa. Kushindwa kuwajibika kwa EWURA kunapelekea kupanda kwa gharama za maisha kwa Watanzania masikini ambao tayari wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na ufisadi wa Serikali ya CCM.

LINAITAKA Serikali ya CCM kupitia Wizara yake ya Fedha na Uchumi na Benki Kuu kudhibiti mfumuko wa bei hapa nchini ili kuwapunguzia makali ya maisha magumu yaliyoletwa na sera zilizoshindwa za CCM ambazo badala ya kuleta Maisha Bora kwa kila Mtanzania zimesababisha Njaa na Balaa kwa kila Mtanzania.

Linapinga vikali Mswada wa Sheria uliopelekwa Bungeni na Serikali ambao unakusudia kuongeza maeneo ya mbuga za wanyama pori hapa nchini na kuwanyang’anya wananchi maeneo yao ya ardhi. Baraza Kuu linasikitishwa na hatua ya Serikali ya CCM kuonekana inajali zaidi nyumbu wanaokuja kuangaliwa na watalii kuliko binadamu walio raia zake ambao inapaswa kulinda haki zao.

linapinga hatua ya Serikali kuingilia mamlaka ya Bunge na hata uongozi wa Bunge kufikia hatua ya kukubali kuchezewa kwa kubadili maamuzi yaliyokwisha pitishwa kwa kuzuia Wabunge kujadili hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Bungeni tarehe 21 Agosti, 2008. Baraza Kuu linaamini kuwa hatua hiyo ya Serikali kuutumia uongozi wa Bunge kuzuia mjadala wa hotuba ya Rais ina lengo la kuzuia mjadala wa ufisadi wa EPA na hatua zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya wahusika. Baraza Kuu linamtaka Spika wa Bunge, Mheshimiwa Samwel Sitta kuheshimu kauli yake na maamuzi ya Bunge kwa kuruhusu mjadala huo uendelee katika kikao hiki kinachoendelea.

linamtaka Waziri wa Elimu, Profesa Jumanne Maghembe, na uongozi wa Baraza la Mitihani la Taifa wawajibike kwa kujiuzulu kutokana na kashfa ya kuvuja kwa mitihani ambayo sasa limegeuka ni jambo la kawaida. Ufisadi wa Serikali ya CCM ambao sasa unafikia hatua ya kuvuja kwa mitihani kiholela unatishia hata msingi wa maisha yajayo wa wanafunzi wetu.

linawapongeza na kuwashukuru sana wananchi wa mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza kwa kujitokeza kwao kwa wingi katika maandamano yaliyoandaliwa na CUF ya kupiga vita ufisadi na kumtaka Rais Jakaya Kikwete awafikishe mahakamani mafisadi wa EPA. Baraza Kuu linawaomba Watanzania katika mikoa na wilaya nyengine kuungana na wenzao hawa kupitia CUF katika mlolongo wa maandamano na mikutano itakayoitishwa yenye lengo la kuipa shinikizo Serikali ichukue hatua dhidi ya mafisadi wanaoifilisi nchi yetu.

linampongeza Rais mstaafu Festus Moegae wa Botswana kwa kushinda Tuzo ya Mo Ibrahim ya Rais Bora barani Afrika kwa mwaka 2008 na linaitaka Serikali ya Tanzania kujifunza na kuiga sera bora za madini za Botswana ambazo zimewanufaisha wananchi wa nchi hiyo na siyo makampuni ya wageni na mafisadi wachache kama ilivyo hapa Tanzania

MWISHO

LINAWAAHIDI Watanzania wote kwamba CUF kikiwa ni chama cha siasa makini hapa nchini kinachojali na kuheshimu misingi ya umoja, amani, utulivu, haki, uadilifu, maendeleo na ustawi wa nchi yetu na watu wake kimejipanga vyema kuwaongoza Watanzania katika kuleta mabadiliko ya uongozi wa Serikali ifikapo mwaka 2010 yatakayowapatia Watanzania uongozi na utumishi wa dhati utakaoheshimu utu wao na kulinda maslahi yao chini ya misingi ya haki sawa kwa wote na uchumi imara unaotoa neema na ajira kwa wananchi wote. CUF inasema TANZANIA BILA YA CCM INAWEZEKANA.

Yametolewa na:

Prof. Ibrahim Lipumba

Mwenyekiti wa Taifa

Kwa niaba ya

BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA

DAR ES SALAAM

30 OKTOBA, 2008