”Mheshimiwa Spika, Utafiti wa nguvukazi wa mwaka 2001 ulionyesha kuwa kila mwaka ajira mpya 400,000 zinaanzishwa wakati nguvu kazi laki saba inaingia katika soko la ajira. Serikali ya awamu ya nne iliahidi itaanzisha ajira mpya milioni moja katika kipindi cha miaka mitano wastani wa ajira laki mbili kila mwaka. Waziri ameeleza kwamba katika kipindi cha miezi 18 kuanzia mwezi Julai 2005 hadi Desemba 2007, ajira mpya 412,608 zilikuwa zimepatikana. Ajira 194,325 zimetokana na sekta rasmi na ajira 218,283 zimetokana na sekta isiyo rasmi. Hata hivyo Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2007 hakina jedwali linaloonyesha ajira hizo na sekta zake. Kitabu hicho kinaonyesha ajira viwandani imeongezeka toka watu 89,316 mwaka 2005 na kufikia watu 91,112, ongezeko la wafanyakazi 1,796 tu. Kwa kadri muundo wa uchumi unavyobadilika ndivyo sekta ya viwanda inavyotegemewa kutoa mchango mkubwa kwa ajira mpya. Aidha, Kambi ya Upinzani inamtaka Mhe. Waziri alieleze Bunge lako tukufu, hizo ajira zaidi ya laki nne ziko sekta gani? Au ajira hizo ni ajira hewa?”
Hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha – 2008/2009 Read the rest of this entry »




Maoni