MEI 21, 2008
Na Jabir Idrissa
ZIPO fitna tatu kuu kwa sasa zinazohusiana na hali ya mambo ilivyo Zanzibar kisiasa kiasi cha kukumbusha mabaya yaliyotokea mara tu baada ya uvurugaji matokeo ya uchaguzi mkuu wa 1995 na 2000.
Fitna ya kwanza ni kuibuka upya kwa hali mbaya ya kisiasa na ya pili, ni hatua ya Jeshi la Polisi kusakama wananchi wa Pemba waliopeleka barua ofisi za Umoja wa Mataifa kushinikiza haki ya kushirikishwa kwenye uongozi wa nchi yao.
Fitna zote hizi zina wenyewe. Ya kwanza imechochewa na Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuzua hoja katika hatua ya mwisho ya kukamilisha mazungumzo iliyokuwa ikifanya na Chama cha Wananchi (CUF) kuhusu utafutaji ufumbuzi wa kudumu wa kile Rais Jakaya Kikwete alichokiita, “mpasuko wa Zanzibar.”
Chama hiki, kitake kisitake, kimevuruga kwa kuleta hoja isiyopata kujadiliwa katika vikao 21 walivyokaa na CUF ndani ya miezi 14 ya majadiliano yaliyoanza kutokana na agizo la Rais Kikwete la 30 Desemba, 2005.
Imethibitika hoja ya Kura ya Maoni haikuwahi kuwasilishwa hata mara moja vikaoni. Inapotokea chama cha rais aliyeagiza mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo la kisiasa, ndio kinavuruga mambo, hiyo huwa ni fitna.
Hilo moja. Lipo la pili: kwamba ni CCM kilichokacha mchakato wa mazungumzo na CUF baada ya kutoa marekebisho ya makubaliano badala ya kuidhinisha na kurudisha rasimu waliyokubaliana.
CCM walipokutana Butiama, kilichotarajiwa kufanyika ni kile kilichofanywa na wenzao CUF 17 Machi, 2008 mjini Zanzibar: kuidhinisha makubaliano na CCM yaliyoandaliwa katika rasimu ya muafaka.
Maamuzi yao yakawa ni kurekebisha makubaliano yaliyofanyiwa kazi kwa vikao 21. Hii ni fitna ndani ya ile fitna ya kwanza ya kuzua hoja mpya.
Baada ya hapo, kumeibuka upya siasa chafu na kauli za kushutumiana zinazojulikana wazi kuwa chanzo cha kuchafuka hali ya hewa Zanzibar.
Kwa hivyo, CCM hawajarudisha rasimu ya muafaka ambayo ingeandaliwa vizuri ili iwe Muafaka wa Tatu na muongozo wa ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa unaoikabili Zanzibar kwa zaidi ya miaka 10 sasa.
Ndio kusema dhamira ya Rais Kikwete haijatimia. Kwa sababu haijatimia, na kwa kuwa utekelezaji wa muafaka ilikuwa ndio matumaini ya wananchi ya kuondokana na mgogoro, unajichimbia mtafaruku.
Mtafaruku umeibua hisia za chuki, hasahasa kwa wananchi wa Pemba. Hawa wamekuwa wakiamini ndio wanaoumia zaidi na siasa chafu zinazojichimbia Zanzibar, wameamua kutafuta namna ya kujitoa katika tanuri la dhiki.
Njia za kujitoa humo ni nyingi. Nyingine za kisiasa ambazo zinaendelezwa na CUF, nyingine za kijamii kama zilizotajwa na mbunge mmoja za wananchi wa Pemba kugoma kupeleka mazao ya chakula Unguja.
Hatua ya wazee 12 kuandika barua na kuipeleka ofisi za Umoja wa Mataifa, Dar es Salaam, ni njia nyingine. Hii si ya kisiasa japo inaweza kuonekana hivyo.
Wazee hawa ni raia katika nchi huru. Wana haki kudai wanachokiamini ni haki. Kudai haki hufanywa kwa njia nyingi; wao wametumia hii inayoshirikisha taasisi ya kimataifa. Wanachokifanya ni kutoa maoni yao baada ya kuona mchafukoge unaendelea kutokana na muafaka kukwama.
Waliamini ungesainiwa na ukaanza kutekelezwa, siasa chafu zingeondoka na kuleta uongozi mzuri ambao matokeo yake ni kuondoka zile dhiki na chuki zinazowaandama.
CCM imefuta matumaini yao. Wafanyeje kama raia wenye haki ya kikatiba ya kuishi kwa amani, utulivu na utengamano wa kweli si wa hisia?
Lazima washinikize mabadiliko. Kupeleka barua inayofahamisha Umoja wa Mataifa kuwa hawawezi kuendelea hivyo na wanaomba msaada kwa taasisi yenye dhamana ya kulinda haki za wamataifa wote duniani, ni shinikizo halali.
Mwaka 1967, Rais Julius Nyerere aliunga mkono kampeni ya wananchi wa Biafra, nchini Nigeria, kutaka kujitenga. Alipeleka jeshi kule kwenda kusaidia wapiganaji wa kundi la MASSOB (Movement for Actualisation of the Sovereign State for Biafra) likiongozwa na Ogumu.
Ogumu na Yakoub Gowon aliyekuwa Rais wa Nigeria wakati huo, leo ni wajumbe wa Baraza la Ushauri la Serikali ya Rais Al Yaradua wa Nigeria.
Wabunge wa Mtwara waliwahi kuitaka Serikali iwaachie wajiunge na Msumbiji ambako ni karibu nao kwa kuwa serikali yao haitaki kuwajengea miundombinu ya kurahisisha shughuli zao za maendeleo. Hawakukamatwa.
(Marehemu) Sebastian Kinyondo alipokuwa Mbunge miaka ya 1990, aliwahi kuitaka serikali iwaachie wananchi wa Mkoa wa Kagera wajiunge na Uganda kwa kuona serikali yao haitaki kuwapatia huduma za jamii kama vile umeme na usafiri wa uhakika. Hakukamatwa.
Wabunge 55 waliounda kundi maarufu likiitwa G55 waliichagiza serikali mwaka 1994 wakitaka irudishwe Tanganyika ili wawe na haki kama walivyo Zanzibar. Hawakukamatwa.
Mchungaji Christopher Mtikila anaamini mpaka leo yeye ni Mtanganyika na angependa itambuliwe hasa Tanganyika ipo. Pamoja na Jamahuri kumfungulia kesi mbalimbali, hakuna kesi kwa hilo. Hajawahi kukamatwa.
Leo Polisi wa Tanzania wanakamata wazee wa Pemba wanaodai haki ya kushirikishwa katika uongozi wa nchi yao. Wangekuwa wabunge, wangedai haki hiyo bungeni, wangekuwa wanasiasa wangedai haki hiyo kwenye jukwaa la kisiasa. Hawa ni raia tu, wameandika barua na kuipeleka Umoja wa Mataifa, tena mchana kweupe.
Kitendo cha Polisi kuwakamata wazee hawa na kuwaandalia kesi si kitisho peke yake, ni fitna ya nguvu.
Nini kama si fitna kugonga milango ya nyumba zao usiku wa manane wakati hawana silaha? Nini maana yake kuwatoa mkuku kutoka vitanda walivyolala na wake zao wakati si magaidi?
Nini maana ya kuwachukua hadi Unguja na Dar es Salaam na kuwaficha kwa siku kadhaa huku wakiwahoji kama vile ni watuhumiwa ujambazi? Haya wangefanyiwa majambazi ningefahamu, wangefanyiwa waleta madawa ya kulevya na majangili ningefahamu. Wanyonge wanaodhalilika nchini mwao wanapodai haki ya kikatiba kwa amani, wametenda kosa gani?
Polisi imeleta fitna isiyo sababu. Inakamata raia anayetoa maoni yake badala ya kumjengea mazingira mazuri ili asahau anachokidai. Halafu Inspekta Jenerali Said Mwema anakataa kwamba Polisi ni wanasiasa. Anakataaje au anataka ushahidi wa Mnyamwezi?
Ni kauli tu lakini haina nguvu. Polisi waliingilia siasa siku zote huko nyuma kama alivyodhihirisha Omar Iddi Mahita kabla hajastaafu. Alijiita ngunguri na hata boti ya Polisi ikapachikwa jina hilo.
Aliisakama CUF na kukamata viongozi wake hadi kutungiwa kesi ya uhaini. Alitia chokochoko chama hicho kisichaguliwe maana kiliingiza mabomu kupitia mkoani Mtwara pamoja na visu kabla ya uchaguzi wa 2005.
Viongozi wa Polisi muache siasa. Nilidhani tatizo lilikuwa Mahita, kumbe kiti cha IGP. Niliandika sana makala, kupitia safu ya Waraka kutoka Unguja, kabla ya uchaguzi wa 2005 nikiwalaumu Polisi kwa uovu huu. Nilisihi wabadilike ili waheshimike kuwa walinzi wa kweli wa raia na mali zao. Hawakusikia wakasaidia kuvuruga uchaguzi, wakaua.
Nasikitika narudishwa kulekule kutokana utendaji wao. Hivi Watanzania wanaotoka Pemba wamekosa nini? Likizuka la ugaidi wao, likija la uhaini wao, likija la mpasuko, wao. Niliamini tu watakamatwa baada ya kusikia Waziri wa Nchi, ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Muhammed Seif Khatibu akisema kudai kujitenga ni “uhaini.”
Vitisho dhidi ya raia Zanzibar huanza hivyo. Hutokea tukio na kada wa CCM akatoa kauli ambayo vyombo vya ulinzi na usalama huichukua ni amri. Inapokuwa wahusika ni wafuasi wa upinzani, inajengwa kesi.
Hizi zote ni fitna. Lengo lake ni kukengeuka tatizo la msingi linaloikabili nchi, Muafaka, ili kulaghai wananchi kwa kupakaza ubaya wanaopigania haki zao.
Polisi hawajawahi kukamata wabunifu na wasambazaji wa vikaratasi vinavyoeneza chuki dhidi ya wanaokandamizwa.
Hawajawahi hata mara moja japokuwa wanawafahamu wanaoendesha operesheni hii ya kishetani. Siku zote makamanda husema “tunachunguza.” Sawa waendelee kuchunguza kama walivyofanya kwa ile milipuko ya kishetani baada ya uchaguzi wa 2000.
Wameshindwa hadi leo kumshitaki askari wa KMKM aliyemuua mwanafunzi wa shule ya msingi Ng’ombeni mjini Mkoani wakati wa kuandikisha wapiga kura.
Hawa ndio walewale waliokuwa wakiandaa mabomu ya petroli na kuwasha kwenye maeneo mbalimbali mjini Zanzibar na kwenye makanisa ili kujenga chuki na kupata sababu ya kukamatwa wafuasi wa upinzani. Polisi mtajifunza lini?
http://www.halihalisi.co.tz/08/05/21/4.php
Maoni